Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Lazima tulipize kisasi mauaji ya Ali Khamenei - Iran

Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, ameapa "kulipiza kisasi damu ya baba yake isiyo na hatia," akiongeza kuwa ni jukumu la taifa hilo kulipiza kisasi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Lazima tulipize kisasi kifo cha Ali Khamenei - Mojtaba Khamenei

    Kiongozi Mkuu wa Iran,Mojtaba Khamenei, amesema kuwa lazima walipize kisasi kifo cha baba yake, Ali Khamenei, akisema hayo ni "matakwa ya taifa" na "lazima yatimizwe."

    Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Telegram, baada ya kukamilika kwa mazishi ya babake aliyekuwa kiongozi wa awali wa Iran, Ali Khamenei.

    Taarifa ya Mojtaba ilisema kuwa:

    "Tunaahidi kulipiza kisasi damu ya kiongozi shahidi mashahidi wote wa vita hivi, kutoka kwa wauaji na wahalifu waliomvunjia heshima."

    Mojtaba Khamenei, ambaye alichukua nafasi ya Kiongozi Mkuu wa Iran baada ya kifo cha baba yake, hakuhudhuria mazishi ya baba yake.

    Soma pia:

  2. Algeria yafungua anga zake kwa safari za ndege kutoka Mali

    Algeria imefungua tena anga zake kwa safari za ndege kutoka Mali, kuanzia hapo jana, na kuruhusu safari zote za ndege zinazoenda na kutoka nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

    Nchi hizo mbili zilikuwa zimefunga anga zao kwa ndege za kila upande mwezi Aprili mwaka wa 2025, baada ya Algeria kusema kuwa jeshi lake lilidungua ndege isiyo na rubani ya upelelezi ya Mali iliyoingia katika anga zake.

    Mali ilipinga tuhuma hizo za Algeria, ikisema kuwa ndege hiyo ilianguka ndani ya eneo la Mali.

    Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, mapema leo pia ameamuru kurejea kwa balozi wa nchi yake katika mji mkuu wa Mali, Bamako.

    Algeria ilikuwa imemuondoa balozi wake kutoka Mali mwezi Aprili mwaka uliopita, kufuatia mzozo wa kidiplomasia ulioibuka kati ya nchi hizo mbili.

    Soma pia:

  3. Watu 17 walifariki katika mashambulizi yaliyotekelezwa na Marekani nchini Iran

    Wizara ya Afya ya Iran imeripoti kuwa watu 17 waliuawa na wengine 115 kujeruhiwa katika mashambulizi ya hivi karibuni yaliyotekelezwa na Marekani.

    Hossein Kermanpour, mkuu wa babari katika Wizara ya Afya ya Iran, amesema kuwa watu 17, akiwemo mwanamke mmoja, waliuawa katika mashambulizi ya Marekani yaliyolenga miji sita.

    Baadhi ya waliojeruhiwa tayari wameondoka hospitalini baada ya kupokea matibabu.

    Marekani ilitekeleza mashambulizi dhidi ya maeneo mbalimbali ya Iran ikiwemo Bandar Abbas, kisiwa cha Qeshm, Sirak, Chabahar na Bushehr.

    Mashambulizi hayo yalitokea baada ya meli tatu za kibiashara kulengwa katika mlango bahari wa Hormuz.

    Soma pia:

  4. Emmanuel Wanyonyi avunja rekodi ya miaka 27 ya mbio za mita 1000

    Mwanariadha wa Kenya Emmanuel Wanyonyi ameweka rekodi mpya ya dunia katika mbio za mita elfu moja baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya Diamond League yaliyofanyika Monaco.

    Wanyonyi alivunja rekodi kwa kumaliza mbio hizo kwa muda wa dakika 2:11.83, nakuipiku rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na Mkenya mwenzake Noah Ngeny kwa tofauti ya sekunde 0.13.

    Rekodi ya Ngeny ilikuwa imedumu kwa miaka 27.

    Mafanikio hayo yamemweka Wanyonyi katika historia ya riadha duniani, na kumfanya kuwa mwanamume wa pili katika historia kumaliza mbio hizo kwa muda wa chini ya dakika 2 na sekunde 12.

    Soma pia:

  5. Watu 10 wajeruhiwa baada ya Urusi kuishambulia Kyiv

    Watu 10 wamejeruhiwa baada ya Urusi kuishambulia mji Kyiv, nchini Ukraine, kwa makombora ya balistiki mapema hii leo.

    Shambulio hilo limefanyika wakati Kyiv inasubiria kupokea vifaa vipya vya ulinzi wa anga, huku kukiwa na uhaba ambao umeacha mji huo katika hatari zaidi ya mashambulizi ya Urusi.

    Kulingana na shirika la habari la Reuters, raia wa mi huo aliwaambia kuwa alisikia milipuko kadhaa mikubwa katika jiji hilo mwendo wa alfajiri kabla ya tahadhari ya mashambulizi ya anga kutolewa na Ukraine.

    Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi ilirusha makombora sita ya balistiki, makombora sita ya masafa marefu na ndege 121 zisizo na rubani.

    Jeshi hilo limesema liliweza kudungua angalau makombora mawili ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani 111 zilizokuwa zikilenga maeneo mbalimbali nchini humo.

    Soma pia:

  6. Moto wa nyika Uhispania wasababisha vifo vya watu 12

    Moto mkubwa wa nyika unaoshuhudiwa kusini mashariki mwa Uhispania umesababisha vifo vya watu 12, wakiwemo raia wanne wa Uingereza, huku watu 23 wakiripotiwa kutoweka.

    Moto huu unaripotiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa Uhispania.

    Mamia ya wazima moto pamoja na wataalamu wengine wametumwa katika mji wa Bidar kusini mashariki mwa Uhispania, kujaribu kudhibiti moto huo ambao unateketeza misitu.

    Mamlaka za eneo la Los Gallardos katika jimbo la Almeria zimeonya kuwa idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka.

    Hispania inaendelea kushuhudia joto kali ya viwango vya juu na hata kufikia nyuzi joto 40, na hii imechochea visa vya moto wa nyika kuripotiwa maneo tofauti kusini mwa Ulaya hasa Ufaransa, Ureno na Uhispania.

  7. Iran na Oman kujadili kuhusu usalama wa Mlango bahari wa Hormuz

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, amewasili mjini Muscat, Oman, kwa mazungumzo na maafisa wa serikali ya Oman.

    Kulingana na vymbo vya habari vya eneo hilo, Waziri huyo anatarajiwa kuongoza mazungumzo kati ya Iran na Oman kuhusu mlango bahari wa Hormuz

    Pande hizo mbili zinatarajiwa kuja na utaratibu utakaohakikisha meli zinapita kwa usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, kwa kuzingatia Kifungu cha 5 cha Hati ya Makubaliano ya Islamabad.

    Ziara hiyo inafanyika wakati mvutano kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz umeongezeka katika siku za hivi karibuni kufuatia mashambulizi kati ya Marekani na Iran.

    Hayo yakijiri, ujumbe wa wapatanishi kutoka Qatar umesafiri kwenda Iran kwa lengo la kuweka mazingira ya kuanza tena mazungumzo kati ya Iran na Marekani pamoja na kupunguza mvutano kati ya pande hizo mbili.

    Soma pia:

  8. Zaidi ya wanafunzi 25 waliotekwa nyara waokolewa Nigeria

    Ikulu ya Nigeria imetoa taarifa kuwa vikosi vya usalama vimewaokoa zaidi ya wanafunzi 25 pamoja na walimu kadhaa waliokuwa wametekwa nyara na watu waliojihami katika jimbo la Oyo mwezi Mei.

    Msemaji wa Rais wa Nigeria, Bayo Onanuga, amechapisha picha za baadhi ya wanafunzi waliotekwa nyara kutoka shule tatu zilizoko eneo la Oriyere.

    Ikulu ya Nigeria imesema hakuna fedha za fidia zilizolipwa ili kuwaachia mateka hao, na kwamba watu wanane wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi lililohusika na utekaji huo wamekamatwa.

    Visa vya utekaji nyara wa wanafunzi umekuwa ukishuhudiwa mara kwa mara kaskazini mwa Nigeria huku vyama vya walimu na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yakitaka serikali kuimarisha ulinzi shuleni.

    Soma pia:

  9. Trump atishia kuiangamiza Iran, iwapo watajaribu kumuua

    Rais wa Marekani Donald Trump ameionya serikali ya Iran kwamba Marekani itafanya mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya Iran ikiwa itachukua hatua yoyote ya kuhatarisha maisha yake au kujaribu kumuua.

    Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump aliandika, "Makombora elfu moja yako tayari na yameelekezwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ikiwa tishio la serikali ya Iran la kumuua Rais wa Marekani litatekelezwa, makombora zaidi ya elfu moja yatafyatuliwa mara moja."

    Trump pia alisema kuwa ametoa maagizo yanayohitajika na kwamba jeshi la Marekani liko tayari "kuangamiza kabisa maeneo yote ya Iran" kwa kipindi cha mwaka mmoja.

    Kauli ya Trump inajiri kufuatia ripoti za ujasusi kutoka Israel zinazodai kuwepo kwa njama mpya ya Iran ya kutaka kumuua Trump, pamoja na picha na mabango zilizoonekana wakati wa mazishi ya Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei.

    Maafisa wa Iran wamekanusha kuwepo kwa mpango wowote wa kumuua Trump.

    Soma pia:

  10. Hatujaomba kufanya mazungumzo na Marekani - Iran

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Iran, Esmail Baghaei, amesema kuwa Tehran haijaomba kufanya mazungumzo na Marekani, lakini imekubali ombi la mpatanishi mmoja wa kikanda kutembelea Iran na kujadili matukio yaliyojiri hivi karibuni.

    Akizungumza katika mahojiano ya televisheni, Baghaei alisema kuwa "Hatukuomba kufanya mazungumzo na Marekani, lakini kwa kuzingatia msimamo wetu wa kuwajibika, hatukukataa ombi la mmoja wa wapatanishi wa kikanda kuja Iran na kujadili hali ya sasa. Ziara hiyo tayari ilifanyika mjini Mashhad, na tuliwasilisha maoni na misimamo yetu kwa upande wa Qatar."

    Msemaji huyo aliongezea kuwa "Marekani imekuwa ikikiuka mara kwa mara vipengele mbalimbali vya makubaliano hayo katika kipindi hiki."

    Baghei alifafanua kuwa matukio ya Jumatano na Alhamisi yalikuwa ukiukaji wa kifungu cha kwanza na cha pili cha makubaliano ya kusitisha mapigano walioafikia na Marekani, huku uamuzi wa kufuta kibali cha kuuza mafuta ya Iran pia ukiwa ukiukaji mkubwa wa kifungu kingine cha makubaliano hayo.

    Kulingana na Baghaei, kuwekewa kwa Iran vikwazo vipya na Marekani ni kinyume na Kifungu cha 9 cha hati hiyo ya makubaliano.

    Hapo jana Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa Iran imewaomba wafanye mazungumzo ya kupata amani na kutangaza kuwa amefutilia mbali usitishaji mapigano.

    Soma pia:

  11. Marekani yaitaka Iran kusitisha mashambulizi katika mlango bahari wa Hormuz

    Marekani inaitaka Iran itangaze wazi kuwa Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi kwa usafiri wa majini na iache kushambulia meli za kibiashara, kama sehemu ya mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika nchini Omanhii leo.

    Vyombo vya habari vya Marekani vimewanukuu maafisa ambao hawakutajwa majina wakisema kwamba Tehran ilikubali kuwa mashambulizi ya meli yalikuwa makosa, huku maafisa hao wa Iran wakidai mashambulizi hayo yalitekelezwa na kundi la waasi nchini humo.

    Trump amesema pande zote mbili zimekubaliana kuendelea na mazungumzo licha ya mapigano ya wiki hii kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz, ambayo Ikulu ya Marekani iliona kuwa yalikiuka makubaliano ya usitishaji mapigano.

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, amesema nchi yake "imetimiza ahadi yake" kuhusu usitishaji mapigano, akidai kupitia mtandao wa X kwamba Marekani ndiyo iliyokiuka makubaliano hayo.

    Mwezi Juni, Marekani na Iran zilitia saini makubaliano ya usitishaji mapigano ambapo, miongoni mwa masharti yake, Iran ilikubali kuhakikisha meli za kibiashara zinapata njia salama ya kupita kutumia Mlango bahari wa Hormuz.

    Soma pia:

  12. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumamosi ya leo