Iran sasa ni taifa la nne kuu duniani - Mojtaba Khamenei
Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, amesema kwamba “leo hii baadhi ya watu wanatuita taifa kuu la nne duniani" na kuongezea kuwa waliokuwa na nia ya kuwachokoza na kuwatawala sasa wanataka vita vikome.
Muhtasari
- Mapigano makali yamezuka Baidoa, kati ya jeshi la Somalia na makundi yaliyojihami
- Ethiopia yazishtumu Eritrea, Misri na Sudan kwa kuchochea vita
- Edward Rukidi Kijanangoma kutawazwa rasmi kuwa mfalme wa Tooro, Uganda
- Iran sasa ni taifa la nne kuu duniani - Mojtaba Khamenei
- Dangote awekeza katika bomba la mafuta Ethiopia-Djibouti
- Iran yasema haina mpango wa kufanya mazungumzo na Marekani
- Visa vya Ebola nchini DRC vimepita 8,000
- Wanajeshi wanane wa Marekani wajeruhiwa Iran
- Moto wazuka tena Mlima Kilimanjaro
- Shambulio la droni lalenga kituo cha televisheni Tigray
- Kenya yapata leseni ya kutengeneza dawa mpya ya kuzuia HIV
- DR Congo yatangaza maombolezo ya kitaifa kufuatia ajali ya ndege
- Sifuna apewa tiketi ya urais 2027 na Linda Mwananchi
- Yemen yadai kuwaua wataalamu wanne wa Iran
- Tetesi za Soka Ulaya Jumatatu: Nyota wa Chelsea Estevao kwenye rada za Barcelona
- Wachezaji wa Ireland wakataa kusalimiana na timu ya Israel
- Ruto afichua mpango wa kuifikisha SGR Tanzania
- Araqchi: Iran iko tayari kwa amani, lakini pia kwa vita vya maangamizi
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Beldeen Waliaula
Mapigano makali yamezuka Baidoa, kati ya jeshi la Somalia na makundi yaliyojihami

Chanzo cha picha, SNA RADIO
Mapigano yamezuka leo asubuhi katika mji mkuu wa jimbo la South West, Baidoa, kati ya wanajeshi wa serikali ya Somalia na wapiganaji wanaomuunga mkono rais wa zamani wa jimbo hilo, Abdirashid Hassan Mohamed, anayejulikana kama Laftagareen.
Vyanzo tofauti vimeiambia BBC kuwa mapigano hayo yaliyoanza ndani ya mji wa Baidoa yameenea katika maeneo kadhaa ya jimbo hilo.
Kwa sasa, haijulikani ukubwa wa uharibifu uliosababishwa na mapigano hayo.
Msemaji wa rais wa zamani Laftagareen amesema vikosi vyake vimepata ushindi mkubwa, lakini BBC haijaweza kuthibitisha madai hayo.
Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Ahmed Moalim Faki, amesema katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa “magaidi” waliohusika na shambulio la Baidoa wameadhibiwa vilivyo.
Waziri huyo amesema wapiganaji hao ni wanajeshi wanaomuunga mkono rais wa zamani wa Jimbo la Kusini Magharibi, Abdirashid Laftagareen, na kuwataja kuwa wanachama wa al-Shabaab, ambao amewatuhumu kuhusika na matukio kama hayo hapo awali.
Aidha serikali ya Somalia imesema bado inadhibiti eneo la Baidoa.
Soma pia:
Ethiopia yazishtumu Eritrea, Misri na Sudan kwa kuchochea vita

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkuu wa jeshi la Ethiopia amezishutumu Eritrea, Misri, Sudan na mataifa mengine kwa kuunga mkono makundi ya waasi yanayopigana katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Mkuu wa jeshi la Ethiopia Birhanu Jula, ametoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza tangu kutanuka kwa mapigano wiki iliyopita katika eneo la Tigray, linalopakana na Eritrea na Sudan.
Mkuu huyo wa majeshi ameishtumu Eritrea kwa kuunga mkono makundi hayo ya waasi kwa lengo la kuidhoofisha Ethiopia, madai ambayo Eritrea imekuwa ikiyakanusha mara kwa mara.
Misri, ambayo ina mzozo na Ethiopia kuhusu Bwawa la Renaissance la Ethiopia (GERD) kwenye Mto Nile, pia imekanusha tuhuma hizo.
Mapigano pia yamezuka katika maeneo mengine ya Ethiopia yanayopakana na Tigray, yakiwemo Amhara na Afar.
Soma pia:
Edward Rukidi Kijanangoma kutawazwa rasmi kuwa mfalme wa Tooro, Uganda

Chanzo cha picha, UBC Uganda
Maelezo ya picha, Picha ya Edward Rukidi Kijanangoma Nyabongo Edward Rukidi Kijanangoma Nyabongo, atatawazwa hapo kesho kuwa mfalme mpya wa ufalme wa Tooro magharibi mwa Uganda.
Mfalme huyo, ameteuliwa na kamati ya wajumbe 21 kutoka ukoo wa kifalme wa Babiito wa Ufalme huo.
Hadi wakati wa kutawazwa kwake, Kijanangoma alikuwa akifanya kazi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kampala.
Mfalme huyo alikuwa mtangazaji wa habari na mhariri, na alikuwa akifanya kazi na shirika la habari la serikali nchini humo, Uganda Broadcasting Corporation (UBC).
Kutawazwa kwa Kijanangoma kunakuja siku chache baada ya mfalme mdogo zaidi duniani, na mfalme wa zamani wa Tooro Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi, kufariki dunia kutokana na aina adimu ya saratani, angiosarcoma.
Kifo chake kimesababisha mzozo wa urithi wa madaraka, huku mama wa Mfalme huyo wa zamani, Malkia Best Kemigisa, na baadhi ya wanafamilia ya kifalme, wakidai kuwa aliacha mtoto wa kiume wa kumrithi.
Iran sasa ni taifa kuu la nne duniani - Mojtaba Khamenei

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Mojtaba Khamenei Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, amesema jeshi la Iran limefanikiwa kumuondoa “adui” kutoka kwenye maji ya kusini mwa Iran hadi Bahari ya Arabia.
Khamenei amesema katika ujumbe wake wa kuadhimisha Vita vya Iran na Iraq pamoja na kumbukumbu ya kuuawa kwa kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, Pamoja na viongozi wengine wa Hezbollah na Israel mwaka wa 2024, alisema kuwa
“Baada ya kupata mapigo makali kutoka kwa wanajeshi wetu adui sasa amesonga hadi Bahari ya Arabia.”
Ameongeza kuwa kila mara adui anapothubutu kufanya hivyo, “hujiingiza katika madhara zaidi”, akidai kwamba muda unakaribia ambapo adui hao wataondolewa kutoka bahari ya Arabia.
Katika ujumbe huo, kiongozi huyo, amesema kuwa,
“Leo, baadhi ya watu wanatuchukulia kuwa taifa kuu la nne duniani.” Hata hivyo, amesema tathmini hiyo inatokana na “tathmini za kidunia” baada ya Iran kusimamia haki.
Mojtaba Khamenei hajaonekana hadharani tangu kumrithi baba yake, na hakuna ujumbe wa sauti au video uliotolewa kutoka kwake tangu achukue madaraka.
Maafisa wa Iran wametaja sababu za kiusalama kuwa sababu ya kiongozi huyo kutoonekana hadharani.
Soma pia:
Dangote awekeza katika bomba la mafuta Ethiopia-Djibouti

Chanzo cha picha, Getty Images
Bilionea wa Nigeria Aliko Dangote, ametangaza kuwa atashiriki katika ufadhili wa mradi mpya wa dola milioni 660 wa kujenga bomba la mafuta linalounganisha Ethiopia na Djibouti.
Mradi huo utahusisha bomba lenye urefu wa kilomita 120, litakalounganisha bandari ya Damerjog nchini Djibouti na kituo cha usambazaji mafuta cha Dewele nchini Ethiopia, pamoja na uwezo wa kuhifadhi takriban lita milioni 400 za mafuta.
Bomba hilo linatarajiwa kuanza kufanya kazi ndani ya miezi 18 ijayo.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amesema bomba hilo, ambalo litakuwa mradi wa ubia kati ya Dangote na Ethiopia, litapunguza muda wa kusafirisha mafuta kutoka bandari ya Djibouti hadi Addis Ababa kutoka siku tano hadi siku moja.
Awamu ya kwanza ya mradi huo itaruhusu usafirishaji wa bidhaa muhimu za petroli, zikiwemo mafuta ya taa, dizeli na petroli.
Ethiopia, ambayo haina bandari, inategemea kwa kiasi kikubwa bandari ya Djibouti kwa bidhaa zake zinazoagizwa kutoka nje, hasa mafuta ya petroli. Miundombinu hiyo mipya inatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa mafuta na kukuza sekta ya uchukuzi, usafiri wa anga,kilimo na ujenzi.
Mradi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Dangote wa kupanua uwekezaji wake katika sekta za miundombinu na uzalishaji viwanda barani Afrika.
Nchini Kenya, kampuni hiyo inatarajiwa kuanza wiki ijayo ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi chenye uwezo wa kusindika mapipa 700,000 kwa sikukatika kisiwa cha Lamu.
Soma pia:
Iran yasema haina mpango wa kufanya mazungumzo na Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la habari la Iran, IRNA, limeripoti likinukuu chanzo kimoja kilicho karibu na ujumbe wa Iran mjini New York, nakusema kuwa, Iran haina mpango wa kufanya mazungumzo na Marekani.
Taarifa hiyo imekuja siku moja tu, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema ana matumaini kuwa mazungumzo na Iran yataanza tena hivi karibuni.
Hata hivyo, Trump amekataa pendekezo la Iran la kusitisha mapigano na kufunguliwa tena kwa Mlango bahari wa Hormuz.
IRNA limenukuu chanzo hicho ambaye alisema kuwa “maoni na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliwasilishwa kwa uwazi, kwa upande wa Marekani Jumanne iliyopita kupitia mpatanishi wa Qatar, na Iran inasubiri jibu kutoka Marekani.”
Soma pia:
Visa vya Ebola nchini DRC vimepita 8,000

Chanzo cha picha, Reuters
Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imepita 8,000 kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mlipuko wa sasa, hii ni kulingana na takwimu za serikali ya taifa hilo zilizotolewa hii leo.
Ripoti e kutoka taasisi ya afya ya umma imeweka idadi ya visa vya Ebola kuwa 8,067, huku watu 3,901 wakiwa wamefariki.
Mlipuko huo, unaosababishwa na aina ya virusi vya Ebola ya Bundibugyo, umekuwa mkubwa na mbaya zaidi katika historia ya DRC,baada ya visa vya sasa na idadi ya waliofariki kupita mlipuko uliotokea mwaka wa 2018 hadi 2020.
Mlipuko huu wa sasa ni wa pili kwa ukubwa baada ya mlipuko wa Ebola uliotokea Afrika Magharibi kati ya mwaka wa 2014 na 2016, ambapo zaidi ya watu 28,600 waliambukizwa na zaidi ya watu 11,000 walifariki nchini Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Soma pia:
Wanajeshi wanane wa Marekani wajeruhiwa Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanajeshi wanane wa Marekani, wakiwemo wanajeshi saba wa majini na afisa mmoja, walijeruhiwa katika shambulio la kombora la Iran iliyolenga meli moja katika Mlango wa Hormuz, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.
Ripoti hiyo ilisema wanajeshi hao hawakupata majeraha makubwa, lakini baadhi walipatwa na madhara ya kuvuta moshi kwa wingi, huku wengine wakipata maumivu ya kichwa.
Mmoja kati ya wanajeshi hao wanane alikuwa afisa wa cheo cha juu, huku wengine wakiwa wanajeshi wa kawaida.
Wote wanane wameripotiwa kurejelea majukumu yao ya kawaida baada ya tukio hilo.
Inaelezwa kuwa wanajeshi hao walikuwa kazini wakati kombora la Iran lilipolenga meli waliyokuwa ndani yake.
Maafisa wa Marekani wamekataa kufichua mmiliki wa meli hiyo, wakisema kwamba haikuwa mali ya Marekani wala meli ya Jeshi la Wanamaji la Marekani.
Pentagon imekabiliwa na maswali na ukosoaji mkali kuhusu kiwango cha majeruhi wanaoripotiwa, huku ikifanya mabadiliko katika namna inavyoripoti idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa na kujeruhiwa tangu kuanza kwa vita na Iran mwezi Februari.
Kufikia wiki jana mfumo wa Pentagon wa kurekodi majeruhi wa kijeshi ulikuwa umerekodi wanajeshi 861 wa Marekani waliojeruhiwa kutokana na mzozo huo.
Majeruhi hao wanane waliingizwa katika hifadhidata hiyo siku 10 baada ya shambulio hilo kutokea tarehe 14 mwezi Septemba.
Soma pia:
Shambulio la droni lalenga kituo cha televisheni Tigray

Chanzo cha picha, Getty Images
Kituo cha televisheni cha Tigray TV, kinachomilikiwa na utawala wa eneo la Tigray nchini Ethiopia, kimeripotiwa kushambuliwa na droni katika mji wa Mekelle siku ya Jumapili, huku mapigano makali kati ya vikosi vya Tigray na serikali ya shirikisho ya Ethiopia yakiendelea.
Kwa mujibu wa ripoti, shambulio hilo liliharibu makao makuu ya kituo hicho na kusababisha kusitishwa kwa matangazo yake. Waandishi wa habari wa kituo hicho waliliambia shirika la habari la AFP kuwa jengo hilo lilishambuliwa majira ya saa tatu asubuhi kwa saa za eneo husika.
Picha zilizochapishwa na AFP zilionyesha jengo lililoharibiwa na sehemu zake kuteketea kwa moto, huku madirisha kadhaa yakiwa yamevunjika kutokana na athari za mlipuko huo.
Mwandishi mmoja wa habari wa kituo hicho alisema wafanyakazi walikimbia baada ya kusikia mlipuko mkubwa uliodhaniwa kuwa wa droni katika eneo la karibu.
"Tulisikia mlipuko mkubwa na tukakimbia nje ya jengo. Muda mfupi baadaye jengo lilishambuliwa na kuharibiwa," alisema.
Tigray TV haikuchapisha taarifa wala maudhui mapya kwenye mitandao yake ya kijamii siku hiyo, na hadi wakati huo haikuwa imetoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo.
Wakati huo huo, chanzo cha kibinadamu kililiambia AFP kwamba vikosi vya Tigray viliteka mji wa Erebti katika eneo la Afar, karibu na mpaka wa Tigray, baada ya mashambulizi makali ya mizinga.
Chanzo hicho kilisema vikosi hivyo vilikuwa vinaendelea kuelekea Afdera, takriban kilomita 100 mashariki mwa Erebti. Aidha, kilikadiria kuwa angalau watu 150,000 wamekimbia makazi yao katika eneo la Afar kutokana na mapigano hayo, ingawa idadi hiyo haijathibitishwa kwa njia huru.
Nakala hii ina mtiririko mzuri, inaeleweka na imepangwa kwa mtindo wa habari wa Afrika Mashariki: tukio kuu kwanza, maelezo ya shambulio, ushuhuda wa mashuhuda, na kisha muktadha wa mapigano na athari zake kwa raia.
Kenya yapata leseni ya kutengeneza dawa mpya ya kuzuia HIV

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kenya imepewa leseni ya kutengeneza dawa mpya ya kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV kwa ajili ya soko la Afrika, hatua inayoiweka miongoni mwa nchi tatu za kwanza barani kushiriki katika uzalishaji wa dawa hiyo tangu hatua za awali za maendeleo yake.
Kampuni ya dawa ya Merck ilitangaza kuwa imezipa kampuni saba duniani leseni za kutengeneza toleo la bei nafuu la dawa ya kila mwezi ya kuzuia HIV inayojulikana kama alimatravir, iwapo itathibitishwa kuwa salama na yenye ufanisi baada ya kukamilika kwa majaribio ya kitabibu yanayoendelea. Miongoni mwa kampuni hizo ni Universal Corporation Limited (UCL) ya Kenya.
Hatua hiyo ni ya kwanza kwa wazalishaji wa Afrika kushirikishwa katika leseni za dawa ya HIV tangu mwanzo wa mchakato wa maendeleo ya dawa hiyo, badala ya kusubiri baada ya kuidhinishwa rasmi.
Majaribio ya hatua ya mwisho ya alimatravir yanaendelea nchini Kenya, Uganda na Afrika Kusini yakihusisha wasichana na wanawake vijana. Utafiti huo unafanywa kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za afya, ukiwemo Kemri, huku ushahidi wa kisayansi ukikusanywa barani Afrika ambako dawa hiyo inatarajiwa kutumika kwa kiwango kikubwa.
Leseni hizo hazitozwi mrabaha na zinahusu nchi 129 zenye kipato cha chini na cha kati. Merck pia imesema itatoa akiba ya awali ya dawa hiyo kwa bei isiyoleta faida ili kuhakikisha upatikanaji wa haraka endapo majaribio yatathibitisha mafanikio ya dawa hiyo mwaka ujao.
Akizungumza katika mkutano wa kando wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais William Ruto alisema Afrika imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa magonjwa duniani huku ikizalisha sehemu ndogo ya dawa na chanjo zinazotumika barani humo. Alisema ushiriki wa Afrika katika utengenezaji wa dawa mpya ni hatua muhimu ya kujitegemea katika sekta ya afya.
Kwa mujibu wa Merck, iwapo itaidhinishwa, alimatravir inaweza kuwa dawa ya kwanza ya kila mwezi ya kumeza kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya HIV, jambo ambalo linaweza kuongeza upatikanaji wa huduma za kinga katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi.
Unaweza kusoma pia:
DR Congo yatangaza maombolezo ya kitaifa kufuatia ajali ya ndege

Chanzo cha picha, FARDC
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa na kuagiza bendera kupeperushwa nusu mlingoti kufuatia ajali ya ndege iliyosababisha vifo vya watu 17, wakiwemo maafisa wawili wa juu wa mahakama ya kijeshi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Wizara ya Mawasiliano ilisema Rais Félix Tshisekedi ameagiza bendera kupeperushwa nusu mlingoti kuanzia Jumatatu Septemba 28 hadi siku ya mazishi ya waathiriwa.
Miongoni mwa waliofariki ni Luteni Jenerali Joseph Mutombo Katalayi Tiende, Rais wa Mahakama Kuu ya Kijeshi, na Luteni Jenerali Lucien-René Likulia Bakumi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kijeshi wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC), pamoja na wajumbe wengine wa ujumbe wao.
Serikali pia imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kabla ya shughuli za mazishi na kuwataka wananchi kuonyesha utulivu, heshima na mshikamano kwa familia za waliofiwa.
Ajali hiyo ilitokea Ijumaa mchana karibu na mji wa Kenge, makao makuu ya jimbo la Kwango, ikihusisha ndege aina ya LET 410 UVP iliyokuwa ikiendeshwa na shirika la ndege la TRACEP Congo Aviation.
Kwa mujibu wa Wizara ya Uchukuzi, ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Kikwit kuelekea Kinshasa ilipopata hitilafu ya kiufundi na kujaribu kuelekezwa Kenge. Hata hivyo, mamlaka za eneo hilo zilisema hakukuwa na uwanja wa ndege unaofanya kazi kwa ajili ya kutua, hivyo ndege ilianguka katika eneo la makazi kabla ya kulipuka na kushika moto.
Wizara hiyo ilisema watu wote 17 waliokuwa ndani ya ndege hiyo, abiria 13 na wahudumu wanne, walifariki dunia. Awali idadi ya vifo ilikuwa imetajwa kuwa 13 kabla ya kuongezwa baada ya operesheni za uokoaji kukamilika.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchukuzi, Jean-Pierre Bemba, ameagiza kusimamishwa mara moja kwa cheti cha uendeshaji wa ndege (Air Operator Certificate) cha TRACEP Congo Aviation hadi uchunguzi rasmi wa ajali hiyo utakapokamilika. Hatua hiyo inasimamisha shughuli zote za shirika hilo nchini.
Serikali imesema wachunguzi kutoka mamlaka ya uchunguzi wa ajali za anga nchini humo wamepelekwa katika eneo la tukio kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Wakati huo huo, Wizara ya Mawasiliano imesema Waziri wa Sheria ameagiza uchunguzi wa kina kufanyika ili kubaini mazingira na sababu za ajali hiyo kwa mujibu wa sheria za Congo.
Rais Tshisekedi ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliofariki, huku serikali ikieleza mshikamano wake na familia hizo, mfumo wa mahakama na wanajeshi walioathiriwa na tukio hilo lililoelezwa kuwa janga la kitaifa.
Mamlaka pia zimewataka wananchi kuepuka kusambaza picha za waathiriwa au kutoa taarifa zinazoweza kudhalilisha heshima yao au kuongeza uchungu kwa familia zao.
Soma Zaidi:
Yemen yadai kuwaua wataalamu wanne wa Iran

Chanzo cha picha, EPA
Msemaji wa jeshi la serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, Kanali Majid Abdullah Al-Nuzaili, amesema vikosi vya serikali vilitekeleza operesheni 756 za kijeshi ndani ya saa 72 zilizopita, na kusababisha kuuawa au kujeruhiwa kwa wapiganaji 2,316 wa Wahouthi pamoja na wataalamu wanne wa Iran.
Al-Nuzaili alisema operesheni hizo zilitumia ndege za kivita, ndege zisizo na rubani, makombora, mizinga na vikosi vya ardhini kulenga ngome, wapiganaji na vifaa vya kijeshi vya Wahouthi katika maeneo kadhaa yakiwemo Taiz, Marib, Al-Jawf, Al-Bayda na Lahj.
Kwa mujibu wa jeshi la Yemen, mashambulizi hayo yaliharibu magari ya kijeshi, majukwaa ya kurushia makombora pamoja na maghala ya silaha na risasi.
Al-Nuzaili alidai kuwa wataalamu wanne wa Iran waliouawa walikuwa wakihusika na uendeshaji wa ndege zisizo na rubani na makombora katika mkoa wa Taiz, jambo alilosema linaonyesha kuendelea kwa uungwaji mkono wa Tehran kwa Wahouthi.
Wakati huo huo, msemaji wa Wahouthi Yahya Saree alisema Saudi Arabia ilifanya mashambulizi 27 ya anga katika mikoa kadhaa ikiwemo Taiz, Marib, Saada, Amran, Ibb na Hajjah. Saudi Arabia nayo ilitangaza kuwa ilidungua ndege mbili zisizo na rubani zilizorushwa kuelekea mji mkuu, Riyadh.
Mapigano kati ya Wahouthi na serikali ya Yemen yameongezeka tangu Julai baada ya kipindi cha utulivu wa miaka kadhaa. Mkoa wa Taiz umekuwa miongoni mwa maeneo makuu ya mapambano katika miezi ya hivi karibuni.
Mfalme Mohammed VI wa Morocco amelaani mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya Saudi Arabia na kusema usalama wa Saudi Arabia ni sehemu ya usalama wa Morocco, huku akitoa wito wa kuongezwa kwa shinikizo la kimataifa dhidi ya kundi hilo.
Vita vya Yemen vilianza mwaka 2014 baada ya Wahouthi kuteka mji mkuu Sana'a, hatua iliyosababisha muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati kijeshi mwaka uliofuata kuunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa.
Soma Zaidi:
Wachezaji wa Ireland wakataa kusalimiana na timu ya Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Wachezaji wa Ireland waliinamisha vichwa vyao wakati wa wimbo wa taifa wa Israel kabla ya mechi. Kocha wa Jamhuri ya Ireland, Heimir Hallgrímsson, amesema wachezaji wake walivutia hisia duniani baada ya kukataa kutekeleza baadhi ya taratibu za kawaida kabla ya mechi yao dhidi ya Israel.
Kabla ya mchezo huo uliochezwa Hungary na kumalizika kwa ushindi wa mabao 3-0 kwa Ireland, wachezaji wa Jamhuri ya Ireland na Israel hawakusalimiana kwa kupeana mikono. Aidha, wachezaji wa Ireland waliinamisha vichwa vyao wakati wimbo wa taifa wa Israel ukipigwa.
Nahodha wa Ireland, Dara O'Shea, na mwenzake wa Israel, Manor Solomon, pia hawakusalimiana kabla ya mechi, huku timu hizo mbili zikikosa kubadilishana bendera za kumbukumbu kama ilivyo kawaida.
Tangu droo ya Kundi B3 ilipofanyika mwezi Februari, mechi kati ya timu hizo zimezua mjadala kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Gaza.
Awali, baadhi ya wachezaji wa Ireland walikabiliwa na wito wa kujiondoa kwenye mashindano hayo, huku kampeni ya "Stop the Game", iliyoandaliwa na kundi la Irish Sport for Palestine, ikipata uungwaji mkono mkubwa katika wiki za hivi karibuni.
Pia unaweza kusoma:
Tetesi za Soka Ulaya Jumatatu: Nyota wa Chelsea Estevao kwenye rada za Barcelona

Chanzo cha picha, Getty Images
Winga wa Brazil Estevao Willian anazidi kukerwa na ukosefu wa muda wa kucheza Chelsea, huku Barcelona ikifuatilia kwa karibu hali ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 19. (Sport - in Spanish)
Mshambuliaji wa Ureno Joao Felix, anayekipiga kwa sasa Al-Nassr, amesema angependa kurejea kucheza soka barani Ulaya, ingawa hajataja klabu anayotamani kujiunga nayo. (AS - in Spanish)
Nyota wa Norway Erling Haaland, 26, ameanza kuvutia macho ya Arsenal na Real Madrid kutokana na hali ya sintofahamu inayoikabili Manchester City. (Football Insider)
Newcastle United inamfuatilia beki wa Morocco Abdelhamid Ait Boudlal, 20, wa Rennes, lakini itakumbana na ushindani kutoka Everton, Brentford na Hull City. (Teamtalk)
Arsenal na Tottenham Hotspur zinatajwa kufuatilia kiungo wa Algeria Ibrahim Maza, 20, wa Bayer Leverkusen. (Teamtalk)
Chelsea inamuwania beki wa kushoto wa England Tyrick Mitchell, 27, wa Crystal Palace, lakini pia inakabiliwa na ushindani kutoka Manchester United na Liverpool. (Caught Offside)
Leeds United haina mpango wa kumuuza beki wa Wales Ethan Ampadu, 26, licha ya taarifa zinazomhusisha na kurejea katika klabu yake ya zamani ya Chelsea. (Football Insider)
Soma Zaidi:
Moto wazuka tena Mlima Kilimanjaro

Maelezo ya picha, Picha kutoka maktaba Moto mwingine umeibuka katika Mlima Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania, wiki tatu tu baada ya moto mwingine uliodumu kwa karibu wiki mbili kudhibitiwa kwenye mlima huo wa juu zaidi barani Afrika.
Mamlaka za Tanzania zimesema moto huo ulianza alfajiri ya Jumatatu katika eneo la Sangarini, karibu na mwinuko wa Kamwanga, kuelekea Shira Plateau upande wa magharibi wa mlima huo.
Katika taarifa yake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Catherine Mbena, amesema timu ya pamoja inayojumuisha wazima moto, maafisa wa uhifadhi, wadau wa utalii na wananchi imepelekwa katika eneo hilo kudhibiti moto huo.
Mbena amesema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na uchunguzi unaendelea kubaini kilichosababisha tukio hilo.
Kwa mujibu wa mamlaka, moto huo unaendelea katika eneo la Shira Plateau lililo katika urefu wa takriban mita 3,800 kutoka usawa wa bahari, huku juhudi za kuuzima zikikabiliwa na changamoto ya upepo mkali na uoto unaowaka kwa urahisi.
Hata hivyo, mamlaka zimesema shughuli za utalii, ikiwemo upandaji wa Mlima Kilimanjaro, zinaendelea kama kawaida.
Mbena amesema kuanza kwa msimu wa mvua katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Tanzania kunatoa matumaini kwamba moto huo utaweza kudhibitiwa haraka.
Tukio hilo linajiri muda mfupi baada ya moto mwingine katika upande wa mashariki wa mlima huo kuteketeza zaidi ya hekta 1,800 za uoto wa asili kabla ya kudhibitiwa. Wakati huo, mamlaka zilieleza kuwa shughuli za kibinadamu huenda zilichangia kuzuka kwa moto huo.
Sifuna apewa tiketi ya urais 2027 na Linda Mwananchi

Chanzo cha picha, Getty Images
Muungano wa kisiasa wa Linda Mwananchi umemtangaza rasmi Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, hatua inayolenga kuondoa uvumi kuhusu migawanyiko ndani ya vuguvugu hilo la upinzani.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya kikao maalum cha viongozi wa muungano huo mwishoni mwa wiki, viongozi walisema wamekubaliana kusonga mbele kwa umoja wakiongozwa na lengo la kushughulikia changamoto za uongozi na utawala nchini Kenya.
Viongozi hao walitangaza kuwa Sifuna ndiye atakayepeperusha bendera ya muungano huo katika kinyang'anyiro cha urais, huku akitarajiwa kutangaza rasmi chama atakachotumia kugombea mwanzoni mwa mwezi Oktoba.
Muungano huo pia ulisema unakusudia kujenga ushirikiano na vyama vingine vya kisiasa vinavyoshiriki maono yake ya kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini Kenya.
Tangazo hilo linajiri wakati kumekuwa na maswali kuhusu mshikamano wa viongozi wa Linda Mwananchi, hasa kufuatia mijadala ya umma kuhusu matarajio ya kisiasa ya baadhi ya viongozi wake.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Sifuna alieleza matumaini kuhusu mustakabali wa muungano huo na kusisitiza kuwa viongozi wake wako pamoja katika safari ya kuelekea 2027.
Kwa upande wake, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alisema viongozi wa muungano huo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wao na kujenga msingi imara wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Msimamo huo wa pamoja unakuja siku chache baada ya Babu Owino kuthibitisha hadharani kumuunga mkono Sifuna katika azma yake ya kuwania urais.
Sifuna amekuwa akitafuta jukwaa jipya la kisiasa baada ya kutofautiana na chama cha ODM, na tangazo la sasa linaweka wazi nafasi yake kama sura kuu ya mkakati wa Linda Mwananchi kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.
Soma Zaidi Hapa:
Ruto afichua mpango wa kuifikisha SGR Tanzania

Chanzo cha picha, Michael Khateli
Rais William Ruto amesema serikali yake inapanga kuipanua reli ya Standard Gauge Railway (SGR) hadi Tanzania ili kuimarisha biashara na shughuli za kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza katika ibada ya kanisa eneo la Mwatate, kaunti ya Taita Taveta, Ruto alisema serikali imetenga takriban shilingi bilioni 5 za Kenya kwa ajili ya mradi huo.
"Tunaendelea kuipanua SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu na mpaka wa Malaba. Wakati huo huo, ni muhimu kuunganisha Voi na Tanzania. Tayari tumetenga takriban shilingi bilioni 5 kwa mradi huo," alisema.
Kenya na Tanzania zinatazamia kuunganisha mitandao yao ya reli ya SGR, hatua itakayorahisisha usafiri na biashara katika eneo la Afrika Mashariki, ikiwemo Uganda, Rwanda na Burundi.
Kenya tayari ina mpango wa kuipanua SGR kutoka Naivasha kupitia Kisumu hadi mpakani Malaba.
Wakati wa tangazo hilo, Ruto pia aliahidi kutoa hati miliki za ardhi kwa wakazi wa Taita Taveta wiki ijayo pamoja na kuanzisha miradi mingine ya maendeleo katika eneo hilo.
Pia unaweza kusoma:
Araqchi: Iran iko tayari kwa amani, lakini pia kwa vita vya maangamizi

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ambaye alisafiri kwenda Marekani pamoja na Rais Masoud Pezeshkian kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema ujumbe wa ngazi ya juu wa Iran ulifika New York ukiwa na lengo la "kuandaa mazingira ya amani."
Hata hivyo, Araqchi alisema Iran itaendelea kusimama imara dhidi ya aina yoyote ya uchokozi, hata kama hali hiyo itasababisha kile alichokiita "vita vya maangamizi."
"Tulikuja New York kutafuta njia ya amani, lakini iwapo italazimu, tuko tayari pia kwa vita vya apokalipsi. Wakati huohuo, tuko tayari kwa diplomasia ya kweli," amesema Araqchi katika mahojiano na vyombo vya habari vya Marekani.
Kauli hiyo imekuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuripotiwa kukataa pendekezo la Iran la kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz, huku baadaye akisema kuwa mazungumzo zaidi kati ya Marekani na Iran yatafanyika katika siku zijazo.
Wiki iliyopita, Araqchi alisema kuwa iwapo Marekani itakubali mpango uliopendekezwa na Iran, Mlango Bahari wa Hormuz unaweza kufunguliwa ndani ya siku saba.
Soma Zaidi Hapa:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 28/09/2026.



















