Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Qatar yashinikiza makubaliano ya amani kati ya Marekani na Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majed al-Ansari, amesema Doha inaendelea kubadilishana ujumbe kati ya pande hizo mbili kwa lengo la kupata mwafaka.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. DRC yaitaka UN kusitisha utekelezaji wa majukumu ya walinda amani wa Rwanda

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda zilirushiana tuhuma mpya katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne, hali iliyoonesha kuendelea kuwepo kwa tofauti kuhusu utekelezaji wa makubaliano ya amani yanayoungwa mkono na Marekani, yenye lengo la kumaliza mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo.

    Akihutubia Baraza hilo, Balozi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa, Martin Ngoga, alisema Kigali inaendelea kujitolea katika michakato ya amani ya Washington na Doha, lakini akasisitiza kuwa kutokomeza tishio la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kundi la waasi la Rwanda linalofanya shughuli zake mashariki mwa Kongo, ndilo kipimo muhimu cha maendeleo katika mchakato huo.

    Ngoga alizishutumu baadhi ya ngome za Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) kwa kuendelea kushirikiana na FDLR, licha ya ahadi zilizotolewa chini ya mfumo wa makubaliano ya amani.

    “FDLR lazima itokomezwe, na hatua hiyo ya kutokomeza tishio lake lazima iwe yenye ufanisi, kamili na inayoweza kuthibitishwa.”

    Alisema kuendelea kuwepo kwa kundi hilo mashariki mwa Kongo kunaleta tishio la moja kwa moja kwa usalama wa Rwanda, na akataka kuwepo kwa viwango sawa vya uthibitishaji na uwajibikaji kwa pande zote.

    Hata hivyo, akijibu mbele ya Baraza hilo, Zénon Mukongo Ngay, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika Umoja wa Mataifa, alikanusha tuhuma za Rwanda na kusema Kinshasa tayari inachukua hatua madhubuti za kulivunja na kuliondoa tishio la FDLR.

    Mukongo Ngay aliliambia Baraza kwamba DRC imetia saini makubaliano ya kuwaondoa wapiganaji katika makundi ya FDLR na kuwasaidia kurejea katika maisha ya kiraia, huku ikiandaa operesheni zaidi dhidi ya kundi hilo kwa msaada wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kudumisha Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO).

    “Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inachukua hatua madhubuti na zinazoweza kuthibitishwa ili kukomesha tishio la FDLR.”

    Mjumbe huyo wa Kongo alisema juhudi hizo zinajumuisha itifaki iliyotiwa saini mwezi Mei pamoja na hatua za hiari za kuweka chini silaha zilizochukuliwa na makundi mengine ya silaha mwezi Agosti.

    Hata hivyo, ombi kali zaidi la Kinshasa lililenga nafasi ya Rwanda katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa. Katika taarifa yake baada ya kikao cha Baraza la Usalama, Mukongo Ngay alitaka kusitishwa kwa upelekaji mpya, mzunguko wa vikosi au ushiriki wa vikosi vya Rwanda katika misheni za Umoja wa Mataifa hadi pale utakapothibitishwa kwamba vikosi vya Rwanda vimeondoka katika ardhi ya Kongo.

    “Nchi ambayo vikosi vyake vinahusika katika mzozo haiwezi, wakati huohuo, kudai kuwa inachangia katika operesheni yenye jukumu la kulinda amani na kudumisha imani ya wananchi.”

    Akirejelea Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2773, pia alitoa wito wa kukomeshwa kwa uungaji mkono kwa kundi la waasi la M23 na kuondolewa kwa vikosi vya Rwanda kutoka DRC.

    “Azimio la 2773 linataka kusitishwa kwa uungaji mkono kwa M23 na kuondolewa kwa vikosi vya Rwanda kutoka katika ardhi ya Kongo.”

    Kigali bado haijatoa majibu ya moja kwa moja kuhusu wito huo wa kusitishwa kwa ushiriki wake katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

    Mabadilishano hayo ya kauli yaliweka wazi kiini cha mzozo unaozunguka juhudi za sasa za kuleta amani: Rwanda inasema amani ya kudumu inategemea kutokomezwa kwa FDLR kwa njia inayoweza kuthibitishwa, huku DRC ikisisitiza kwamba maendeleo katika mchakato wa amani lazima pia yahusishe kuondolewa kwa vikosi vya Rwanda, kukomeshwa kwa madai ya uungaji mkono kwa M23, pamoja na kusitishwa kwa ushiriki wa Rwanda katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa hadi masharti hayo yatakapotimizwa.

    Hata hivyo, nchi zote mbili zilithibitisha tena dhamira yao ya kuendelea na michakato ya amani ya Washington na Doha.

  2. Madereva waendelea na mgomo licha ya maagizo ya Katambi

    Madereva wa mabasi wameendelea na mgomo katika Stendi ya Mabasi Magufuli, Dar es Salaam, licha ya Serikali kuchukua hatua za kusitisha kwa muda mfumo wa kukata pointi kwenye leseni zao.

    Hadi saa 2:50 asubuhi leo Jumatano, Septemba 30, 2026, hakuna basi lililoondoka stendi hiyo kutoa huduma, huku madereva wakisema bado hawajaridhishwa na hatua zilizotangazwa na Serikali.

    Mgomo huo ulianza jana Jumanne, Septemba 29, 2026, huku madereva wakishinikiza kushughulikiwa kwa madai mbalimbali, yakiwamo suala la kukatwa pointi, kufungiwa madereva na kuondolewa kwa leseni zao kwenye mfumo.

    Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, alifika katika stendi hiyo na kuagiza Jeshi la Polisi kusitisha kwa muda mfumo wa kukata pointi ili kuruhusu tathmini ya kina kuhusu mfumo huo.

    Katambi pia aliwataka madereva kurejea kazini na kuendelea na shughuli zao kwa amani, huku akiliagiza Jeshi la Polisi kutowabughudhi madereva kwa kipindi cha siku 14 cha mpito, wakati Serikali ikifanyia kazi hoja zao.

    Hata hivyo, maagizo hayo hayajaondoa mgomo, huku madereva wakiendelea kugoma hadi watakapopata majibu wanayoyataka kuhusu madai yao.

    Hali hiyo imewaweka katika wakati mgumu abiria waliokuwa wakitarajia kuendelea na safari leo. Baadhi yao wameonekana wakihangaika kurejeshewa nauli zao na kutafuta usafiri mbadala.

    Hapo jana, Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania, Majura Kafumu, aliwasilisha madai na changamoto wanazokabiliana nazo.

    Miongoni mwa masuala yaliyotajwa ni mikataba ya ajira na utekelezaji wa Sheria za Kazi, namna Jeshi la Polisi linavyosimamia Sheria za Barabarani, mfumo wa VTS pamoja na hali ya miundombinu ya barabara.

    Madereva hao walianza kugoma kutoa huduma tangu asubuhi ya Jumanne, hatua iliyosababisha usumbufu kwa wasafiri katika baadhi ya maeneo.

    Baada ya kukutana na Waziri Katambi, Serikali ilisema itaanza kushughulikia masuala yaliyowasilishwa, huku ikiwataka madereva kurejea kazini.

    Soma Zaidi:

  3. Marais sita kuhudhuria uzinduzi wa kiwanda cha mafuta cha Dangote Lamu

    Marais sita wanatarajiwa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Lamu, mradi unaokadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi trilioni 2 za Kenya.

    Rais William Ruto ataungana na viongozi wenzake akiwemo Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Abiy Ahmed wa Ethiopia na Évariste Ndayishimiye wa Burundi.

    Viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria ni Romuald Wadagni wa Benin na Jean-Lucien Savi de Tové wa Togo, huku waalikwa wengine wakisubiri kuthibitishwa.

    Kiwanda cha Dangote East Africa Refinery kinatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu na kitakuwa kikisambaza bidhaa za mafuta zilizochakatwa kwa Kenya na nchi jirani za Afrika Mashariki.

    Mradi huo unalenga kupunguza utegemezi wa kanda hiyo kwa mafuta yanayoagizwa kutoka nje na kuhudumia masoko ya Kenya, Ethiopia, Sudan Kusini, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

    Mwenyekiti wa Dangote Group, Aliko Dangote, amesema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku.

    Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha zaidi ya lita milioni 100 za petroli, dizeli na mafuta ya ndege kila siku.

    Mradi huo unatarajiwa kuwa uwekezaji mkubwa zaidi wa Dangote Group katika sekta ya kusafisha mafuta nje ya Nigeria.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Maharamia wa Somalia waua wafanyakazi wa meli ya mafuta

    Wafanyakazi watano wa meli ya mafuta ya MT Honer 25 waliuawa na maharamia kabla ya vikosi vya usalama vya Puntland kuanzisha operesheni ya kuikomboa meli hiyo, naibu waziri wa habari wa Puntland ameambia BBC.

    Bile Qabowsade amesema vikosi vya Puntland vilianzisha operesheni ya kuirejesha meli hiyo chini ya udhibiti wa serikali, lakini maharamia walikuwa tayari wamewaua watu watano waliokuwa ndani yake.

    "Kwa bahati mbaya, maharamia walikuwa tayari wamewaua watu watano waliokuwa ndani kabla ya operesheni kuanza," alisema.

    Qabowsade alikanusha madai kwamba wafanyakazi hao waliuawa wakati wa mapigano kati ya maharamia na vikosi vya Puntland wakati wa operesheni hiyo.

    Kwa mujibu wa mamlaka za Puntland, waliofariki ni raia watatu wa Pakistan, mmoja wa India na mmoja wa Myanmar.

    Wafanyakazi wengine wanne walijeruhiwa, wakiwemo raia watatu wa Pakistan na mmoja wa India.

    Mamlaka za Puntland zilisema operesheni hiyo imekamilika na kwamba meli hiyo sasa iko salama chini ya udhibiti wa vikosi vya serikali.

    Maharamia 16 walikamatwa huku wengine wakitoroka na kuendelea kusakwa.

    Qabowsade pia alikanusha madai kuwa baadhi ya maharamia walisaidiwa kutoroka na vikosi vya Puntland.

    Vifo vya wafanyakazi hao vinaonekana kuwa vya kwanza vinavyohusishwa na maharamia wa Somalia katika zaidi ya miaka 10, kulingana na taarifa za mamlaka za Puntland. Serikali imekanusha madai kwamba waliuawa katika makabiliano kati ya vikosi vya usalama na maharamia wakati wa operesheni ya uokoaji.

    Pia unaweza kusoma

  5. China yaonya EU dhidi ya vita vya kibiashara

    China imeahidi kutoa "jibu thabiti" ili kulinda sekta zake za viwanda iwapo Umoja wa Ulaya (EU) utaendelea na mpango wa kuweka vizuizi dhidi ya kampuni au bidhaa za China.

    Wizara ya Biashara ya China ilitoa onyo hilo ikijibu taarifa za waraka wa pamoja ulioandaliwa na baadhi ya nchi wanachama wa EU, unaopendekeza kuanzishwa kwa chombo maalum cha kushughulikia kile kinachoelezwa kuwa biashara isiyo ya haki na kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya China.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumanne usiku, wizara hiyo ilisema mpango huo ni "hatua ya ulinzi wa soko na ya upande mmoja" ambayo inaweza kuvuruga uthabiti wa biashara kati ya China na EU.

    "Iwapo upande wa Ulaya utaendelea kufanya mazungumzo na mashauriano na China huku ukiongeza shinikizo dhidi yake, hatua hiyo itadhoofisha kwa kiasi kikubwa imani ya pande zote na kuathiri mchakato mzima wa mazungumzo," wizara hiyo ilionya.

    Gazeti la serikali la Global Times liliripoti kuwa China inaweza kujibu kupitia hatua mbalimbali za sera, ikiwemo uchunguzi dhidi ya ubaguzi wa kibiashara, ukaguzi wa usalama wa sekta za viwanda na usambazaji, pamoja na kuchunguza athari za ruzuku zinazotolewa na serikali za kigeni.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Marekani yatoa zawadi nono kwa taarifa za makamanda wa Iran

    Kitengo cha Usalama wa Kitaifa cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kimetangaza zawadi ya jumla ya dola milioni 15 kwa taarifa zitakazosaidia kuwatambua au kubaini walipo makamanda watatu wa ngazi za juu wa Kikosi cha Anga na Anga za Juu cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC).

    Katika tangazo lililotolewa Jumanne chini ya programu ya "Rewards for Justice", jina la kwanza lililotajwa ni Brigedia Jenerali Abdullah Mehrabi, mkuu wa Shirika la Utafiti wa Kijeshi na Kujitegemea la Kikosi cha Anga cha IRGC.

    Jina la pili ni Ahmad Jafarabadi, aliyetajwa kama kamanda mwandamizi wa Kikosi cha Anga cha IRGC anayesimamia shughuli za operesheni za kikosi hicho. Hata hivyo, haijabainika wazi ikiwa anahusiana na Brigedia Jenerali Ali Jafarabadi, kamanda wa mpango wa anga za juu wa kikosi hicho, au ni mtu mwingine.

    Ali Asghar Norouzi, naibu kamanda anayehusika na utayari na kusaidia kikosi cha IRGC, ndiye mtu wa tatu ambaye Marekani imeahidi kutoa zawadi kwa taarifa zitakazosaidia kumtambua au kubaini alipo.

    Siku hiyo hiyo, Marekani pia iliweka vikwazo dhidi ya watu na taasisi 10 zinazohusishwa na Wizara ya Ulinzi ya Iran.

    Orodha hiyo, iliyotangazwa na Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) ya Wizara ya Fedha ya Marekani, inajumuisha raia kutoka Iran, Mexico, China na Pakistan.

    Hatua hiyo inakuja baada ya kusambaratika kwa makubaliano ya Islamabad ambayo yalitarajiwa kufungua njia kuelekea makubaliano ya kudumu ya amani kati ya Iran na Marekani.

    Tangu kushindwa kwa makubaliano hayo, Marekani imeongeza shinikizo kwa Iran kupitia vikwazo vipya, ikiwemo hatua zinazolenga safari za kimataifa za mashirika ya ndege ya Iran.

    Soma Pia:

  7. Dangote na Ruto kuzindua kiwanda cha mafuta cha dola bilioni 16 Kenya

    Bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote, na Rais wa Kenya William Ruto wanatarajiwa kuzindua rasmi Jumatano ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha dola bilioni 16, mradi unaolenga kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya bidhaa za petroli katika Afrika Mashariki.

    Dangote anataka kuiga mafanikio ya kiwanda chake cha kusafisha mafuta chenye uwezo wa mapipa 700,000 kwa siku nchini Nigeria, wakati mataifa kama Kenya na Uganda yakijiandaa kuanza uzalishaji wa mafuta ghafi.

    Kiwanda hicho kinatarajiwa kukamilika mwaka 2030, kikilenga kupunguza gharama za mafuta katika kanda na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa za mafuta zilizokwisha kusafishwa.

    "Ukiangalia Afrika Mashariki, na hata nchi nyingi kati ya 54 za Afrika, bado zinaagiza bidhaa za petroli kutoka nje," Dangote aliwaambia waandishi wa habari jijini Nairobi Jumanne.

    "Tunataka kuhakikisha tunajitosheleza katika bidhaa tunazotumia," aliongeza.

    Dangote amezipa serikali za nchi za kanda hiyo nafasi ya kumiliki kwa pamoja asilimia 30 ya hisa za kiwanda hicho.

    Mshauri Mkuu wa Uchumi wa Rais Ruto, David Ndii, amesema mahitaji ya bidhaa za petroli katika Afrika Mashariki yanakadiriwa kuwa kati ya tani milioni 20 na milioni 30 kwa mwaka.

    Kwa mujibu wa wataalamu wa sekta hiyo, kukidhi mahitaji hayo kutahitaji uwezo wa kusafisha zaidi ya mapipa milioni moja ya mafuta kwa siku.

    Soma Zaidi:

  8. Walowezi wa Israel wazuia familia ya Wapalestina kurejea nyumbani

    Zaidi ya walowezi 100 wa Israel wameshambulia kijiji cha Jalud katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, na kuzuia familia ya Kipalestina kurejea nyumbani huku wakikabiliana na wanajeshi wa Israel, kwa mujibu wa mashahidi.

    Nyumba mbili za familia ya Tubasi katika kijiji hicho zilichukuliwa na walowezi wiki kadhaa zilizopita, wakati mashambulizi ya walowezi na unyakuzi wa ardhi yakiongezeka, hali ambayo imezua lawama kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

    Familia hiyo ilikuwa imehifadhiwa sehemu nyingine ndani ya kijiji hicho, kilicho kaskazini mwa mji wa Ramallah, hadi jeshi la Israel lilipokubali kuisindikiza kurejea nyumbani usiku wa Jumatatu na kuipa ulinzi dhidi ya walowezi.

    Hata hivyo, mashahidi walisema kuwa dakika chache baada ya familia hiyo kufika nyumbani, kundi la walowezi zaidi ya 100 lilifika eneo hilo.

    Walowezi hao walichoma nyumba hizo moto, wakaziba barabara za kuingia eneo hilo na kuwarushia mawe maafisa wa Israel. Jeshi la Israel limesema maafisa wake watatu walijeruhiwa katika vurugu hizo.

    "Kutokana na ghasia hizo, operesheni ya kuirejesha familia hiyo nyumbani haikukamilika," jeshi la Israel lilisema katika taarifa.

    Kwa mujibu wa mashahidi, wanajeshi waliwaelekeza wanafamilia hao kupanda juu ya paa la nyumba walipoingia walowezi, kabla ya kuwaondoa eneo hilo wakati makabiliano yalipozidi kuwa makali.

    Tukio hilo limeibua tena maswali kuhusu uwezo wa jeshi la Israel kudhibiti walowezi wanaopata ujasiri zaidi chini ya serikali ya mrengo wa kulia ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambayo imesimamia upanuzi wa makazi na vituo vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi.

    Soma Zaidi Hapa:

    Walowezi wa Israel wananyakua ardhi za Wapalestina wakati huu wa vita

  9. Real Madrid yamnyemelea nahodha wa Liverpool Van Dijk

    Real Madrid wanafikiria kumsajili nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk, mwenye umri wa miaka 35, huku beki huyo wa Uholanzi akitarajiwa kuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu. (Mundo Deportivo - in Spanish)

    Bayern Munich inatarajiwa kumpa mshambuliaji Mfaransa Michael Olise mkataba mpya hadi mwaka 2032, huku mkataba wake wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2029. (Bild - in German)

    Hata hivyo, klabu hiyo ya Ujerumani imepuuzilia mbali uwezekano wa kumsajili kipa wa Everton na timu ya taifa ya England, Jordan Pickford, mwenye umri wa miaka 32.(TeamTalk)

    Mshambuliaji wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ufaransa, Jean-Philippe Mateta, mwenye umri wa miaka 29, ni miongoni mwa wachezaji wanaolengwa na Manchester United huku klabu hiyo ikitafuta kuimarisha safu yake ya ushambuliaji. (TeamTalk)

    Manchester United pia inapanga kumpa beki wa England Luke Shaw, mwenye umri wa miaka 31, mkataba mpya, huku mkataba wake wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu. (Football Insider)

    Bayern Munich pia inamnyemelea beki Mfaransa Jules Koundé, mwenye umri wa miaka 27, huku mchezaji huyo akianza msimu akiwa hapewi kipaumbele katika kikosi cha Barcelona. (Sport - in Spanish)

    Tottenham Hotspur imeonyesha nia ya kumsajili beki wa Korea Kusini Kim Min-jae, mwenye umri wa miaka 29, kutoka Bayern Munich. (Sport - in Spanish)

    Beki wa zamani wa Manchester United, Matteo Darmian, 36, anatarajiwa kuanza mazoezi na Bologna Jumatano, baada ya kuachana na Inter Milan mwishoni mwa msimu uliopita. (Gianluca Di Marzio - in Italian)

    Pia unaweza kusoma:

  10. Qatar yashinikiza makubaliano ya amani kati ya Marekani na Iran

    Qatar imesema siku ya Jumanne kuwa ina matumaini juhudi zake za upatanishi kati ya Iran na Marekani zinaweza kuleta mafanikio, licha ya Rais wa Marekani Donald Trump kukanusha ripoti za vyombo vya habari zilizodai kuwa yuko tayari kulegeza vikwazo na kuachilia fedha za Iran zilizozuiwa ili kupata makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majed al-Ansari, amesema Doha inaendelea kubadilishana ujumbe kati ya pande hizo mbili kwa lengo la kupata mwafaka ambao unaweza kuzuia madhara zaidi ya mzozo huo.

    "Tunabadilishana ujumbe kati ya pande husika na tunafanya kazi ya kutafuta msingi wa pamoja ili kufikia makubaliano yatakayotuokoa sote dhidi ya athari za mzozo huu," alisema al-Ansari.

    Marekani na Iran hadi sasa zimashindwa kupata suluhu ya kumaliza vita vilivyoanza mwezi wa nane. Mazungumzo yalionekana kuongezeka wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita mjini New York, lakini hayajazaa matokeo kuhusu kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz.

    Qatar kwa mara nyingine imeibuka kama mpatanishi katika mzozo huo baada ya awali kusaidia kufanikisha makubaliano ya mwezi Juni yaliyosababisha kusitishwa kwa mapigano kwa muda mfupi. Maafisa wa Marekani na Iran walifanya mazungumzo tofauti na wapatanishi wa Qatar siku ya Jumatatu, ingawa haikufahamika kama mawasiliano zaidi yalifanyika Jumanne.

    Trump amesisitiza msimamo wake kwamba Iran haipaswi kuwa na silaha za nyuklia na kusema vita hivyo vitaisha hivi karibuni.

    Mzozo huo umeathiri uwezo wa kijeshi wa Iran na kudhoofisha zaidi uchumi wake, lakini Tehran imejibu kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba.

    Pia imezuia sehemu ya usafiri wa meli za mafuta katika Mlango Bahari wa Hormuz, hali iliyochangia kupanda kwa bei za nishati duniani.

    "Sijui kama wako tayari kujisalimisha, lakini watajisalimisha tu," Trump aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumanne.

    Aliongeza kuwa, "Wanapitia hali mbaya sana."

    Usiku wa Jumatatu, Trump alikanusha kupitia mtandao wake wa Truth Social ripoti za Axios na CNN zilizodai kuwa alikuwa tayari kutoa nafuu ya vikwazo na kuachilia fedha za Iran zilizozuiwa nje ya nchi kama sehemu ya makubaliano ya mwisho, kwa sharti kwamba Iran ionyeshe maendeleo ya wazi kuhusu suala la nyuklia.

    "Hii si kweli. Sijawapa chochote," aliandika Trump kwenye Truth Social.

    Soma Zaidi Hapa:

  11. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara.