Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump akanusha madai ya kuilegezea Iran vikwazo

Akizungumza kupitia mtandao wake wa Truth Social Jumatatu jioni, Trump alisema hajatoa ahadi yoyote kwa Iran na akaitaja ripoti hiyo kuwa ya uongo.

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Tanzania: Waziri Katambi awasihi madereva kuepuka vurugu wakati wa mgomo

    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amefika katika Stendi ya Mabasi ya Magufuli jijini Dar es Salaam na kuzungumza na madereva wanaopinga baadhi ya changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

    Katambi amewataka madereva kutokubali kushinikizwa kufanya vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu nchini, akisema mgogoro huo unaweza kuathiri uchumi wa taifa.

    “Msikubali kushinikizwa kuvuruga amani, kwani shughuli hii inaathiri uchumi wa nchi. Yeyote anayefanya vurugu, jitenge naye; mjue tunawaona,” alisema Katambi.

    Aidha, Katambi amewataka madereva kutoruhusu suala hilo kutumiwa kwa maslahi ya kisiasa, akisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhu bila kuingiza siasa katika changamoto zinazowakabili.

    “Lakini isije mtu akatumia hadhara hii kwa maslahi yake. Hatupaswi kuiingiza kisiasa,” alisema.

    Waziri huyo pia amewataka madereva na wananchi kwa ujumla kuepuka uharibifu wa mali wakati wa kushughulikia madai yao.

    “Tujiepushe kuharibu mali kwa sababu ya hili,” alisisitiza Katambi.

    Kuhusu changamoto zilizowasilishwa na madereva, Katambi amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imepokea hoja zao na iko tayari kuzifanyia kazi.

    “Kutokana na changamoto mlizowasilisha, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani inawahakikishia dhamira ya kutatua changamoto,” alisema Katambi.

    Kauli ya Katambi imekuja wakati kukiwa na mvutano kuhusu mfumo wa pointi za leseni, ambao madereva wanaupinga wakidai unaathiri ajira zao.

    Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Waziri Katambi kujiuzulu, kikimtuhumu kushindwa kuchukua hatua kwa wakati na kusikiliza malalamiko ya madereva kuhusu mfumo huo.

    ACT Wazalendo pia imesema inaunga mkono madereva katika kupinga kile inachokiita ukandamizaji na kusimamia usalama wa ajira zao.

  2. Kenya: Rais Ruto amewakosoa wanaojaribu kukwamisha mradi wa Dangote

    Rais William Ruto amewaonya watu anaowatuhumu kujaribu kuvuruga ujenzi wa kiwanda cha kusafishia mafuta cha Dangote huko Lamu, mradi unaokadiriwa kugharimu Sh2.2 trilioni.

    Akizungumza Kilifi Jumanne wakati wa hafla ya utoaji wa hati miliki, Ruto amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kubadilisha uchumi wa Kenya na kuvutia uwekezaji mkubwa wa kigeni.

    “Kesho, Mungu akipenda, tutafanya rasmi uzinduzi wa kiwanda cha kusafishia mafuta cha Lamu,” alisema Ruto.

    Ruto amewaonya wanaopinga uwekezaji huo dhidi ya kujaribu kuvuruga mradi huo kwa kuweka masharti mbalimbali, ikiwemo kudai hisa katika kiwanda hicho.

    “Safari hii hamtafanikiwa kutudanganya wala kutupotosha,” alisema Rais Ruto.

    Ruto pia aliwashutumu watu aliowaita “madalali” kwa kuchangia kupotea kwa baadhi ya uwekezaji mkubwa nchini Kenya hapo awali. Alitoa mfano wa jaribio la awali la Dangote kujenga kiwanda cha saruji nchini Kenya, pamoja na uamuzi wa kupitisha bomba la mafuta ghafi la Uganda kupitia Tanzania badala ya Kenya.

    Rais anatarajiwa kuongoza hafla ya uzinduzi wa mradi huo Lamu Jumatano.

    Kiwanda hicho, kinachoungwa mkono na mfanyabiashara wa Nigeria Aliko Dangote, kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku.

  3. Dangote apuuzia amri ya mahakama inayotishia ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta Lamu

    Mwenyekiti wa Dangote Group na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote, ameonekana kutotishwa na uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama unaotishia kusitisha ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta chenye thamani ya shilingi trilioni mbili za Kenya mjini Lamu.

    Akizungumza katika mkutano wa wawekezaji jijini Nairobi Jumanne, Septemba 19, Dangote alisema changamoto kama hizo za kisheria ni jambo la kawaida barani Afrika na akasisitiza kuwa mradi huo utaendelea.

    “Baadhi yenu huenda mmeona kwamba mahakama moja imetoa amri kwamba tusifanye ujenzi. Nilisema, hapana, hapana. Hili ni jambo la kawaida kwetu Afrika. Kwa kweli, hili ni dogo,” alisema Dangote.

    Aliongeza kuwa yuko tayari kukabiliana na yeyote atakayejaribu kuzuia mradi huo.

    Awali, Dangote Group ilisema shughuli katika eneo la mradi Lamu zinaweza kuathiriwa na uamuzi huo, lakini ikasisitiza kuwa mahakama haijasitisha hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi iliyopangwa kufanyika Jumatano, Septemba 30.

    Hata hivyo, kwa mujibu wa kampuni hiyo, pande zote zimeagizwa kutofanya shughuli katika eneo hilo hadi kesi hiyo itakaposikilizwa Oktoba 14.

    Kiwanda hicho cha Lamu kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafisha mafuta kwa kiwango kinacholenga kuiga mafanikio ya kiwanda cha Dangote chenye uwezo wa mapipa 700,000 kwa siku, kilichopo karibu na Lagos nchini Nigeria.

    Kiwanda cha Lagos kimeisaidia Nigeria kupunguza utegemezi wa uagizaji wa mafuta na kuanza kuongeza mauzo ya mafuta nje ya nchi. Tofauti na Nigeria, Kenya kwa sasa haina uzalishaji wa mafuta wa kibiashara.

  4. Maelfu ya Waburundi warejea nyumbani kutoka Kenya

    Takriban raia 7,000 wa Burundi wanaripotiwa kuwa wamerejea nchini kwao kufuatia msako dhidi ya wageni wanaoendesha biashara ndogo ndogo nchini Kenya, ulioanza mapema mwezi huu.

    Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari wa wawakilishi wa taasisi za serikali siku ya Jumanne, Carine Nduwayo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Burundi alisema kuwa hadi sasa, wanaume 6,309, wanawake 593 na watoto 86 walio chini ya umri wa miaka mitano wamekwisharejea nchini.

    Msako huo uliotarajiwa kuanza Septemba 7, kufuatia agizo la Rais William Ruto, ambaye katika mkutano aliokuwa amefanya awali alisema kuwa kuna baadhi ya biashara zilizokusudiwa kufanywa na Wakenya pekee.

    Hata hivyo, baadaye serikali ya Kenya ilifafanua kuwa wageni wanaoendesha biashara kwa mujibu wa sheria wako huru kufanya biashara nchini humo.

    Ufafanuzi huo ulitolewa baada ya mamia ya raia wa Burundi tayari kuanza harakati za kupata nyaraka za kusafiria, huku kukiwa na sintofahamu kuhusu iwapo wangeruhusiwa kuendelea kubaki nchini Kenya.

  5. Polisi Tanzania yatoa onyo kwa wanaozuia mabasi na malori barabarani

    Jeshi la Polisi Tanzania limewaonya watu au vikundi vinavyojaribu kuzuia mabasi na malori kuendelea na safari zao, wakati kukiwa na taarifa za vuguvugu la mgomo wa madereva katika baadhi ya mikoa nchini.

    Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumanne, Septemba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, CP Awadh Juma, amesema ni kosa kisheria kumzuia dereva kufanya kazi au kufanya hujuma dhidi ya vyombo vya usafiri na abiria.

    “Polisi wanaelekeza kuwa haitasita kuchukua hatua kali sana kwa mtu yeyote yule atakayebainika kuzuia gari, siyo kuzuia tu, hata kufanya kitu chochote ambacho ni kinyume cha Sheria dhidi ya mabasi hayo au kufanya hujuma yeyote dhidi ya madereva,” ameonya CP Awadh.

    Kuhusu taarifa zinazozunguka kuhusu mfumo wa pointi za leseni, CP Awadh amesema mfumo huo bado haujaanza kutumika. Amewataka wananchi na madereva kutokubali kuongozwa na taarifa zisizo sahihi zinazozagaa mitandaoni.

    Aidha, amewahakikishia wamiliki wa mabasi na malori pamoja na madereva kwamba usalama umeimarishwa, na kuwataka kuendelea na huduma zao bila hofu.

    Soma zaidi:

  6. Amnesty International yashutumu Jeshi la Mali na wapiganaji wa Urusi kwa kukiuka haki za kibinadamu

    Shirika la kutetea haki za kibinadamu Amnesty International imelishutumu Jeshi la Mali pamoja na wapiganaji wa Urusi kwa madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa operesheni dhidi ya makundi ya kijihadi.

    Ripoti hiyo inasema wanajeshi wa Mali na wapiganaji wanaohusishwa na Wagner, kundi la kijeshi la Urusi, waliwaua raia kinyume cha sheria, kuwatesa watu waliokuwa kizuizini na kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kati ya mwaka 2023 na 2025.

    Haya ni madai mapya yanayoongeza mjadala kuhusu mkakati wa usalama wa Mali na madhara ambayo vita dhidi ya makundi ya kijihadi imewasababishia raia.

    Amnesty inasema angalau raia 34 waliuawa wakati wa operesheni za kijeshi katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Mali. Pia inasema baadhi ya waliokuwa kizuizini walipigwa, walipigwa shoti za umeme na kufanyiwa aina nyingine za mateso.

    Amnesty pia inadai kuwa mashambulizi mawili ya ndege zisizo na rubani yaliua watu wasiopungua 23, wakiwemo watoto watano. Shirika hilo linasema halikupata ushahidi wa kuwepo kwa mashambulizi ya kijeshi katika maeneo yaliyoshambuliwa.

    Amnesty inataka uchunguzi huru ufanywe kuhusu madai hayo. Hadi sasa, serikali ya kijeshi ya Mali haijatoa majibu kuhusu tuhuma hizo.

  7. Burundi: Jeshi lathibitisha wanajeshi wawili kuzuiliwa Kongo

    Msemaji wa Jeshi la Burundi, Brigedia Jenerali Gaspard Baratuza, amethibitisha kwamba Meja Jérémie Nitunga na Kapteni Félicien Kanjori, wanajeshi wawili wa Burundi, walikamatwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini amekanusha kwamba walizuiliwa Kinshasa.

    Akijibu swali la mwandishi wa habari katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ngozi siku ya Jumanne, Baratuza alisema kuwa wanajeshi hao walikuwa katika makao makuu ya jeshi mjini Baraka, Kivu Kusini, ambako uchunguzi ulikuwa ukiendelea.

    Alisema wanajeshi hao walienda katika kambi ya kijeshi na kuanza kupiga picha za eneo hilo. Kitendo hicho ndicho kilichosababisha wakamatwe ili kubaini sababu iliyowafanya wapige picha hizo.

    Baratuza alisema Jeshi la Burundi linafuatilia kwa karibu uchunguzi huo na kuwaomba watu wasubiri matokeo ya uchunguzi, kwa kuwa huo ni utaratibu wa kawaida wa kijeshi.

    Kauli hiyo imekuja baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanajeshi hao walikamatwa na jeshi la DRC kwa tuhuma za kuwa watoa taarifa wa Rwanda, kisha wakapelekwa Kinshasa na kuzuiliwa huko. Taarifa hizo pia zilidai kwamba Jeshi la Burundi halikuwa likichukua hatua yoyote kuhusu suala hilo.

    Wakati huo huo, Baratuza amekanusha pia taarifa kwamba wanajeshi wa Tanzania waliingia Burundi wakiwa wamevalia sare za kijeshi za Burundi ili kusaidia katika mapigano nchini DRC.

    Baratuza pia alikanusha taarifa kwamba wanajeshi wa Tanzania waliingia Burundi wakiwa wamevalia sare za kijeshi za Burundi ili kusaidia Burundi katika mapigano nchini DRC.

    Alisema Jeshi la Burundi lipo nchini DRC kihalali, hivyo hakuna sababu ya kuwaficha wanajeshi wake walioko nchini humo. Aliongeza kuwa hakuna makubaliano kati ya Burundi na Tanzania kuhusu kubadilishana wanajeshi.

  8. Iran yatoa taarifa kuhusu vikwazo vilivyowekwa dhidi ya ndege zake

    Msemaji wa serikali ya Iran alisema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba marufuku dhidi ya safari za ndege za Iran ni “ushahidi wa shinikizo kutoka Marekani.”

    Fatemeh Mohajerani alisema kuwa Iran imewasilisha malalamiko kwa mashirika ya kimataifa na inachukua hatua za kisheria na kidiplomasia.

    Mkuu wa Shirika la Usafiri wa Anga la Iran, Abuzar Shiroudi, alisema Jumatatu kwamba amewasilisha malalamiko rasmi kwa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga la Umoja wa Mataifa (ICAO), akipinga vikwazo vilivyowekwa dhidi ya safari za ndege za Iran.

    Shiroudi alisema malalamiko hayo yaliambatanishwa na nyaraka zinazoeleza athari za vikwazo hivyo kwa safari za ndege za Iran.

    Tangu wiki iliyopita, wakati vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya mashirika ya ndege ya Iran vilipoanza kutekelezwa, viwanja vya ndege katika nchi kadhaa vimesitisha au kuweka vizuizi kwa safari za mashirika ya ndege ya Iran.

  9. Ukraine yadai Korea Kaskazini yaongeza maelfu ya wanajeshi kusaidia Urusi

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, amesema zaidi ya wanajeshi 8,000 wa Korea Kaskazini kwa sasa wako katika eneo la Urusi, huku maandalizi yakiendelea ya kutuma wanajeshi wengine 10,000 kusaidia vita dhidi ya Ukraine.

    Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Zelensky alisema taarifa mpya za kijasusi zinaonyesha wanajeshi hao wanachaguliwa kwa ajili ya mafunzo kabla ya kupelekwa Urusi.

    Mnamo mwezi Agosti, Zelensky alisema hadi wanajeshi 50,000 wa Korea Kaskazini wanaweza kutumwa kupigana upande wa Urusi, na kuitaka Korea Kusini kuongeza msaada wake kwa Ukraine, hususan katika ulinzi wa anga.

    Korea Kusini ilitangaza mwezi Julai kifurushi cha msaada wa dola milioni 100 kwa Ukraine, ingawa hakikujumuisha silaha za kivita.

    Kauli zake zinakuja wakati wa mvutano wa kidiplomasia kati ya Kyiv na Seoul kufuatia tangazo la Ukraine wiki iliyopita kwamba imewahamishia Korea Kusini wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini waliokamatwa vitani. Korea Kusini ilieleza kusikitishwa na tangazo hilo, ikisema kulikuwa na makubaliano ya kuweka uhamisho huo siri.

    Kwa mujibu wa makadirio ya Ukraine na Korea Kusini, Korea Kaskazini imepeleka kati ya wanajeshi 14,000 na 15,000 kusaidia vita vya Urusi tangu mwaka 2024. Wengi wao walitumwa katika eneo la Kursk kusaidia kuzuia mashambulizi ya majeshi ya Ukraine.

    Soma Zaidi:

  10. Amnesty yatuhumu jeshi la Mali na wapiganaji wa Urusi kwa mauaji ya raia

    Jeshi la Mali na wapiganaji wa Urusi wanatuhumiwa kuwaua raia, kuwatesa mahabusu na kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kinyume cha sheria, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Amnesty International kuhusu athari za vita dhidi ya wanajihadi nchini humo.

    Shirika hilo linasema watu wasiopungua 34 waliuawa kinyume cha sheria wakati wa operesheni za kijeshi katika maeneo saba ya mikoa ya Ségou, Mopti na Timbuktu.

    Uchunguzi wake unaeleza visa vya watu kupigwa risasi walipokuwa wakikimbia au baada ya kukamatwa, pamoja na raia kufanyiwa ukatili mkubwa ikiwemo kupigwa, kuzamishwa majini, kupewa shoti za umeme na aina nyingine za mateso.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, takribani mahabusu watano walifariki wakiwa kizuizini kutokana na mateso au mazingira mabaya ya mahabusu.

    Amnesty inadai ukiukaji huo ulifanywa na wanachama wa vikosi vya usalama vya Mali pamoja na wapiganaji wa kundi la Wagner la Urusi wakati wa operesheni zilizofanyika kati ya mwaka 2023 na 2025.

    Waathiriwa wengi waliotambuliwa walitoka katika jamii za Fulani, Waarabu na Tuareg, hali inayozua wasiwasi kuwa huenda walilengwa kutokana na kabila lao au kuishi katika maeneo yenye shughuli za makundi yenye silaha.

    Shirika hilo pia linadai mashambulizi mawili ya ndege zisizo na rubani yaliyofanywa na jeshi la Mali mwaka 2025 yaliua watu wasiopungua 23, wakiwemo watoto watano. Shambulizi moja linadaiwa kulenga soko la Ejdeir na jingine nyumba ya familia mjini Tangata. Amnesty inasema haikupata ushahidi wowote wa kuwepo kwa wapiganaji au malengo ya kijeshi katika maeneo hayo.

    Madai hayo yanajitokeza wakati serikali ya kijeshi ya Mali ikiendelea kukabiliana na uasi wa wanajihadi baada ya kuvunja ushirikiano wake wa muda mrefu wa kijeshi na Ufaransa na kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na Urusi.

    Kundi la Wagner liliondoka rasmi Mali mwezi Juni 2025, lakini nafasi yake ilichukuliwa na kikosi cha Africa Corps cha Urusi.

    Amnesty inasema iliwasilisha matokeo ya uchunguzi wake kwa mamlaka za Mali tarehe 3 Agosti, lakini haikupokea majibu kabla ya kuchapisha ripoti hiyo Septemba 29, 2026. Shirika hilo linataka uchunguzi huru ufanyike na hatua zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na ukiukaji huo.

    Utawala wa kijeshi wa Mali bado haujatoa majibu kuhusu ripoti hiyo wala madai yaliyomo ndani yake.

    Soma Zaidi:

  11. Anthropic yaonya AI inaweza kutishia uwepo wa binadamu

    Kampuni ya akili bandia ya Anthropic imewaonya wawekezaji wake kwamba teknolojia ya AI inaweza kuleta manufaa makubwa duniani, lakini pia inaweza kusababisha madhara makubwa au hata kutishia uwepo wa binadamu iwapo haitadhibitiwa kwa usahihi.

    Katika hati yake ya kujiandaa kuorodheshwa sokoni (IPO), kampuni hiyo imesema mifumo yake ya AI inaweza kuonyesha tabia za kujihifadhi, zikiwemo kujaribu kuepuka kuzimwa, kuficha au kupotosha taarifa, na hata kuonyesha mienendo inayofanana na usaliti au ulaghai wa kulazimisha watu kufanya jambo fulani.

    Anthropic imesema kuwa kadri inavyoendelea kutengeneza mifumo yenye uwezo mkubwa zaidi na kupanua matumizi yake, ndivyo hatari ya mifumo hiyo kusababisha madhara inavyoongezeka. Kampuni hiyo imeeleza kuwa AI inaweza kuwa na athari kubwa kwa jamii sawa na mapinduzi ya viwanda au ugunduzi wa umeme, lakini pia inaweza kusababisha uharibifu usioweza kurekebishwa ikitumiwa vibaya.

    Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni uwezo wa mifumo ya AI kutambua inapofanyiwa majaribio ya usalama na kubadili tabia yake, jambo ambalo linaweza kufanya tathmini ya usalama kuwa ngumu zaidi. Kampuni hiyo pia imeonya kuwa wakati mwingine mifumo hupata uwezo mpya usiotarajiwa wakati wa mafunzo ambao unaweza kugunduliwa tu baada ya kuanza kutumika.

    Onyo hilo linakuja wakati kampuni za AI, zikiwemo Anthropic na OpenAI, zikiendelea kukabiliwa na maswali kuhusu usalama wa teknolojia hiyo baada ya matukio kadhaa ambapo mifumo ya majaribio ilionyesha tabia zisizotarajiwa.

    Anthropic, ambayo inajitangaza kama kampuni inayoweka kipaumbele kwenye usalama wa AI, ilitumia karibu kurasa 80 za hati yake ya IPO kueleza hatari mbalimbali zinazohusiana na teknolojia hiyo, idadi kubwa kuliko sehemu iliyoeleza shughuli zake za biashara.

    Aidha, mtafiti wa usalama wa AI wa kampuni hiyo, Evan Hubinger, amewahi kusema kuwa anaona uwezekano wa zaidi ya asilimia 10 kwamba AI inaweza kusababisha vifo vya binadamu katika kipindi cha miaka 10 ijayo, akisisitiza wasiwasi unaoongezeka kuhusu hatari zinazoweza kuletwa na mifumo ya AI yenye uwezo mkubwa.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Mcheza dansi Nigeria afukuzia rekodi ya dunia

    Mcheza dansi kutoka Nigeria anajaribu kuweka rekodi mpya ya dunia kwa kucheza bila kusimama kwa siku saba mfululizo.

    Benjamin Daniel, anayejulikana kama Ben Dancer, analenga kucheza kwa saa 168, ikiwa ni saa 41 zaidi ya rekodi ya sasa.

    Shirika la Guinness World Records bado halijathibitisha iwapo jaribio hilo linakidhi vigezo vya kutambuliwa rasmi kama rekodi ya dunia. BBC imewasiliana na shirika hilo kwa maoni zaidi.

    Katika siku za hivi karibuni, mamia ya vijana wamekuwa wakikusanyika katika uwanja wa Freedom Park jijini Lagos kumshangilia, huku wengine wakirekodi kila hatua yake na kushiriki kucheza dansi.

    Mmoja wa mashuhuda, Uche Anumudu, amesema ni jambo la kufurahisha kuona jinsi Ben Dancer alivyojitahidi kufikia hatua hiyo na kwamba anajivunia mafanikio yake.

    Rekodi ya sasa ya kucheza dansi kwa muda mrefu zaidi inashikiliwa na mchezaji wa India, Srushti Sudhir Jagtap, aliyefikia saa 127 mwaka 2023 akiwa na umri wa miaka 16.

    Ben Dancer mwenye umri wa miaka 33 amekuwa akifanya dansi kitaaluma kwa miaka 18. Jaribio lake lilianza tarehe 22 Septemba na iwapo atakamilisha saa zote 168 zilizopangwa, anatarajiwa kufikia lengo hilo mapema Jumanne.

  13. Juhudi za kusimamisha mradi wa Dangote Lamu zagonga mwamba mahakamani

    Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Malindi imekataa ombi la kusimamisha mradi uliopangwa wa kiwanda cha kusafisha mafuta wa Dangote wenye thamani ya takriban Sh2 trilioni katika kaunti ya Lamu.

    Uamuzi huo unafuatia kesi iliyowasilishwa na wakazi 133 wa Chandavai wanaopinga mradi huo kwa madai kwamba unatekelezwa kwenye ardhi wanayoitambua kuwa ya mababu zao.

    Katika uamuzi uliotolewa Septemba 25, Jaji Jane Onyango alikataa kuidhinisha ombi hilo kama la dharura, lakini akaagiza hali ya sasa ibaki kama ilivyo hadi kesi itakaposikilizwa.

    Kwa mujibu wa agizo la mahakama, hali ilivyo katika kipande cha ardhi kinachojulikana kama Land Reference No. 13061 katika eneo la Manda Magogoni, Lamu, itabaki kama ilivyo hadi Oktoba 14, wakati ombi hilo litakaposikilizwa.

    Mahakama pia imeagiza walalamikiwa kupewa nyaraka za kesi na kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 14 kabla ya kusikilizwa kwa hoja za pande zote.

    Wakazi hao wanadai familia zao zimekuwa zikiishi na kutumia ardhi hiyo kwa vizazi vingi na kwamba hawajapatiwa fidia ya kutosha wala mpango wa wazi wa kuwahamisha.

    Kwa mujibu wa walalamikaji, sehemu za ardhi hiyo zinatumika kwa kilimo na ufugaji, huku pia zikiwa na makazi, misikiti, maeneo ya ibada za jadi na makaburi ya familia, jambo linalofanya eneo hilo kuwa muhimu kwa maisha na utambulisho wa jamii hiyo.

    Mradi huo wa Dangote unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumatano mjini Lamu.

    Kiwanda hicho cha kusafisha mafuta kinakadiriwa kugharimu takriban Sh2 trilioni (dola bilioni 16) na kinatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa zaidi vya aina yake barani Afrika, kikiwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku.

    Mradi huo unalenga kuhudumia soko la Kenya pamoja na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

    Soma Pia:

  14. Njia mbili za Mlima Kilimanjaro zafungwa kufuatia moto mpya

    Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imesitisha kwa muda matumizi ya njia za Lemosho na Londorosi za kupanda Mlima Kilimanjaro kufuatia kuzuka kwa moto mpya wa porini ndani ya hifadhi hiyo.

    Kwa mujibu wa taarifa ya TANAPA, moto huo ulizuka katika eneo la Sangarini-Kamwanga na ulikuwa ukienea kuelekea Shira ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.

    Watalii waliokuwa wamepanga kutumia njia hizo mbili sasa wataelekezwa kutumia njia za Machame, Marangu au Rongai.

    Wakati huo huo, juhudi za kuuzima moto huo zinaendelea kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori ya Enduimet, vikosi vya akiba, wakazi wa eneo hilo na wadau wengine wa utalii.

    Moto huo unazuka wiki chache baada ya moto mwingine kuzuka Septemba 3 katika eneo la Kikererwa karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya. Moto huo wa awali ulikuwa umedhibitiwa kwa zaidi ya asilimia 90 kufikia Septemba 5.

    TANAPA imesema usalama wa watumishi, watalii na wadau wengine unabaki kuwa kipaumbele chake kikuu, huku ikihakikisha kuwa rasilimali zote zinazopatikana zinaelekezwa kudhibiti moto huo.

    Soma Zaidi Hapa:

  15. Uingereza yajaribu kuzuia marufuku ya dizeli ya Trump

    Serikali ya Uingereza imesema inaendelea na mazungumzo na Marekani kuhusu uwezekano wa kusitishwa kwa usafirishaji wa dizeli, huku ikianza pia kujiandaa kwa hatua hiyo iwapo itatekelezwa.

    Waziri wa Fedha wa Uingereza, John Healey, amesema serikali inazungumza na maafisa wa Marekani huku ikihakikisha pia ina akiba ya kutosha ya dizeli nchini humo.

    Bei za dizeli nchini Uingereza zilifikia kiwango kipya cha juu siku ya Jumatatu kutokana na shinikizo la upatikanaji wa mafuta linalochangiwa na mzozo unaohusisha Marekani, Israel na Iran pamoja na vita vya Ukraine.

    Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kupiga marufuku usafirishaji wa dizeli kwenda nje ya nchi ili kupunguza bei za mafuta kwa watumiaji wa ndani wa Marekani, akisema mwishoni mwa wiki kwamba suala hilo linafuatiliwa kwa umakini mkubwa.

    Akizungumza kando ya mkutano wa chama cha Labour mjini Liverpool, Healey amesema Uingereza inaendelea kushirikiana kwa karibu na Marekani katika kutafuta suluhisho la kidiplomasia litakalosaidia kupunguza mvutano na kumaliza mapigano yanayohusisha Iran.

    Uingereza hutegemea Marekani kwa karibu theluthi moja ya mahitaji yake ya dizeli kutoka nje, na wachambuzi wanaonya kuwa marufuku yoyote ya usafirishaji inaweza kusababisha bei kupanda zaidi.

    Soma Pia:

  16. Manchester City yaapa kupambana na hukumu ya mashtaka 115

    Mtendaji Mkuu wa Manchester City, Ferran Soriano, ametuma ujumbe wenye msimamo mkali kwa viongozi wa vilabu vingine baada ya klabu hiyo kupatikana na hatia kwa sehemu kubwa ya mashtaka yaliyoletwa dhidi yake na Ligi Kuu ya England.

    Kwa mujibu wa taarifa, Soriano alizungumza wakati wa mkutano wa bodi ya European Football Clubs mjini Copenhagen kabla ya mkutano mkuu wa mashirika hayo siku ya Jumanne.

    Akinukuliwa na Press Association, Soriano alisema Manchester City itaendelea kupinga mashtaka hayo na kwamba mchakato huo bado una safari ndefu, akisisitiza msimamo uliotolewa pia na mwenyekiti wa klabu hiyo, Khaldoon Al Mubarak.

    Soriano alidai kuwa imechukua miaka minane kufikia hatua ya sasa tangu uchunguzi wa Ligi Kuu uanze mwaka 2018 na kwamba suala hilo bado litachukua muda mrefu zaidi. Baada ya kauli hiyo, aliondoka kwenye mkutano bila kujibu maswali ya wanahabari.

    Manchester City ilishtakiwa kwa ukiukaji mbalimbali wa kanuni za kifedha, ikiwemo madai ya kuongeza mapato ya udhamini kutoka kwa kampuni zinazohusishwa nayo na kufanya malipo mengine yasiyoonyeshwa kwenye hesabu rasmi ili kukwepa kanuni za kifedha.

    Ijumaa iliyopita ilibainika kuwa klabu hiyo ilipatikana na hatia kwa sehemu kubwa ya mashtaka 115 iliyokuwa ikikabiliwa nayo.

    Wakati huohuo, vilabu vya Ligi Kuu vinaendelea kutafuta ushauri wa kisheria kuhusu uwezekano wa kudai fidia, huku taarifa zikieleza kwamba Manchester City inapanga kukata rufaa.

    Adhabu zinazoweza kutolewa bado hazijatangazwa, lakini zinaweza kujumuisha kupokwa alama, kushushwa daraja au kutozwa faini kubwa.

    Kwa upande wake, mwenyekiti wa klabu hiyo Khaldoon Al Mubarak amesema ana imani Manchester City hatimaye itathibitisha kutokuwa na hatia katika kesi hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Watu zaidi ya 80 watoweka baada ya utekaji mkubwa Nigeria

    Zaidi ya watu 80, wengi wao wakiwa wanawake, hawajulikani walipo kufuatia matukio mawili tofauti ya utekaji nyara yaliyotokea mwishoni mwa wiki kaskazini mwa Nigeria.

    Makundi yenye silaha yalivamia jamii za wakulima katika majimbo ya Niger na Zamfara.

    Takriban wakulima 47 walitekwa nyara katika Jimbo la Niger siku ya Jumamosi walipokuwa wakivuna karanga, kwa mujibu wa vyanzo vya eneo hilo.

    Siku iliyofuata, wanawake wapatao 40 waliripotiwa kutekwa katika Jimbo jirani la Zamfara.

    Wakazi wa Zamfara walisema pia nyumba kadhaa zilichomwa moto wakati wa shambulio hilo na kuonya kwamba huenda idadi ya waliopotea ni kubwa zaidi.

    Makundi wahalifu yenye silaha yamekuwa yakifanya mara kwa mara utekaji nyara na mashambulizi dhidi ya vijiji kaskazini mwa Nigeria, mara nyingi yakidai fidia ili kuwaachilia wale wanaowateka.

    Soma Zaidi:

  18. Man Utd na Arsenal zamnyatia nyota wa Porto

    Manchester United na Arsenal zote zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya beki wa kulia wa Ureno, Alberto Costa, mwenye umri wa miaka 22, anayekipiga Porto. Hata hivyo, zinakabiliwa na ushindani kutoka Paris St-Germain (PSG). (Caughtoffside)

    Manchester City itaweka bei kubwa kwa mshambuliaji wake wa Norway, Erling Haaland, 26, iwapo itashushwa daraja kutoka Ligi Kuu ya England kutokana na ukiukaji wa kanuni za kifedha. (Football Insider)

    Chelsea, Arsenal, Bayern Munich, Real Madrid na Barcelona ni miongoni mwa klabu zinazomnyatia Haaland na kufuatilia kwa karibu hali ya Manchester City kutokana na uwezekano wa klabu hiyo kupewa adhabu. (Fichajes - in Spanish)

    Winga wa zamani wa Chelsea na Manchester City, Raheem Sterling, amepewa ofa kwa klabu mbili za Ligue 1 nchini Ufaransa, lakini zote zimekataa kumsajili Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 31, ambaye kwa sasa ni mchezaji huru. (Foot Mercato - in French)

    Rais wa Besiktas, Serdal Adali, ameahidi kumsajili Joe Willock, 27, kutoka Newcastle mwezi Januari, akidai kiungo huyo Mwingereza tayari amechagua kuhamia Uturuki. (Talksport)

    Kocha wa zamani wa Newcastle, Eddie Howe, hatarajii kurejea katika ukocha wa Ligi Kuu ya England akiongoza klabu ya chini au zilizopo kwenye nafasi za kati kama Crystal Palace au Fulham. Badala yake, angependa kuinoa klabu kubwa ambayo haifanyi vizuri. (Telegraph - subscription required)

    Liverpool bado inamnyatia kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, Aurélien Tchouaméni, licha ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kusaini mkataba mpya wa muda mrefu na klabu hiyo ya La Liga msimu huu wa joto. (Teamtalk)

    Soma Zaidi:

  19. Trump akanusha madai ya kuilegezea Iran vikwazo

    Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha madai kwamba ameipa Iran ahadi ya kulegezewa vikwazo na kuachiliwa kwa fedha zilizozuiliwa nje ya nchi ili ikubali kufanya maridhiano kuhusu mpango wake wa nyuklia.

    Kauli hiyo inafuatia ripoti ya Axios iliyodai, ikinukuu maafisa wa Marekani, kwamba Trump alikuwa tayari kulegeza baadhi ya vikwazo dhidi ya Iran kwa masharti kwamba Iran ichukue hatua madhubuti kuhusu mpango wake wa nyuklia.

    Akizungumza kupitia mtandao wake wa Truth Social Jumatatu jioni, Trump alisema hajatoa ahadi yoyote kwa Iran na akaitaja ripoti hiyo kuwa ya uongo.

    Aidha, aliishutumu Axios kwa kuchapisha kile alichokiita habari za kutunga zinazochochewa na chuki dhidi yake.

    Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amesema Tehran imewasilisha mapendekezo kupitia wapatanishi wa Qatar yatakayowasilishwa kwa Marekani.

    Araqchi amesema anatarajia jibu la mwisho kutoka Marekani kupitia Doha siku ya Jumanne, huku juhudi za kidiplomasia za kumaliza mzozo huo zikiendelea.

    Amesema pia kwamba Iran imeifahamisha Marekani na jumuiya ya kimataifa kuhusu masharti yaliyowekwa na Kiongozi Mkuu wa Iran kwa ajili ya kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, lakini hakutoa maelezo zaidi.

    Araqchi ameongeza kuwa ikiwa Marekani ina nia ya kufikia makubaliano au suluhisho la amani, Iran tayari imewasilisha pendekezo lake.

  20. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 29/09/2026.