Wanasiasa 7 barani Afrika wanaokabiliwa na mashtaka ya uhaini

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kesi za hivi karibuni zinazohusisha mashtaka ya uhaini au vitendo vinavyotishia usalama wa taifa, ambapo wanasiasa mashuhuri barani Afrika wamekuwa wakishtakiwa, zimeibua maswali kuhusu iwapo walio madarakani wanalinda kweli usalama wa taifa, au wanatumia mfumo wa haki kudhoofisha wapinzani wao wa kisiasa au watu wengine wanaoonekana kuwa tishio.

Katika kesi hizi, washtakiwa au wafuasi wao mara nyingi hudai kuwa mashtaka hayo yana misukumo ya kisiasa, huku wakikanusha tuhuma zinazowakabili.

Kwa upande mwingine, viongozi wa serikali wanasema kuwa mahakama ni huru na mamlaka za sheria zina uhuru wa kumchukulia hatua mtu yeyote wanayeona anapaswa kushtakiwa.

Hizi ni kesi saba za hivi karibuni zinazohusisha watu wanaotuhumiwa kwa uhaini.

1. Burundi: Alain-Guillaume Bunyoni

Alain-Guillaume Bunyoni, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Burundi, alihukumiwa kifungo cha maisha mwezi Disemba mwaka wa 2023. Alishtakiwa kwa kujaribu kumuua rais kwa kutumia silaha, kujaribu kuipindua serikali iliyochaguliwa na wananchi, kuhujumu uchumi wa nchi pamoja na rushwa.

Bunyoni alikanusha mashtaka hayo, akidai kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi unaoonyesha alivyotekeleza makosa aliyotuhumiwa.

Moja ya mashtaka anayokabiliwa nayo, ni kujaribu Rais kwa kutumia silaha.

Hata hivyo, hukumu yake ilithibitishwa katika rufaa ya mwezi Juni 2024. Bunyoni aliachiliwa kwa dhamana kwa sababu za kiafya mwezi Machi 2026.

Kabla ya Jenerali Alain Guillaume Bunyoni kukamatwa, alikuwa miongoni mwa vigogo waliodumu kwa muda mrefu katika serikali ya CNDD-FDD, chama alichopigania wakati bado kilikuwa kundi la waasi katika kipindi cha miaka 10 cha mapigano kilichoishia mwaka wa 2003. Kukamatwa kwake kuliwafanya baadhi ya watu kujiuliza ikiwa kulihusiana na mzozo wa ndani wa kugombea madaraka katika chama hicho.

2. Rwanda: Victoire Ingabire

Mwanasiasa wa upinzani, Victoire Ingabire, alikamatwa tena mwezi Juni mwaka wa 2025.

Waendesha mashtaka wanamtuhumu kwa makosa ikiwemo kuunda kundi la kihalifu na kupanga njama za kuchochea machafuko miongoni mwa wananchi. Ingabire amekanusha tuhuma hizo na kusema kesi yake ina misukumo ya kisiasa.

Mamlaka za Rwanda zinasema alikamatwa kisheria kutokana na makosa anayodaiwa kutenda, na si kwa sababu ya misimamo yake ya kisiasa.

Victoire Ingabire aliachiliwa mwezi Septemba 2018 baada ya kukaa gerezani kwa miaka minane, kufuatia hukumu ya kifungo cha miaka 15 alichopewa baada ya kutuhumiwa kuwachochea wananchi kuipinga serikali, kuandaa kundi la waasi kwa ajili ya kuishambulia nchi, pamoja na kupuuzia au kupunguza uzito wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

3. DR Congo: Joseph Kabila

Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilimpea hukumu ya kifo Joseph Kabila, aliyekuwa rais wa nchi hiyo kwa miaka 18. Hukumu hiyo ilitolewa akiwa hayupo mahakamani mwezi Septemba mwaka 2025.

Kabila alishtakiwa kwa makosa yakiwemo uhaini, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na kushiriki katika mpango wa kuipindua serikali.

Waendesha mashtaka walimtuhumu kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 linalopigana na serikali ya Congo mashariki mwa nchi hiyo.

Kabila alikanusha mashtaka hayo, akisema kesi yake ina misukumo ya kisiasa. Hakuhudhuria kesi hiyo na hakuwa na wakili aliyemwakilisha.

4. Tanzania: Tundu Lissu

Tundu Lissu, mmoja wa viongozi mashuhuri wa upinzani nchini Tanzania, alikamatwa mwezi Aprili mwaka wa 2025 na kushtakiwa kwa uhaini. Hatua hiyo ilifuatia wito wake wa kutaka mageuzi ya sheria za uchaguzi, chini ya kaulimbiu: "Hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi."

Waendesha mashtaka wanasema kauli hiyo ililenga kuwachochea wananchi kuasi serikali. Lissu amekanusha tuhuma hizo, akisema kesi yake inalenga kunyamazisha upinzani.

Mamlaka za Tanzania, hata hivyo, zinakanusha kuwa kesi hiyo ina misukumo ya kisiasa.

Lissu alirejea nchini Tanzania mwaka wa 2020, miaka mitatu baada ya kunusurika jaribio la kuuawa ambapo alipigwa risasi mara 16. Baadaye alifanyiwa zaidi ya operesheni 20 nchini Kenya na Ubelgiji.

5. Uganda: Kizza Besigye

Kizza Besigye, mwanasiasa wa muda mrefu wa upinzani nchini Uganda, alishtakiwa kwa uhaini mwezi Februari mwaka 2025.

Waendesha mashtaka wanamtuhumu yeye pamoja na wengine kwa kupanga njama ya kuipindua serikali ya Rais Yoweri Museveni.

Besigye, ambaye amewahi kushindana na Museveni katika uchaguzi wa urais mara nne, amekanusha tuhuma hizo. Mawakili wake na wafuasi wake wanasema anaandamwa kwa sababu za kisiasa, huku mamlaka za Uganda zikisisitiza kuwa kesi hiyo inahusu makosa ya jinai.

6. Zambia: Brian Mundubile

Brian Mundubile, kiongozi wa upinzani nchini Zambia, pamoja na mgombea mwenzake katika uchaguzi, Makebi Zulu, wameshtakiwa kwa uhaini mwezi Agosti 2026, kwa mujibu wa wakili wao.

Mashtaka hayo yalifuatia uchaguzi wa urais uliokuwa na utata, ambapo Mundubile alishika nafasi ya pili nyuma ya Rais Hakainde Hichilema.

Awali, mamlaka hazikutoa maelezo mengi kuhusu kosa mahususi waliloshtakiwa.

Mundubile alikataa kukubaliana na matokeo ya uchaguzi na kusema kuwa tuhuma dhidi yake zilitengenezwa kwa lengo la kumuadhibu.

7. Sudan Kusini: Riek Machar

Riek Machar, kiongozi wa upinzani nchini Sudan Kusini, alishtakiwa mwezi Septemba mwaka wa 2025 kwa makosa ya uhaini, mauaji na uhalifu dhidi ya binadamu.

Serikali inamtuhumu kuhusika katika shambulio lililofanywa na kundi la wapiganaji kutoka jamii ya Nuer dhidi ya wanajeshi wa serikali katika eneo la Nasir.

Chama chake kimekanusha kwamba Machar alikuwa na mamlaka juu ya wapiganaji hao, kikisema kesi hiyo inaweza kuhatarisha zaidi makubaliano ya amani ya nchi ambayo tayari yako katika hali tete.

Mashtaka ya uhaini hayajitokezi barani Afrika pekee. Kesi zinazohusisha uhaini au vitendo vinavyotajwa kuwa vinahatarisha usalama wa taifa zimewahi kutumika pia bara Asia, Ulaya na Amerika.

Serikali zinasema sheria hizo ni muhimu kwa ajili ya kulinda taasisi za taifa na katiba za nchi.

Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaonya kwamba makosa yanayohusisha usalama wa taifa, iwapo hayatafafanuliwa kwa uwazi katika sheria, yanaweza kutumiwa kuwazuia wanasiasa kutekeleza shughuli zao za kisiasa kwa amani