Saudia Arabia yaapa kulipiza kisasi mashambulio ya Wahouthi
“Matukio ya wiki za hivi karibuni ni makubwa. Jibu letu lazima liwe kali kwa kiwango hicho hicho,” alisema Mwanamfalme Abdul Aziz bin Salman.
Muhtasari
- Makaazi ya Ilhan Omar yapekuliwa kwenye msako Marekani
- Rais wa zamani wa Congo (DRC) amkosoa Tshisekedi kuhusu makubaliano ya madini na Marekani
- Waziri wa Saudi Arabia aahidi kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Wahouthi kwenye viwanja vya ndege
- Wito wa kufungwa kwa shughuli za kila siku Jamhuri ya Afrika ya Kati wazua hisia tofauti
- Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Navi Pillay, atetea taasisi za haki za kimataifa
- Marekani yaonya mashirika ya ndege kuhusu hatari ya kutumia anga ya Saudi Arabia
- China: Mashambulizi ya Riyadh yanatia wasiwasi mkubwa
- Urusi imekishambulia kiwanda cha umeme cha Kharkiv 'mara baada ya' Trump kusimamisha mapigano
- Mtawa ashtakiwa kwa kujaribu kumfanyia unyanyasaji wa kingono mwanamke Mfaransa
- Wahamiaji 139, wakiwemo watoto, wafariki baada ya boti kuzama pwani ya Djibouti
- Mtu mmoja afariki katika shambulio jipya kwenye uwanja wa ndege wa Saudi Arabia, siku moja baada ya shambulio la Wahouthi kuwaua watu 13
- Shirikisho la Soka la Ureno limechukulia hatua za kinidhamu Ronaldo, kulikoni?
- Wachimbaji dhahabu kadhaa wauawa katika mashambulizi kwenye mpaka wa Misri na Sudan, kundi la haki za binadamu lasema
- Zelensky akaribisha mpango wa Trump wa kusitisha mashambulizi, je Putin atajibu?
Moja kwa moja
Na Dinah Gahamanyi & Faidha Ngaga
Naibu mkuu wa polisi Afrika Kusini ajiuzulu baada ya kushtakiwa kwa unyanyasaji wa kingono

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Luteni Jenerali Shadrack Sibiya amekanusha mashtaka yote yanayomkabili. Wakili anayemwakilisha Luteni Jenerali Shadrack Sibiya aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu wakati wa kikao cha kinidhamu Jumatatu, msemaji wa polisi amesema.
Mashtaka hayo yanahusiana na madai kwamba alimshawishi na kumwandaa msichana mwenye umri wa miaka 16 kwa ajili ya unyanyasaji wa kingono, na kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 18. Pia anakabiliwa na shtaka la usafirishaji haramu wa binadamu.
Sibiya amekanusha mashtaka yote. Lakini amekiri kufanya ngono na mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 18, lakini anasema walikubaliana kufanya hivyo.
Amekuwa kizuizini tangu alipokamatwa wiki tatu zilizopita, baada ya ombi lake la dhamana kukataliwa.
Msemaji wa polisi, Athlenda Mathe, alisema katika chapisho kwenye mtandao wa X kwamba kuondoka kwa Sibiya katika jeshi la polisi kunachukuliwa kuwa kufukuzwa kwa aibu.
Kesi hiyo imeibuka wakati jeshi la polisi likichunguzwa katika tume kubwa ya uchunguzi wa umma kuhusu madai ya ufisadi na kushirikiana na wahalifu.
Uchunguzi huo, unaojulikana kama Tume ya Madlanga, ulianza Septemba 2025 na umesikiliza madai kwamba Sibiya alipokea zawadi ya swala 20 kutoka kwa mtu anayedaiwa kuwa kinara wa uhalifu, kama malipo ya kumpatia mkataba wa polisi.
Sibiya amekanusha madai hayo.
Unaweza pia kusoma:
Maafisa wa uhamiaji wamfanyia msako Ilhan Omar

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wa Usalama wa Ndani wa Marekani wamefanya msako katika nyumba ya mbunge wa chama cha Democratic, Ilhan Omar, jijini Washington, kabla ya mapambazuko.
Taarifa zinasema kuwa hati ya upekuzi inahusiana na uchunguzi kuhusu nyaraka za uhamiaji ambazo baba yake aliwasilisha kwa niaba yake alipokuwa mtoto.
Mwezi uliopita, Tom Homan, afisa wa Ikulu ya Marekani anayesimamia masuala ya mpaka, alithibitisha kuwa Omar alikuwa akichunguzwa katika makosa ya jinai. Omar amewahi kukanusha madai ya Rais Donald Trump kwamba uraia wake ulipatikana kwa njia ya udanganyifu, akisema mashambulizi yake ya mara kwa mara dhidi yake yana nia za kisiasa.
Omar alizaliwa nchini Somalia na alifika Marekani akiwa na umri wa miaka nane, akikimbia vita. Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge wa Congress mwaka 2018, na amekuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Donald Trump.
Kwa sasa, Bunge la Marekani halifanyi vikao, na haijulikani iwapo Omar alikuwa nyumbani wakati wa msako huo.
BBC imewasiliana na Omar ili kupata maoni yake kuhusu tukio hilo.
Unaweza pia kusoma:
Kabila aukosoa mkataba wa madini wa DR- Congo na Marekani

Chanzo cha picha, AFP
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila, amemshutumu mrithi wake, Felix Tshisekedi, kwa kusaini makubaliano na Marekani kuhusu madini muhimu, akisema alifanya hivyo kwa matumaini ya kupata uungwaji mkono wa Marekani bila masharti, jambo alilolitaja kuwa ni dhana potofu. Kabila alitoa kauli hiyo jana, hii ni kwa mujibu wa chombo cha habari cha kujitegemea cha Actualite.cd,
Katika hotuba yake ya tarehe 9 Oktoba, Kabila alisema kuwa makubaliano ya madini ya aina hiyo hufanywa kati ya mataifa, badala ya tawala za kisiasa, na hivyo hayahakikishi kuendelea kuwepo madarakani kwa serikali husika.
Rais huyo wa zamani aliahidi kutangaza hatua madhubuti zinazolenga “kuiokoa” nchi kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa na kiusalama, akionya kuwa kuna matumaini machache ya hali kuboreka chini ya uongozi wa Tshisekedi.
Pia aliwataka wananchi kuchukua jukumu la kuamua mustakabali wa nchi yao, akiahidi kuchukua hatua zaidi katika “saa, siku na wiki zijazo”.
Kauli zake zinatolewa wakati kukiwa na kutokubaliana kuhusu mpango wa Tshisekedi wa kufanya mazungumzo ya kitaifa, uliotangazwa mwezi Agosti kwa lengo la kushughulikia migawanyiko ya kisiasa na ukosefu wa utulivu uliodumu kwa muda mrefu.
Washirika wa kisiasa wa Kabila wamehoji iwapo mazungumzo hayo yaliyopendekezwa yatawashirikisha wadau wote kwa usawa, na kutaka kuwepo kwa dhamana imara zaidi kuhusu maandalizi yake, uratibu na ushiriki wa washiriki.
Mvutano huo wa kisiasa unaendelea huku mapigano yakiendelea mashariki mwa DR Congo kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Muungano wa Mto Congo AFC/M23, wanaoungwa mkono na Rwanda, licha ya juhudi za kidiplomasia zinazoongozwa na Marekani na Qatar za kufanikisha amani.
Unaweza pia kusoma
Waziri wa Saudi Arabia aahidi kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Wahouthi kwenye viwanja vya ndege

Chanzo cha picha, AP
Maelezo ya picha, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia Mwanamfalme Abdul Aziz bin Salman Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia Mwanamfalme Abdul Aziz bin Salman ameahidi kutoa jibu kali kufuatia mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu katika viwanja vya ndege na miundombinu ya mafuta na gesi ya nchi hiyo, yaliyofanywa na kundi la Wahouthi la Yemen linaloungwa mkono na Iran.
“Matukio ya wiki za hivi karibuni ni makubwa. Jibu letu lazima liwe kali kwa kiwango hicho hicho,” alisema Prince Abdul Aziz bin Salman wakati wa Kongamano la Nishati la WPC lililofanyika Riyadh.
Siku ya Jumapili, raia mmoja wa Pakistan aliuawa katika shambulizi lililolenga jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid, katika mji mkuu wa Riyadh, kwa mujibu wa mamlaka za Saudi Arabia. Shambulizi hilo lilitokea siku moja baada ya kombora la Wahouthi kulipiga jengo jingine la abiria, na kuua watu 13 na kulazimisha jengo hilo kufungwa.
Wahouthi walisema walifanya mashambulizi hayo kulipiza kisasi dhidi ya kile walichokiita “uchokozi wa kikatili wa Saudi Arabia” katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao magharibi mwa Yemen.
Wizara ya Afya inayoendeshwa na Wahouthi ilisema mtoto mmoja aliuawa na watu wengine sita kujeruhiwa katika shambulizi la anga la Saudi Arabia lililolenga nyumba moja katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, siku ya Jumapili.
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukitoa msaada wa mashambulizi ya anga kwa vikosi vya serikali ya Yemen vinavyopambana na Wahouthi katika pwani ya Bahari Nyekundu na maeneo mengine nchini humo.
Yemen imekumbwa na uharibifu mkubwa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2014, wakati Wahouthi walipoiondoa serikali madarakani katika mji mkuu, Sanaa. Mzozo huo ulizidi kuwa mkubwa mwaka 2015, baada ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati kwa lengo la kurejesha utawala wa serikali.
Unaweza pia kusoma:
Wito wa kufungwa kwa shughuli za kila siku Jamhuri ya Afrika ya Kati wazua hisia tofauti

Wito wa kusitisha shughuli za kila siku nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati umetatiza maisha katika mji mkuu, Bangui, huku wakazi wakionyesha hasira kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta.
Hatua hiyo ya maandamano inafuatia uamuzi wa serikali wa tarehe 1 Oktoba kuongeza bei ya mafuta kwa faranga 150 za CFA, sawa na takriban senti 27 za Marekani.
Makundi ya kiraia yaliwataka watu kubaki nyumbani Jumatatu na kuepuka kwenda kazini, shuleni au madukani. Hatua hiyo ilikusudiwa kusimamisha shughuli za kila siku badala ya kufanya maandamano ya barabarani.
Baadhi ya biashara na ofisi za serikali zimeendelea na shughuli zake, huku magari yakiendelea kupita na biashara zikiendelea katika maeneo kadhaa ya mji. Hata hivyo, shughuli zimeendelea kuwa chache katika maeneo mengine na baadhi ya shule zimefungwa.
Mkazi mmoja aliiambia BBC kuwa mji ulikuwa na utulivu usio wa kawaida, hata katikati ya jiji.
Katika jitihada za kupunguza hali hiyo, serikali imefungua tena baadhi ya vituo vya mafuta katika mji mkuu, Bangui, na kuruhusu kila dereva wa bodaboda kupata lita 10 za mafuta bila malipo, kwa mujibu wa mkazi aliyezungumza na BBC.
Mamia ya madereva wameonekana wakipanga foleni kupata mafuta ili waweze kurejea katika shughuli za kusafirisha abiria mjini humo.
Baadhi ya barabara pia zimefungwa, zikiwemo barabara kutoka Padre Pio kupitia Carrière hadi kwenye lango la kuingia katika Daraja la Jackson, kuelekea Barabara ya Barthélémy Boganda.
Kupanda kwa bei ya mafuta kumeongeza gharama za usafiri na kuongeza shinikizo kwa kaya na biashara ambazo tayari zinakabiliwa na gharama kubwa za maisha.
Hali hiyo inajitokeza wakati kukiwa na mvutano huko Mashariki ya Kati, unaotishia upatikanaji wa nishati na kuchangia kupanda kwa gharama duniani. Nchi zinazotegemea mafuta yanayoagizwa kutoka nje ziko katika hatari zaidi ya kuathiriwa na mabadiliko ya bei ya mafuta, ambayo yanaweza kusababisha kupanda kwa nauli za usafiri na bei za bidhaa za kila siku.
Unaweza pia kusoma:
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Navi Pillay, atetea taasisi za haki za kimataifa

Chanzo cha picha, AFP
Navi Pillay, ametetea taasisi za haki za kimataifa na kujibu ukosoaji wa Rais wa Marekani, Donald Trump, akisema kipimo halisi cha haki ni maana yake kwa waathiriwa wa migogoro na ukatili.
Trump alielezea uamuzi uliofanyika mwaka huu wa Tuzo ya Amani ya Nobel kuwa ni wa “aibu” na “wa kuaibisha”, akisema kuwa hajawahi kumsikia mwanasheria huyo kutoka Afrika Kusini.
Katika mahojiano na BBC, Pillay, aliyewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, alitetea kazi yake na kuonya dhidi ya juhudi za kudhoofisha taasisi zinazolenga kuwawajibisha waliohusika na uhalifu mkubwa.
Akijibu ukosoaji wa Trump, Pillay aliwakumbusha watu walionusurika katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994, ambao wengi wao walisubiri kwa miaka mingi kupata haki.
“Nadhani washauri wa kisheria wa Rais Trump wanapaswa kumweleza mambo haya yote na kumfahamisha umuhimu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) katika kudumisha amani duniani,” alisema.
Pillay, ambaye aliwahi kuwa jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, alizungumza wakati mahakama hiyo ikikabiliwa na shinikizo jipya kufuatia vikwazo vya Marekani.
Alisema anakusudia kuwatia moyo wafanyakazi wa mahakama hiyo na anaamini kuwa shinikizo hilo litakuwa la muda tu, kwa kuwa nchi wanachama zinaendelea kuunga mkono taasisi hiyo.
Pillay pia alitetea matokeo ya uchunguzi wa tume ya Umoja wa Mataifa aliyoiongoza, ambayo ilihitimisha kuwa mauaji ya kimbari yalikuwa yakitokea Gaza, madai yaliyokataliwa na Israel.
Alisema hitimisho la tume hiyo lilitokana na ushahidi uliothibitishwa na kusisitiza kuwa wachunguzi wanapaswa kuruhusiwa kuendelea na juhudi za kuwawajibisha wahusika bila kutishwa.
Kwa Pillay, Tuzo ya Amani ya Nobel haitambui tu mapambano yake ya miongo kadhaa dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na kujitolea kwake kwa haki za kimataifa, bali pia umuhimu mpana wa kuwawajibisha waliohusika na uhalifu mkubwa.
Mshindi huyo wa tuzo ya mwaka 2026 alisema vijana kote barani Afrika wanampa matumaini, licha ya kile alichokitaja kuwa kuendelea kwa utawala wa kimabavu na ukandamizaji wa maandamano.
“Vijana ndio wanaonipa matumaini. Wanafahamu haki zao na wanadai mabadiliko. Wanaingia mitaani kuandamana. Wana haki ya kuandamana, lakini maandamano hayo yanakandamizwa,” alisema.
Pillay alisema yeye na wenzake wanataka kuongeza uelewa wa haki za binadamu miongoni mwa vijana wa Afrika na kuhamasisha kizazi kipya kupigania mabadiliko.
Pia alielezea wasiwasi wake kuhusu kutokuwa na usawa kwa wanawake, hususan katika nchi maskini na maeneo yenye migogoro, akisema anatumai kutumia mwangaza unaotokana na tuzo hiyo kuangazia suala hilo.
“Nimejizatiti kuangazia ukosefu wa usawa na kutokuwa kwa usawa kwa wanawake, hasa katika nyanja ya uchumi,” alieleza.
Pillay alisema kushirikisha watu maarifa kuhusu haki zao kunawawezesha kudai mabadiliko, somo ambalo anatumai litapata mwitikio kote Afrika na kwingineko duniani.
Unaweza pia kusoma:
Marekani yaonya mashirika ya ndege kuhusu hatari ya kutumia anga ya Saudi Arabia

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka ya Usafiri wa Anga wa Marekani (FAA) umeyaonya mashirika ya ndege nchini humo kuwa makini yanaposafiri kwa ndege kwenda Saudi Arabia au kupitia anga yake.
Shirika hilo limesema onyo hilo limetolewa kutokana na vitisho vya kiusalama vinavyotokana na operesheni za kijeshi zinazoendelea pamoja na hitilafu katika mifumo ya uelekezaji wa ndege, likielezea hali ya sasa kuwa “inayoweza kuwa hatari”.
Onyo hilo, ambalo litaendelea kutumika hadi Desemba 10, limetolewa baada ya mashambulizi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Riyadh siku ya Jumamosi na Jumapili. Shambulizi la Jumamosi liliua watu 13 na kujeruhi zaidi ya 300.
FAA imesema hatari hizo zinaweza kuhatarisha ndege katika mwinuko wowote, zikiwemo ndege zinazopita juu ya anga ya nchi hiyo, zinazokaribia viwanja vya ndege kwa ajili ya kutua na zinazopaa. Onyo hilo pia linahusu ndege zilizosajiliwa nchini Marekani.
Uwanja wa Ndege wa Riyadh unatarajiwa kuendelea kufungwa hadi angalau Jumatatu jioni kwa saa za Pwani ya Mashariki ya Marekani.
Wakati huo huo, shirika la ndege la Delta Air Lines linapanga kuanza safari za moja kwa moja kati ya Atlanta, Marekani, na Riyadh Oktoba 23.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ed Bastian, aliwahi kusema kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu kurejesha safari hizo utategemea masuala ya usalama.
Delta bado haijajibu ombi la shirika la habari la Reuters la kutoa maoni kuhusu onyo la FAA.
Unaweza pia kusoma:
China: Mashambulizi ya Riyadh yanatia wasiwasi mkubwa

Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imelaani Jumatatu hii mashambulizi dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Riyadh, Saudi Arabia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning, amewaambia waandishi wa habari mjini Beijing Jumatatu kuwa serikali ya China inaeleza "wasiwasi mkubwa" kuhusu kuongezeka kwa mzozo huo.
Mashambulizi dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Riyadh yaliendelea Jumapili.
Maafisa wa Saudi Arabia wamesema mtu mmoja aliuawa na wengine 11 kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa na waasi wa Houthi Jumapili katika uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Riyadh. Hilo lilikuwa shambulizi la tatu lililosababisha vifo katika uwanja huo ndani ya siku nne.
Watu 13 waliuawa katika shambulizi la Jumamosi.
Takribani safari zote za ndege kutoka uwanja huo zimefutwa. Waasi wa Houthi nchini Yemen, wanaoungwa mkono na Iran, wameonya mashirika ya ndege na wasafiri dhidi ya kutumia anga ya Saudi Arabia.
Houthi pia walitangaza kuwa walilenga Uwanja wa Ndege wa Dammam, mashariki mwa Saudi Arabia, pamoja na miundombinu ya mafuta ya nchi hiyo.
Msemaji wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia amesema vikosi vya muungano huo vimefanikiwa kuzuia na kuharibu ndege kadhaa zisizo na rubani pamoja na makombora ya Houthi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) pia imeyashauri mashirika ya ndege ya Marekani kuchukua tahadhari yanaposafiri kuelekea Saudi Arabia au kupitia anga ya nchi hiyo.
Unaweza pia kusoma:
Urusi imekishambulia kiwanda cha umeme cha Kharkiv 'mara baada ya' Trump kusimamisha mapigano

Chanzo cha picha, Getty Images
Zelensky anasema jana usiku viwanda vya kusafisha mafuta vya Urusi "havikuwa vikiteketea", lakini usiku wa manane, Urusi ilikishambulia kituo cha uzalishaji wa gesi nchini Ukraine na pia kulikuwa na mashambulizi kwenye kituo cha kawaida cha mafuta yaliyohusisha "droni kadhaa".
"Hili ndilo jibu la Putin kwa Trump: mashambulizi ya Urusi," anasema.
Ukraine inasubiri maelezo zaidi kuhusu mazungumzo kati ya Wamarekani na Warusi, Zelensky ameongeza, akimaanisha makubaliano ya Trump ya dizeli aliyotangaza wiki iliyopita.
"Usitishaji huu wa mapigano ya unaohusisha nishati unaweza kutekelezwa na unaweza kuwa hatua kubwa kuelekea kukomesha vita, ikiwa Wamarekani wataingilia kati kweli sasa na kuhakikisha Warusi wanaheshimu usitishaji wa mapigano wa nishati," anasema, akiongeza kuwa"anaishukuru" Marekani.
Unaweza pia kusoma:
Mtawa ashtakiwa kwa kujaribu kumfanyia unyanyasaji wa kingono mwanamke Mfaransa

Chanzo cha picha, Getty Images
Kijana wa kike Mfaransa anayetembelea Sri Lanka amedai kwamba mtawa mmoja katika hekalu katika eneo la Tangalle alijaribu kufanya uhalifu wa kingono dhidi yake.
Mtawa husika amekamatwa na kufikishwa mahakamani kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na mwanamke huyo kijana na mwenzake Mjerumani katika Polisi wa Tangalle.
Mwanamke huyo kijana anasema nini?
Mwanamke huyo Mfaransa mwenye umri wa miaka 32 ambaye inadaiwa alikumbana na tukio hili anasema kwamba mnamo Oktoba 2, alienda kwenye hekalu lililoko takriban dakika 10 kutoka mahali alipokuwa akiishi, kwa nia ya kutafakari.
Anasema "Kwa kuwa sikuweza kupata mahali pa kutafakari au kuabudu, nilimuuliza mtawa kuhusu hilo. Aliniomba niende naye na akanipeleka kwenye jengo dogo lenye sanamu kubwa ya Buddha. Ilibainika kuwa jengo hilo kwa kawaida lilikuwa limefungwa...
Ndani ya [jengo], mtawa alikaribia sana nyuma yangu, niliweza kumhisi akipumua. Nilihisi vibaya, kwa hivyo nilitoka chumbani. Kisha akasema kwamba chumba cha maombi kilikuwa mahali pengine, na akaniomba nimfuate tena. Aliniongoza zaidi ndani ya jengo, kwenye korido ndefu na yenye giza.
Kadri usumbufu niliohisi ulivyoongezeka, niliamua kugeuka na kutoka nje. Kisha mtawa akanifuata na kunishika mkono. Nilijitahidi na kutoroka.
Nilikimbia ili kutoka nje ya jengo. Alinifuata moja kwa moja na kunishika tena. Nilipiga kelele kwa sauti kubwa nilipokuwa nikijaribu kuondoka. Aliendelea kujaribu kuninyamazisha kwa kusema "Nyamaza, nyamaza/nyamaza". Alinisukuma ukutani na kushikilia mabega yangu ukutani, akinizuia kutoka.
"Nilipigana kwa bidii niwezavyo, na hatimaye nikafanikiwa kumtoroka na kutoka nje ya jengo. Hakutoka nje kunifuata."
Unaweza pia kusoma:
Wahamiaji 139, wakiwemo watoto, wafariki baada ya boti kuzama pwani ya Djibouti

Chanzo cha picha, IOM
Maelezo ya picha, Wafanyakazi wa IOM wakiwapokea wahamiaji karibu na Guhere, kaskazini mwa mji wa bandari wa Obock. Takriban wahamiaji 139, wakiwemo watoto 15, wamefariki baada ya boti yao kuzama karibu na pwani ya Djibouti, huku wengine wengi wakiwa hawajulikani walipo, kulingana na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa(IOM).
Boti hiyo ilikuwa imeondoka Djibouti, kuelekea Yemen, na ilikuwa imebeba watu 305 ilipozama Alhamisi usiku, karibu na mji wa bandari wa Obock.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) linaema kwamba takriban watu 82 wameokolewa.
Alexandre Coissac, mkuu wa ofisi ya IOM huko Djibouti, alilitaja janga hilo "ukumbusho dhahiri" wa hatari zinazowakabili wahamiaji wanapotafuta maisha mapya kwingineko.
Shirika hilo lilisema kwamba kila mwaka makumi ya maelfu ya wahamiaji kutoka Pembe ya Afrika hufanya safari hii hatari, wakitarajia kufika nchi za Ghuba kwa usalama na kazi.
Siku ya Jumapili IOM ilisema idadi ya vifo iliongezeka kutoka 109 hadi 139, baada ya miili ya watu wengine 30 kupatikana.
"Ni hasara ya kusikitisha sana ya maisha," alisema Coissac.
Unaweza pia kusoma:
Mtu mmoja afariki katika shambulio jipya kwenye uwanja wa ndege wa Saudi Arabia, siku moja baada ya shambulio la Wahouthi kuwaua watu 13

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtu mmoja ameuawa na karibu watu kumi na wawili kujeruhiwa katika shambulio jipya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Riyadh siku ya Jumapili, mamlaka ya Saudi Arabia iliripoti.
Shambulizi hili linakuja siku moja baada ya shambulio lingine lililodaiwa kutekelezwa na Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen ambalo liliua watu 13 na kujeruhi zaidi ya 300.
Vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen vilisema kombora lisilojulikana lililenga kituo cha 4 cha uwanja wa ndege wa kimataifa wa Riyadh siku ya Jumapili, na kusababisha moto. Watu kumi na mmoja walijeruhiwa ambapo mtu mmoja aliawa mamlaka ya usafiri wa anga ya Saudi Arabia ilisema.
Vikosi vya muungano pia vilisema ulinzi wa anga wa Saudi Arabia ulinasa kombora la kitalii karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid.
Baadaye waliongeza kuwa ndege isiyo na rubani pia ilikamatwa na kuharibiwa katika Mkoa wa Mashariki wa nchi hiyo, na kombora la balestiki lililorushwa kuelekea Khamis Mushait lilikuwa limedunguliwa pia.
Tahadhari za dharura pia zilitolewa huko Abha, kusini, mapema Jumatatu lakini hatari hiyo ilikuwa imepita tangu wakati huo, Ulinzi wa Raia wa Saudi Arabia ulisema.
Mashambulizi hayo yamefichua udhaifu katika uwezo wa ulinzi wa Saudi Arabia huku ufalme ukiendesha kampeni ya anga dhidi ya Wahouthi, ambao wanapigana vita vya ardhini nchini Yemen dhidi ya serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia.
Unaweza pia kusoma:
Shirikisho la Soka la Ureno limemchukulia hatua za kinidhamu Ronaldo, kulikoni?

Chanzo cha picha, Getty Images
Cristiano Ronaldo amesimamishwa kwa muda na Shirikisho la Soka la Ureno (FPF) baada ya kuondoka katika kambi ya timu yake ya taifa mwezi uliopita.
Nahodha huyo mwenye umri wa miaka 41 alijiondoa kwenye kikosi cha Ligi ya kuu ya taifa ya Ureno mnamo Septemba baada ya kuachwa nje ya kikosi kilichocheza mechi dhidi ya Norway na kugundua kuwa hangeanza mechi dhidi ya Denmark.
Katika taarifa ndefu kwa vyombo vya habari, mshambuliaji huyo wa Al-Nassr baadaye alieleza kwamba aliondoka kwa sababu kocha wa Ureno Jorge Jesus "alikuwa amevunja ahadi yake" mara mbili, akimshutumu kwa "uvunjaji wa uaminifu wa waziwazi".
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na FPF ilisema kwamba "kikwazo cha muda" kiliwekwa kwa mchezaji huyo mnamo Oktoba 9, na kwamba kesi hiyo iliainishwa kama "ya dharura".
Sheria za FPF zinasema kwamba mchezaji yeyote ambaye atashindwa kuripoti au kuacha kazi ya timu ya taifa anaweza kukabiliwa na kusimamishwa kwa kati ya mwezi mmoja na sita, pamoja na faini ya kifedha.
Rais wa FPF, Pedro Proenc, aliliambia gazeti la Ureno Record: "Ni wakati ambapo utulivu unahitajika. Sote tumeketi mezani."
"Kuna hamu kubwa ya kumrudisha nahodha wetu. Kutakuwa na mchakato wa kawaida wa nidhamu." alisema.
Unaweza pia kusoma:
Wachimbaji dhahabu kadhaa wauawa katika mashambulizi kwenye mpaka wa Misri na Sudan, kundi la haki za binadamu lasema

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais takriban 72 waliokuwa wakitafuta dhahabu katika eneo la mpakani mwa Sudan wameuawa katika mashambulizi ya anga, kundi la haki za binadamu la kikanda linasema.
Taasisi ya haki za binadamu Emergency Lawyers, yenye makao yao makuu katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, walisema ndege za kivita ziliwalenga wachimbaji madini wa kitaalamu katika maeneo maarufu ya uchimbaji wa dhahabu katika jimbo la Mto Nile nchini Sudan siku ya Jumamosi.
Serikali ya Misri wala mamlaka ya Sudan hazijatoa maoni hadi sasa kuhusina na tukio hilo.
Hapo awali Cairo imekabiliwa na tuhuma za mashambulizi makali dhidi ya wachimbaji dhahabu kama sehemu ya msako dhidi ya shughuli haramu katika mpaka wake wa kusini.
Emergency Lawyers ilibainisha madai ya mashambulizi ya awali na kusema hayakuwa tu ukiukaji wa eneo huru la Sudan bali pia yalionyesha ukosefu wa udhibiti wa serikali katika eneo hilo.
"Kulenga raia wasio na silaha kimakusudi kunakiuka sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki ya kuishi," ilisema katika taarifa Jumapili. "Vitendo hivi vinaweza kuwa uhalifu wa kivita."
Ilibainisha kuwa idadi ya vifo vyake ilikuwa ya muda na inaweza kuongezeka.
Gazeti la Sudan Tribune la jijini Paris liliripoti kwamba idadi ya vifo inaweza kuzidi idadi iliyoripotiwa taasisi ya Emergency Lawyers, likimnukuu manusura wa shambulio la Jumamosi ambaye alisema watu wengi zaidi wamejeruhiwa.
Unaweza pia kusoma:
Zelensky akaribisha mpango wa Trump wa kusitisha mashambulizi, je Putin atajibu?

Chanzo cha picha, Getty Images
Donald Trump amedai kwamba Urusi na Ukraine zimekubaliana kuhusu "kusitishwa kwa mapigano ya nishati", huku Kyiv ikisema itaunga mkono hatua kama hiyo lakini Moscow bado haijatoa maoni.
Rais wa Marekani alisisitiza kwamba " unaanza kutekelezwa mara moja" lakini hakutoa maelezo yoyote.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky awali alielezea kushangazwa na tangazo hilo, kabla ya kusema Kyiv ingeunga mkono ikiwa Moscow ingeunga mkono. Pia aliishutumu Urusi kwa kushambulia vituo vya nishati vya Ukraine baada ya ujumbe wa Trump.
Trump amekuwa akiihimiza Ukraine kusimamisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Urusi - ambayo Kyiv inasema ni muhimu katika kupunguza mapato ya yatokanayo na vita ya Moscow, ili Urusi iweze kutimiza makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni ya kutoa dizeli kwa Marekani na soko la kimataifa.
Mkataba huo wa dizeli, unaofutia vikwazo vya Urus , umekosolewa. Rais Zelensky aliuita zawadi kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin. Maafisa wa Ulaya na baadhi ya wanasiasa wa Marekani, wakiwemo kutoka chama cha Republican cha Trump, wamesema hawauungi mkono.
Mkataba huo ni juhudi za hivi karibuni za Trump za kupunguza bei ya mafuta ya ndani ya Marekani kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula, baada ya kutumia miezi kadhaa akikabiliana na athari za kisiasa za vita na Iran ambavyo vimeongeza bei za mafuta duniani, hasa zile za dizeli.
Hilo limechafua sifa ya Trump miongoni mwa umma wa Marekani, ambao wamechoshwa na bei za juu za pampu na athari mbaya zilizosababisha mfumuko wa bei kwa wote.
Unaweza pia kusoma:
Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara tukikuletea taarifa za kikanda na kimatafa.



















