Kizuizi cha kijeshi ni nini na kitafanyaje kazi katika Mlango-Bahari wa Hormuz?

l

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump
    • Author, George Wrightand & Rachel Clun
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Jeshi la Marekani limesema litaanza kutekeleza amri ya kuzuia shughuli zote za baharini kwa meli zinazoingia na kutoka katika bandari za Iran siku ya Jumatatu.

Meli zinazoingia au kutoka nchi zingine zitaruhusiwa kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya maji ambayo Iran iliifunga kutokana na mashambulizi ya Marekani na Israel.

Hii inakuja baada ya wapatanishi kutoka pande zote mbili kushindwa kufikia makubaliano ya kusitisha vita, vilivyoanza tarehe 28 Februari.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema mazungumzo ya moja kwa moja na Iran nchini Pakistan yalishindwa kwa sababu Iran "haikuwa tayari kuachana na mpango wake wa nyuklia."

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran alisema Marekani ilitoa "matakwa mengi mno na maombi yasiyo halali.”

Trump anataka kuzuia nini?

Katika chapisho lake kwenye Truth Social siku ya Jumapili, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Marekani itaanza "kuzuia meli zote zinazoingia au kutoka, kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.”

"Pia nimewaagiza Wanamaji wetu kutafuta na kuizuia kila meli katika Maji ya Kimataifa ambayo imelipa ushuru kwa Iran. Hakuna mtu anayelipa ushuru haramu atakayepitia salama baharini," Trump alisema.

Aliongeza Marekani pia itaanza kuharibu mabomu aliyosema Iran imeyaweka kwenye eneo hilo la Mlango.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Mwirani yeyote atakayetufyatulia risasi, au kufyatulia meli zingine, atapelekwa jehanamu!" aliendelea.

Aliongeza katika chapisho jingine kwamba "Iran iliahidi kuufungua Mlango-Bahari wa Hormuz, na kwa makusudi wameshindwa kufanya hivyo."

Kitabu cha mwongozo cha mwaka 2022 cha Kamandi ya Jeshi la Wanamaji la Marekani kuhusu sheria juu ya operesheni za majini kinafafanua kizuizi kama "operesheni ya kuzuia meli au ndege za Mataifa yote, adui na wasioegemea upande wowote, kuingia au kutoka bandari, viwanja vya ndege, au maeneo ya pwani yaliyoainishwa ambayo yanamilikiwa, au yanayokaliwa, au yako chini ya udhibiti wa Nchi adui."

Katika chapisho kupitia X, Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) imesema vikosi vyake vitaanza kutekeleza agizo la Trump siku ya Jumatatu.

"Kizuizi hicho kitatekelezwa bila upendeleo dhidi ya meli za mataifa yote - zinazoingia au kutoka bandari za Iran na maeneo ya pwani, ikiwa ni pamoja na bandari zote za Iran kwenye Ghuba ya Uarabuni na Ghuba ya Oman.”

Centcom iliongeza kuwa vikosi vya Marekani havitazuia vyombo vya usafiri vinavyoingia na kutoka bandari zisizo za Iran, na taarifa za ziada zitatolewa kwa mabaharia kupitia taarifa rasmi kabla ya kizuizi kuanza.

Trump alisema nchi zingine zitahusika katika kutekeleza mpango huo, lakini hakusema ni zipi. BBC inaelewa kwamba Uingereza haitahusika katika mpango huo.

Trump pia aliiambia Fox News kwamba Nato imejitolea kusaidia "kuisafisha" njia hiyo, na kuongeza kuwa itakuwa tayari kutumika tena.

Trump alisema Marekani itapeleka wategua mabomu, na Uingereza - mwanachama wa Nato - pia itapeleka.

"Naelewa Uingereza na nchi zingine kadhaa zitatuma wategua mabomu," alisema.

Waziri Mkuu Keir Starmer amesema mifumo ya kijeshi ya uteguaji mabomu ya Uingereza tayari iko katika eneo hilo.

Msemaji wa Serikali ya Uingereza alisema: "Tunaendelea kuunga mkono uhuru wa safari za baharini na kuufungua Mlango-Bahari wa Hormuz, ili kusaidia uchumi wa dunia na kupunguza gharama ya maisha nyumbani."

"Tunafanya kazi kwa haraka na Ufaransa na washirika wengine ili kuunda muungano mpana wa kulinda safari za mlango huo.”

Wataalamu watatu wa sheria nchini Marekani wameiambia BBC kizuizi kinaweza kukiuka sheria za baharini. Mmoja pia alihoji ikiwa kizuizi hicho, ambacho kinatekelezwa kijeshi, kitakiuka makubaliano ya sasa ya kusitisha mapigano au la.

Mpango wa Marekani umekaaje?

Jiografia ya mlangobahari huo inairuhusu Iran kuutumia kama mtaji wakati wa vita, kwa kuzuia vyombo vya majini kupita kwenye njia nyembamba ya maji na kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Tehran imekuwa ikitoza kiasi kikubwa cha pesa kwa baadhi ya vyombo vya majini ili kupita.

Kwa kufunga mlango-bahari, Trump ataweza kukata chanzo kikubwa cha mapato kwa serikali ya Iran - ingawa hilo linaweza kusababisha kupanda zaidi kwa bei ya mafuta na gesi.

Aliiambia Fox News "hatutaiacha Iran ipate pesa kwa kuuza mafuta kwa watu inaowapenda na kutouza kwa watu isiowapenda," na kusema lengo ni kuruhusu "wote” wapite kwenye njia hiyo.

Wachambuzi wamependekeza kwamba kauli ya rais wa Marekani inalenga kuiwekea Iran shinikizo ili kufikia makubaliano kwa masharti ya Marekani.

Katika kipindi cha CBS cha Face the Nation, mbunge wa chama cha Republican Mike Turner wa Ohio alisema kizuizi hicho ni njia ya kulazimisha kupatikana kwa suluhisho.

Lakini Seneta Mark Warner wa Virginia, kutoka chama cha Democratc ambaye yupo katika Kamati ya Ujasusi ya Seneti, aliiambia CNN Jumapili: "Sielewi kuziba mlango-bahari huo kutakavyowasukuma Wairani kuufungua."

Mtaalamu wa meli Lars Jensen ameiambia BBC, agizo la Trump la kuziba mlango bahari huo litaathiri tu vyombo vichache ambavyo bado vinaendelea na safari zake za majini.

"Ikiwa hili litafanywa na Marekani, litazuia meli chache sana. Kwa ujumla, halibadilishi chochote," anasema.

Jensen, mtendaji mkuu wa Vespucci Maritime, anasema agizo la Trump la kuzuia meli zote zinazolipa ushuru kwa Iran pia halitakuwa na athari kubwa kwani meli zinazofanya hivyo tayari ziko chini ya vikwazo.

"Kwanza kabisa, kuna meli chache sana zinazopita. Na zile zinazolipa ushuru ni chache zaidi, na zile zinazolipa ushuru tayari ziko chini ya vikwazo vya Marekani," anasema.

Makampuni mengi ya usafirishaji yataendelea kusubiri ili kuona kama kuna makubaliano ya amani au makubaliano yatadumu, Jensen anasema, na ikiwa hilo litatokea, ongezeko la polepole la usafirishaji linaweza kuanza tena.

Hali ikoje kwa sasa?

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Idadi ndogo ya meli zimepitia tangu kusitishwa mapigano

Usitishaji mapigano wa wiki mbili katika vita vya Marekani na Israeli na Iran ulikubaliwa tarehe 7 Aprili, na ulijumuisha sharti kwamba safari kupitia njia nyembamba ya maji ziendelee.

Hata hivyo, meli katika eneo hilo zilipokea ujumbe kwamba "zitashambuliwa na kuharibiwa" ikiwa zitavuta mlango-bahari bila ruhusa, na ni meli chache tu zilizofanya safari katika siku tatu za kwanza baada ya kutangazwa kusitishwa mapigano.

Kufikia Aprili 10, meli 19 pekee ndizo zilipita kwenye mlango bahari tangu kusitishwa mapigano, kulingana na BBC Verify kwa kutumia data kutoka MarineTraffic.

Kati ya hizi, nne zilikuwa ni meli zilizobeba mafuta, gesi au kemikali. Zilizosalia zimeorodheshwa kama meli za kubeba mizigo au meli za makontena za aina mbalimbali.

Meli zingine zimesafiri kwa kuzima GPS zao.

Kwa wastani meli 138 zilikuwa zinapita kwenye mlango bahari huo kila siku kabla ya mzozo kuanza tarehe 28 Februari.