Jinsi China inavyocheza kati ya Iran na nchi za Ghuba

Chanzo cha picha, Getty Images
China inajaribu kusawazisha kwa umakini uhusiano wake kati ya Iran na nchi za Ghuba, huku Bahrain pamoja na nchi nyingine za Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) zikisukuma hatua zaidi kupitia Umoja wa Mataifa ili kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz.
Licha ya Beijing kupinga katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa matumizi ya nguvu kulinda njia za usafirishaji, China pia imeweka wazi kuwa haiungi mkono mashambulizi ya Iran dhidi ya nchi za Ghuba. Hii ni mara ya pili kwa China kutumia lugha hiyo kupinga maazimio yanayohusiana na Ghuba.
Tangu vita kuanza, mawasiliano ya wazi ya Beijing na Iran yamekuwa hafifu ikilinganishwa na uhusiano wake na nchi za Ghuba kama Saudi Arabia na Falme za Kiarabu.
Wachambuzi wanaamini China haitakuwa tayari kuiunga mkono Tehran ikiwa itahatarisha uhusiano wake na nchi za Kiarabu, hasa kwa kuwa mahusiano yake ya kiuchumi na nchi za GCC ni makubwa zaidi kuliko yale iliyonayo na Iran.
Msimamo wa China kuhusu matumizi ya nguvu katika Mlango wa Hormuz ni upi?
China imepinga juhudi za Bahrain, Rais wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuendeleza azimio litakaloruhusu nchi wanachama kutumia "njia zote zinazohitajika" kulinda usafiri wa kibiashara katika Mlango wa Hormuz.
Vyombo vya habari kama vile Guncha viliripoti Aprili tarehe 3 kuwa rasimu hiyo, iliyoungwa mkono na Marekani na nchi za Kiarabu za Ghuba, ilipingwa na China, Urusi na Ufaransa, ambazo zilipinga wazi lugha inayoruhusu matumizi ya nguvu.
Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Fu Kong, alisema hatua hiyo ingehalalisha matumizi mabaya ya nguvu na kuongeza mvutano.
Katika mazungumzo ya simu na waziri wa mambo ya nje wa Bahrain, Abdul Latif bin Rashid Al Zayani mwezi Machi tarehe 2, China pia ilipendekeza mpango wa pamoja wa pointi tano pamoja na Pakistan, ukisisitiza kulindwa kwa usalama wa mlango huo na kurejeshwa kwa usafiri wa kawaida wa meli.
Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi alisisitiza kuwa hatua za Baraza la Usalama zinapaswa kupunguza mvutano, kusitisha vita na kurejesha mazungumzo, badala ya kuhalalisha vita au kuongeza hali mbaya.
China imesema nini kuhusu mashambulizi dhidi ya nchi za Ghuba?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
China imeeleza wazi kupinga mashambulizi ya Iran dhidi ya nchi za GCC.
Fu Kong aliambia Baraza la Usalama kuwa China Aprili ya tarehe 2 "haiungi mkono mashambulizi ya Iran dhidi ya nchi za Ghuba."
Hata hivyo, China pia ilikataa kuunga mkono azimio la kulaani Iran, ikisema halikuwasilisha kwa usawa chanzo na picha kamili ya mzozo huo.
Aidha, China ilieleza kuwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran ndiyo chanzo cha vita, na kuyaita ukiukaji wa wazi wa mkataba wa Umoja wa Mataifa. Ilitoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi hayo kama suluhisho la msingi.
Katika hotuba yake tarehe 2 Aprili, Fu Kong alitaja mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kuwa "chimbuko" la vita, ambayo alisema ni "ukiukaji wa wazi" wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na akataka kusitishwa kwa vitendo vyao vya kijeshi kama "suluhisho la msingi" ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.
China ilijieleza kama "rafiki na mshirika mzuri" wa nchi za GCC, ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka, usalama na mipaka yao, huku ikilaani mashambulizi dhidi ya raia na kulinda usalama wa njia za usafirishaji.
Mahusiano ya kisiasa ya China yakoje kuhusu vita vya Iran?
Beijing imekuwa makini katika juhudi zake za kidiplomasia kuelekea Tehran.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China iliepuka kutoa majibu ya moja kwa moja kuhusu mazungumzo na Iran, ikisema tu kuwa mpango uliopendekezwa ni wa wazi kwa pande zote.
Kwa mujibu wa takwimu ziliozokusanywa na BBC Monitoring, China imekuwa na mawasiliano kidogo ya wazi na Iran ikilinganishwa na nchi za Ghuba kama Bahrain, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu.
Wang Yi alizungumza kwa simu mara mbili na mwenzake wa Iran Abbas Araghchi, huku mwakilishi maalum wa China Mashariki ya Kati, Zhai Jun, akikutana na balozi wa Iran mjini Beijing.
Katika mawasiliano ya hivi karibuni, China imehimiza mazungumzo badala ya vita, ikisema kuwa amani ni bora kwa Iran na wananchi wake.
Kinyume chake, alisema katika wito wa Machi 2 kwamba China inathamini "urafiki wake wa jadi" na Iran na inaunga mkono Tehran katika kudumisha mamlaka yake, usalama, uadilifu wa eneo na heshima ya kitaifa.
Ni mambo gani ya kisiasa na kiuchumi yanayoiongoza China?
Mchambuzi Deng Yuwen amesema kuwa kutokana na masuala ya usalama wa Ghuba, nishati, njia za usafirishaji, na uhusiano na nchi za Kiarabu, China haitaiunga mkono Iran ikiwa itasababisha kuyumba kwa Mashariki ya Kati.
Katika matamshi yaliyochapishwa na Shirika la Habari la Taiwan, Deng Yuwen alitaja maneno ya Zhai Jun, ambayo yalielezea msimamo wa China kuwa "kusaidia wale ambao wana busara, sio wale walio karibu na wewe," na kuona kuwa ni ishara ya Beijing kujitenga na mshirika wake wa karibu, Tehran.
Biashara kati ya China na nchi za GCC inakadiriwa kuzidi dola bilioni 288 mwaka 2024, wakati uwekezaji wa China nchini Iran umekuwa chini ya dola bilioni 5 tangu 2007.
Hata hivyo, gazeti la kibinafsi la Hong Kong la South China Morning Post lilitaja wachambuzi wakisema kwamba mbinu ya China ya kuepuka vita ni chanya. Walisema sera hiyo inaweza kuiruhusu Beijing kuinua uhusiano wake wa karibu na Iran na kurahisisha upitishaji wa shehena zaidi kwenye Mlango wa bahari wa Hormuz.
Kwa kuongezea, vita vinavyoendelea vinaweza kuifanya Marekani kubaki Mashariki ya Kati na kupunguza umakini wake katika maeneo kama Mlango wa Taiwan na Bahari ya China Kusini.
Wachambuzi pia wanatabiri kwamba nguvu laini ya China itaimarishwa zaidi kwa "kutegemea ushawishi badala ya kulazimishwa," hasa kwa kulinganisha na sera za Donald Trump, ambazo wanasema "zimepunguza imani ya kimataifa kwa Washington na kucheza mikononi mwa China."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












