Iran yakanusha kuhusika na mashambulizi ya Wahouthi nchini Saudi Arabia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amekataa madai yoyote yanayoiunganisha nchi hiyo na mashambulizi ya Wahouthiakieleza wako tayari kuwa wapatanishi kati ya Wahouthi na Riyadh ili kufanikisha maridhiano.
Muhtasari
- Maandamano Ufaransa: Makumi wakamatwa huku maandamano ya kitaifa yakianza
- DRC yapiga marufuku mawasiliano kati ya wafanyakazi wa Ikulu na Ubalozi wa Ubelgiji
- Uingereza yawataka raia wake kuepuka safari zisizo za lazima Saudi Arabia
- Iran yakanusha kuhusika na mashambulizi ya Wahouthi nchini Saudi Arabia
- Meli nyingine ya mafuta yashambuliwa kwa roketi katika pwani ya Saudi Arabia
- Sisi: Katiba ya Misri haitabadilishwa, muhula wangu wa urais utaisha mwaka 2030
- Wagombea wote 7 wa ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wakabiliwa na upinzani katika kura za siri
- Msemaji mpya wa Ikulu ya White House ajiuzulu siku tano baada ya kuanza kazi
- Mshindi wa taji la Miss Grand International 2026, Jihan Dimack, apokelewa kwa shangwe Tanzania
- Bei ya mafuta yapanda hadi dola 110 kwa pipa kwa mara ya kwanza ndani ya miezi sita
- Trump adai Marekani inaweza kusikiliza mazungumzo yote ya viongozi wa Iran
- Serikali ya Ethiopia yaweka Tigray chini ya utawala wa mpito wa miezi sita
- Waziri Mkuu wa Uhispania asema vita dhidi ya Iran vimegharimu Ulaya zaidi ya euro bilioni 100
- Korea Kaskazini yafanyia majaribio torpedo inayoongozwa kwa kutumia akili unde
- Tetesi za Soka Jumamosi: Bellingham akubali mkataba mpya Real Madrid
- Trump asitisha kwa muda vikwazo vingi vipya dhidi ya Urusi
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid
Maandamano Ufaransa: Makumi wakamatwa huku maandamano ya kitaifa yakianza

Chanzo cha picha, Getty Images
Polisi nchini Ufaransa wamewakamata makumi ya watu mjini Paris, huku mapigano kati ya polisi na waandamanaji yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha watu wakirusha fataki na moshi wa rangi ukitanda katika mji mkuu, Paris. Picha kutoka Marseille, kwa upande mwingine, zinaonekana kuwaonyesha polisi wakitumia mabomu ya machozi.
Maelfu ya watu wanatarajiwa kuandamana katika maandamano yanayowajumuisha vyama vya wafanyakazi, wanafunzi na kundi la Yellow Vests. Waandamanaji wanapinga kupanda kwa bei ya mafuta, gharama ya bidhaa muhimu na kuzorota kwa huduma za umma, zikiwemo shule.
Mwanafunzi mmoja ameiambia shirika la habari la Reuters kuwa maandamano hayo yanalenga kuwaunganisha watu kutoka makundi na maisha tofauti.
Kundi la Yellow Vests, lililoandaa maandamano ya leo, liliendesha maandamano kwa zaidi ya mwaka mmoja kuanzia 2018, likipinga kupanda kwa bei na gharama ya maisha. Tovuti ya kundi hilo inaonyesha kuwa mamia ya maandamano yamepangwa kufanyika kote nchini, huku wakulima, wafanyakazi, wanaharakati wa mazingira na wazee wakihimizwa kushiriki.
Maandamano hayo mapya yanafuatia wiki kadhaa za wanafunzi kuandamana wakitaka kuboreshwa kwa masomo na mbinu za ufundishaji. Kumekuwa na mapigano ya hapa na pale kati ya wanafunzi na polisi, pamoja na hali ya sintofahamu katika baadhi ya maeneo.
Mapema mwezi huu, mvulana mwenye umri wa miaka 15 alijeruhiwa vibaya baada ya mkono wake kukatika katika mlipuko.
Soma Pia:
DRC yapiga marufuku mawasiliano kati ya wafanyakazi wa Ikulu na Ubalozi wa Ubelgiji

Chanzo cha picha, Reuters
Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imepiga marufuku wafanyakazi wake kuwasiliana au kuwa na uhusiano wowote na Ubalozi wa Ubelgiji mjini Kinshasa.
Barua ya Oktoba 15, iliyotiwa saini na Anthony Nkinzo Kamole, mkuu wa ofisi ya mawasiliano ya Rais Félix Tshisekedi, inaelekeza wafanyakazi wote wa Ikulu kujizuia, hadi watakapotaarifiwa vinginevyo, kufanya mawasiliano yoyote na ubalozi huo, yawe ya moja kwa moja au kupitia watu wengine.
Uamuzi huo unaonekana kuishangaza serikali ya Ubelgiji. Kwa mujibu wa kituo cha redio cha Ufaransa, RFI, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji imesema haioni sababu ya kuzuia watu kuwasiliana na ubalozi huo au kupata taarifa kutoka kwake, na kwamba imeshangazwa na hatua hiyo.
Barua hiyo haijaeleza wazi sababu za uamuzi huo.
Hata hivyo, imetolewa siku moja tu baada ya waendesha mashtaka wa Ubelgiji kufanya upekuzi katika makazi ya baadhi ya wanafamilia wa Rais Tshisekedi.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa kitaifa wa Ubelgiji, upekuzi huo unahusiana na tuhuma za hivi karibuni za utakatishaji fedha na kujilimbikizia mali kinyume cha sheria zinazowakabili wanafamilia hao.
Tuhuma hizo ziliwasilishwa Aprili 2025 na muungano wa DESC/RDC, unaojumuisha mashirika yanayotetea haki za kiuchumi nchini DRC. Muungano huo unaituhumu familia ya Tshisekedi kwa kupora madini na kutwaa migodi katika jimbo la Katanga.
Kwa mujibu wa barua ya Ofisi ya Rais wa DRC, iwapo kutatokea haja ya dharura na ya msingi ya kuwasiliana na ubalozi huo, mawasiliano yote lazima yaidhinishwe na Wizara ya Mambo ya Nje.
Soma Pia:
Uingereza yawataka raia wake kuepuka safari zisizo za lazima Saudi Arabia

Chanzo cha picha, Getty Images
Uingereza imewaonya raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Saudi Arabia isipokuwa pale ambapo safari hiyo ni ya lazima kabisa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilitoa tahadhari hiyo Ijumaa, ikieleza kuwa inashauri dhidi ya safari zote zisizo za lazima kwenda nchini humo kutokana na mashambulizi yanayofanywa na waasi wa Kihouthi wa Yemen.
Nchi nyingine kadhaa tayari zilikuwa zimetoa tahadhari kama hiyo kwa raia wake kuhusu kusafiri kwenda Saudi Arabia.
Wakati huohuo, Ubalozi wa Marekani nchini Saudi Arabia umewashauri raia wa Marekani kuwa, kutokana na mashambulizi dhidi ya viwanja vya ndege vya nchi hiyo, kutumia magari binafsi, treni au mabasi kunaweza kuwa salama zaidi kuliko kusafiri kwa ndege kuingia au kutoka nchini humo.
Soma Pia;
Iran yakanusha kuhusika na mashambulizi ya Wahouthi nchini Saudi Arabia

Chanzo cha picha, Getty Images
Iran imekanusha madai ya Saudi Arabia kwamba inahusika na mashambulizi yanayofanywa na waasi wa Kihouthi wa Yemen dhidi ya nchi hiyo. Tehran pia imetangaza utayari wake wa kusaidia kupatanisha pande hizo mbili.
Katika taarifa yake ya Ijumaa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alikataa madai yoyote yanayoiunganisha nchi hiyo na mashambulizi ya Wahouthi. Alisema Tehran iko tayari kuwa mpatanishi kati ya Wahouthi na Riyadh ili kufanikisha maridhiano.
Baghaei alisema Iran imekuwa tayari kusaidia kukomesha ghasia na itaendelea kutumia uwezo wake wote kufanikisha hilo iwapo pande zinazohusika zitaomba msaada huo.
Katika wiki za hivi karibuni, wapiganaji wa Kihouthi wamefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya maeneo mbalimbali nchini Saudi Arabia, yakiwemo meli katika Bahari Nyekundu, miundombinu ya mafuta na uwanja wa ndege wa Riyadh.
Katika mojawapo ya mashambulizi hayo wiki iliyopita, watu 13 walipoteza maisha.
Wakati huo huo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umeendelea kufanya mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Kihouthi.
Pia Unaweza Kusoma:
Meli nyingine ya mafuta yashambuliwa kwa roketi katika pwani ya Saudi Arabia

Chanzo cha picha, EPA
Shirika la Uendeshaji wa Biashara ya Baharini la Uingereza (UKMTO) limeripoti kushambuliwa kwa meli nyingine ya mafuta katika pwani ya kaskazini mashariki mwa Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa shirika hilo, nahodha wa meli hiyo alisema boti ndogo iliikaribia ikiwa umbali wa takriban kilomita 144 kutoka pwani ya Jubail, kisha kufyatua roketi ya kurushwa begani aina ya RPG. Shambulio hilo liliharibu sehemu ya nyuma ya meli upande wa kushoto.
Nahodha alisema washambuliaji waliondoka eneo hilo baada ya kufyatua roketi, huku meli ikiendelea na safari yake.
UKMTO imethibitisha kuwa hakuna mfanyakazi wa meli aliyejeruhiwa katika shambulio hilo.
Tukio hilo limetokea saa moja tu baada ya shirika hilo kuripoti kushambuliwa kwa meli nyingine ya mafuta katika eneo hilo hilo.
Katika tukio la awali, kifaa kisichojulikana kiligonga meli hiyo ikiwa umbali wa takriban kilomita 126 kutoka Jubail. Hakuna aliyejeruhiwa katika shambulio hilo pia.
Pia unaweza kusoma:
Sisi: Katiba ya Misri haitabadilishwa, muhula wangu wa urais utaisha mwaka 2030

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Misri, Abdel Fattah al Sisi, amesema muhula wake wa urais utakamilika mwaka 2030.
Akizungumza na wahitimu wapya wa chuo cha kijeshi nchini humo, Sisi alisema 'suala hilo tayari limetatuliwa kabisa' na kwamba kipengele cha katiba kinachoweka ukomo wa mihula miwili ya urais hakitabadilishwa.
Aidha, alisema hatang'atuka madarakani hadi serikali ya Misri itakapokuwa na watu wenye uwezo wa kubeba majukumu ya uongozi.
Sisi alichukua madaraka mwaka 2013 kufuatia maandamano dhidi ya rais wa wakati huo, Mohamed Morsi. Mwaka mmoja baadaye, alichaguliwa kuwa rais wa Misri baada ya kushinda uchaguzi.
Mwaka 2019, serikali ya Misri iliongeza muda wa kila muhula wa urais kupitia kura ya maoni, lakini ikaendelea kudumisha ukomo wa mihula miwili ya urais.
Pia Soma:
Wagombea wote 7 wa ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wakabiliwa na upinzani katika kura za siri

Chanzo cha picha, Getty Images
Wagombea wote saba wanaowania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wamepata kura za kutopendekezwa kutoka kwa angalau mmoja wa wajumbe watano wa kudumu wa Baraza la Usalama, hatua inayoweza kuwa kikwazo kikubwa katika azma yao ya kuwania nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja, matokeo hayo yalijitokeza katika kura za maoni zisizo rasmi zilizofanyika Ijumaa.
Kwa mara ya kwanza katika utaratibu huo wa upigaji kura wa siri, Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani zilitumia vijiti vya rangi kuashiria wagombea wanaowapinga, huku wajumbe 10 waliochaguliwa wa Baraza la Usalama wakiendelea kutumia vijiti visivyo na rangi.
Rebeca Grynspan wa Costa Rica, ambaye amekuwa miongoni mwa wagombea waliopewa nafasi kubwa ya kushinda katika duru tano zilizopita, alipata kura nyingi zaidi za kuungwa mkono katika duru hii. Hata hivyo, alipata pia kura tano za kutopendekezwa, zikiwemo mbili kutoka kwa wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama.
Taarifa za vyombo vya habari vya Marekani zinaashiria kuwa Washington inawapinga wagombea wote saba wanaowania nafasi hiyo.
Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, alikataa kutoa maoni kuhusu taarifa hizo. Hata hivyo, alisema Ijumaa kuwa nchi yake imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kumpata mgombea bora zaidi.
Kuhusu uwezekano wa wagombea wengine kuingia katika kinyang'anyiro hicho, Waltz alisema nchi zina haki ya kuwasilisha wagombea zaidi, akisisitiza kuwa uamuzi huo ni sehemu ya mamlaka yao ya kujitawala.
Miongoni mwa wanaotajwa na wanadiplomasia kuwa huenda wakaingia katika kinyang'anyiro hicho ni Nickolay Mladenov, mwakilishi mkuu wa masuala ya Gaza chini ya Bodi ya Amani inayoungwa mkono na Marekani, pamoja na Lana Nusseibeh, waziri wa nchi anayeshughulikia masuala ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu.
Jina la Feridun Hadi Sinirlioglu wa Uturuki, Katibu Mkuu wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE, pia limetajwa miongoni mwa wanaoweza kuwania nafasi hiyo.
Grynspan amekuwa akifanya vizuri zaidi kwa wastani katika duru za awali za upigaji kura, na aliibuka tena kinara katika kura za Ijumaa licha ya kukabiliwa na kura mbili za turufu kutoka kwa wajumbe wa kudumu.
Wagombea wengine ni Carolyn Rodrigues Birkett, aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Guyana; Rafael Grossi wa Argentina, ambaye kwa sasa anaongoza Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki; rais wa zamani wa Senegal Macky Sall; Ivonne A Baki na Maria Fernanda Espinosa wa Ecuador; pamoja na Olara Otunnu wa Uganda.
Katibu Mkuu wa sasa, Antonio Guterres wa Ureno, anatarajiwa kumaliza muhula wake wa pili wa miaka mitano tarehe 31 Desemba 2026.
Ili mgombea aweze kupendekezwa na Baraza la Usalama, anahitaji kupata angalau kura tisa kati ya 15. Hata hivyo, idadi hiyo pekee haitoshi, kwani pia anatakiwa kuepuka kura ya turufu kutoka kwa mojawapo ya mataifa matano yenye mamlaka ya kudumu katika baraza hilo.
Baada ya kupita hatua hiyo, jina la mgombea anayependekezwa litawasilishwa kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, linalojumuisha nchi zote wanachama, kwa ajili ya kuthibitishwa.
Soma Pia:
Msemaji mpya wa Ikulu ya White House ajiuzulu siku tano baada ya kuanza kazi

Chanzo cha picha, IKULU YA WHITE HOUSE
Katie Zacharias ameondoka katika nafasi yake ya msemaji wa Ikulu ya White House, siku tano tu baada ya kufanya mkutano wake wa kwanza rasmi na wanahabari, ambao uliibua ukosoaji mkubwa.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema alimshauri Zacharias kutafakari upya uamuzi wake wa kuendelea na kazi hiyo iwapo hakuwa ameridhika nayo, akidai kuwa vyombo vya habari vilimuandama kwa ukali.
Mkutano wake wa kwanza na wanahabari, uliofanyika Jumanne, ulidumu kwa muda usiozidi dakika 15 na ulihusisha maswali matatu pekee. Katika mkutano huo, Zacharias pia alikabiliwa na maswali kuhusu sifa na maandalizi yake ya kushika wadhifa huo.
Mzozo mkubwa ulizuka kuhusu sifa zake za kisheria baada ya kubainika kuwa hakuwa amefaulu mtihani wa kuhitimu kuwa wakili nchini Marekani, licha ya Trump na watu wengine kumtaja awali kuwa ni wakili.
Siku ya Alhamisi, Zacharias alikiri kuwa hakufaulu mtihani huo, lakini akasema alikuwa amefanya kazi nchini China katika masuala ya sheria ya biashara ya kimataifa, akiwa na ujuzi na sifa alizodai zinahitajika katika eneo hilo.
Katika mahojiano na kituo cha Fox News, alisema aliajiriwa kwa ajili ya mawasiliano na mahusiano ya umma, wala si kushughulikia masuala ya kisheria.
Kwa upande mwingine, Chama cha Democratic kinatumia kuondoka kwake kuikosoa Ikulu ya White House inayoongozwa na chama cha Republican, kikieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kushindwa kwa utawala huo.
Kuondoka kwa Zacharias kunatajwa kuwa mojawapo ya vipindi vifupi zaidi vya kuhudumu katika timu ya mawasiliano ya Ikulu ya White House chini ya Trump. Katika muhula wake wa kwanza, Anthony Scaramucci aliondoka katika nafasi ya mkurugenzi wa mawasiliano wa Ikulu baada ya siku 10 tu.
Mshindi wa taji la Miss Grand International 2026, Jihan Dimack, apokelewa kwa shangwe Tanzania

Chanzo cha picha, Miss Grand International
Mshindi wa taji la Miss Grand International 2026, Jihan Dimack, amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, akirejea kutoka Thailand.
Jihan amepokelewa kwa shangwe na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania, waliokusanyika kumpongeza kwa kuiwakilisha vyema nchi hiyo katika jukwaa la kimataifa la urembo.
Mapokezi hayo yamehudhuriwa na wasanii, akiwemo Rayvanny, pamoja na wadau mbalimbali wa tasnia ya urembo na burudani nchini Tanzania.
Akiwa nchini Thailand kwa ajili ya kushiriki shindano hilo, Jihan alitoa wito kwa mataifa duniani kuendeleza amani, upendo na umoja. Alieleza kuwa watu wengi wasio na hatia wanaendelea kupoteza maisha, familia zao, makazi na ndoto zao kutokana na migogoro inayoendelea katika maeneo mbalimbali duniani.
Jihan amesema anajivunia kuzaliwa Tanzania, nchi anayoitaja kuwa mfano wa amani, upendo na umoja. Alieleza kuwa Watanzania wana utamaduni wa kuishi na kufanya kazi kwa ushirikiano, bila kujali tofauti za asili, dini au mila.
Alisisitiza kuwa amani ni ishara ya ujasiri, wala si udhaifu.
“Haijalishi unatoka wapi, tuuache ubinadamu upewe nafasi yake na tusiruhusu mioyo yetu kutawaliwa na chuki. Tueneze amani na upendo, na tuishi kwa maelewano. Asanteni,” amesema Jihan.
Bei ya mafuta yapanda hadi dola 110 kwa pipa kwa mara ya kwanza ndani ya miezi sita

Chanzo cha picha, Getty Images
Bei ya mafuta ghafi duniani imepanda na kufikia karibu dola 110 kwa pipa kwa mara ya kwanza tangu mwezi Mei, huku hofu ya kuongezeka kwa mvutano wa Mashariki ya Kati ikichangia kupanda kwa bei hiyo.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa uchumi, ongezeko hilo linatokana na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuzidi kwa mivutano katika eneo hilo, hali inayoweza kuvuruga uzalishaji na usambazaji wa mafuta katika soko la dunia.
Siku ya Ijumaa, bei ya mafuta ghafi aina ya Brent ilipanda kwa dola 3.94 na kufikia dola 109.86 kwa pipa, kiwango cha juu zaidi tangu Mei 19.
Wakati huohuo, bei ya mafuta ghafi aina ya West Texas Intermediate (WTI) ya Marekani iliongezeka kwa dola 3.44 na kufikia dola 101.41 kwa pipa, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi tangu Septemba 17.
Pia unaweza kusoma:
Trump adai Marekani inaweza kusikiliza mazungumzo yote ya viongozi wa Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa BBC Urdu, Rais wa Marekani, Donald Trump, amedai kuwa nchi yake ina uwezo wa kusikiliza kila kitu kinachozungumzwa na maafisa na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, Trump alisema: “Bila shaka, hili ni jambo la siri, lakini sasa nimeliweka wazi kwa umma.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, rais huyo wa Marekani aliuelezea vita dhidi ya Iran kama “zoezi la kijeshi.”
Trump pia aliibua swali kuhusu jinsi nchi za Kiarabu zingepokea pendekezo la kubadilisha jina la Mlango-Bahari wa Hormuz na kuuita “Mlango-Bahari wa Trump.”
Alisema kuwa Marekani inaweza kutekeleza mabadiliko hayo kwa urahisi.
Pia unaweza Kusoma:
Serikali ya Ethiopia yaweka Tigray chini ya utawala wa mpito wa miezi sita

Chanzo cha picha, Ofisi ya Waziri Mkuu /Ethiopian
Baraza la Mawaziri la Ethiopia limeteua utawala wa mpito wa shirikisho kusimamia Mkoa wa Tigray kwa kipindi cha miezi sita ijayo.
Serikali imesema hatua hiyo inalenga kurejesha usalama na utulivu katika eneo hilo, pamoja na kuweka mazingira yatakayowezesha maandalizi ya uchaguzi ujao.
Uamuzi wa kuanzisha utawala huo mpya uliidhinishwa na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Shirikisho, kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa.
Serikali ya Ethiopia imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya juhudi za kutatua mzozo wa Tigray chini ya Makubaliano ya Pretoria kushindwa kufanikiwa, ikidai kuwa hali hiyo imesababishwa na kile ilichokitaja kuwa ni vikwazo vilivyowekwa na chama cha TPLF.
Katika taarifa yake, serikali imedai kuwa viongozi wa TPLF hawakuwa na nia ya kuleta amani, na kwamba vita vya nne vilivyoanzishwa na chama hicho viliishia katika kushindwa.
Kwa upande wake, TPLF imekuwa ikiishutumu mara kwa mara serikali ya Ethiopia kwa kukiuka Makubaliano ya Pretoria, kuzuia wakimbizi wa ndani kurejea makwao na kushindwa kutekeleza wajibu wake chini ya makubaliano hayo.
Utawala huo mpya wa mpito, ambao utakuwa ukipokea maagizo na maelekezo moja kwa moja kutoka kwa serikali ya shirikisho, umepewa jukumu la kurejesha miundombinu na mifumo ya huduma za msingi za kijamii iliyoharibiwa, kukarabati miundombinu iliyoharibiwa, kufufua shughuli za kiuchumi na kuwezesha kurejea kwa watu waliokimbia makazi yao.
Aidha, unatarajiwa kuratibu masuala ya usalama kwa kushirikiana na vikosi vya usalama vya shirikisho, polisi na vikosi vya usalama vya Tigray. Ushirikiano huo unalenga kuwezesha makabidhiano ya silaha na kuwawezesha wananchi kurejea katika maisha ya amani.
Waziri Mkuu wa Uhispania asema vita dhidi ya Iran vimegharimu Ulaya zaidi ya euro bilioni 100

Chanzo cha picha, EPA
Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez, amesema kuwa vita dhidi ya Iran vimewagharimu raia wa Ulaya zaidi ya euro bilioni 100 hadi sasa, huku mzigo wa kiuchumi unaotokana na vita hivyo ukiwaathiri pakubwa wananchi wa kawaida.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, Sánchez aliambatanisha video yenye ujumbe wake, akisema: “Sisi tulioinua sauti zetu kupinga vita hivi tulikuwa sahihi tuliposema ‘hapana’ kwa vita.”
Aliongeza kuwa walifahamu tangu mwanzo kwamba, hatimaye, wananchi wa kawaida ndio ambao wangelipa gharama ya vita hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa Baraza la Ulaya uliofanyika mjini Brussels siku ya Ijumaa, Sánchez alisema kuwa msimamo wa wale waliopinga vita hivyo umethibitishwa kuwa sahihi.
Alieleza kuwa msimamo huo ulikuwa sahihi “si tu kwa kuzingatia sheria za kimataifa na kuheshimu haki za binadamu, bali pia kutokana na athari za kiuchumi na kijamii ambazo wananchi wetu wanazikabili tena.”
“Hatimaye, wananchi wa kawaida ndio wanaolipa gharama, na kwa bahati mbaya, athari hizo zinaendelea kuonekana hata sasa,” alisema.
Waziri mkuu huyo wa Uhispania aliongeza kuwa bunge la nchi hiyo limeidhinisha kifurushi cha msaada chenye thamani ya zaidi ya euro bilioni 12, kwa ajili ya kusaidia sekta zilizoathirika pamoja na wananchi wanaotumia magari yao binafsi.
Alisisitiza kuwa jambo muhimu kwa sasa ni kukomesha janga hilo haraka iwezekanavyo.
Soma pia:
Korea Kaskazini yafanyia majaribio torpedo inayoongozwa kwa kutumia akili unde

Chanzo cha picha, KCTV
Korea Kaskazini imefanyia majaribio mfumo wa torpedo inayoongozwa kwa kutumia teknolojia ya akili unde (AI), inayoiwezesha kutambua shabaha na kuelekezwa kuifikia.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo, jaribio la torpedo hiyo yenye kasi ya juu sana, aina ya Zam-2, lilifanyika Alhamisi kwa lengo la kuthibitisha “mafanikio ya maboresho ya kiteknolojia” yaliyofanywa kwenye silaha hiyo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa torpedo hiyo yenye uwezo wa kulenga shabaha kwa usahihi na kusafiri kwa kasi kubwa hutumia teknolojia ya akili unde kutambua shabaha na kujielekeza kuifikia.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA), katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, “majaribio zaidi ya 180 ya aina mbalimbali” yamefanyika katika eneo hilo la teknolojia ya silaha.
Kwa mujibu wa wachambuzi, ingawa torpedo hizo zimeundwa kushambulia shabaha za adui chini ya maji kwa kasi kubwa, matumizi ya akili unde yanaweza kuiwezesha Korea Kaskazini kuvuruga mikakati ya adui kwa kukwepa mashambulizi na kufanya maamuzi kwa kujitegemea.
Taarifa hiyo imechapishwa siku chache baada ya Korea Kaskazini kutangaza kuwa ilikuwa imerusha aina mbili za makombora ya masafa marefu ya kuruka kwa mwelekeo maalumu (cruise missiles) kutoka kwenye manowari.
Soma Pia:
Tetesi za Soka Jumamosi: Bellingham akubali mkataba mpya Real Madrid

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiungo wa timu ya taifa ya England, Jude Bellingham, mwenye umri wa miaka 23, amefikia makubaliano ya kuongeza mkataba wake na Real Madrid hadi mwaka 2031. (AS - in Spanish)
Arsenal na Liverpool zingelazimika kulipa zaidi ya pauni milioni 60 ili kumsajili winga wa timu ya taifa ya Ujerumani, Kevin Schade, mwenye umri wa miaka 24, kutoka Brentford. (Teamtalk)
Leeds United inafuatilia kwa karibu hali ya mshambuliaji wa Brazil, Igor Paixão, katika klabu ya Marseille. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ni miongoni mwa wachezaji ambao klabu hiyo ya Ufaransa huenda ikalazimika kuwauza kutokana na changamoto za kifedha. (Football Insider)
Chelsea, Manchester United, Arsenal, Liverpool na Bayern Munich zinafuatilia kwa karibu mustakabali wa beki wa Ufaransa, Jules Koundé, katika Barcelona. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 anatafakari hatma yake katika klabu hiyo ya Catalonia.(4-4-2.ch - in German)
Barcelona haitaki kuingia katika ushindani wa zabuni ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Manchester United, JJ Gabriel, mwenye umri wa miaka 16. Real Madrid na Paris Saint-Germain ziko tayari kutoa ofa kubwa zaidi ya kifedha kwa ajili ya mchezaji huyo. (Sport - in Spanish)
Newcastle United bado haijapiga hatua katika mazungumzo ya kumshawishi kiungo wa England, Joe Willock, mwenye umri wa miaka 27, kusaini mkataba mpya. Hata hivyo, kocha wa Newcastle, Matthias Jaissle, anavutiwa na uwezo wa mchezaji huyo. (Newcastle Chronicle)
Kocha wa Leeds United, Daniel Farke, amefikia makubaliano ya mkataba mpya utakaomweka katika klabu hiyo inayotumia uwanja wa Elland Road hadi mwaka 2029. Farke ana umri wa miaka 49 na anatoka Ujerumani. (The Athletic - subscription required)
Mkurugenzi wa michezo wa Bayern Munich, Max Eberl, amesema mazungumzo na mshambuliaji wa England, Harry Kane, kuhusu mkataba mpya yanaendelea vizuri, ingawa bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa. Sky Sports Germany - in German)
Beki wa England anayeichezea AC Milan, Fikayo Tomori, mwenye umri wa miaka 28, ataondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu mkataba wake utakapomalizika. Hakuna uwezekano wa kuongezewa mkataba mpya kwa mchezaji huyo wa zamani wa Chelsea katika uwanja wa San Siro. (Calciomercato - in Italian)
Real Madrid inaweza kumruhusu mshambuliaji wa Morocco, Brahim Díaz, mwenye umri wa miaka 27, kuondoka kwa mkopo katika dirisha la usajili la Januari. Hatua hiyo inakuja baada ya mshambuliaji wa Brazil, Endrick, mwenye umri wa miaka 20, kumpiku katika mpangilio wa wachezaji wanaopewa kipaumbele kikosini hapo. (Marca - in Spanish), external
Soma Pia:
Trump asitisha kwa muda vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametumia mamlaka yake ya urais kuzuia utekelezaji wa vikwazo kadhaa dhidi ya Urusi vilivyoidhinishwa hivi karibuni na Bunge la Marekani, kwa lengo la kuiadhibu nchi hiyo kutokana na vita vyake dhidi ya Ukraine.
Katika amri ya rais aliyotoa Ijumaa usiku, Donald Trump alisema kuwa kuzuia utekelezaji wa baadhi ya vikwazo hivyo ni kwa ajili ya kulinda “maslahi ya taifa” la Marekani. Trump alisaini muswada wa vikwazo hivyo kuwa sheria mwezi Septemba, na ulitarajiwa kuanza kutekelezwa Jumapili.
Hatua hiyo inajiri siku chache baada ya Trump kusema kuwa Marekani ingeagiza dizeli kutoka Urusi kwa lengo la kupunguza bei za nishati nchini humo kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa urais utakaofanyika mwezi Novemba, ambao utaamua ni chama gani kitakachodhibiti Bunge la Marekani.
Mpango huo umewashangaza wabunge na kusababisha upinzani kutoka kwa wanasiasa wa vyama vyote viwili vikuu nchini Marekani, yaani Chama cha Republican na Chama cha Democratic.
Sheria ya vikwazo vya Marekani imepewa jina la Seneta wa Republican wa jimbo la South Carolina, Lindsey Graham, aliyefariki dunia. Kabla ya kifo chake Julai 11, Graham alikuwa miongoni mwa watetezi wakuu wa Ukraine mjini Washington.
Sheria hiyo ililenga uchumi wa Urusi na kumpa Trump mamlaka mapana ya kutoza ushuru wa hadi asilimia 100 kwa nchi tano zinazonunua kwa wingi mafuta na gesi kutoka Urusi, hususan China na India.
Aidha, sheria hiyo inajumuisha vikwazo dhidi ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin, maafisa waandamizi wa serikali ya Urusi, benki na taasisi nyingine za kifedha, pamoja na kile kinachojulikana kama “meli za kivuli” za Urusi, kundi la meli za mafuta zinazotumiwa kukwepa vikwazo vilivyopo.
Siku ya Alhamisi, kundi la wabunge 20 wa Marekani kutoka vyama vyote viwili lilitoa barua likimtaka Trump kuheshimu sheria hiyo mpya, ambayo ilitarajiwa kuanza kutekelezwa tarehe 18 Oktoba.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 17/10/2026.



















