Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gachagua apata pigo huku Mahakama Kuu ikitupilia mbali ombi la kupinga kuondolewa kwake madarakani
Aliyekuwa Naibu Rais nchini Kenya Rigathi Gachagua amepata pigo baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi aliyowasilisha na kutoa uamuzi kuwa Bunge lilichukua hatua kulingana na Katiba ya nchi kumuondoa madarakani.
Uamuzi huo uliotolewa na majaji watatu, ulitupilia mbali ombi la Gachagua la kupinga kuondolewa kwake madarakani, na kusema kuwa Bunge la Taifa pamoja na Seneti walifuata sheria na kwamba walimpa fursa ya kujitetea kutokana na hoja zilizowasilishwa dhidi yake.
Majaji hao pia walisema kwamba ushirikishi wa umma uliofanywa kabla ya Gachagua kuondolewa madarakani kulizingatia Katiba na kwamba Bunge lilikuwa na haki ya kutekeleza jukumu lake la kusimamia, kufuatilia na kutathmini maafisa wa serikali.
Uamuzi huo umetolewa katika moja ya kesi za kihistoria ya kisiasa nchini Kenya na kuthibitisha kuwa Gachagua aliondolewa afisini kihalali.
Katika uamuzi wa awali, mahakama ilisema kwamba hakukuwa na ushahidi ulioonyesha kuwa kulikuwa na upendeleo, maamuzi yaliyopangwa mapema au mgongano wa kimaslahi katika mchakato wa kumtimua madarakani Rigathi Gachagua.
Akitoa uamuzi huo kwa niaba ya jopo la majaji watatu, Jaji Eric Ogola ameshikilia kuwa ushiriki wa kisiasa na maoni ya wabunge peke yake, hakuwezi kuthibitisha kuwa ni upendeleo wa kikatiba.
"Ukweli kwamba Wabunge waliunga mkono au kupinga kuondolewa madarakano kwa Mheshimiwa Gachagua hakuwezi, kujisimamia, kuthibitisha kuwa ni upendeleo wa kikatiba," mahakama ilisema.
Jaji alisisitiza kuwa kuondolewa madarakani ni mchakato wa kawaida wa kisiasa na kikatiba ambapo wabunge hawatarajiwi kuangazia hoja iliyowasilishwa mbele yao bila kufahamu suala husika au maoni ya kisiasa.
Kinachotakiwa kwa mujibu wa Katiba, mahakama ilisema, si kukosekana kwa mielekeo ya kisiasa bali kuwepo kwa ushirikiano wa nia njema na ushahidi na hoja wakati wa mchakato.
"Kile ambacho Katiba inahitaji ni uwepo wa uwazi wakati wa kusikiliza ushahidi, kusikiliza hoja, na kutekeleza wajibu wao wa kikatiba kwa uaminifu na ndani ya mipaka ya kikatiba", hakimu amesema.
Kwa msingi huo, mahakama ilikataa madai ya mlalamikaji kwamba wabunge walikuwa wamefanya maamuzi mapema au walishawishiwa na mgongano wa maslahi, na kusema kuwa madai hayo hayakuwa na ushahidi wa kutosha.
"Hivyo basi, madai ya upendeleo, kwamba kulikuwa na uamuzi uliofanywa mapema, na mgongano wa kimaslahi yaliyowasilishwa na mlalamishi dhidi ya Maspika, Wabunge na Maseneta, kulingana na nyaraka mbele ya Mahakama hii, ni madai yasiyo na uthibitisho yaliyoegemea tuhuma za kisiasa na dhana tu, badala ya ushahidi halisi," Jaji Ogola amesema.
Akizungumzia suala pana la mfumo wa katiba, mahakama ilisema kwamba mchakato wa kutokuwa na imani naye ni halali na unaweza kuchunguzwa na mahakama pale ambapo kunadaiwa kuwa na ukiukwaji wa katiba.
"Tumeona kuwa mchakato wa kuondolewa madarakani ambao umepingwa katika malalamishi yaliyowasilishwa ni halali, na Mahakama hii ina mamlaka chini ya Vifungu 23, 22 na 165 vya Katiba kubaini iwapo mabunge ya Kitaifa na Seneti yalichukua hatua kwa mujibu wa kikatiba," Ogola alisema.
Hata hivyo, mahakama ilifafanua mipaka ya mamlaka yake, ikisisitiza kuwa haifanyi maamuzi kama chombo cha kisiasa ili kubaini sifa au utoshelezi wa mashtaka ya kuwashtaki kuondolewa madarakani.
"Tunasisitiza kwamba Mahakama si mwamuzi wa kisiasa bali ni wa kikatiba," Jaji amesema.
Jaji Ogola aliongeza kuwa ingawa mahakama zinaweza kukagua uhalali wa mchakato huo, haziwezi kubadilisha uamuzi wa kisiasa wa Bunge na tathmini yao wenyewe kuhusu uzito wa madai.
"Tunakubaliana kimsingi na hoja ya kwamba si kazi ya Mahakama hii kubainisha iwapo mashtaka dhidi ya Mheshimiwa Gachagua yalikuwa na uzito wa kutosha kuwezesha kuondolewe afisini," alisema.
Jaji Freda Mutuma katika uamuzi huo amesema kwamba suala la Bunge la Seneti kusikiliza kesi dhidi ya Gachagua kwa siku kumi hakujakiuka katiba wala sheria za Bunge.
Gachagua alilalamika kwamba siku hizo kumi zilikuwa chache mno na hazikumuwezesha kuandaa utetezi wa kutosha.
Mahakama imesema kwamba japo Bunge la Seneti lilijipangia siku hizo kumi, hatua hiyo haikukiuka katiba ya Nchi.
Aidha, mahakama hiyo imesema kwamba hoja aliyowasilisha na Gachagua kwamba uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais hakukukiuka katiba ya Kenya.
Gachagua aliiambia mahakama kwamba Kindiki alikuwa anahudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Kitaifa na hakuwa amejiuzulu kazini alipoteuliwa na Rais William Ruto kuchukuwa nafasi ya Gachagua ambaye alikuwa ameondolewa madarakani na uamuzi wa Bunge la Seneti.
Uamuzi huo pia umesema kuwa ushirikishi wa umma uliofanywa na Bunge la Kitaifa ulizingatia katiba.
"Bunge la Seneti halikukiuka vifungu vya 10 wala 118 vya Katiba kwa kutofanya ushirikishi wa umma ulio huru," mahakama imesema.
Mahakama ilibaini kuwa Bunge lilitoa ilani na kuhusisha ushirikishi kupitia vyanzo mbalimbali.