Shakahola: Mahakama yampata na hatia Mackenzie na wenzake 28 kwa mashtaka 191 ya mauaji

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Shakahola: Paul Mackenzie apatikana na hatia ya mauaji ya watu 191

Mhubiri wa Kenya Paul Nthenge Mackenzie amepatikana na hatia ya mauaji ya watu 191, wakiwemo watoto 190, katika kesi inayohusiana na vifo vya wafuasi wake katika msitu wa Shakahola, pwani ya Kenya.

Mackenzie na viongozi wengine 29 wa dhehebu lake walipatikana na hatia kufuatia hukumu iliyosomwa na Jaji Diana Mochache katika Mahakama ya Mombasa Jumatatu, Oktoba 19.

Tahadhari: Makala hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuyaona kuwa ya kusikitisha au ya kutatiza.

Mahakama ilieleza kuwa Mackenzie aliwashawishi wafuasi wake kuamini kuwa wangekutana na Yesu mbinguni kwa kufunga hadi kufa. Mafundisho yake yalipinga elimu rasmi na huduma za kisasa za afya, ambazo alizihusisha na maovu.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takriban saa nane, jaji alieleza jinsi mfumo wa mafundisho ya Mackenzie ulivyowafanya wafuasi wake kujitenga na jamii na kuamini kuwa kufa kwa njaa kungewawezesha kupata wokovu wa kiroho.

Mackenzie anatarajiwa kuhukumiwa Novemba 6.

Watoto walilazimishwa kufunga hadi kufa

Katika hukumu yake, Jaji Mochache alisema Mackenzie aliwaelekeza wafuasi wake kufunga hadi kufa ili waweze kwenda mbinguni kukutana na Yesu.

Mahakama ilielezwa kuwa baadhi ya watoto walilazimishwa kushiriki katika mfungo huo mkali, huku wakinyimwa chakula na maji. Baadhi yao walipigwa walipoomba chakula au kujaribu kupinga masharti hayo.

Mmoja wa washtakiwa wenzake aliambia mahakama kuwa Mackenzie alikuwa amewaeleza wafuasi wake kwamba yeyote ambaye angekataa agizo la kufunga alipaswa kulazimishwa kwenda mbinguni kwa "mangumi na mateke".

Kwa mujibu wa jaji, wafuasi wa Mackenzie walimwona kama msemaji wa Yesu duniani na waliamini kuwa maagizo yake yalikuwa na mamlaka ya kiroho.

Mahakama pia ilisikia ushahidi kuhusu namna vifo vilivyokuwa vikichukuliwa ndani ya dhehebu hilo. Mazishi msituni yalitajwa kuwa "harusi", huku waliofariki wakielezwa kuwa wamefunga ndoa na Yesu.

.

Mama alizuiwa kumnyonyesha mtoto wake

Miongoni mwa ushahidi uliotolewa mahakamani ni simulizi kuhusu mwanamke mjamzito ambaye alizuiwa kumnyonyesha mtoto wake mchanga.

Kwa mujibu wa shahidi mmoja, mtoto huyo alifariki siku 12 baada ya kuzaliwa. Mama yake alikuwa ameagizwa kufunga hadi kufa na kuwafuata watoto wake waliokuwa wamefariki.

Ushahidi huo ulionyesha jinsi mafundisho ya dhehebu hilo yalivyoathiri hata watoto wachanga ambao hawakuwa na uwezo wa kujilinda au kufanya maamuzi kuhusu maisha yao.

Mahakama pia ilisikiliza ushahidi kuhusu wazazi waliowazuia watoto wao kula, wakiamini kuwa kufunga kungewasaidia kupata wokovu.

Hata hivyo, si wote waliokuwa sehemu ya dhehebu hilo waliamini kwamba Mackenzie alikuwa amewalazimisha watu kufunga. Baadhi ya wafuasi wake wa zamani walisema watu walifanya hivyo kwa hiari kutokana na imani zao.

Miili ilipatikana katika makaburi ya pamoja

Kesi hiyo ilitokana na uchunguzi uliofuata kupatikana kwa makaburi ya pamoja katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi, mwaka 2023.

Mamlaka za Kenya zilisema mamia ya miili ilipatikana katika makaburi hayo. Kwa ujumla, miili 429 imefukuliwa kutoka eneo hilo, ingawa kesi ya sasa ya mauaji inahusiana na watu 191.

Kati ya wahanga hao 191, watoto walikuwa 190 na mtu mzima alikuwa mmoja.

Baadhi ya miili ilikuwa imeharibika kiasi cha kufanya iwe vigumu kutambua wahanga au kubaini chanzo cha vifo vyao. Hata hivyo, ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulijumuisha taarifa za uchunguzi wa miili, ushahidi wa mashahidi na mazingira ambayo wahanga walipatikana.

Jaji alieleza kuwa katika baadhi ya visa, ripoti za uchunguzi wa miili hazikuweza kubaini chanzo cha kifo kwa uhakika. Hata hivyo, mahakama ilizingatia ushahidi mwingine uliowasilishwa kuhusiana na vifo hivyo.

Watu waliokuwa wakichimba makaburi

.

Watu kutoka maeneo ya karibu na Shakahola walihusika katika uchimbaji wa baadhi ya makaburi yaliyokuwa na miili ya wahanga.

Mmoja wa wachimbaji hao, James, aliiambia BBC kuwa kila kaburi walilolifukua lilikuwa na angalau miili mitatu.

Alisimulia jinsi walivyowahi kupata miili ya watoto 12 ikiwa imepangwa katika mstari ndani ya kaburi moja, mmoja juu ya mwingine.

Mchimbaji mwingine, Salim Karisa, alisema baadhi ya watu kutoka katika dhehebu hilo walikuwa wakipelekwa msituni kwa pikipiki, lakini usiri wa shughuli zilizokuwa zikiendelea ndani ya msitu uliwafanya wakazi wa karibu wasielewe kilichokuwa kikitokea.

Baadhi ya wafuasi wa Mackenzie walikuwa wametoka sehemu mbalimbali za Kenya na kuhamia Shakahola baada ya kuamini mafundisho yake.

Baba aliyepoteza watoto wake wote sita

.

Stephen Mwiti, mwenye umri wa miaka 48, ni mmoja wa watu walioathiriwa na mkasa huo. Alipoteza watoto wake wote sita waliokuwa sehemu ya dhehebu hilo.

Mwiti aliiambia BBC kuwa alikwenda kumkabili Mackenzie baada ya kuona watu wengi wakiishi katika mazingira ya kutisha. Alikumbuka kuona wanawake wengi wenye vichwa vilivyonyolewa na watoto wengi wakiwa karibu na mhubiri huyo.

Mackenzie alikuwa amepiga marufuku vipodozi na baadhi ya mitindo ya nywele, akiwaagiza wanawake kunyoa vichwa vyao au kuacha nywele zao bila kuzitengeneza.

Mwiti alisema alipata na kuzika mabaki ya mwili wa mwanawe mmoja tu, Samuel.

Mke wake wa zamani alikuwa miongoni mwa watu waliopatikana na hatia ya mauaji pamoja na Mackenzie.

Alipoulizwa na BBC kuhusu hisia zake kwa mhubiri huyo, Mwiti alisema bado ana uchungu mkubwa kutokana na kupoteza watoto wake wote sita.

Kanisa lilianza mwaka 2003

.

Mackenzie alianzisha kanisa la Good News International Ministries mwaka 2003. Kwa miaka iliyofuata, kanisa hilo lilipata wafuasi wengi katika matawi yake mbalimbali nchini Kenya.

Kanisa hilo pia lilikuwa na kituo cha televisheni kilichoitwa Times TV, ambacho kilirusha mahubiri ya Mackenzie kutoka kanisani kwake Malindi.

Mahubiri yake kuhusu siku za mwisho yalijumuisha madai kwamba elimu ilikuwa uovu, huduma za afya zilipingana na mafundisho ya dini na vitambulisho vya kidijitali vilikuwa "alama ya shetani".

Kanisa kuu lilifungwa mwaka 2019, na Mackenzie akahamia msitu wa Shakahola, ambako aliwahimiza wafuasi wake kumfuata.

Baadhi ya wafuasi hao waliamini kwamba kuacha elimu na dawa za hospitali na kujitenga na jamii kungewasaidia kuwa tayari kwa kurudi kwa Yesu.

Baadhi ya wafuasi bado wanamtetea

.

Peter Shukrani, mwenye umri wa miaka 23, aliambia BBC kuwa mama yake alimpeleka katika kanisa la Mackenzie alipokuwa na umri wa miaka minane.

Alisema alihisi Mackenzie alikuwa baba yake wa kiroho na bado alimpenda, licha ya matukio yaliyotokea Shakahola.

Shukrani alisema alipokuwa msituni aliugua, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya kwa sababu mama yake alitupa dawa alizohitaji, akiamini kuwa Mungu pekee ndiye angeweza kumponya.

Alisema huenda angefariki kama hangeokolewa kutoka msituni mwaka 2023.

Mwana wa Mackenzie, Dan Paul Mackenzie, ambaye alisema aliwahi kufanya kazi kama mpiga picha katika kanisa la baba yake, alikuwa na mtazamo tofauti. Kabla ya hukumu kutolewa, alisema baba yake alipaswa kupatikana na hatia kwa sababu alikuwa kiongozi ambaye wafuasi wake walimtegemea.

Kesi nyingine bado zinamkabili

Peter Shukrani, mwenye umri wa miaka 23, aliambia BBC kuwa mama yake alimpeleka katika kanisa la Mackenzie alipokuwa na umri wa miaka minane.

Alisema alihisi Mackenzie alikuwa baba yake wa kiroho na bado alimpenda, licha ya matukio yaliyotokea Shakahola.

Shukrani alisema alipokuwa msituni aliugua, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya kwa sababu mama yake alitupa dawa alizohitaji, akiamini kuwa Mungu pekee ndiye angeweza kumponya.

Alisema huenda angefariki kama hangeokolewa kutoka msituni mwaka 2023.

Mwana wa Mackenzie, Dan Paul Mackenzie, ambaye alisema aliwahi kufanya kazi kama mpiga picha katika kanisa la baba yake, alikuwa na mtazamo tofauti. Kabla ya hukumu kutolewa, alisema baba yake alipaswa kupatikana na hatia kwa sababu alikuwa kiongozi ambaye wafuasi wake walimtegemea.

Mbali na hukumu ya mauaji, Mackenzie na baadhi ya washirika wake wanakabiliwa na kesi nyingine zinazohusiana na ugaidi, kueneza misimamo mikali na makosa dhidi ya watoto.

Kesi ya sasa ndiyo ya kwanza ambayo Mackenzie amepata hukumu katika mashtaka mazito ya mauaji yanayohusiana na mkasa wa Shakahola.

Tukio hilo limezua mjadala mkubwa nchini Kenya kuhusu uhuru wa dini, udhibiti wa taasisi za kidini, ulinzi wa watoto na wajibu wa serikali kuzuia mafundisho yanayoweza kuhatarisha maisha ya waumini.

Hukumu hiyo ni hatua muhimu katika mchakato wa kutafuta haki kwa wahanga na familia zao, huku kesi nyingine zinazomkabili Mackenzie zikiendelea kufuatiliwa.