Na hapa ndipo tunatamatisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.
Meli zilizowekewa vikwazo na Marekani zapita Mlango wa Hormuz huku China ikiita kizuizi cha Trump kuwa ‘hatari’
Meli nne zinazohusishwa na Iran, zimepita katika Mlango bahari wa Hormuz baada ya kizuizi cha kijeshi cha Marekani kuanza kutekelezwa
Muhtasari
- Polisi Tanzania wamhoji Joseph MCcan na kuzuia pasipoti yake
- IMF yaonya kuwa huenda uchumi wa dunia ukadorora zaidi
- Iran yasema imepata hasara ya takriban dola billioni 270 tangu vita kuanza
- Italia yasitisha makubaliano yake ya ulinzi na Israel
- "Shinikizo la kijeshi litachochea zaidi matatizo yaliyoanzishwa na Marekani" - Rais wa Iran
- Meli nne zinazohusiana na Iran zapita katika mlango bahari wa Hormuz
- "Kizuizi cha Marekani ni hatari na kitazidisha mvutano" - China
- Kiongozi wa Hezbollah adinda kufanya mazungumzo na Israel
- Netanyahu azungumzia mzingiro wa Mlango-Bahari wa Hormuz
- Iran yatishia kuonyesha nguvu isiyo na mfano wake dhidi ya adui
- Iran yataka mataifa ya uarabuni kuwalipa fidia ya vita vinavyoendelea mashariki ya kati
- Ujumbe wa Israel na Lebanon watarajiwa kufanya mazungumzo ya amani huko Marekani
- Iran yapendekeza kusitisha shughuli zake za nyuklia, ikiwemo urutubishaji wa urani - ripoti
- Wazazi wa Ashly Robinson watafuta majibu kuhusu kifo chake kilichotokea Zanzibar
- Kifo cha Ashly Robinson Zanzibar chazua maswali na mjadala mkubwa mitandaoni
- Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Benin kutangazwa leo Jumanne
- Trump aelezea sababu za kufuta picha inayomfananisha na Yesu katika mtandao wake
- UN yawahimiza Iran na Marekani kurejea katika meza ya mazungumzo
- Makamu wa rais wa Marekani JD Vance aishutumu Iran kwa "ugaidi wa kiuchumi"
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Beldeen Waliaula
Polisi Tanzania wamhoji Joseph MCcan na kuzuia pasipoti yake

Chanzo cha picha, Social
Idara ya polisi nchini Tanzani kupitia taarifa imesema kuwa, imezuia pasipoti ya Joseph Mccan huku wakiendelea kumhoji baada ya kuripotiwa kufariki kwa mpenziwe Ashly Jenae mwenye umri wa miaka 31.
Polisi nchini Tanzania pia wamesema wanaendelea kufanya uchunguzi wakisubiria majibu kutoka kwa madaktari cha kubaini kisa cha kifo cha mwanadada huyo raia wa Marekani.
Ashly na mpenziwe Joseph Isaac Maccann mwenye umri wa miaka 45 waliwasili kisiwani Zanzibar tarehe 4 mwezi Aprili na walikuwa na malumbano ambapo hoteli waliokuwa wakikaa ikawatengenisha na kuwapa vyumba viwili kwa ajili ya usalama wao.
IMF yaonya kuwa huenda uchumi wa dunia ukadorora zaidi

Chanzo cha picha, Getty Images
Uchumi wa dunia uko katika hatari ya kudorora iwapo vita kati ya Marekani na Iran vitaendelea, na bei ya mafuta kuendelea kupanda, shirika la fedha la kimataifa IMF limeonya.
Katika ripoti yake ya World Economic Outlook, IMF imesema iwapo bei ya mafuta na gesi zitasalia kuwa juu mwaka huu na mwaka ujao, ukuaji wa uchumi wa dunia utashuka hadi 2% mwaka huu wa 2026.
“Hii itamaanisha tutarekodi kuterereka kwa uchumi wa dunia, jambo ambalo limetokea tu mara nne tangu mwaka wa 1980” imesema IMF, ikifafanua kuwa tukio la hivi karibuni lilitokea wakati wa janga la Covid 19.
Bei ya mafuta na gesi zimepanda tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kufungwa kwa mlango bahari wa Hormuz, pamoja na mazungumzo ya amani kati ya Iran na Israel kutibuka.
IMF imesema kuwa hali inayoweza kusababisha kudorora kwa uchumi wa dunia, ni pamoja na bei ya mafuta kufikia wastani wa dola 110 kwa pipa mwaka huu na kupanda hadi dola 125 mwaka wa 2027.
IMF imesema mfumuko wa bei unaweza kufikia hadi 6% mwaka ujao. Hii inaweza kulazimisha benki kuu za mataifa kuongeza viwango vya riba ili kudhibiti kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa.
Pia unaweza kusoma:
Iran yasema imepata hasara ya takriban dola billioni 270 tangu vita kuanza

Chanzo cha picha, Getty Images
Iran imekuwa ikifanya tathmini ya gharama ya uharibifu uliosababishwa na vita kama sehemu ya juhudi zake za kujumuisha fidia katika mapendekezo ya kusitisha mapigano, shirika la habari la Tasnim limeripoti.
Akizungumza na vyombo vya habari vya Urusi, msemaji wa serikali ya Iran, Fatemeh Mohajerani, amesema makadirio ya awali na ya jumla yanaonyesha kuwa hasara waliopata imefikia takriban dola bilioni 270 kufikia sasa, lakini huenda idadi hiyo ikaongezeka.
Msemaji huyo ameongezea kuwa maafisa wa Iran wanaendelea kufanya tathmini, ambazo zinajumuisha kuangalia uharibifu wa majengo na mapato yaliyopotea kutokana na kusimamishwa kwa shughuli za viwanda na biashara zingine, hii ni kulingana na shirika la habari la Tasnim.
Mohajerani amesema kuwa suala la fidia lilikuwa miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika mazungumzo kati ya Marekani na Iran mwishoni mwa wiki iliyopita.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, hapo awali alisema kuwa walifanya “mazungumzo ya kina” lakini hawakuafikia makubaliano.
Pia unaweza kusoma:
Italia yasitisha makubaliano yake ya ulinzi na Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, amesema kuwa taifa lake limesitisha makubaliano ya kijeshi walionayo na Israel.
Makubaliano hayo ya kijeshi ya Italia na Israel yanahusisha kubadilishana silaha za kijeshi na utafiti wa pamoja.
“Kwa kuzingatia hali ya sasa, serikali imeamua kusitisha kuafikia makubaliano mapya ya ulinzi na Israel.”
Waziri huyo mkuu aliwaambia wanahabari kuwa “juhudi zote zinafaa kuwekwa” kuhakikisha mlango bahari wa Hormuz unafunguliwa.
Makubaliano kati ya Italia na Israel hurejelewa kila baada ya miaka mitano, na yamekuwepo kwa muda mrefu.
Uhusiano kati ya Israel na Italia umekua wa mshike mshike katika siku za hivi karibuni baada ya Israel kutaka balozi wa Italia nchini humo, kujibu mbona waziri wa mambo ya kigeni wa Italia Antonio Tajani alikashifu mashambulizi ya Israel nchini Lebanon kwa kusema “hayakubaliki”.
Italia nayo ilimhoji balozi wa Israel nchini humo baada ya wajumbe wa umoja wa mataifa kutoka Italia walioko nchini Lebanon kulengwa na majeshi ya Israel na kuharibu gari walilokuwa nalo na kuwajeruhi watu kadhaa.
Italia ni taifa la tatu linaloiuzia Israel silaha za kijeshi baada ya Marekani na Ujerumani.
Soma zaidi:
'Shinikizo la kijeshi litachochea zaidi matatizo yaliyoanzishwa na Marekani' - Rais wa Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Iran iko tayari kuendelea na mazungumzo ya kupata amani, na kuwa diplomasia ndiyo njia pekee ya kusuluhisha migogoro.
Pezeshkian aliyasema haya wakati akizungumza na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kulingana na vyombo vya habari vya Iran.
Inasemekana rais huyo alimuambia Macron kuwa vitisho, shinikizo na hatua za kijeshi hazisaidii na zitazidisha “matatizo yalioanzishwa na Marekani”
Pezeshkian aliongezea kuwa Ulaya inafaa kuihimiza Marekani kufuata kanuni na sheria za kimataifa.
Pia unaweza kusoma :
Meli nne zinazohusiana na Iran zapita katika mlango bahari wa Hormuz

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na data iliyochambuliwa na kitengo cha BBC Verify, meli nne za Iran, zimepita katika mlango bahari wa Hormuz, licha ya Marekani kuweka kizuizi cha kijeshi eneo hilo.
Meli mbili zilikuwa katika bandari ya Iran kulingana na shirika la ufuatiliaji la MarineTraffic. Meli kwa jina Christianna ilipita katika mlango huo wa bahari siku ya Jumatatu baada ya kizuizi hicho kuanza kutekelezwa.
Meli ya Rich Starry ambayo imewekewa vikwazo na Marekani, ili safiri kutoka eneo la Sharjah Falme za Kiarabu na kupitia mlango wa bahari wa Hormuz.
Meli ya kubeba mafuta ya Murlikishan, ambayo pia imewekewa vikwazo na Marekani kwa kuhusiana na Iran, ilisafiri kutoka eneo la Lanshan China na kupitia mlango bahari wa Hormuz majira ya usiku. Kulingana na shirika la MarineTraffic meli hiyo imeoneka katika kisiwa cha Iran cha Qeshm.
Meli nyingine ya mafuta, Elpis, ilipita katika mlango bahari wa Hormuz ikielekea eneo la mashariki siku ya Jumanne kutoka bandari ya Bushehr nchini Iran. Meli hii pia imewekewa vikwazo na Marekani.
Pia kuna uwezekano wa meli hizi kutoa taarifa potovu za kuhusu maeneo yao, ili kujificha.
Jeshi la Marekani lilisema limeanza kutekeleza kizuizi cha kijeshi siku ya Jumatatu jioni saa kumi na moja saa za Afrika Mashariki na kuzuia “meli zote zinazoingia na kutoka bandari za Iran.”
Pia unaweza kusoma :
"Kizuizi cha Marekani ni hatari na kitazidisha mvutano" - China

Chanzo cha picha, EPA-EFE/Shutterstock
Wizara ya mambo ya kigeni ya China, imelaani hatua ya Marekani kudhibiti bandari za Iran na kuita kuwa “hatari na inayokosa uwajibikaji.”
Kizuizi hicho kilianza kutekelezwa siku ya Jumatatu, baada ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani kutibuka.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa China, Guo Jiakun, ameonya kuwa kizuizi hicho “kitazidisha mvutano uliopo na kudhoofisha juhudi za kupata makubaliano ya kusitisha mapigano hayo.”
“Huu ni mwenendo hatari usiowajibika” Jiakun aliwaambia waandishi wa habari.
Jiakun ameongezea kuwa taarifa za kuwa China ilikuwa inapanga kupeleka mifumo ya ulinzi wa anga nchini Iran si za kweli.
Ripoti hizo zilifanya rais Trump kutishia kuiongezea China ushuru wa 50% kwa bidhaa zinazouzwa Marekani iwapo watatoa msaada wa kijeshi kwa Iran.
“Ikiwa Marekani itasisitiza kutumia hili kama kisingizio cha kutuwekea ushuru wa ziada, China itachukua hatua madhubuti za kujibu,” alisema Jiakun.
Mwandishi wa masuala ya diplomasia wa BBC James Landale, anasema China hupata kiwango kikubwa cha mafuta yake kutoka Iran “na ina maslahi ya kutaka kuona mzozo huu unamalizika na utulivu unarejea katika soko la kimataifa.”
Maelezo zaidi:
Kiongozi wa Hezbollah adinda kufanya mazungumzo na Israel

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Maelezo ya picha, Picha ya Naim Qassem Kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassem, amekataa mazungumzo kati ya Israel na serikali ya Lebanon, akisema hayana faida.
Kauli hiyo inakuja wakati maafisa wa serikali ya Lebanon wakijiandaa kusafiri kwenda Washington, DC Jumanne kwa mazungumzo na maafisa wa Israel na Marekani.
Serikali ya Lebanon imepiga marufuku operesheni za kijeshi za Hezbollah inayoungwa mkono na Iran, siku chache baada ya vita vyake na Israel kuanza mapema Machi.
Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, amekosoa kundi hilo, akilishutumu kwa kuingiza nchi hiyo katika vita pana vya kikanda.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim News Agency, linalohusishwa na Walinzi wa Mapinduzi wa Iran, Naim Qassem amesema kuwa “Lebanon yote” ni shabaha ya Israel, na kwamba ni wajibu wa serikali ya Lebanon “kuhamasisha jeshi.”
Pia aliuliza serikali ya Lebanon: “Mnasema mnataka usitishaji mapigano, lakini wao wana nini? Ninyi mna nini cha kuwawekea shinikizo?”
Hatimaye, Naim Qassem alisema kuwa uamuzi wa Hezbollah si kusitisha mapigano wala kujisalimisha.
Soma pia:
Netanyahu azungumzia mzingiro wa Mlango-Bahari wa Hormuz

Chanzo cha picha, Getty Images
Benjamin Netanyahu amesema Israel itaunga mkono uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuweka zuio dhidi ya Mlango-Bahari wa Hormuz wa Iran.
Netanyahu pia alisema kuwa Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alimuarifu kuhusu mazungumzo aliyofanya na Iran baada ya kuondoka Pakistan, ambayo bado hayajafikia makubaliano.
Ikumbukwe kuwa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (US Central Command) imetangaza kuwa mzingiro wa bandari za Iran katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman umeanza kutekelezwa, kwa amri ya Rais Trump.
Kwa upande mwingine, Iran imeonya kuwa meli yoyote ya kijeshi inayokaribia Mlango-Bahari wa Hormuz itachukuliwa kuwa ni uvunjaji wa mipaka ya nchi hiyo.
Soma zaidi:
Iran yatishia kuonyesha nguvu isiyo na mfano wake dhidi ya adui

Chanzo cha picha, Morteza Nikoubazl/NurPhoto via Getty Images
Walinzi wa Mapinduzi wa Iran wameonya kuwa Iran bado haijaonesha ukubwa kamili wa uwezo wake, wakisema: “Ikiwa vita vitaendelea, tutaonyesha uwezo ambao adui haaufahamu,” walisema.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, msemaji wa Walinzi wa Mapinduzi wa Iran, Hossein Mohebi, amesema kuwa Iran itatumia mbinu za kisasa za kivita ambazo adui atakuwa na uwezo mdogo sana wa kuzizuia, msemaji huyo alidai.
Soma zaidi:
Iran yataka mataifa ya uarabuni kuwalipa fidia ya vita vinavyoendelea mashariki ya kati
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amewasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akidai fidia kwa uharibifu uliosababishwa nchini Iran wakati wa vita.
Katika barua hiyo, iliyoripotiwa na shirika la habari la IRNA, Bw. Irvani alimwandikia Bw. Guterres akisema kuwa nchi hizo tano, kupitia ukiukwaji wa kimataifa, zimekiuka wajibu wao wa kimataifa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran chini ya sheria za kimataifa, na hivyo zimewajibika kisheria, na zinapaswa “kulipa fidia kamili kwa uharibifu uliosababishwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwemo malipo ya fidia kwa madhara yote ya kimali na kimaadili yaliyotokana na ukiukwaji huo wa kimataifa.”
Pia unaweza kusoma:
Ujumbe wa Israel na Lebanon watarajiwa kufanya mazungumzo ya amani huko Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Mabalozi wa Israel na Lebanon nchini Marekani wanatarajiwa kufanya mazungumzo ya nadra mjini Washington baadaye leo.
Itakuwa ni mara ya kwanza katika miongo kadhaa kwa maafisa wa nchi hizi mbili, ambazo hazina uhusiano wa kidiplomasia, kukutana ana kwa ana kwa mazungumzo ya moja kwa moja.
Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani, Marco Rubio, anatarajiwa kujiunga na mazungumzo hayo ya nadra katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Mazungumzo hayo yanafanyika siku chache tu baada ya Marekani na Iran kushindwa kufikia makubaliano ya kumaliza vita pana vya Mashariki ya Kati. 40
Mabalozi wa Lebanon na Israel wanatarajiwa kujadili uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo ya moja kwa moja ya ngazi ya juu kati ya nchi zao.
Mamlaka za Lebanon zinataka kwanza kufanikisha usitishaji mapigano katika vita vinavyoendelea kati ya Israel na kundi la Hezbollah.
Hata hivyo, Israel imekataa hilo, ikisisitiza kuwa kundi hilo linaloungwa mkono na Iran lazima livuliwe silaha. Nalo Hezbollah limekataa mazungumzo hayo na kusema halitaheshimu makubaliano yoyote yatakayofikiwa.
Mapigano ya hivi karibuni kati ya Israel na Hezbollah yamekuwa na athari kubwa kwa Lebanon.
Zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao na zaidi ya watu 2,000 wameuawa wakiwemo takriban wanawake 500, watoto na wahudumu wa afya.
Soma zaidi:
Iran yapendekeza kusitisha shughuli zake za nyuklia, ikiwemo urutubishaji wa urani - ripoti

Chanzo cha picha, Getty Images
Iran imependekeza kusitisha shughuli zake za nyuklia kwa kipindi cha hadi miaka mitano, pendekezo ambalo limekataliwa na Marekani iliyosisitiza muda wa miaka 20, kwa mujibu wa gazeti la The New York Times likinukuu maafisa waandamizi wa Iran na Marekani.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa Marekani na Iran zilikuwa zikibadilishana mapendekezo kuhusu kusitisha shughuli za nyuklia za Tehran wakati wa mazungumzo yaliyofanyika Pakistan, lakini bado zilikuwa mbali kufikia makubaliano.
Hata hivyo, majadiliano hayo yanaashiria kuwa huenda bado kuna njia ya kufikia makubaliano ya amani, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kufanyika kwa duru ya pili ya mazungumzo ya ana kwa ana.
BBC imewasiliana na Ikulu ya Marekani (White House) kuomba maoni.
Mipango ya nyuklia ya Iran imekuwa kikwazo kikubwa katika mgogoro huo, huku Donald Trump akisisitiza tena Jumapili kuwa Marekani itahakikisha Iran haimiliki silaha za nyuklia.
Soma zaidi:
Polisi Tanzania wamhoji mpenziwe Ashly na kuzuia pasipoti yake

Chanzo cha picha, social
Maelezo ya picha, Picha ya mwanamitindo Ashly Robinson Idara ya polisi nchini Tanzani kupitia taarifa imesema kuwa, imezuia pasipoti ya Joseph Mccan huku wakiendelea kumhoji baada ya kuripotiwa kufariki kwa mpenziwe Ashly Jenae mwenye umri wa miaka 31.
Polisi nchini Tanzania pia wamesema wanaendelea kufanya uchunguzi wakisubiria majibu kutoka kwa madaktari cha kubaini kisa cha kifo cha mwanadada huyo raia wa Marekani.
Ashly na mpenziwe Joseph Isaac Maccann mwenye umri wa miaka 45 waliwasili kisiwani Zanzibar tarehe 4 mwezi Aprili na walikuwa na malumbano ambapo hoteli waliokuwa wakikaa ikawatengenisha na kuwapa vyumba viwili kwa ajili ya usalama wao.
Katika mahojiano yao ya kwanza na chombo cha habari cha kitaifa, wazazi wa Ashly Robinson, mshawishi wa mitindo ya maisha wa Marekani mwenye umri wa miaka 31 aliyefariki chini ya mazingira yasiyoeleweka akiwa likizoni Zanzibar pamoja na mchumba wake, wanajaribu kufahamu kilichompata binti yao aliyekuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa na uchumba wake.
“Alipaswa kuwa na furaha,” mama yake, Yolanda Endres, aliiambia CBS News kupitia @iamthatreporterjd. “Kisha ghafla akawa hayupo.”
Endres pamoja na baba wa Robinson, Harry Robinson, walisema walipokea taarifa mara moja tu kutoka kwa mchumba wa binti yao, Joe McCann, saa 11 baada ya tukio linalodaiwa kusababisha kifo chake. Baadaye walifahamishwa na hoteli waliokuwa wamekodisha kwamba Ashly alikuwa amefariki.
CBS News imewasiliana na kampuni ya McCann, Asymmetric, kuomba maoni, lakini haikupata majibu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha kwa CBS News kuwa raia wa Marekani amefariki Zanzibar, lakini haikutoa maelezo zaidi kwa sababu za faragha.
Kifo cha Ashly Robinson Zanzibar chazua maswali na mjadala mkubwa mitandaoni

Chanzo cha picha, Ashly Jenae/Ig
Maelezo ya picha, Picha ya pamoja ya Ashly na mchumba wake Joe wakijivinjari Zanzibar saa chache kabla ya tukio Polisi Zanzibar wanasema kuwa mwanamitindo anayeishi Marekani, Ashly Robinson maarufu kama Ashlee Jenae, alifariki kwa kujitoa uhai alipokuwa likizoni kisiwani humo pamoja na mchumba wake, Joe McCann.
Kisa hicho kimevutia umakini mkubwa kwenye mitandao ya kijamii katika siku tatu zilizopita, huku mamlaka zikisema zinasubiri matokeo ya uchunguzi wa maiti.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Benedict Mapujira, aliiambia BBC siku ya Jumatatu kuwa tukio hilo lilitokea Jumatano, Aprili 8, ambapo mwanamke huyo anadaiwa kujinyonga kwa kutumia kipande cha kitambaa.
Mapujira alisema wawili hao waliripotiwa kutoelewana, hali iliyosababisha uongozi wa hoteli kuwatenganisha na kuwapatia vyumba tofauti.
Alisema: “Mwanamke huyo alikuwa na mchumba wake, McCann, na walikuwa kisiwani kwa mapumziko... tunaambiwa walikuwa mzozano, na hoteli iliwapatia makazi tofauti; mwanamke alikuwa na chumba chake, na mwanaume pia alikuwa na chumba chake.”
Polisi walisema tukio hilo liliripotiwa usiku katika kituo cha polisi cha karibu baada ya wafanyakazi wa hoteli kutoa taarifa kwamba kulikuwa na mgeni aliyeshukiwa kuwa katika hatari ya kujitoa uhai.
“Ashly alipelekwa hospitalini usiku huo kwa matibabu, lakini alifariki siku iliyofuata (Aprili 9),” polisi waliiambia BBC, wakiongeza kuwa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kwa mujibu wa mamlaka, mwili wake bado uko Zanzibar ukisubiri uchunguzi zaidi kabla ya taratibu za kuusafirisha kurejeshwa nyumbani kufanyika.
Kwa mujibu wa taarifa zinazosambaa mitandaoni, mshauri huyo alisafiri kwenda Tanzania kusherehekea siku yake ya kuzaliwa Aprili 5, na alichapisha picha katika ukurasa wake wa Instagram siku hiyo, zikiwa zimepigwa katika hifadhi ya wanyama iliyoko mkoa wa Kilimanjaro.
Ujumbe kwenye akaunti ya Instagram ya Ashly umechanganya salamu za rambirambi pamoja na wito wa haki.
Kwa mujibu wa vyanzo, wakati wa safari hiyo, McCann pia alimshangaza kwa kumvisha pete ya uchumba, tukio lililoelezwa baadaye na familia yake kuwa la kukumbukwa.
Taarifa ya pamoja inayodaiwa kutoka kwa familia za Robinson na Endres, na kusambazwa sana mtandaoni, ilisomeka: “Wakati mmoja alikuwa akisherehekea upendo na maisha kwa namna yake ya kipekee, na muda mfupi baadaye, akawa hayupo tena.”
Familia hizo zinasema zinaendelea kushirikiana na mamlaka za Zanzibar huku uchunguzi ukiendelea.
Katika mitandao ya kijamii kama X na Instagram, tukio hilo limeibua mjadala mkubwa, huku baadhi ya watumiaji wakitaka uchunguzi wa kina kuhusu kifo chake.
Wazazi wa Ashly wameripotiwa kuwa wanasafiri kuelekea Zanzibar kutathmini hali.
Soma zaidi:
Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Benin kutangazwa leo

Chanzo cha picha, Getty Images
Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais nchini Benin yanaonesha waziri wa Fedha, Romuald Wadagni ameshinda kwa asilimia 94 ya kura.
Mgombea pekee wa upinzani katika uchaguzi huo Paul Hounkpe ametangaza amekubali kushindwa.
Ushindi wa Bwana Wadagni ambaye alichaguliwa na Rais anayeondoka madarakani Patrice Talon kuwa mrithi wake ulitarajiwa baada ya chama kikuu cha upinzani kushindwa kupata wabunge wa kutosha kuidhinisha mgombea wao wa urais.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo mkuu uliofanyika Jumapili yanatarajiwa kutangazwa leo Jumanne na Tume ya Uchaguzi.
Soma zaidi:
Trump aelezea sababu za kufuta picha inayomfananisha na Yesu katika mtandao wake

Chanzo cha picha, AFP Via Getty
Rais wa Marekani Donald Trump amefuta picha aliyokuwa ameichapisha katika mtandao wake wa kijamii inayomfananisha na Yesu baada ya viongozi wa kidini kumkosoa vikali na kuitaja dhihaka na kukufuru.
Rais Trump anasema alidhani Picha hiyo aliyotengeza kwa kutumia akili mnemba inamuonesha kama Daktari na sio Yesu.
Hayo yanakuja baada ya Kiongozi huyo wa Marekani kujibizana vikali na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Leo kuhusu vita vya Mashariki ya Kati.
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema Makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatican yanapaswa kujikita katika masuala ya kimaadili na kumuacha Rais Trump kujikita katika masuala ya Sera za Kisiasa.
Pia unaweza kusoma:
UN yawahimiza Iran na Marekani kurejea katika meza ya mazungumzo

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, António Guterres pia alisema ana wasiwasi mkubwa kuhusu "ukiukwaji wa wazi wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu" huko Gaza. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametoa wito wa kuanza tena kwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran, akieleza matumaini kuwa hatua hiyo itasaidia kumaliza vita.
Alisisitiza kuwa ni “dhahiri kabisa” kwamba “hakuna suluhisho la kijeshi kwa vita hii.”
Bw. Guterres pia alisema kuwa usitishaji mapigano “lazima udumishwe kikamilifu” na kwamba “ukiukwaji wote lazima ukome,” akiongeza: “Natoa wito wa kurejea kwa mazungumzo ili kufikia makubaliano.”
Aidha, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alizitaka nchi zote “kuheshimu uhuru wa usafiri wa majini, ikiwemo katika Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa sheria za kimataifa.”
Pia unaweza kusoma :
Makamu wa rais wa Marekani JD Vance aishutumu Iran kwa "ugaidi wa kiuchumi"

Chanzo cha picha, Getty Images
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance,ameishutumu serikali ya Iran kwa kujihusisha na “kitendo cha ugaidi wa kiuchumi” kwa kuzuia usafiri kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Vance amemwambia Brett Baier wa Fox News kuwa Rais Donald Trump ameonyesha kwamba “wote wawili wanaweza kucheza mchezo huo”.
Anasema ikiwa Wairani “watajihusisha na ugaidi wa kiuchumi”, basi Marekani itazingatia kanuni kwamba “hakuna meli za Iran zitakazoruhusiwa kutoka katika mlango bahari wa Hormuz”.
Vance pia amezungumzia mazungumzo na Iran yaliyofanyika mwishoni mwa wiki, akisema kuwa maendeleo makubwa yamepatikana.
“Mpira uko upande wa Iran,” amesema.
Makamu huyo wa rais wa Marekani pia ametaja kuwa Iran inapaswa kuwa tayari kubadilika na kukubali “mambo muhimu” yanayodaiwa na Marekani, udhibiti wa Marekani juu ya urani Iliyorutubishwa Iran, pamoja na utaratibu wa uthibitishaji ili kuhakikisha kuwa haijatengeneza silaha ya nyuklia.
Pia unaweza kusoma :
