Akili Mnemba (AI) yatikisa Ajira: Kazi gani ziko Hatarini?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kampuni zinazojihusisha na nyanja ya akili mnemba (AI) hutoa madai mapana kuhusu uwezo wa zana zao kuchukua nafasi ya nguvu kazi ya binadamu.

Baadhi ya kazi zitaendeshwa kikamilifu na mifumo ya kiotomatiki, huku nyingine zikibadilishwa na kuboreshwa kwa kutumia akili mnemba.

Viongozi wa makampuni makubwa zaidi duniani wanawekeza mabilioni ya dola katika teknolojia hizi, huku wakijua kuwa matumizi ya zana hizo yanaweza kupunguza gharama za nguvu kazi.

Siku hizi, watendaji wa makampuni wanaambiwa kuwa "kudumisha idadi ileile ya wafanyakazi ni ishara ya mafanikio na tija," wakati huohuo wawekezaji wakihoji iwapo kazi zinapaswa kukabidhiwa kwa wafanyakazi wapya au kwa "mawakala wa akili mnemba" wafanyakazi wa kidijitali walioajiriwa kufanya kazi mahususi, ambapo baadhi yao wana uwezo hata wa kufanya kazi zinazohitaji utaalamu maalum.

Ikiwa hata nusu ya madai haya ni ya kweli, athari zake zitahisiwa na sisi sote, katika sekta mbalimbali za uchumi na katika taaluma zetu. Mabadiliko haya yanaweza kutokea mapema zaidi kuliko tunavyodhani.

Wanauchumi waliotunukiwa Tuzo ya Nobel hivi karibuni walionya kuwa dunia lazima "ichukue hatua sasa" ili kuhakikisha kuwa akili mnemba inaleta ustawi na kuboresha viwango vya maisha, badala ya kusababisha upotevu mkubwa wa ajira.

Mwezi uliopita, wafanyabiashara jijini London walionya kuwa wanapata changamoto kupata ujuzi wanaohitaji huku akili mnemba ikileta mabadiliko makubwa katika soko la ajira.

Bado tuko katika hatua za mapema, lakini takwimu tayari zinaonyesha mwelekeo fulani wa kuvutia. Takwimu hizo zinaonyesha jinsi mifumo mbalimbali ya akili mnemba inavyoweza kufanya kazi ambazo hapo awali zilifanywa na binadamu.

Kulingana na kipimo hiki, miaka mitatu tu iliyopita, mifumo mikubwa ya lugha (LLMs) iliweza tu kufanya kwa ufanisi kazi ambazo zingemchukua binadamu sekunde chache au dakika chache kukamilisha. Sasa, mifumo hii inazidi kuwa na uwezo wa kufanya kazi ngumu zaidi zinazochukua takriban saa moja.

Baadhi ya mifumo mikubwa ya lugha sasa ina uwezo hata wa kubaini matatizo katika mikataba ya sarafu za kidijitali, na kuunda au kuboresha mfumo huo wenyewe, kazi ambazo zingemchukua binadamu saa kadhaa kukamilisha.

Ajira zinazotikiswa na AI

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kizazi kipya cha mifumo hii kinatarajiwa kuweza kujifanyia sehemu kubwa ya kazi zake za uundaji na uendelezaji bila kutegemea msaada wa nje, ndani ya mwaka mmoja hivi ujao.

Hali hii inaonekana wazi kwa sasa katika nyanja ya uandishi wa programu na uundaji wa mifumo ya kompyuta, ingawa mwelekeo kama huo bado uko katika hatua za awali, unaonekana pia katika nyanja nyingine kama vile uchanganuzi wa kifedha, kazi za awali za kisheria, na hata baadhi ya kazi za kwanza katika sekta za ubunifu.

Utafiti wa kina zaidi kufikia sasa unatoka Marekani, ukitumia data ya miaka minne kuhusu hali ya ajira ya makundi mbalimbali ya umri katika kazi zenye kiwango cha juu na cha chini cha kuathiriwa na Akili Bandia (AI).

Kazi hizi zinajumuisha kuanzia watengenezaji wa programu na wafanyakazi wa vituo vya huduma kwa wateja hadi wahudumu wa afya, walezi wa watoto na vinyozi.

Uchambuzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Stanford kuhusu data za mishahara na ajira unaonyesha kuwa tangu kuibuka kwa chatbots (programu za mazungumzo ya kiotomatiki), ajira kwa vijana wenye umri wa miaka 22 hadi 25 imeshuka kwa asilimia 2.7. Kushuka huko kunafikia asilimia 12.8 katika sekta zilizoathirika zaidi na AI, zikiwemo sekta ya fedha, utengenezaji wa programu, na viwanda vya ubunifu.

Bila shaka, si wachumi wote wanaokubaliana na hitimisho hili. Baadhi wanaamini kuwa mambo mengine, ikiwemo kupanda kwa viwango vya riba na hali ya jumla ya uchumi, yanaweza pia kuelezea mabadiliko haya katika soko la ajira.

Matangazo ya kazi mtandaoni pia yameathiriwa na ChatGPT pamoja na mifumo mingine mikubwa ya lugha (LLMs).

Bila shaka, kuna mambo mengine mengi yanayochangia hali hii, kuanzia viwango vya riba hadi sera za kodi.

Hata hivyo, mojawapo ya matokeo ya kushangaza katika uchambuzi wa hivi karibuni uliofanywa na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) ni tofauti iliyopo kati ya idadi ya matangazo ya kazi katika sekta zilizoathirika zaidi na AI na zile zilizoathirika kidogo.

Katika utafiti huo, kazi kama vile uuzaji wa bidhaa kwa njia ya simu, na huduma za kisheria zilikuwa miongoni mwa sekta zilizoathirika zaidi na AI, huku maeneo kama vile ujenzi, huduma za usafi na uandaaji wa chakula yakiwa miongoni mwa yale yaliyoathirika kidogo.

Uingereza imeshuhudia kushuka kwa kiasi kikubwa kwa kiashirio hiki, wakati ambapo viwango vya riba vimebaki vilevile au kushuka, na mwenendo huu ulianza pia kabla ya gharama kupanda mwaka jana.

Kulingana na viashirio vingi vya kimataifa, utegemezi mkubwa wa uchumi wa Uingereza kwa sekta ya huduma unaifanya nchi hiyo kuwa katika hatari zaidi ya kupoteza ajira kutokana na kuenea kwa Akili Mnemba.

Kampuni zatafuta kupunguza gharama

Matumizi ya AI hupimwa kwa kipimo kinachoitwa "token."

Tokens ni vipande vidogo vya maandishi ambavyo mifumo ya AI hutumia kuelewa, kuchambua, na kuzalisha lugha. Kwa wastani, kila *token* ni takriban robo tatu ya neno la Kiingereza.

Kampuni kubwa zaidi duniani zinazotumia akili mnemba (AI) zimeanzisha hata "orodha za viongozi wa matumizi ya *token*" ili kuwahamasisha wafanyakazi wao kufikia viwango vya juu zaidi vya tija kwa kutumia mifumo ya kisasa zaidi.

Katika miezi michache iliyopita, matumizi ya token yamefikia trilioni, na wakati mwingine makumi ya trilioni au hata *quadrillion, hasa kupitia matumizi ya "mawakala wa AI", mifumo inayoweza kutekeleza kazi mbalimbali bila kuingiliwa na binadamu.

Hata hivyo, kumekuwa na changamoto, gharama ya kutumia teknolojia hizi imeongezeka kwa kiasi kikubwa, kiasi kwamba kampuni nyingi sasa zinalazimika kudhibiti na kupunguza matumizi ya mifumo hiyo.

Jambo hili ni muhimu kwa sababu linaweza kuashiria kuwa kuna mipaka katika uwezo wa kutumia mifumo ya kujiendesha yenyewe.

Katika baadhi ya matukio, "wafanyakazi wa kidijitali" wanaweza kuwa na gharama kubwa zaidi kuliko wafanyakazi wa kibinadamu, kulingana na aina ya kazi inayofanyika.

Hata hivyo, kuna jambo lingine muhimu la kuzingatia, kampuni nyingi, zikiwemo zile za nchi za Magharibi, zimeanza kutumia mifumo ya AI ya gharama nafuu zaidi, mifumo iliyojengwa kwa teknolojia zilizotengenezwa nchini China na kuwekwa sokoni bure au kwa gharama nafuu sana.

Kwa hivyo, bado kuna kutokuwa na uhakika mwingi kuhusu athari za AI kwenye soko la ajira, lakini tayari kuna mwelekeo unaojitokeza.