Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini ndege za Urusi zinadondosha mabomu katika himaya yake?
Mlipuko mkubwa ulitikisa mji wa Belgorod nchini Urusi usiku wa tarehe 20 mwezi Aprili 2023.
Video za kamera za CCTV kutoka eneo hilo zinaonyesha sauti kali ya mluzi, inayofanana na sauti ya injini ya ndege ya kivita.
Mara tu baada ya sauti hiyo, kulitokea mlipuko mkubwa. Mlipuko huo ulikuwa na nguvu kiasi kwamba ulitengeneza shimo kubwa katikati ya eneo la makazi, na gari moja lilirushwa hewani na kuanguka juu ya paa la duka.
Mlipuko wa Belgorod ni tukio lililoandikwa vizuri linalohusishwa na ndege ya kivita ya Urusi kudondosha bomu kimakosa kwenye eneo lake yenyewe, huenda kwa sababu ulitokea ndani ya mji mkubwa.
Hata hivyo, watafiti wanadai kuwa kuna mamia ya matukio mengine kama hayo ambayo mamlaka ya Urusi yanataka kuyaficha.
Chombo huru cha habari cha Astra kinakadiria kuwa ndege za kivita za Urusi zimedondosha kwa bahati mbaya angalau mabomu 334 ndani ya Urusi au maeneo ya Ukraine yanayokaliwa na Urusi tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulipoanza Februari 2022. Kulingana na Astra, angalau mabomu 26 yamedondoshwa kwa njia hiyo mwaka huu pekee.
Mhariri mkuu wa Astra, Anastasia Chumakova, alisema kuwa idadi hiyo ni makadirio ya tahadhari, yakijumuisha tu matukio yaliyothibitishwa na vyanzo vya huduma za dharura, mashahidi wa macho au ushahidi wa maandishi na picha.
"Nadhani idadi halisi ni kubwa zaidi sana," aliiambia BBC.
Katika moja ya matukio ya hivi karibuni, treni ya abiria ilitoka kwenye reli baada ya bomu kudondoka kwenye njia ya reli. Katika tukio jingine, mwanaume mmoja aliuawa baada ya bomu kudondoka kwa bahati mbaya kwenye nyumba yake. Matukio yote mawili yaliripotiwa mwezi Mei katika eneo la Yaroslavl nchini Urusi, linalopakana na Ukraine.
Idadi kubwa ya silaha zinazorushwa kutoka kwenye ndege za kivita za Urusi ni mabomu ya kuruka kwa kuelekezwa (glide bombs). Mabomu haya hutumia vifaa vipya vilivyotengenezwa ambavyo huongezwa kwenye mabomu hayo ili kuweka sehemu zinazofanana na mabawa zinazoweza kufunguka na kusaidia bomu kuruka kuelekea lengo lake.
Lengo la kutengeneza mabomu haya ya kuruka kwa kuelekezwa (glide bombs) ni kuzipa ndege za kivita za Urusi uwezo wa kushambulia malengo nchini Ukraine zikiwa ndani ya anga lao wenyewe, mbali na uwezo wa mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine.
Yakiwa yamewekewa kifaa cha kurushia na kuelekeza kinachojulikana kama UMP glide kit, mabomu haya hufikia malengo yake kwa kuruka angani kwa mtindo wa kuelea.
Hata hivyo, mabawa ya kifaa hicho cha kuelekeza yanaposhindwa kufunguka baada ya bomu kurushwa, mabomu hayo huanguka ndani ya eneo la Urusi.
Ruslan Loyev, mkuu wa kikundi huru cha uchunguzi kinachoitwa Conflict Intelligence Team, anaamini kuwa sababu mojawapo inayowezekana ni hitilafu katika vilipuzi vinavyoanzisha mfumo wa chemchemi, ambapo chemchemi hiyo ndiyo hufungua sehemu zinazofanana na mabawa za kifaa cha kuelekeza cha bomu la kuruka.
"Mabomu kama hayo huwa mabomu ya kawaida tu yanayoanguka chini badala ya kuwa silaha za masafa marefu zinazoweza kuruka kuelekezwa," aliiambia BBC.
Zaidi ya mabomu 300 ni idadi kubwa, lakini Ruslan Loyev anasema kiwango cha mabomu yanayopotea si cha ajabu ukilinganisha na jumla ya mabomu ya kuruka kwa kuelekezwa (glide bombs) ambayo Urusi imeyatumia.
"Hili ni jambo la kawaida katika vita. Wakati mwingine hata mifumo ya kisasa zaidi hupata hitilafu," alisema.
Anaamini kuwa idadi iliyotolewa na Astra si kubwa sana. Anakadiria kuwa huenda idadi hiyo iko kati ya mabomu 100 na 200 kwa mwaka, lakini Urusi hutumia zaidi ya mabomu 6,000 ya aina hiyo kila mwezi.
Kwa mujibu wa Pavel Aksyonov, mwandishi wa masuala ya ulinzi na anga wa Huduma ya Kirusi ya BBC, kuendelea kutumwa kwa ndege za mabomu za Urusi kunaweza pia kuwa sababu ya hitilafu hizi.
Anasema kuwa katika hali kama hiyo, ubora wa matengenezo ya ndege hupungua.
"Hali moja ni kwamba unarudi kutoka kwenye misheni ya kivita, kisha wataalamu wanakagua ndege yako kwa siku kadhaa zinazofuata. Lakini unapomaliza misheni ya kivita na mara moja unatumwa kwenye misheni nyingine, hiyo ni hali tofauti kabisa. Hali hiyo husababisha hitilafu nyingi," alisema.
Watafiti wanasema kuwa matukio mengi ya mabomu kudondoka kwa bahati mbaya hutokea katika eneo la Belgorod nchini Urusi, linalopakana na eneo la Kharkiv nchini Ukraine ambalo lina viwanda vingi. Maeneo hayo yanaaminika kuwa ndiyo yanayolengwa na mabomu ya Urusi ya kuruka kwa kuelekezwa yanayorushwa kutoka upande wa pili wa mpaka.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye akaunti ya Telegram ya Oleh Syniehubov, mkuu wa utawala wa jimbo la Kharkiv, Urusi imefanya mashambulizi 473 kwa kutumia mabomu ya kuruka kwa kuelekezwa katika eneo hilo tangu mwanzo wa mwaka 2026 hadi tarehe 29 Juni.
Mabomu yanayodondoka kwa bahati mbaya karibu hayakubaliwi kamwe rasmi nchini Urusi, na mamlaka hujaribu kuficha suala hilo. Usiri unaolizunguka jambo hili unafanya iwe vigumu kutathmini athari zake halisi.
Ripoti zinaonyesha kuwa, mbali na hasara za kifedha, raia wengi waliuawa na kujeruhiwa katika matukio haya. Hata hivyo, mradi mabomu ya kuruka kwa kuelekezwa (glide bombs) yataendelea kuwa miongoni mwa silaha zenye ufanisi mkubwa na zinazotumiwa sana katika ghala la silaha la Urusi, Urusi itaendelea kukubali hasara hizo kama gharama ya kuendeleza vita vyake dhidi ya Ukraine.