Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
WARIDI WA BBC: 'Nilitokwa na haja ndogo bila kukoma kwa miaka minne'
Kwa miaka mingi, aliishi kwa kujificha na ukimya usio kifani, alihisi aibu kutokana na kile alichokuwa anakipitia.
Kwa sababu ya nini?
Nasuri yaani fistula tatizo ambalo huathiri maelfu ya wanawake kila wakati hasa barani Afrika.
Shirika la afya ya uzazi la Umoja wa Mataifa - UNFPA na Wakfu wa Fistula wanakadiria kuwa visa vipya vya fistula 1,000 hadi 3,000 hutokea nchini Kenya kila mwaka.
Ugonjwa huu mara nyingi hutokana na kutoweza kupata matibabu ya dharura wakati mama mjamzito anapokuwa kwenye chumba cha kujifungua.
Katika Waridi wa BBC hii leo, Asha Juma amezungumza na Annifah Adhiambo ambaye amekabiliana na ugonjwa huu kwa miaka 4.
Annifah anasema siku ya kwenda kujifungua kila kitu kilikuwa sawa lakini ghafla akasikia madaktari wakinong'onezana neno ambalo lilimuacha na wasiwasi.
"Nilikuwa na uchungu kama kawaida, lakini nilivyoenda kujifungua nikasikia madaktari wakisema, mtoto amechoka sana inafaa niende kufanyiwa upasuaji na bahati mbaya mtoto alikuwa amechoka kiasi kwamba alitoka akiwa amekufa," Annifah anasema.
Kile ambacho Annifah hakukijua ni kuwa mtoto huyo alimuacha na ugonjwa wa fistula ingawa wakati huo hakujua ni nini. Lakini alichokuwa anakiona machoni pake kilikuwa kinamtia hofu.
"Nilikuwa ninaona damu ikitoka, haitoki peke yake, inatoka na maji fulani hivi, kitu kilichokuwa tofauti, hadi ninashangaa haya maji yanatoka wapi na ni maji ya nini na hayakuwa yameanza kutoa harufu ambayo ingenifanya nihisi kuwa ni mkojo," Annifah anasema.
'Sikuwa nanywa chai wala maji'
Na baada ya miezi miwili, Annifa ndio alijua kuwa kile anachokiona sio maji bali ni mkojo.
"Nilikuwa nimeenda kliniki kuangaliwa jinsi ninavyoendelea kwa sababu ya upasuaji, na hapo ndipo nilipomsimulia daktari kile ninachopitia. Moja kwa moja akaniarifu kuwa ni ugonjwa unaojulikana kama fistula lakini unatibika," Annifa anasema.
Annifah anazungumzia alichoanza kukumbana nacho baada ya kutoka hospitalini.
"Ninakumbuka tu kuona mkojo ikinitoka. Hayo maji yalikuwa yanatoka tu, siwezi kuhisi kwenda haja ndogo," Annifah anaongeza.
"Mikojo yangu ilikuwa inamalizikia mahali nimekaa. Nikiketi itatoka, nikisimama itatoka, nikitembea itatoka. Sikuwa ninahisi kwamba ndiyo hiyo inatoka bali nitahisi tu nimeloa," anakumbuka Annifah.
"Kwa miaka minne sikunywa chai wala maji. Ningekula chakula chochote lakini maji haikuwa rahisi ninywe kwa sababu nilifikiri kadiri ninavyokunywa maji ndivyo mikojo inavyotoka. Nilikuwa nikijiambia hivyo lakini huo haukuwa ukweli. Mikojo ilikuwa inatoka tu hata kama sijakunywa maji wala chai," anasema Annifah.
Annifah alitumia nini kujistiri?
"Mwanzo nilikuwa natumia pedi, lakini nikaja nikaona natumia nyingi zaidi, kwa sababu nikiiweka baada ya muda kidogo tu, inajaa, nikasema acha nitumie nepi, hali ikawa ile ile. Nikasema hapa lazima ninunue shuka za masai na nikazinunua sita. Hiyo ndiyo nilikuwa natumia," Annifah anasema.
"Kwangu nilikuwa na kiti changu peke yangu cha mbao. Hiyo shuka ndio nitaiweka juu, mikojo itoke tu. Nikihisi imejaa, naitoa naweka shuka nyingine," Annifah anakumbuka .
Annifah anasema kando na shuka za masai pia alikuwa na vitambaa vya pamba vinavyoweza kunyonya mikojo.
"Vitambaa hivi nilikuwa naviweka kwenye begi natembea navyo, na ikiwa pengine naenda mahali, nina vitumia.
"Nikiwa ndani ya nyumba, sikuwa navaa nguo. Nilikuwa naweza kuvaa fulana kisha upande wa chini nitajifunika. Nitakaa tu hapo mikojo itoke, ikishajaa, nabadilisha kisha naenda kuosha shuka," Annifah anasema.
Katika dunia, hakuna anayeweza kuishi peke yake Annifa aliweza vipi kukabliana na hali hii mbele ya rafiki zake.
"Marafiki walikuwa wakipiga simu nina waambia kuwa mtoto aliaga dunia lakini nilikuwa ninawajengea mazingira wasije nyumbani kwa sababu ya hali yangu ilivyo. Kuna rafiki yangu ambaye aliwahi kuja kunitembelea lakini siku hiyo nilijifanya ninaumwa sana hata siwezi kuketi," anasema Annifah.
Annifa alikuwa mgonjwa lakini ukweli ni kwamba hakutaka rafiki yake ajue kinachomsibu.
Upande wa yeye kuwatembelea, anasema alibadili mwenendo ikawa anapofika kwa wengine, atahakikisha anatumia muda mfupi iwezekanavyo na kuanza safari ya kurejea kwake.
Ni wakati gani alihisi kukata tamaa?
Annifah anasema kuna kipindi aliamua kwenda kijijini wakati tayari ameshajua kuwa ana ugonjwa wa fistula lakini hakujua kuwa unaweza kutibika. Na maswali yaliyokuwa yakimlaza macho aliamua kuyaelekeza kwa mama yake.
"Mama yangu aliniangalia na kusema ugonjwa kama huo alikuwa anauona kwa mabibi. Aliamini kuwa ni uchawi kwa sababu hakuwa amewahi kuona mwanamke kijana kama mimi akitokwa na haja ndogo," anasema Annifah.
Kulingana na Annifah, hali yake ilimfanya aanze kujifungia ndani ya nyumba peke yake.
"Ningeweka kufuli kwa ndani, mtu akija, atagusa kitasa kisha ataona kuwa siko. Lakini mimi niko ndani. Hata akipigia simu, ilikuwa na mlio wa kimya," anasema Annifah.
Kuna jirani yake mmoja aligundua kuwa mama huyo huwa anajifungia na alipo jaribu kuzungumza naye ili kutaka kujua tatizo ni nini. Annifah alikanusha madai hayo.
"Nilimwambia mimi huwa siko. Sina tatizo. Lakini aliniambia wazi wazi kwamba amegundua mimi huwa najifungia sana na kuonyesha wasiwasi kuwa siko sawa, Annifa anaongeza, mimi nilimficha ukweli na hata kama alijua nina tatizo, hakujua kutoka kwangu," Annifa anasema.
Familia ilivyosimama naye
Wakati Annifah yuko kwenye safari hii, anasema jinsi familia yake ya karibu ilivyokuwa imemshika mkono ni jambo ambalo hawezi kulisahau.
"Hali kwangu haikuwa mbaya kwa sababu familia ilinikumbatia," Annifah anasema.
Mama huyu anachukulia mfano wa shuka za masai alizokuwa anafua. Zilianza kutoa harufu ya mkojo wakati zikiwa kambani zinakauka.
"Kwanza nilikuwa nikiziosha na sabuni ya unga kisha naziweka manukato, kumbe ndiyo nimeita harufu mbaya. Kamba nzima itaanuka hadi ikabidi nianze kuzifua usiku badala ya mchana. Asubuhi na mapema mume wangu alikuwa anazitoa na kuziingiza ndani ya nyumba, kisha anazikunja na kuziweka vizuri.
"Mume wangu hakuwahi kukataa chakula changu wala kunionyesha kuwa mimi ni mchafu," Annifah anakumbuka.
Mkojo ilikuwa imemchoma hadi amegeuka kuwa mweupe. Lakini mumewe kila alipooa amefikia kiwango hicho, alimuomba watoke kwenda kutembea tembea mtaani.
"Yeye mwenyewe alikuwa ananiambia nisivae chochote. Kwa hiyo, ningetembea tu mikojo ikidondoka. Hakuna mahali tunaenda ila alikuwa anajaribu tu kunitoa fikra zangu kwa kile ninachopitia nisione kama ni changamoto kubwa," Annifah anaongeza.
Anachosema ni kwamba daima atamshukuru mume wake kwa kusimama na yeye kipindi anapitia magumu na kumpa nguvu ya kusonga mbele.
Safari ya matibabu
Safari ya matibabu ya Annifah ilianza kimiujiza tu, kwa tangazo alilolisikia kwenye radio kupitia simu yake ya mkononi.
"Hiyo siku nilisikia wakitangaza kambi ya matibabu ya fistula. Nikajiuliza, huu si ni ugonjwa unaonitatiza. Nikaendelea kufuatilia lakini taarifa hiyo baada ya muda mfupi ikawa imeshapita," Annifah anasema.
Bahati nzuri, walirudia tangazo hilo na hapo ndipo alipopata fursa ya kuchukua mawasiliano.
"Iliporudiwa tu, mimi huyo nikachukua kalamu. Nilichokuwa ninataka kusikia ni kama fistula inatibika na nichukue mawasiliano," Annifah anasema.
Lakini licha ya hatua hiyo, bado Annifah alikuwa na uwoga wa kupiga simu na kupata taarifa zaidi alizohitaji.
"Nilichukua namba ya simu nikapiga, mama ndio alichukua. Nikaanza kumueleza kuwa nina rafiki yangu ambaye anatokwa na haja ndogo, lakini ghafla aliangua kicheko. Akaniuliza, unajua nacheka nini? Nafurahi kwa sababu utatibika. Na pia huu si ugonjwa wa kuficha. Usiseme ni rafiki yako ilihali wewe mwenyewe ndiye mwenye tatizo. Utatibiwa na kurudi kama kawaida," Annifah anasema.
Mama huyu anasema maneno hayo yalimtia moyo na matumaini na kumpa tabasamu hata kabla ya kuanza kwa matibabu.
Na siku ilipofika, Annifah alikuwa wa kwanza kuwasili katika eneo la kambi ya matibabu.
"Nilipofika nilikuwa peke yangu hadi nikajiuliza, mbona mimi peke yangu ndiyo mwenye huu ugonjwa. Lakini baada ya muda kidogo, watu wengi walianza kuingia na hapo ndipo nilipogundua kuwa fistula sio kutokwa na mkojo peke yake," Anasema Annifah.
Kambi ya matibabu ilimfanya Annifah kujua kuwa wanawake wanaoteseka ni wengi kwa sababu alikutana hata na wenye fistula ya haja kubwa.
"Wakati nimechaguliwa kuwa kati ya watakaopata matibabu, nilikuwa nimechomeka sana hadi nimekuwa mweupe, hata singeweza kujiosha nijishike, nalihisi uchungu mwingi," anasema Annifah.
"Aliyeniangalia alisema tupa hivi vitambaa pale kwenye jalala. Na kama kuna vingine kwenye begi pia vitupe, nikapewa nepi, na hapo nikapata matumaini ya kupona, kizuri zaidi waliniambia nisikae nayo, nikiona tu nepi imejaa niitupe kwa sababu nilikuwa nimechomeka mno," Annifah anasema.
Annifah alitoka kwenye chumba cha upasuaji akiwa amewekewa mipira miwili. Na baada ya mwezi mmoja, alianza kuona matokeo.
"Ulitolewa mpira wa kwanza na siku ya kutolewa wa pili, nilimuona muuguzi akimuonyesha ishara mwenzake kuwa mambo yako sawa. Nilihisi vizuri. Akaniambia nikihisi kwenda haja ndogo, nisiende kwanza, nijizuie kwa saa tatu. Nikasema kama hili litanifanya nirudi kuwa sawa, nitajizuia, Aniffah anasema.
Ujumbe wa Annifah kwa wanaopitia ugonjwa huu ni kwamba fistula si uchawi na unatibika kwa urahisi sana mradi tu umepata matibabu stahiki.
Ushauri wa Daktari
BBC Swahili ilipata fusra ya kuzungumza na daktari bingwa wa ugonjwa wa fistula Daniel Oluoch, ambaye alielezea mazingira gani ambayo yanaweza kumueka mama katika hatari ya kupata ugonjwa wa fistula.
"Kutoweza kupata matibabu ya dharura wakati anapokuwa kwenye chumba cha kujifungua kwa sababu mtoto anajifinya kwenye mifupa na kusababisha tundu kujitokeza kwenye sehemu ya siri," anasema Daktari Oluoch.
Tatizo la fistula linaweza kutambulika wakati mama hawezi kuzuia mikojo au haja kubwa. Daktari anasema fistula inaweza kuzuiwa na pia kutibika.
"Kuzuia ni kuweza kuhakikisha kwamba kina mama wanapata huduma ya dharura wakati wanapotaka kujifungua. Hiyo itachangia pakubwa kupunguza ama kuzuia fistula.
"Na wakati fistula inapojitokeza, ni vizuri kina mama kufika hospitalini, waweze kuangaliwa, na matibabu yapo ambayo ni kupitia njia ya upasuaji ili kuziba lile tundu ambalo linaleta matatizo," Daktari Oluoch anasema.
Daktari anaongeza kuwa matibabu yanategemea aina ya fistula lakini ya mkojo huchukua muda mrefu zaidi kupona.
Tatizo jingine ambalo amelibaini ni kutokuwa na maelezo ya kutosha ya wazi wazi kuhusu fistula jambo ambalo linachangia kina mama wengi wanaougua kutojua pa kwenda ili kupata matibabu.