Wanajeshi wa Marekani waondoka Iraq baada ya miaka 20, nini kitafuata?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Marekani inapanga kuwaondoa wanajeshi wake wote waliosalia nchini Iraq kufikia tarehe 30 mwezi Septemba, hatua hii itaondoa uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini humo.

Wanajeshi wa Marekani wamekuwa nchini Iraq kwa muda wa miaka ishirini.

Hatua ya kuondoka nchini Iraq inajiri baada ya kumalizika kwa operesheni ya kijeshi iliyoanza mwaka wa 2003, wakati Marekani ilipoivamia Iraq na kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa wakati huo Saddam Hussein. Uvamizi huo ulifuatiwa na miaka ya uasi wa kutumia silaha pamoja na ghasia za kikabila.

Ingawa jeshi la Marekani liliondoka Iraq mwaka wa 2011, lilirejea tena mwaka 2014 kusaidia katika mapambano ya kudhibiti kundi la kigaidi la Islamic State (IS).

Kuondoka kwa wanajeshi hao kunajiri wakati kuna mvutano unaoendelea kati ya Marekani na Iran, hali ambayo imewaweka wanajeshi wa Marekani nchini Iraq katika hatari ya kushambuliwa.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani hakumaanishi kwamba ushawishi wa Marekani nchini Iraq umekwisha.

Kwanini wanaondoka wakati huu?

Kuondoka kwa wanajeshi hao kunatokana na makubaliano ya mwaka wa 2024 kati ya Washington na Baghdad ya kukomesha operesheni ya Inherent Resolve, kampeni iliyoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la ISIS.

Katika kilele cha vita vya Iraq mwaka wa 2007, Marekani ilikuwa imetuma zaidi ya wanajeshi 170,000 nchini humo.

Kufikia mwezi Disemba 2023, kabla ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kuwaondoa wanajeshi hao, idadi hiyo ilikuwa imeshuka hadi takribani wanajeshi 2,400, kulingana na kituo kinachoendesha shughuli za kijeshi za Marekani(CENTCOM).

Tangu wakati huo, Marekani imeendelea kupunguza uwepo wake wa kijeshi na sasa kimesalia kikosi kidogo katika eneo la Kurdistan, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.

"Kuondoka kwa wanajeshi hawa kulikubaliwa na serikali ya awali ya Iraq kwa sababu operesheni ya kuishinda ISIS ilikuwa imetimiza malengo yake nchini Iraq," alisema Safwan Al-Amin, mtafiti mwandamizi katika shirika la Atlantic Council.

Hatua hiyo pia inaakisi shinikizo la kisiasa linaloendelea ndani ya Iraq.

Douglas Silliman, aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Iraq kuanzia mwaka wa 2016 hadi 2019, amesema serikali mbalimbali za Iraq zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo la kuondoa uwepo wa kijeshi wa Marekani, kwa sababu watu wengi wameuchukulia uwepo huo kama ukiukaji wa mamlaka ya Iraq kama taifa huru.

"Baadhi ya serikali za Iraq, zimekabiliwa na shinikizo kutoka kwa makundi yanayoiunga mkono Iran pamoja na sehemu ya jamii ya Washia, zimekuwa zikitaka wanajeshi hao kuondoka nchini humo," anasema Silliman.

Jeshi la Marekani liliondoka Iraq mwaka wa 2011 wakati wa utawala wa Rais Barack Obama, lakini lilirejea miaka mitatu baadaye baada ya ombi la serikali ya Baghdad, kufuatia ISIS kuteka maeneo mengi nchini humo.

Tangu wakati huo, jukumu la Marekani limebadilika kutoka mapambano ya moja kwa moja hadi kutoa mafunzo, ushauri wa kijeshi na kushirikiana katika masuala ya kijasusi.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema muda wa kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani mwezi huu unatokana zaidi na masuala ya usalama kuliko kukamilika rasmi kwa operesheni dhidi ya ISIS.

"Kinachozingatiwa hapa ni hatari ya usalama, si ISIS. Hoja hiyo ilipoteza umuhimu wake miaka kadhaa iliyopita," alisema HA Hellyer, mtaalamu mwandamizi katika Royal United Services Institute (RUSI) nchini Uingereza.

Hellyer alirejelea mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya vituo vya Marekani kaskazini mwa Iraq, kufuatia mvutano uliopo na Iran.

Washington inazidi kuwaona wanajeshi wake waliosalia Iraq kama 'walengwa' walio katika hatari ya kushambuliwa.

Al-Amin pia amekubaliana na mtazamo huo, akibainisha kuwa maafisa wa Marekani na Iraq walikuwa wamejadili awali uwezekano wa kubakiza kikosi kidogo cha Marekani hata baada ya kumalizika kwa operesheni ya muungano dhidi ya ISIS.

Urithi wa Marekani nchini Iraq ni upi?

Zaidi ya miongo miwili baada ya uvamizi wa Iraq, bado kuna mitazamo tofauti kuhusu urithi ulioachwa na jeshi la Marekani nchini humo.

Al-Amin anaelezea urithi huo kama "mchoro wenye rangi nyingi."

"Uvamizi wa Marekani haukutimiza malengo yake yaliyotangazwa, wala mabadiliko ya utawala hayakukidhi matarajio ya Wairaq ya kuwa na nchi yenye utulivu na ustawi" , vita hivyo vilivuruga utulivu wa eneo hilo na kuunda mazingira yaliyoiwezesha Iran kupanua ushawishi wake.

Bw. Silliman alikubaliana kwamba kipindi cha mpito kilikuwa na misukosuko, lakini anasema Wairaq wengi walimwambia kwamba walithamini mabadiliko ya kisiasa yaliyofuatia kuondolewa kwa Saddam Hussein madarakani.

Anaongezea kuwa dhana kwamba "Iraq inapaswa kuongozwa kwa demokrasia inayowakilisha wananchi" imeanza kukita mizizi hatua kwa hatua, ingawa "kujenga utamaduni wa kidemokrasia katika jamii ambayo haijawahi kuipitia itachukua muda mrefu"

Yerevan Saeed, mkurugenzi wa Kurdish Global Peace Initiative katika chuo cha American University mjini Washington, ana mtazamo chanya, anasema,

"Kuondolewa kwa utawala wa zamani ilikuwa hatua kubwa ya mabadiliko,"

Licha ya kuwepo kwa ufisadi unaoendelea, anaamini kuwa Iraq ya sasa ina uhuru mkubwa zaidi wa kisiasa na wigo mpana zaidi wa misimamo ya kisiasa kuliko ilivyokuwa kabla ya 2003, hususan katika eneo la Kurdistan nchini Iraq.

Wakati huo huo, Hellyer alikataa wazo la kutathmini urithi wa Marekani nchini Iraq kwa kuzingatia demokrasia pekee.

"Watu wanapaswa kuacha kuuliza, 'Je, Marekani inaweza kujenga demokrasia nchini Iraq?' Jibu ni hapana, na hilo tayari limebainika,"

Hata hivyo, wataalamu wote wanne wanakubaliana kwamba Iraq bado iko mbali na mfano wa demokrasia thabiti ambao watunga sera wa Marekani waliutarajia mwaka 2003.

Kwa mujibu wao, ufisadi bado umeenea, huku makundi yenye silaha yakiendelea kuwa na ushawishi mkubwa sambamba na taasisi rasmi za serikali.

Hali hii inaonekana wazi katika Popular Mobilization Forces (PMF), ambayo kwa kiasi kikubwa inaundwa na wanamgambo wa Kishia. Serikali ya Baghdad bado inajaribu kuhakikisha kikosi hicho kiko chini ya udhibiti kamili wa serikali.

Nini kitafuata?

Al-Amin anasema kuwa kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani hakumaanishi mwisho wa ushawishi wa Marekani nchini Iraq.

"Marekani bado ina ushawishi mkubwa kwa sababu Iraq inategemea mauzo ya mafuta yanayofanyika kwa kutumia dola ya Marekani. Iraq pia inaendelea kutegemea Marekani kwa ununuzi wa silaha na inahitaji msaada wa kidiplomasia kutoka Washington katika kushughulikia changamoto kutoka nchi jirani," anasema Al-Amin.

Kwa mujibu wa Saeed, sehemu ya ushawishi huo inadumishwa kupitia uwepo wa kidiplomasia wa Washington nchini Iraq.

"Marekani ina ubalozi mkubwa zaidi duniani mjini Baghdad. Pia ina ubalozi mdogo mkuu mkubwa zaidi duniani mjini Erbil," alisema, akiongezea kuwa vituo hivyo vyote vitaendelea kuhitaji ulinzi hata baada ya kuondoka kwa jeshi la Marekani.

Bw. Silliman anasema kuwa uhusiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili utaendelea, ikiwemo kutoa mafunzo na kusaidia katika mipango ya kijeshi kwa jeshi la Iraq, Kikosi cha Iraq cha Kukabiliana na Ugaidi (CTS), pamoja na vikosi vya Peshmerga vya eneo linalojitawala la Kurdistan.

Hata hivyo, swali kubwa lisilo na jibu bado linahusu makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na Iran nchini Iraq. Waziri Mkuu wa Iraq, Ali al-Zaidi, awali alitaka makundi hayo yawekwe kikamilifu chini ya udhibiti wa serikali kabla ya tarehe ya mwisho ya Septemba 30. Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo, makundi hayo yanataka muda huo uongezwe hadi mwisho wa mwaka 2027.

Saeed pia alielezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa ISIS kuimarika tena, kama ilivyotokea baada ya Marekani kuondoka Iraq mwaka 2011.

Huku kukiwa na wasiwasi mpya ndani ya jamii ya Kisunni kuhusu namna watakavyotendewa, Saeed alionya kuwa hatari ya watu kujiunga na makundi yenye misimamo mikali bado ni kubwa.

Kwa upande mwingine, Silliman alikuwa na mtazamo tofauti, akisema kuwa vikosi vya usalama vya Iraq sasa vina nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa muongo mmoja uliopita na vina uwezo wa kukabiliana na vitisho vya aina hiyo.

Wataalamu wanaamini kuwa kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani kunazua pia maswali mapya kuhusu mizani ya nguvu kati ya Marekani na Iran nchini Iraq.

Al-Amin alitabiri kuwa Iran itajaribu "kuimarisha ushawishi wake kadiri itakavyowezekana," huku akionya dhidi ya kuchukulia kuondoka kwa wanajeshi hao kama mwisho wa uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq.

"Jeshi la Marekani liliondoka Iraq mwaka 2011, lakini lilirejea miaka michache baadaye. Hii ni mwisho wa sura moja, lakini si sura ya mwisho ya hadithi hii," alisema.