Watu 38 hawajulikani walipo baada ya jengo kuanguka Nairobi.
Kulingana na Susan Auma Mang’eni, ambaye ni Katibu Mkuu katika Idara ya Serikali inayoshughulikia Maendeleo ya Biashara ndogo ndogo na za Kati (MSME) nchini Kenya, bado kuna watu ambao hawajulikani walipo kufuatia kuanguka kwa jengo,lenye ghorofa 18 katika mtaa wa Eastleigh mjini Nairobi siku ya Ijumaa.
"Hadi kufikia sasa, takriban watu 38 wameripotiwa kupotea," alisema Mang’eni.
Kulingana na katibu huyo,familia zimetoa taarifa kuhusu ndugu zao waliopotea kwa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya na timu nyingine zinazoshiriki katika shughuli za uokoaji, ikiwemo Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na vyombo vya usalama.
Mang’eni alisema mamlaka zinafuatilia kila taarifa ili kubaini walipo watu hao waliopotea, akiongeza kuwa namba za simu zilizotolewa na familia zinaweza kusaidia wachunguzi kuwafuatilia.
"Wakati mwingine mkitupa simu, tunaweza kubaini mahali ambapo namba hiyo inapatikana," alisema.
Mang’eni alisema watu tisa wamepatikana, huku baadhi wakipatikana katika eneo la tukio. Wengine, alisema, hawakuwepo eneo hilo siku jengo hilo lilipoanguka.
Namba za simu za watu hao tisa ziliendana na simu zilizopatikana kwenye vifusi.