Moja kwa moja, Marekani na Iran zashambuliana wakati Khamenei akizikwa

Marekani na Iran zimeendelea kushambuliana kwa mashambulizi yaliyodumu hadi Alhamisi, wakati Ayatollah Ali Khamenei alipokuwa akizikwa baada ya siku sita za shughuli za maombolezo.

Skip Video and continue reading
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Beldeen Waliaula

  1. Moto waua watu 28 katika kiwanda cha viatu China

    Mji wa Jinjiang, ulioko katika jimbo la Fujian nchini China, unaripotiwa kuzalisha takriban asilimia 20 ya viatu vya michezo vinavyotengenezwa duniani, jambo linaloufanya ujulikane kama "mji mkuu wa viatu" wa China.

    Chanzo cha picha, China News Service via Getty Images

    Takriban watu 28 wamefariki dunia kufuatia moto mkubwa ulioteketeza kiwanda cha kutengeneza viatu katika mji wa Jinjiang, kusini mashariki mwa China, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali, Xinhua.

    Picha za video zilizochapishwa na Xinhua zilionesha moshi mzito mweusi ukifuka kutoka kwenye jengo la kiwanda, huku baadhi ya watu wakionekana wamenaswa juu ya paa wakisubiri kuokolewa.

    Rais wa China, Xi Jinping, alisema moto huo umesababisha "vifo vingi", na kusisitiza kuwa yeyote atakayebainika kuwajibika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

    Mji wa Jinjiang, ulioko katika jimbo la Fujian, unajulikana kama "mji mkuu wa viatu" wa China kutokana na kuzalisha takribani asilimia 20 ya viatu vya michezo vinavyotengenezwa duniani.

    Moto huo ulizuka katika kiwanda cha Huiteng Footwear majira ya saa sita mchana kwa saa za eneo hilo siku ya Alhamisi.

    Mamia ya waokoaji walipelekwa eneo la tukio, huku zaidi ya watu 200 wakihamishwa kutoka kiwandani kwa usalama, kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya CCTV.

    Bado haijafahamika ni watu wangapi wamejeruhiwa.

    Mamlaka zilisema zaidi ya wafanyakazi 500 wa zimamoto na uokoaji walitumwa kuzima moto huo na kuwaokoa watu waliokuwa wamenaswa ndani ya kiwanda.

  2. Ofisi ya Benjamin Netanyahu yatangaza mazungumzo ya simu na Trump

    Trump na Netanyahu

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vyombo vya habari vya Israel viliripoti, vikinukuu ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kwamba Rais wa Marekani Donald Trump alijadili masuala yanayohusu Iran katika mazungumzo ya simu na Bw. Netanyahu siku ya Alhamisi.

    Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, pande hizo mbili zilijadili "hatua za pamoja katika nyanja mbalimbali," na Donald Trump alimpa taarifa Benjamin Netanyahu kuhusu hatua za Marekani dhidi ya Iran.

    Taarifa hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel pia ilieleza kuwa katika mazungumzo hayo, Netanyahu alikosoa kauli za Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na washirika wake wa karibu dhidi ya kuwepo kwa Taifa la Israel na kusisitiza umuhimu wa kudumisha maeneo ya usalama kando ya mipaka ya Israel na Lebanon.

    Uturuki iliandaa mkutano wa kilele wa NATO siku za hivi karibuni.

    Maafisa nchini humo wameishutumu mara kwa mara Israel kwa kuhujumu maelewano kati ya Marekani na Iran.

    Kwa upande mwingine, Israel imeeleza mara kwa mara wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kuuzwa kwa ndege za kisasa za kivita aina ya F-35 kwa Uturuki, suala ambalo lilisababisha kufutwa kwa ziara ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegsett nchini humo.

    Unaweza kusoma;

  3. Iran ina "mpango mpya wa kumuua Donald Trump"

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Gazeti la The Wall Street Journal linaripoti kuwa Israel imeipatia Washington taarifa zinazoonesha kuwa Iran inazingatia mpango mpya wa kutaka kumuua Donald Trump.

    Taarifa hizi zinaonekana kuathiri mtazamo wa Rais wa Marekani zaidi kuliko hapo awali.

    Katika siku za hivi karibuni, Trump amezungumzia hadharani vitisho vya kuuawa kwake mara kadhaa, akisema: "Wanataka kumuondoa kiongozi wa Marekani, yaani mimi," na "Jina langu liko kwenye orodha zao zote."

    Taarifa hizi ambazo Israel ilimpa Trump, pamoja na jaribio lililoshindwa la kutaka kumuua huko Pennsylvania mnamo Julai 2024, ambalo Donald Trump anadai lilikuwa mpango wa Jamhuri ya Kiislamu, zimemfanya rais huyo wa Marekani kubadilisha suala hilo la jaribio la mauaji kutoka kuwa suala la kiusalama tu na kulifanya kuwa sehemu ya simulizi yake ya kisiasa.

    Kundi la wakosoaji wa Trump linasema kuwa hii ni njia ya kujipatia huruma na uungwaji mkono nchini Marekani; hata hivyo, wengi wanachukulia tishio la Jamhuri ya Kiislamu kutaka kumuua Trump kuwa ni jambo zito sana, wakirejelea jaribio la jeshi la Iran la kutaka kumuua John Bolton, aliyekuwa mshauri wa usalama wa taifa wa Trump, mnamo mwaka 2022.

    Lakini hata kama Donald Trump anatumia suala hili kwa ajili ya propaganda za kisiasa, uzoefu wa kihistoria nchini Marekani unaonesha kuwa majaribio ya kuwaua marais hayaleti lazima ongezeko la umaarufu wao wa kisiasa.

    Kumekuwa na takribani majaribio sita ya kuwaua marais wa Marekani tangu mwaka 1950, kuanzia mauaji yaliyofanikiwa ya John F. Kennedy hadi majaribio yaliyoshindwa dhidi ya Harry Truman, Gerald Ford, na Ronald Reagan.

    Wakati Truman na Ford walishindwa kubadili hali ya kushuka kwa viwango vyao vya kukubalika baada ya mashambulizi hayo, Reagan alikuwa tofauti; ucheshi na utulivu wake baada ya kupigwa risasi mwaka 1981 vilizua wimbi la huruma ya umma na kusababisha ongezeko kubwa la viwango vyake vya kukubalika.

    Sasa, wengi wanaamini kuwa Trump, ambaye rais anayempenda zaidi ni Reagan, anajaribu kuonesha taswira kama hiyo ya uthabiti na uongozi kwa kusisitiza mara kwa mara kuhusu tishio dhidi ya maisha yake.

    Unaweza kusoma;

  4. Watu 12 Wafariki kwa moto Hispania huku kiwango cha joto kikiongezeka kusini mwa Ulaya

    Afisa akizima moto

    Chanzo cha picha, EPA

    Takriban watu 12 wamefariki dunia kutokana na moto mkubwa wa porini uliozuka katika eneo la Los Gallardos, Almería kusini mashariki mwa Hispania, kwa mujibu wa serikali ya eneo la Andalusia. Watu wengine sita wamejeruhiwa.

    Baadhi ya miili ya waliofariki ilipatikana ndani ya magari yaliyoteketezwa na moto huo.

    Mashuhuda wamesema moto huo ulianza baada ya waya wa umeme kuanguka na kusababisha moto ulioenea haraka hadi kwenye eneo la msitu. Hata hivyo, mamlaka bado hazijathibitisha chanzo rasmi cha moto huo.

    Joto kali lenye viwango vya takribani nyuzi joto 40 limechochea milipuko ya moto wa porini katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Ulaya.

    Mamia ya maafisa zimamoto wanaendelea kupambana na moto mkubwa nchini Hispania, Ufaransa na Ureno, huku maelfu ya wakazi wakilazimika kuhama makazi yao kwa usalama.

    Serikali ya Andalusia ilisema idadi ya vifo imeongezeka hadi 12 baada ya kuthibitishwa kwa vifo sita zaidi.

    Rais wa serikali ya Andalusia, Juanma Moreno, alielezea tukio hilo kuwa ni janga kubwa. Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, alisema: "Mioyo yetu imejaa huzuni na tumegubikwa na majonzi."

    Takribani maafisa zima moto 150 walikuwa wakifanya juhudi za kuuzima moto katika kijiji cha Bedar.

    Miongoni mwa waliojeruhiwa, mmoja alipelekwa hospitalini baada ya kuvuta moshi mwingi, huku mwingine akipata majeraha ya moto.

    Watu wengine wanne walipatiwa matibabu katika eneo la tukio kutokana na majeraha madogo ya moto na matatizo ya kupumua yaliyosababishwa na moshi mzito.

    Moto huo pia ulisababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara, huku wakazi wapatao 1,000 wakihamishwa kutoka makazi yao kwa tahadhari, kwa mujibu wa huduma za dharura.

  5. Majaji wa Uganda wapinga mpango wa mawakili wa kufuta vyeo vya "heshima vya kikoloni"

    Chama cha Wanasheria Uganda (Uganda Law Society - ULS) kimewaelekeza wanachama wake kuacha kuwahutubia majaji kwa vyeo vya heshima kama "My Lord" na "My Lady".

    Chanzo cha picha, The Uganda Law Society/X

    Mahakama ya Uganda imepinga agizo la Chama cha Wanasheria Uganda (Uganda Law Society - ULS) lililowaelekeza wanachama wake kuacha kuwaita majaji kwa vyeo vya heshima kama "My Lord" na "My Lady", pamoja na kusitisha utamaduni wa kuwainamia wanapoingia mahakamani.

    Katika agizo hilo, ULS ilisema kuwa vyeo hivyo ni mabaki ya mfumo wa kikoloni ambao huwapa majaji hadhi ya juu kuliko raia, ilhali wananchi ndio waajiri wao kupitia mamlaka ya dola.

    Hata hivyo, msemaji wa Mahakama ya Uganda, James Ereemye, aliiambia BBC kuwa ULS haina mamlaka ya kuwaelekeza majaji jinsi ya kuendesha mahakama au namna ya kuheshimiwa. Alisisitiza kuwa mahakama itaendelea kudai maadili na heshima za kawaida kutoka kwa mawakili.

    Kama ilivyo kwa nchi nyingi zilizokuwa makoloni ya Uingereza, Uganda ilirithi mfumo wake wa sheria pamoja na mila nyingi za mahakama kutoka Uingereza.

    ULS imesema mfumo huo wa kikoloni na taratibu zake za zamani umechangia kudhoofika kwa mfumo wa utoaji haki nchini Uganda.

    Chama hicho pia kilieleza kuwa desturi za kuwainamia majaji na kutumia vyeo vya heshima zinawalazimisha Waganda kujidhalilisha mbele ya wenye mamlaka.

    Katika taarifa iliyotiwa saini na rais wa ULS, Isaac Ssemakadde, chama hicho kilipiga marufuku wanachama wake kuwainamia maafisa wa mahakama na kuwataka waache kutumia vyeo kama "My Lord", "Your Lordship", "My Lady" na "Your Worship", kama sehemu ya juhudi za kuondoa athari za ukoloni katika mfumo wa haki na kurejesha heshima kwa wananchi.

    Badala yake, Chama cha Wanasheria Uganda (ULS) kimewataka mawakili kutumia namna rahisi za kuwahutubia maafisa wa mahakama kama vile "Bw. Jaji", "Bi. Jaji", "Bw. Hakimu", "Bi. Hakimu", au kutumia majina yao ya ukoo pale inapofaa.

    ULS pia ilisema kuwa mawakili na washtaki na washtakiwa wote wanaofika mbele ya mahakama au vyombo vya utoaji haki wanapaswa kusimama wima na kuzungumza kama raia huru, bila kuonesha ishara zozote za unyenyekevu wa lazima.

    Akijibu agizo hilo, msemaji wa Mahakama ya Uganda, James Ereemye, alisema mahakama ni mhimili huru wa serikali na haiwezi kupewa maelekezo na chombo chochote cha nje kuhusu namna ya kuendesha shughuli zake.

    Aliipuuza ULS akisema ni "kikundi cha vijana ambao hawajaelewa misingi ya kuweka ajenda katika usimamizi na utawala."

    Ereemye aliongeza kuwa ikiwa kuna hoja kuhusu mabadiliko ya taratibu za mahakama, zinapaswa kuwasilishwa kupitia vikao rasmi vya majadiliano ili zikikubalika, ziwe sehemu ya sera au miongozo rasmi ya mahakama.

  6. Mbappe, Dembele waiongoza Ufaransa kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia

    Wachezaji wa Timu ya taifa ya Ufaransa

    Chanzo cha picha, BBC Sport

    Kylian Mbappe alifunga bao lake la nane katika Kombe hili la Dunia na kufidia penalti aliyokosa mapema, Ufaransa ikiishinda Morocco na kutinga hatua ya nusu fainali.

    Mbappe aliipatia Ufaransa penalti katika kipindi cha kwanza baada ya kuchezewa madhambi na mlinzi wa Morocco, Noussair Mazraoui, lakini mkwaju wake dhaifu uliokolewa kwa urahisi na mlinda lango Yassine Bounou.

    Mshambuliaji huyo wa Real Madrid alijirekebisha dakika ya 60 kwa kufunga bao maridadi la mpira wa kona kutoka nje kidogo ya eneo la penalti na kuipa Ufaransa uongozi uliostahili.

    Dakika sita baadaye, mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or, Ousmane Dembele, aliongeza bao la pili baada ya kupenya safu ya ulinzi ya Morocco na kupiga mkwaju wa chini uliomshinda Bounou licha ya mlinda lango huyo kuugusa mpira.

    Bao la Mbappe limemfanya afikishe mabao manane katika mashindano haya, sawa na Lionel Messi wa Argentina. Hata hivyo, Mbappe anaongoza mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu kutokana na kuwa na pasi nyingi zaidi za mabao kuliko Messi.

    Wawili hao pia wanaendelea kushindana kuwania rekodi ya mfungaji bora wa muda wote katika historia ya Kombe la Dunia. Mbappe mwenye umri wa miaka 27 sasa ana mabao 20, huku Messi mwenye miaka 39 akiwa na rekodi ya mabao 21.

    Ufaransa, mabingwa mara mbili wa Kombe la Dunia ambao walipoteza kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Argentina katika fainali ya mwaka 2022, sasa watakutana na Hispania au Ubelgiji katika nusu fainali itakayochezwa mjini Dallas siku ya Jumanne.

    Unaweza kusoma;

  7. Marekani na Iran zashambuliana wakati Khamenei akizikwa

    Shughuli za mazishi ya Khamenei

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani na Iran zimeendelea kushambuliana kwa mashambulizi yaliyodumu hadi Alhamisi, wakati Ayatollah Ali Khamenei alipokuwa akizikwa baada ya siku sita za shughuli za maombolezo.

    Marekani imesema ilishambulia malengo 90 ya kijeshi, baadhi yake yakiwa karibu na Mlango bahari wa Hormuz, huku waangalizi wakiripoti kupungua kwa kiasi kikubwa kwa idadi ya meli zinazopita katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

    Kwa upande wake, Iran imesema watu 14 wameuawa katika siku mbili zilizopita. Vyombo vya habari vya serikali pia viliripoti kuwa maeneo karibu na kinu cha nyuklia cha Bushehr yalilengwa katika mashambulizi hayo, ingawa Marekani haijasema chochote kuhusu taarifa hizo.

    Iran ilisema ilijibu kwa kushambulia mali na vituo vya Marekani nchini Kuwait, Bahrain na Qatar. Baadaye Alhamisi, vyombo vya habari vinavyohusishwa na serikali vilidai kuwa Tehran ilifanya mashambulizi mengine dhidi ya maeneo nchini Kuwait, Jordan na Iraq.

    Wakati huo huo, maelfu ya waombolezaji walikusanyika katika mji wa Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran, kuhudhuria mazishi ya Ayatollah Ali Khamenei. Wengi walikuwa wakipeperusha bendera za Iran, huku baadhi wakibeba mabango yaliyokuwa na vitisho dhidi ya Rais wa Marekani, Donald Trump.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Khamenei aliuawa tarehe 28 Februari katika saa za mwanzo za mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Unaweza kusoma;

  8. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo