Ndani ya mji wa Yemen ulio mstari wa mbele ambapo Wahouthi wanapigania udhibiti

- Author, Nawal Al-Maghafi
- Nafasi, Mwandishi Mwandamizi wa Uchunguzi wa Kimataifa.
- Akiripoti kutoka, Taiz, Yemen
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
"Hii ni ndege isiyo na rubani ya kwanza," alisema mwanajeshi aliyekuwa akisafiri nasi kusini-magharibi mwa Yemen. "Kwa kawaida hufuatiwa na shambulio."
Sauti ya mlio wa ndege hiyo juu yetu ilizidi kuwa kubwa tulipojificha chini ya vichaka, kabla ya kupanda tena kwenye gari na kuondoka.
Takribani dakika 10 baadaye, milio mikubwa ya mashambulizi ilianza kusikika, mmoja baada ya mwingine, ingawa haikufahamika yalilenga maeneo gani.
Ni vigumu kutambua mstari wa mbele unapoanzia katika milima iliyoko kusini-magharibi mwa mji wa Taiz.
Vikosi vinavyounga mkono serikali na vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia vinapambana kuwasukuma nyuma wapiganaji wa Kihouthi, ambao mwanzoni mwa mwezi huu walishuka kupitia pwani ya Bahari ya Shamu, wakachukua udhibiti wa eneo muhimu la kupitisha meli na kuongeza makali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen.
Tulitembea pamoja na vikosi vya serikali kutoka Taiz, tukipitia vituo vya ukaguzi hadi kufika kwenye eneo ambalo udhibiti wao unaishia na kuanza eneo lisilodhibitiwa na upande wowote, ili kujionea mapigano kwa karibu.

Nyumba zimetawanyika kwenye miteremko ya milima, lakini nyingi zimeachwa baada ya familia kukimbia ili kujinusuru kutokana na mapigano.
Ni eneo lenye ukimya wa kutisha, hakuna sauti za magari au pikipiki zinazoendelea kupita kwa kasi mjini. Kitu pekee kinachosikika ni milio ya mifugo na sauti za risasi na makombora yanayorushwa na kurudi.
"Mabomu mawili yalianguka hapa kwenye mali yangu," alisema Ali, akiwa ameketi nje ya nyumba yake pamoja na kundi la mbuzi, takribani kilomita moja kutoka mstari wa mbele.

Chanzo cha picha, Liam Weir/BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aliniambia kuwa amewapeleka watoto wake kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani kwa sababu hawakuweza tena kuvumilia mashambulizi ya mabomu na milio ya risasi. Yeye amebaki na mke wake na dada zake ili kuwatunza wanyama wao.
"Ninaogopa sana," alisema, "lakini sina chaguo. Bila wanyama wetu sote tutakosa chakula na hatimaye tutakufa."
Alitoa jina lake la kwanza pekee, akihofia madhara iwapo Wahouthi watachukua udhibiti wa eneo hilo katika siku zijazo. Watu waliowasiliana nasi kutoka upande wa Wahouthi wametuambia kuwa wanakusanya na kuimarisha vikosi vyao, wakijiandaa kwa mashambulizi makubwa. Tulipowauliza wanajeshi wa serikali kuhusu hilo, walisema wanafahamu hali hiyo na pia wanajiandaa.
Katika kituo cha ukaguzi kilicho karibu zaidi na mstari wa mbele, tulikutana na baadhi ya wapiganaji waliokuwa wamerejea kutoka kwenye maeneo yao ya mapigano juu ya mlima, umbali wa mita mia chache tu kutoka kwa Wahouthi waliokuwa wakisonga mbele.
Mmoja wao alisema miili ya wanajeshi 18 wa serikali ilikuwa imelala katika eneo ambalo kikosi chake kinaweza kulishambulia kwa risasi lakini hakiwezi kufika kulichukua.
"Tunawafyatulia risasi kutoka juu, lakini hatuwezi kuwatoa," alisema.
Mapigano karibu na Taiz yameongezeka tangu Wahouthi walipoutwaa bandari ya kimkakati ya Mokha, kilomita 85 magharibi mwa mji huo, tarehe 10 Septemba, baada ya usitishaji mapigano uliodumu kwa kiasi kikubwa kwa miaka minne kuvunjika.
Kundi hilo lilichukua udhibiti wa eneo kubwa linalotazama Mlango wa Bab al-Mandab, njia muhimu ya usafirishaji inayounganisha Ulaya na Asia. Hatua hiyo ilichangia kupanda kwa bei ya mafuta huku hofu ikiongezeka kwamba usambazaji kutoka eneo hilo unaweza kuvurugika zaidi.

Taiz ni mji wa tatu kwa ukubwa nchini Yemen na unachukuliwa kuwa mji mkuu wa utamaduni wa nchi hiyo. Una wakazi karibu milioni moja. Uko katika eneo muhimu linalounganisha maeneo ya kaskazini mwa Yemen yanayodhibitiwa na Wahouthi na maeneo ya kusini yanayodhibitiwa na serikali, huku ukiwa umezungukwa na mistari ya mapigano kutoka pande kadhaa.
Vikosi vya serikali vinadhibiti katikati ya Taiz, huku maeneo ya Wahouthi yakiwa kaskazini na mashariki mwa mji huo. Mapigano makali zaidi hivi karibuni yamekuwa katika maeneo ya magharibi, ambako pande hizo mbili zinapigania maeneo ya juu yanayoangalia njia ya kusini ya mji.
Iwapo Wahouthi watadhibiti maeneo hayo, vikosi vya serikali vinaweza kupata ugumu zaidi katika kuutwaa tena Mokha.
Tulikwenda Taiz kutoka Aden kusini, ambako Baraza la Uongozi wa Rais na serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa zina makao yao.
Takribani vituo 30 vya ukaguzi njiani vilionyesha maeneo ya barabara yanayodhibitiwa na makamanda tofauti, ishara ya wazi ya mgawanyiko uliopo miongoni mwa vikosi vinavyopigana upande wa serikali.
Tulipokaribia mji huo, magari ya wagonjwa yalianza kutupita. Tulihesabu angalau matano ndani ya nusu saa, yakielekea hospitali kuu ya Taiz. Ilikuwa wazi kwamba tulikuwa tukiingia katika mji ulio katikati ya vita vikali.
Tulifika baada ya giza kuingia. Maduka yalikuwa yamewashwa taa, migahawa ilikuwa imejaa watu na watoto walikuwa wakicheza mitaani. Lakini kila baada ya muda, sauti nyingine zilisikika — milio ya makombora na milio ya risasi kutoka milimani inayouzunguka mji.

Chanzo cha picha, Liam Weir/BBC
Taiz imekuwa moja ya maeneo makuu ya mapigano katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha uharibifu mkubwa nchini humo.
Baada ya kuiondoa serikali kutoka Sanaa mwaka 2015, Wahouthi walijaribu pia kuutwaa udhibiti wa Taiz, lakini walifukuzwa kutoka sehemu kubwa ya mji na wanamgambo wa eneo hilo.
Sasa, katika mashambulizi yao mapya, Wahouthi wanatumia kwa kiasi kikubwa ndege zisizo na rubani pamoja na silaha nyingine.
Iran ndiyo inatajwa kuwa mshirika wao mkuu wa nje, ikiwa imewapatia silaha, fedha na ushauri wa kijeshi, kwa mujibu wa Saudi Arabia, nchi za Magharibi na wataalamu wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, Iran imewahi kukanusha kuwapatia Wahouthi silaha na kusema inawaunga mkono kisiasa pekee.
Kwa miaka mingi kumekuwa na ripoti za mara kwa mara kwamba Wahouthi wanawaajiri watoto kuwa wapiganaji, na mwanajeshi wa serikali alituambia kuwa amewakabili watoto hao kwenye mstari wa mbele.
"Ni vigumu kumtazama mtoto wa Yemen na kumpiga risasi. Lakini mtoto huyo anakuwa amekuelekezea bunduki na lazima ujilinde," alisema.
Wahouthi walitia saini "mpango wa utekelezaji" na Umoja wa Mataifa mwaka 2022, wakiahidi kukomesha matumizi ya watoto katika mapigano. BBC pia imezungumza na vijana wanaohudumu katika vikosi vya serikali.
Wakati huohuo, muungano unaoongozwa na Saudi Arabia unaiunga mkono serikali ya Yemen na kuipatia silaha. Jeshi la Saudi limefanya mamia ya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya Wahouthi kwenye pwani ya Bahari ya Shamu, huku Wahouthi wakirusha ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya miji na miundombinu kusini-magharibi mwa Saudi Arabia.

Chanzo cha picha, Liam Weir/BBC News
Jioni, katika hospitali ya al-Thawra mjini Taiz, majeruhi kutoka mstari wa mbele walikuwa wakiletwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi, ambapo kila kitanda tulichokiona kilikuwa kimejaa.
Baadhi ya wagonjwa walikuwa wapiganaji, huku wengine wakiwa raia.
Ghana Nabeel mwenye umri wa miaka 12 alikuwa akichunga mbuzi wakati vipande vya mabaki ya mlipuko vilipompiga kichwani. Familia yake ilisema kombora la chokaa lililorushwa na Wahouthi lilikuwa limeanguka karibu naye.
Alikuwa amelala bila fahamu, kichwa chake kikiwa kimefungwa bandeji, huku uso wake ukiwa umevimba na kujaa michubuko. Familia yake ilikuwa pembeni ya kitanda ikisubiri kujua maisha yake yatakuwaje iwapo ataamka.
Daktari aliniambia kuwa jeraha hilo limeharibu ubongo wake.
"Hatawahi kuwa kama alivyokuwa tena," alisema.

Chanzo cha picha, Liam Weir/BBC
Takribani kilomita 20 kusini mwa Taiz, katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya al-Monig, familia zilizokimbia Mokha na vijiji vilivyoathiriwa na mapigano zilikuwa zikiwasili, katika eneo lenye mamia ya mahema.
Tuliambiwa kuwa familia 200 zilikuwa zimewasili katika kipindi cha siku 10 zilizopita.
Maryam Saleh, ambalo si jina lake halisi, alikuwa amewasili wiki moja iliyopita kutoka Mokha pamoja na mumewe na watoto wao watano. Mtoto wao mdogo ana umri wa miaka saba.
Maryam alikuwa ameketi akifuma kofia ili kuiuza na kupata fedha za kununua chakula cha siku hiyo.
"Tulitembea bila viatu na hatukuondoka na kitu chochote, isipokuwa watoto wetu," aliniambia.
Alisema mpwa wake aliuawa na vipande vya mabaki ya kombora alipokuwa akikimbia pamoja nao. Alikuwa akitembea nyuma yake.
Alielezea mapigano na milio ya risasi kutoka mbele na nyuma yao, kabla ya kuwaona wanaume wenye silaha mlimani.
"Tulidhani tumekwisha," alisema.
Aliongeza kuwa watoto walikuwa wakipiga kelele na kulia, lakini familia iliendelea kutembea.

Chanzo cha picha, Liam Weir/BBC
Fatma Mohammed Saleh alikuwa amelala kwenye gunia tupu la mchele nje ya hema la familia nyingine. Ana ulemavu na hawezi kutembea, na aliniambia kuwa hana mahali pake pa kulala.
"Sina chochote... sina makazi, sina godoro, sina familia. Sina chochote," alisema.
Fatma alisema alikuwa pamoja na wanawe wawili na watoto wao wakati mapigano yalipofika katika kijiji chao. Lakini kwa sababu alikuwa akiwachelewesha, aliwaambia wawachukue watoto na kukimbia, alisema.
Alitumia siku mbili zilizofuata akijikokota kwa mikono na magoti, alisema.
"Nilikuwa najikokota huku risasi zikija kutoka huku na makombora yakiwa kule. Risasi zilikuwa huku, makombora kule. Na juu yangu kulikuwa kama ngurumo. Nilikuwa nikimuomba Mungu."
Mwanaume mmoja aliyekuwa kwenye pikipiki alimwona na kumpeleka kambini, alisema.
Tangu wakati huo hajawaona tena wanafamilia wake.
Mnamo Septemba 22, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema kuwa zaidi ya watu 130,000 walikuwa wamekimbia makazi yao katika maeneo mbalimbali ya Yemen katika mwezi huo pekee, juu ya watu milioni 5.2 ambao tayari walikuwa wamehamishwa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Shirika hilo lilionya kwamba watu wengine 100,000 wanaweza — kama Fatma — kulazimika kuondoka kwenye makazi yao katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Imetafsiriwa na Faidha Ngaga na kuhaririwa wa Ambia Hirsi
































