Michael Olisse: Nyota wa soka anayependa kukagua ubora wa nyasi kwa ndala zake

Michael Olisse

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8

Michael Olisse sio mchezaji soka wa kawaida.

Alizaliwa na kulelewa England, lakini sasa anag'aa katika michuano ya Kombe la Dunia akiichezea timu ya taifa ya Ufaransa.

Mshambuliaji huyo wa klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani, ambaye aliwahi kuchezea Reading na Crystal Palace, hujiepusha na vyombo vya habari, anapenda mchezo wa chess, ni nadra sana kumuona akisherehekea baada ya kufunga bao, hapendi kufanya mahojiano, na tofauti na mastaa wa soka, hana mikataba ya utangazaji na makampuni ya viatu au mavazi ya michezo.

Baada ya kuwa na msimu mzuri sana katika ligi ya Bundesliga ambapo alifunga mabao 25 ​​na kutoa pasi za mabao 28, Olisse ni mmoja wa wachezaji bora duniani akiwa na umri wa miaka 24.

Ni mchezaji wa kwanza tangu Mjerumani Thomas Hessler mwaka 1994 kutoa pasi tano za mabao katika michuano ya Kombe la Dunia.

Kwa mujibu wa watu wanaomfahamu tangu utotoni, hulka yake ya upole na kutopenda kujichanganya haipaswi kuchukuliwa kama kiburi.

Alizaliwa jijini London na mama mwenye asili ya Ufaransa na Algeria na baba Mnigeria. Kipaji cha Oliseh kilionekana wazi tangu akiwa mdogo.

Mwalimu wake wa elimu ya viungo katika shule ya msingi Daniel Coker, , aliambia BBC Sport: "Siku moja walimu wa elimu ya viungo walinifuata na kuniambia, 'Je, umemwona huyu mvulana wa darasa la pili? Nilipomwona akicheza, papo hapo nilijua kwamba angekuwa mchezaji mahiri.'"

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulingana na Coker, wakati huo Olisse alikuwa katika chuo cha mafunzo ya soka cha Chelsea na alifanya vizuri katika kila mchezo alioujaribu: "Alipokuwa na umri wa miaka 10 au 11, nilijaribu kumtumia katika kila mashindano. Alijaribu kila aina ya mchezo, na alimshangaza kila mtu kwa uwezo wake wa kipekee."

Lakini hata katika umri huo, hakupenda kuvutia umakini au macho ya watu.

"Michael alikuwa mvulana mtulivu na mwenye haya," anasema Coker."Alitoa pasi nyingi za mabao na kufunga mabao mengi, lakini hakuwahi kusherehekea bao kwa muda; alirejea haraka katikati ya uwanja ili kuanza tena mchezo."

"Yeye si mtu wa kupenda kufurahia wakati huo au kuwa kivutio cha watu. Hadi wa leo, namwona akicheza bila kusherehekea baada ya kufunga bao au kugeuka haraka na kurudi, kama tu alivyokuwa akifanya utotoni."

Rachel Anderson, mkuu wa shule, pia anakumbuka kuwa ilikuwa vigumu kumrudisha darasani baada ya soka, hasa kama timu yake haikushinda.

Anasema, "Baada ya mchezo, alikuwa akipiga mpira darasani, na tulilazimika kumwambia, 'Michael, inatosha!' Shule nyingine zilikatishwa tamaa zilipomwona Michael katika timu yetu, kwa sababu zilijua hazina nafasi ya kushinda."

Kulingana na Anderson, alikuwa mtu aliyependa ukamilifu na kuchunguza kila jambo kwa kina kupita kiasi. Pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kiakili darasani.

Ilionekana wazi tangu wakati huo kwamba huenda angechagua timu ya taifa ya Ufaransa; ingawa angeweza pia kuichezea Uingereza, Nigeria au Algeria.

"Rachel aliniuliza kama nilidhani angeichezea Uingereza," anasema Coker. "Nilijibu, 'Sina uhakika kama tungekuwa na bahati hiyo.' Michael aliipenda sana utamaduni wa Ufaransa. Alisafiri huko mara kwa mara na kufurahia kujifunza lugha ya Kifaransa."

Lakini haikuwa safari rahisi kufikia hatua hii.

Michael olisse (kulia) Alianza kucheza soka la kulipwa mnamo Machi 2019, katika mechi ya Reading dhidi ya Leeds United kwenye ligi ya Championship (daraja la pili la soka la Uingereza).

Chanzo cha picha, Getty Images

Olisse aliwahi kucheza soka kwa kipindi kifupi huko Arsenal, baadaye kujiunga na chuo cha soka cha Chelsea kwa miaka saba., lakini klabu hiyo ilimuachilia akiwa na umri wa miaka 14.Baadaye alihamia Manchester City kwa muda mfupi.

Mdogo wake Olisse, Richard (21), naye ni mchezaji wa soka wa kulipwa. Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa Michael—aliondoka Chelsea muongo mmoja uliopita—yeye pia aliachiliwa huru na klabu yake msimu huu wa joto.

Hatimaye, klabu ya Reading, ambayo wakati huo ilikuwa ikicheza ligi ya Championship, iliingilia kati na kumsajili.

Brendan Flanagan, mkuu wa kitengo cha kusaka vipaji huko Reading, anasema alihangaika kuishawishi bodi ya klabu hiyo kumsajili kijana huyo mwenye umri wa miaka 16 katika majira ya joto ya mwaka 2018: "Ilinichukua muda kuishawishi klabu kutokana na dhana hasi walizokuwa nazo kumhusu. Baadhi ya watu walisema lazima alikuwa na matatizo ya kinidhamu kwa kuwa aliwahi kutimuliwa na Chelsea na Manchester City."

Lakini Flanagan hakuona mambo hivyo: "Kile ambacho huenda kilionekana katika baadhi ya klabu kama tatizo la tabia kwa Michael, kwa kweli ilikuwa ni hali yake tu ya kuwa mtulivu, mwenye haya na asiyependa kujichanganya sana. Kwetu sisi, sifa hizo hazikuwa matatizo; bali zilimfanya kuwa wa kipekee."

Hata hivyo, mama yake Olisse aliomba klabu hiyo kusubiri kidogo ili mwanawe aweze kujenga upya kujiamini kwake baada ya kukumbwa na changamoto hizo mbili.

"Mama yake alisema walitaka afanye kazi na mtaalamu wa saikolojia ya michezo kwa muda ili aweze kujiamini tena," anasema Flanagan. "Nilidhani dili hilo limefeli na kwamba tungelishtukia amejiunga na timu pinzani siku zijazo. Lakini wiki nne baadaye, mama yake alipiga simu na kusema sasa wako tayari."

"Walitimiza ahadi yao. Ni familia ya watu waaminifu na wenye heshima. Hatujawahi kupata tatizo hata kidogo naye tangu siku alipowasili klabuni hapa. Bila shaka, yeye ndiye mchezaji bora zaidi niliyewahi kumleta katika klabu hii."

Olisse alikuwa na hofu sana ya kuchelewa hali iliyomfanya kufika mazoezini mapema sana; aliwahi kulala ndani ya gari lake saa moja asubuhi kwa ajili ya mazoezi yaliyoanza saa tatu asubuhi, na wakati mwingine hata alikosa kuanza kwa mazoezi hayo.

Alianza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Reading dhidi ya Leeds mwezi Machi 2019 akiwa na umri wa miaka 17, na aliendelea kuichezea timu hiyo mara 73 katika misimu mitatu, akifunga mabao saba; katika kipindi hicho, aliitwa kujiunga na timu ya vijana ya Ufaransa.

"Sikushangazwa na uamuzi wake wa kuichagua Ufaransa kwa sababu ndiyo nchi ya kwanza aliyofika," anasema Flanagan. "Michael ni mmoja wa watu wanaosema, 'Nyinyi ndio mliokuwa wa kwanza kuniomba,' kwa hiyo sasa ninaichezea nchi iliyoniamini kwanza.''

ichael Ulisse (left) wore Cristiano Ronaldo's number 7 shirt during his school days and a few years later, in 2021, he played against the Portuguese legend in the English Premier League.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda mfupi baadaye Olise alionyesha uwezo wake katika Ligi Kuu ya England (EPL). Katika misimu yake miwili ya kwanza, alicheza zaidi kama kiungo mshambuliaji, akifanikiwa kutoa pasi 19 za mabao na kufunga mabao 6.

Katika majira ya joto ya mwaka 2023, Chelsea iliamua kumrejesha kwa kulipa kipengele cha kuvunja mkataba wake kilichokuwa na thamani ya pauni milioni 35.

Lakini kinyume na matarajio ya wengi, Olise alisani mkataba mpya Crystal Palace na kuwa mchezaji wa kudumu wa klabu hiyo.

Katika msimu wake wa mwisho huko Selhurst Park (uwanja wa nyumbani wa Crystal Palace), aligeuka kuwa mfungaji mahiri na, licha ya kukumbwa na majeraha mara mbili, alifanikiwa kufunga mabao 10 na kutoa pasi 6 za mabao katika mechi 19, ambazo katika 14 kati yake alianza kikosi cha kwanza.

Mwishoni mwa msimu huo, Olise aliichezea timu ya Ufaransa katika Michezo ya Olimpiki ya Paris, timu iliyofundishwa na Thierry Henry akisaidiwa na Gael Clichy.

"Nililisikia jina lake kwa mara ya kwanza nilipokuwa Manchester City, na kisha nilipokuwa Crystal Palace niligundua ni mchezaji wa kiwango cha juu sana. Mchezaji ambaye alifuata njia tofauti," anasema Clichy.

Kabla ya kuanza kwa Michezo ya Olimpiki, Bayern Munich ilimsajili kwa ada ya takriban pauni milioni 50.

Klabu hazilazimiki kuwaruhusu wachezaji kushiriki katika Michezo ya Olimpiki, na Bayern haikumruhusu mwenzake wa Ufaransa, Mathis Tel, kushiriki.

Lakini kulingana na Clichy, Olise aliwaambia viongozi wa Bayern: "Nina hamu moja tu; nataka kupata uzoefu wa kushiriki Olimpiki na timu ya taifa ya Ufaransa."

Clichy anaona tabia hiyo kama kielelezo cha utu wake: "Tuligundua mara moja kwamba hakuwa tu mchezaji mahiri wa soka, bali pia mtu mwema sana."

Hatimaye Ufaransa ilifika fainali ya Olimpiki lakini ikafungwa na Uhispania katika muda wa ziada.

Olisse ameshida mataji mawili ya Bundesliga na Kombe moja la Ujerumani akiwa na Bayern Munich.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Olisse ameshida mataji mawili ya Bundesliga na Kombe moja la Ujerumani akiwa na Bayern Munich.

Baada ya kujiunga na Bayern Munich chini ya Vincent Kompany, Olisse alifikia kiwango kipya cha soka na haikuchukua muda alijumuishwa kwenye timu taifa ya Ufaransa.

Katika msimu wake wa kwanza akiwa Bayern, alifunga mabao 17 na kutoa pasi 18 za mabao, na katika msimu wa pili, alifunga mabao 25 ​​na kutoa pasi 28; hii ina maana kuwa alichangia moja kwa moja jumla ya mabao 88 ya timu yake katika misimu hiyo miwili.

Mshambuliaji wa zamani wa Ufaransa na mchambuzi wa BBC, Olivier Giroud alisema hivi kumhusu: "Anafanyia timu yake kazi ya ajabu. Ana kipaji kikubwa, lakini jambo la muhimu ni kwamba anacheza kwa maslahi ya timu, sio kwa maslahi yake mwenyewe. Anapopiga krosi kwa utulivu akitumia mguu wake wa kushoto, kila mtu anajua nini atakachofanya; kama ilivyokuwa kwa Arjen Robben katika kipindi chake bora."

Video nyingi za Ulisse zilizotazamwa zaidi akiwa Bayern hazitokani na mabao yake, bali ni mwenendo wake wa kipekee—kuanzia kujaribu kukwepa sherehe za ubingwa hadi kuepuka mahojiano ya televisheni au hata kunyanyua kombe la Bundesliga kwa namna isiyo ya kawaida au ya ajabu.

Hata huingia uwanjani akiwa amevaa ndala kabla ya mechi ili kukagua ubora wa nyasi.

Gael Clichy anasema: "Inachekesha kumuona uwanjani akiwa amevaa ndala, lakini hiyo ndiyo tabia yake halisi. Michael ni mtu asiye na majivuno, lakini miguu yake inajua jinsi ya kuudhihirisha umahiri wake."

Mafanikio ya Olisse yamemfanya ashindwe kujitoa machoni pa watu, baadhi ya wachambuzi wanamuona kama mgombea wa tuzo ya Ballon-d'Or hapo baadaye.

Nafasi yake itakuwa kubwa zaidi endapo Ufaransa itafanikiwa kushinda Kombe la Dunia. Anahitaji pasi moja tu ya bao ili kufikia rekodi ya muda wote ya Pele ya pasi sita katika Kombe moja la Dunia.

Olivier Giroud anasema: "Siku moja Michael anaweza kuwa mmoja wa washindani wakuu wa tuzo ya Ballon-d'Or. Akishinda mataji makubwa, tuzo ya Ballon-d'Or nayo itakuja. Lakini anajali zaidi mafanikio ya timu kuliko ufanisi wa kibinafsi, na hiyo ndio hulka yake halisi." "Unapoangalia uwanjani, unaona ni wapi anapoweza kupiga pasi, hufanya hivyo hata pale anapokuwa na nafasi ya kufunga. Napenda hilo. Yeye ni mbunifu wa kweli wa soka na mchezaji anayejali timu; hayo ndiyo yanayomfanya kuwa na utofauti wa kipekee na kustahili kufikia kiwango cha juu kabisa katika soka la dunia."