Ziara ya Rais Samia Urusi: Tulichojifunza na maswali mapya

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiitembelea Urusi wiki hii, vichwa vya habari katika vyombo vya habari vya kimataifa, vinasomeka, “Rais wa Tanzania aitembelea Urusi, huku uhusiano na Magharibi ukizorota.”

Rais Samia alipowasili Urusi, haikuwa tu safari ya kidiplomasia. Ilikuwa pia ni mara ya kwanza kwa rais wa Tanzania kutembelea Urusi tangu Mwalimu Julius Nyerere aliposafiri kwenda Umoja wa Kisovieti 1969.

Kuzungumza katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026) na kushikana mikono na Rais Vladimir Putin wa Urusi, kumesababisha tafsiri tofauti kutoka miji mikuu ya nchi za Magharibi na Afrika.

Ili kuelewa uzito wa ziara hii iliyotamatika, mtu ni lazima aangalie mitazamo yote:

Mtazamo wa Magharibi

Kutoka Washington, London, na Brussels, safari ya Rais Samia kwenda Kremlin inatazamwa kwa wasiwasi. Wanadiplomasia wa Magharibi wanaona kama ni kuzorota kwa demokrasia na kiongozi wa Afrika anajiweka karibu na Moscow iliyotengwa.

Kwa miaka michache ya kwanza ya urais wake, Samia alisherehekewa na Magharibi kama mtu mwenye msimamo wa mageuzi ambaye alikuwa akibadilisha mwelekeo wa mtangulizi wake.

Hata hivyo, nia njema hiyo ilitoweka kufuatia uchaguzi wa Oktoba 2025, ambao ulimfanya apate ushindi wa 98% huku kukiwa na ripoti za ukandamizaji, vurugu, utekaji nyara, na mamia ya vifo.

Huku mataifa ya Magharibi yakipitia upya uhusiano na Tanzania na kutoa vikwazo dhidi ya maafisa wa usalama wa Tanzania, Magharibi inaona safari hii ya Moscow kama jibu la moja kwa moja la hatua za Magharibi.

Mbele ya wachambuzi wa Magharibi, Samia anatafuta ulinzi wa kisiasa kutoka kwa utawala ambao hautegemei urafiki kwa kuzingatia haki za binadamu, uchaguzi huru, au utawala bora.

Kwa kumkumbatia Putin, ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wa kwanza kumpongeza kwa ushindi wake wa 2025, Rais Samia anaonekana kuashiria kwamba ukosoaji wa Magharibi hauna tena umuhimu kama ilivyo kuwa hapo awali.

Akitangaza kuwepo kwa maeneo makubwa ya uwekezaji nchini Tanzania na kuanza kwa safari za ndege za moja kwa moja zilizotangazwa hivi karibuni kati ya Dar es Salaam na Moscow, haya yote yanawakilisha mabadiliko ya hali ya mambo.

Mtazamo wa Afrika

Katika jiji la Dar es Salaam au maeneo mengine ya Afrika, kuna simulizi tofauti. Kwa mtazamo wa Afrika, ziara ya Rais Samia si kuzikimbia nchi za Magharibi, bali ni kutumia "uhuru" wake ndani ya ulimwengu wenye migawanyiko mingi.

Mataifa ya Afrika yamechoka kwa muda mrefu kuchukuliwa kama uwanja wa vita vya kiitikadi ambapo ushirikiano wa Magharibi unaunganishwa na maadili na kanuni kali za Kimagharibi.

Wakati washirika wa Magharibi wanapotishia kuitenga baada ya machafuko ya kisiasa ya 2025, Tanzania imefanya kile ambacho taifa lolote huru linalotaka kulinda mustakabali wake wa kiuchumi lingefanya: imetanua mwelekeo wake.

Zaidi ya hayo, Urusi ina historia kubwa katika bara zima. Wakati wa mazungumzo yake na Putin, Samia aliishukuru Urusi haswa kwa michango yake ya kihistoria kwa harakati za ukombozi wa Afrika dhidi ya ukoloni. Historia hii ya pamoja hutoa msingi wa kihisia na kisiasa ambao mara nyingi Magharibi hupuuza.

Kiuchumi, biashara ya pande mbili kati ya Urusi na Tanzania imekuwa ikikua. Ujumbe wa biashara ulioandamana na Samia hauangalii vita vya Ukraine au siasa za kijiografia za G7; unatafuta kukamilisha mikataba ya miundombinu, kuongeza utalii, na kuanzisha uchimbaji wa urani uliochelewa kwa muda mrefu.

Kwa wafuasi wa Rais Samia, kupata Shahada ya Uzamivu ya Heshima kutoka Chuo Kikuu cha RUDN na kuzungumza katika mkutano wa SPIEF ni ishara ya heshima na ushirikiano wa kimataifa, na sio kujisalimisha kwa mtawala Putin.

Tanzania ni rafiki wa wote. Sera yake ya mambo ya kigeni inaongozwa na malengo ya maendeleo, na sio mgawanyiko wa kijiografia wa Magharibi na Mashariki mwa Dunia.

Huku mataifa ya Magharibi yakiitazama ziara hiyo kupitia jicho la demokrasia dhidi ya utawala wa Putin, Tanzania inaitazama kupitia lenzi ya maslahi ya kitaifa.

Rais Samia anaonyesha kwamba mwaka 2026, mataifa ya Afrika yanakataa kuwekwa kwenye kona moja.

Ikiwa ziara hii itaharibu kabisa uhusiano muhimu wa Tanzania na Magharibi, utaharibika wakati Tanzania tayari imeweka wazi kwamba njia yake kusaka maendeleo itafika katika mji mkuu wowote itakao.

Kwa Urusi

Kwa Urusi kuwa mwenyeji wa kiongozi kutoka taifa la Afrika Mashariki, kunatuma ujumbe dhahiri kwa Magharibi: Majaribio ya Washington ya kuitenga Urusi kidiplomasia yanashindwa.

Wachambuzi wa Urusi wanaona ziara hiyo kuwa ni jambo la kawaida katika uhusiano na Afrika, huku bara hilo likikumbuka na kuthamini msaada wa kihistoria wa Moscow kwa ukombozi na kupinga ukoloni.