Washauri wa Roman Abramovich walimsaidiaje kuficha utajiri wake?

    • Author, James Oliver
    • Author, Rory Tinman
    • Nafasi, BBC Panorama
    • Author, Simon Lock
    • Nafasi, the Bureau of Investigative Journalism
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Uchunguzi wa kipindi cha BBC Panorama umebaini kuwa kampuni kubwa zaidi ya uhasibu duniani ilisaidia kughushi nyaraka ili kuficha utajiri wa Roman Abramovich na kukwepa kulipa kodi.

Hesabu zilizothibitishwa na Deloitte nchini Cyprus zilisababisha mali zenye thamani ya dola milioni 672 (£508m), zikiwemo boti za kifahari, majumba ya kifahari na ndege binafsi, kutoweka katika hesabu za kampuni za Abramovich.

Deloitte pia inaonekana kutoa ushauri kuhusu mpango wa kukwepa kulipa kiasi kikubwa cha kodi inayotokana na utajiri wa bilionea huyo kupitia kughushi nyaraka.

Wakili Andrew Mitchell KC, mtaalamu wa sheria za huduma za kifedha, alisema ushahidi uliopatikana na Panorama unaonesha kuwa huo ulikuwa ukwepaji kodi wa wazi kabisa.

Alisema: "Hili haliwezi kuwa wazi na dhahiri zaidi ya hivi."

Mawakili wa Roman Abramovich walisema anakanusha madai kwamba alikwepa kulipa kodi au kuficha utajiri wake. Walisema Panorama haikutoa ushahidi wowote unaoonesha kuwa alijua kuhusu kughushi nyaraka hizo, aliidhinisha au kuelekeza hatua hizo, na kuongeza kuwa ilikuwa halali kwake kutegemea ushauri wa wataalamu.

Deloitte Cyprus ilisema kampuni hiyo "inafanya kazi kwa kuzingatia sheria zinazotumika".

Matokeo hayo yanafichuliwa kufuatia uchunguzi wa pamoja uliofanywa na BBC Panorama na Bureau of Investigative Journalism.

Kwa karibu miongo miwili, Roman Abramovich alikuwa oligarki maarufu zaidi wa Urusi nchini Uingereza. Alikaribishwa London ambako alinunua klabu ya Chelsea mwaka 2003 na kuifadhili katika kipindi chake cha mafanikio makubwa zaidi.

Hata hivyo, baada ya Urusi kuivamia Ukraine kikamilifu mwaka 2022, serikali ya Uingereza iliweka vikwazo dhidi yake kwa kumhusisha na Rais Vladimir Putin, na kumlazimisha kuiuza klabu hiyo.

Inaripotiwa kuwa Abramovich anaishi Uturuki, nchi ambayo imekuwa mahali salama kwake kwa sababu haikutekeleza vikwazo hivyo.

Katika kisiwa cha Jersey, mali zake zenye thamani ya pauni bilioni 5.4 zimeendelea kuzuiliwa, huku uchunguzi wa jinai ukiendelea kwa miaka minne.

Mawakili wa bilionea huyo waliiambia BBC kuwa anakanusha madai katika uchunguzi unaoendelea Jersey na kwamba uchunguzi huo "ulifanywa kwa madhumuni ya kisiasa".

Uchunguzi wetu umebaini ushahidi mpya kuhusu namna himaya ya biashara ya Abramovich ilivyoendeshwa. Pia umeibua maswali mazito kuhusu uadilifu wa baadhi ya washauri wake wa kitaaluma.

Ushahidi huo unatokana na nyaraka zilizovuja, zikiwemo maelfu ya hati kuhusu fedha za bilionea huyo na shughuli za mtandao wa kampuni za nje ya nchi (offshore) zilizosimamiwa kutoka Cyprus kati ya mwaka 1995 na 2022. Cyprus ilikuwa kituo maarufu cha kuegesha fedha kwa ajili ya kukwepa kodi, hasa miongoni mwa Warusi.

BBC na washirika wake wa vyombo vya habari, wakiwemo The Guardian, Paper Trail Media, Organised Crime and Corruption Reporting Project, Cyprus Investigative Reporting Network na Bureau of Investigative Journalism, wamekuwa wakiripoti kuhusu nyaraka hizo zilizovuja tangu mwaka 2023 kama sehemu ya uchunguzi wa Cyprus Confidential uliofanywa na International Consortium of Investigative Journalists.

Mwaka 2022, Panorama pia iliripoti namna Abramovich alivyopata utajiri wake kupitia mkataba uliokumbwa na tuhuma za ufisadi wa kununua kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Urusi katika miaka ya 1990, kisha kuiuzia serikali hiyo tena muongo mmoja baadaye na kupata faida ya mabilioni ya dola.

Awali, Abramovich amekanusha madai ya ufisadi kuhusiana na mkataba huo.

Faida iliyotokana na biashara zake za mafuta nchini Urusi ilihamishiwa kwenye mtandao wa kampuni za nje ya nchi. Kampuni hizo zilisimamiwa kutoka Cyprus na kampuni ya huduma za usimamizi wa biashara iitwayo MeritServus, iliyoko Limassol, mji wa pili kwa ukubwa katika kisiwa hicho.

Hadi mwaka 2005, Deloitte, ambayo kwa sasa ndiyo kampuni kubwa zaidi kati ya kampuni nne kubwa zinazotawala sekta ya uhasibu duniani, ilikuwa inamiliki MeritServus.

Baada ya kampuni hizo kutengana, ziliendelea kushirikiana kwa karibu na washirika wa Abramovich kusimamia utajiri wake wa kimataifa.

Nyaraka zilizovuja kutoka MeritServus zinafichua baadhi ya mbinu walizotumia.

Mfano wetu wa kwanza wa nyaraka zilizowekwa tarehe za nyuma ulitokea mwaka 2006, baada ya sheria mpya nchini Cyprus kuanza kuhitaji hesabu za kampuni kuchapishwa kwa umma.

Sheria hiyo mpya ya uwazi ilitishia kufichua siri kuhusu utajiri mkubwa wa Abramovich.

Deloitte Cyprus ilikuwa imeandaa rasimu ya hesabu za mwaka 2003 za kampuni yake ya Cyprus, Amiscan Investments, lakini haikuwa bado imezikamilisha. Hesabu hizo ziliorodhesha mali za kifahari zenye thamani ya dola milioni 672.

Mali hizo zilijumuisha jumba la kifahari huko West Sussex, flati ya kifahari jijini London na shamba kubwa kusini mwa Ufaransa. Pia kulikuwa na helikopta, ndege binafsi na boti kadhaa alizomiliki bilionea huyo wakati huo, zikiwemo Pelorus iliyokuwa na thamani ya dola milioni 147.5.

Ili kuzuia mali hizo kufichuliwa, washirika wa Abramovich na MeritServus waliamua kubadilisha historia ya miamala hiyo.

Walibuni mpango wa kukwepa sheria ya uwazi kwa kuhamishia mali hizo kwa kampuni mama ya Amiscan iliyokuwa katika Visiwa vya Virgin vya Uingereza (BVI), ambako zingeweza kufichwa.

Pia waliweka tarehe za nyuma kwa uhamisho huo kwa miaka mitatu ili ionekane kuwa mali hizo zilihamishwa mwaka 2003.

Deloitte Cyprus ilikagua nyaraka hizo zilizowekwa tarehe za nyuma na kusema zilikuwa "zinatosha" kuruhusu mali hizo kuondolewa katika hesabu za Amiscan.

Hesabu za mwaka 2003 zilipothibitishwa na Deloitte mwaka 2006, majumba, ndege na boti hizo zilitoweka katika hesabu hizo kwa kubadilishwa kwa maandishi machache tu.

Mali zilizobaki zilikuwa na thamani ya dola 75,000 pekee.

Deloitte ilithibitisha hesabu hizo licha ya nyaraka zilizovuja kuonesha kuwa ilijua hazikuwa na taarifa za kweli na sahihi.

Lord Sikka, profesa wa uhasibu katika Chuo Kikuu cha Sheffield, alisema kupotosha tarehe za miamala na kushindwa kuchapisha hesabu zinazoonesha hali halisi ya kifedha kulikuwa ni "ukiukaji wa wajibu wa kisheria" na jambo "la kusikitisha sana".

Panorama pia ilipata ushahidi kuwa nyaraka zilizowekwa tarehe za nyuma zilitumika katika mpango wa kukwepa kodi.

Mpango huo ulihusisha kampuni nyingine ya Abramovich iliyosajiliwa Cyprus, Kravin Investments, ambayo ilikuwa na karibu dola bilioni mbili benki mwaka 2003.

Kampuni hiyo ilikuwa ikipata kiasi kikubwa cha fedha kutokana na riba, hivyo ilipaswa kulipa kodi ya mapato hayo ya riba kwa mamlaka za Cyprus.

Lakini washauri wa Abramovich walikuwa na wazo jingine la kubadilisha historia.

Barua pepe iliyotumwa na MeritServus kwa washirika wa Abramovich nchini Urusi mwezi Agosti 2005 ilisema mpango huo ulikuwa umebuniwa baada ya mkutano na Deloitte.

"Ikiwa mtakubaliana, itakuwa muhimu kubadilisha taarifa za fedha na kumbukumbu za uhasibu ipasavyo kwa miaka ya 2003 na 2004," barua pepe hiyo ilisomeka.

MeritServus iliwaeleza washirika wa bilionea huyo nchini Urusi kuwa makadirio ya kodi ya muda ya Kravin kwa mwaka 2005 yangewasilishwa yakionesha kuwa kampuni hiyo haikupata mapato yoyote kutokana na fedha hizo.

Mwezi mmoja baadaye, mshirika mmoja nchini Urusi alijibu kwa barua pepe akisema: "Ninakubaliana."

MeritServus kisha iliandaa nyaraka kadhaa zenye tarehe za nyuma ambazo zilionesha kwa uongo kuwa Kravin ilikuwa inashikilia na kuwekeza fedha hizo kwa niaba ya kampuni yake mama iliyokuwa BVI.

Hatua hiyo ilifanya ionekane kana kwamba Kravin haikuwa mmiliki halisi wa fedha hizo, hivyo haikupaswa kulipa kodi nchini Cyprus.

Katika barua pepe ya Septemba 2005, Deloitte iliandika kuwa "mabadiliko fulani yatalazimika kufanywa kwenye hesabu (salio la akaunti za benki, mapato ya riba, taarifa ya faida na hasara)" kutokana na mabadiliko yaliyofanywa kwa nyaraka za Kravin zenye tarehe za nyuma.

Kwa hiyo, Deloitte inaonekana kutoa ushauri kuhusu kughushi kumbukumbu za kifedha. Ushahidi unaonesha kuwa iliruhusu kampuni ya Abramovich kukwepa kulipa kodi ya mamilioni ya dola.

Andrew Mitchell KC aliiambia Panorama kuwa huo ulikuwa ukwepaji kodi wa wazi kabisa.

"Endapo jambo hilo lingetokea nchini Uingereza na kuhusisha mamilioni ya pauni, Mamlaka ya Mapato na Forodha ya Uingereza (HMRC) ingekuwa inafikiria kufungua mashtaka," alisema.

Mbunge wa Cyprus, Christos Christofides, alisema ikiwa kodi ilikwepwa, basi "tunapaswa kuona namna ya kurejesha fedha zetu na, ikiwa baadhi ya watu wana hatia, wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria zetu".

Mbali na nyaraka ambazo Deloitte ilisaidia kuweka tarehe za nyuma, washauri wa Abramovich katika MeritServus walighushi seti ya tatu ya kumbukumbu.

Safari hii, suala lilihusu utajiri mkubwa wa biashara wa bilionea huyo, wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 10, uliokuwa unashikiliwa na kampuni iitwayo Electus Investments nchini Cyprus.

MeritServus iliweka tarehe za nyuma kwenye nyaraka ili kuonesha kuwa Electus haikuwa inamiliki utajiri huo.

Ilitumia kampuni nyingine ya Abramovich iliyokuwa na jina hilohilo, Electus Investments, lakini kampuni hiyo ilikuwa imesajiliwa katika Visiwa vya Virgin vya Uingereza (BVI), ambako hesabu za kampuni hazikuhitajika kuwekwa wazi kwa umma.

Barua pepe zinaonesha kuwa mwaka 2006, MeritServus ilikiri kuwa utajiri huo ulimilikiwa na Electus Cyprus.

Hata hivyo, ilipendekeza tena kubadilisha historia, safari hii kwa "kuhamisha umiliki halisi kwenda Electus Investments ya BVI" na kufanya ionekane kuwa mabadiliko hayo yalifanyika miaka mitatu iliyotangulia.

MeritServus ilisaini na kuweka tarehe za nyuma kwenye nyaraka zilizodai kwa uongo kuwa kampuni ya BVI ilikuwa inamiliki utajiri wa dola bilioni 10 tangu tarehe 20 Novemba 2003.

Kwa hiyo, hesabu za kampuni ya Cyprus yenye jina hilohilo zilipowekwa wazi kwa umma, ilionekana kuwa na mali zenye thamani ya dola 145,000 pekee.

Mabilioni ya Roman Abramovich yalikuwa yamefanywa kutoweka.

Andrew Mitchell KC aliiambia Panorama: "Jambo unalolichukua kutokana na hili ni kwamba kuna wataalamu walio tayari kupindisha na kuvunja kanuni za taaluma zao na, kwa kufanya hivyo, kuvunja sheria. Inaonekana wako tayari kufanya lolote, hata kuunda nyaraka za uongo."

Vladimir Milov, aliyekuwa naibu waziri wa nishati wa Urusi wakati Abramovich alipokuwa akijenga himaya yake ya biashara na ambaye sasa ni mkosoaji wa serikali ya Urusi, alisema:

"Kwa kila oligarki wa Urusi, Mashariki ya Kati au Afrika anayehusishwa na ufisadi, kuna jeshi la watoa huduma za kifedha, kisheria na mahusiano ya umma kutoka nchi za Magharibi, ambao wako tayari kupokea fedha ili kusafisha sifa zao na kuwafanya waonekane watu wa kawaida."

Wakikanusha madai ya makosa yoyote yaliyofanywa na bilionea huyo, mawakili wa Roman Abramovich walisema kuwa "hakuhusika katika uendeshaji wa kila siku wa kampuni hizo".

Walisema kuwa pale ambapo mipango ilipendekezwa na washauri wa kitaaluma, "kutegemea ushauri huo kulikuwa jambo sahihi na halali kabisa".

Deloitte Cyprus ilisema haiwezi kutoa maoni kuhusu madai mahususi kwa sababu nyaraka hizo zina zaidi ya miaka 20 na hazipatikani tena.

MeritServus ilifungwa kufuatia kuvuja kwa nyaraka katika uchunguzi wa Cyprus Confidential.

Imetafsiriwa na Faidha Ngaga na kuhaririwa na Ambia Hirsi