Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, 'Marekani iko tayari kuanza tena mashambulizi dhidi ya Iran ikiwa hakuna makubaliano'

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amesema 'uwezo wetu wa kuanza upya mashambulizi inapobidi...tunao na tuko tayari sana'.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Kocha wa Liverpool afutwa kazi

    Kocha wa Liverpool Arne Slot amefutwa kazi baada ya kuwa naye kwa misimu miwili.

    Mholanzi Arne Slot, mwenye umri wa miaka 47, aliwaongoza Reds kutwaa taji lao la 20 la ligi katika msimu wake wa kwanza lakini wamejitahidi katika mwaka wake wa pili, wakimaliza katika nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu.

    Kocha wa Bournemouth aliyeondoka hivi karibuni, Andoni Iraola, ndiye anayeongoza kati ya wanaopigiwa upatu kuchukua nafasi ya Slot.

    "Huu ulikuwa uamuzi mgumu kwetu kama klabu. Mchango wa Arne ndani ya Liverpool FC katika kipindi ambacho amekuwa nasi umekuwa muhimu, wenye maana na – cha msingi zaidi kwa mashabiki na sisi wenyewe - wenye mafanikio," wamiliki wa Liverpool Fenway Sports Group (FSG) walisema katika taarifa.

    "Kwa hivyo, shukrani zetu kwa kila kitu alichofanikisha, haswa katika maadili ya kazi, bidii na kiwango cha utaalamu ambacho kilisisitiza zaidi mtazamo wetu kwamba yeye ni kiongozi katika tasnia yake."

    "Tangu tulipokutana na Arne kwa mara ya kwanza, ilikuwa wazi mara moja kwamba yeye ni mtu ambaye hakubali tu jukumu, bali analikumbatia."

    Uamuzi huo ulifanywa na Michael Edwards, mtendaji mkuu wa FSG, na Richard Hughes, mkurugenzi wa michezo wa Liverpool.

    Katika msimu mzima, Liverpool ilisisitiza kwamba mabadiliko ya kocha mkuu hayakuwa kwenye ajenda, lakini baada ya kutathmini hali baada ya mwisho wa msimu wikendi iliyopita, uongozi wa klabu hiyo unaamini awamu inayofuata inahitaji mtindo wa soka ulioimara zaidi, wa kisasa na kwa haraka.

    Slot alichukua nafasi ya Jurgen Klopp kama kocha wa Liverpool mwaka wa 2024 baada ya Mjerumani huyo kujiuzulu Anfield baada ya miaka tisa kama meneja.

    Mapema mwezi huu, mshambuliaji Mohamed Salah alisema klabu hiyo lazima irudi kuwa "timu ya ushambuliaji wa kiwango cha juu ambayo wapinzani wanaiogopa" baada ya "kushindwa" na Aston Villa.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Katika Picha: Baadhi ya wazazi washindwa kujizuia walipokuwa wakitazama miili ya wapendwa wao Kenya

    Utambuzi wa DNA kwa watoto wa shule waliochomeka moto unaendelea nchini Kenya.

    Baadhi ya wazazi walishindwa kujizuia walipokuwa wakitazama miili ya wapendwa wao.

  3. Uchunguzi wa DNA kwa watoto wa shule 16 waliochomeka moto unaendelea Kenya

    Uchunguzi wa DNA kwa watoto wa shule 16 waliochomeka moto unaendelea Kenya na kufikia sasa, ni familia tatu pekee zilizoweza kutambua wapendwa wao huku miili mingine ikihitaji kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba zaidi.

    Vyanzo vya habari kuhusu mchakato huo vilivyozungumza na BBC kwa sharti la kutotajwa majina vilisema miili mitatu kati ya kumi na sita iliteketea kiasi cha kutotambulika, jambo linaloonyesha ukubwa wa mkasa uliotokea wakati bweni la shule liliposhika moto.

    Hisia zilijitokeza wakati jamaa waliokuwa wamekusanyika katika kituo cha utambulisho katika makafani ya Naivasha walipokuwa wakitazama miili ya wapendwa wao huku maafisa wakikamilisha mchakato wa kuweka kumbukumbu.

    Uchunguzi wa chanzo cha moto huo mbaya bado unaendelea. Polisi wamewakamata wanafunzi wanane kwa tuhuma za kuchoma shule hiyo.

    Soma zaidi:

  4. Marekani iko tayari kuanza tena mashambulizi dhidi ya Iran ikiwa hakuna makubaliano - Waziri wa Ulinzi

    Marekani iko tayari kuanzisha upya mashambulizi dhidi ya Iran ikiwa makubaliano hayatafikiwa, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth amesema leo Jumamosi, huku wapatanishi kutoka Marekani na Iran wakijitahidi kupunguza tofauti kubwa zinazozuia makubaliano.

    "Uwezo wetu wa kuanza upya inapobidi...tunao na tuko tayari sana," Hegseth alisema akiwa Singapore.

    "Hifadhi zetu za silaha ziko imara zaidi kwa hilo, huko na kote ulimwenguni, kwa hivyo tumejipanga vizuri," ameongeza.

    Hegseth, akizungumza hayo katika kongamano kuu la Asia kwa viongozi wa ulinzi, wanajeshi na wanadiplomasia, alisema Marekani haijalipa kisogo eneo la Asia-Pasifiki.

    "Tunaweza kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja. Tunaongeza nguvu zaidi katika kituo chetu cha ulinzi ili tuwe na silaha mara 2, 3, 4 zaidi hivi karibuni ili kuhakikisha kwamba mipango yetu yote (ya operesheni) inafadhiliwa ipasavyo kote ulimwenguni," alisema.

    Hegseth alisema Rais Donald Trump alikuwa "mvumilivu" na anataka kufanya "makubaliano makubwa" ambayo yatahakikisha Iran haipati silaha.

    Soma zaidi:

  5. Marekani yaonyesha matumaini licha ya pingamizi la ujenzi wa kituo cha Ebola Kenya

    Serikali ya Marekani imeelezea matumaini yake kuwa itasuluhisha wasiwasi uliozushwa juu ya mipango ya kuanzisha kituo cha kutenga watu na kuwatibu ugonjwa wa Ebola nchini Kenya, hata kama Mahakama Kuu imesimamisha mradi huo kwa muda kufuatia pingamizi la kisheria.

    Katika taarifa iliyotolewa kujibu hatua ya mahakama, Marekani chini ya Wizara ya Msaada wa Kigeni, Masuala ya Kibinadamu na Uhuru wa Kidini ilisema Washington ilikuwa ikiwashirikisha mamlaka za Kenya juu ya suala hilo na inasalia kuwa na matumaini kwamba pingamizi litashughulikiwa.

    Tunafahamu juu ya kesi iliyowasilishwa mahakamani nchini Kenya dhidi ya ujenzi wa kituo cha kutenga na kutibu wagonjwa wa Ebola. Tunawasiliana na mamlaka za Kenya na tuna matumaini tunaweza kutatua malalamiko", taarifa hiyo ilisema.

    Hilo linawadia baada ya Mahakama Kuu siku ya Ijumaa, kutoa maagizo ya kuzuia kwa muda serikali kuweka karantini na kituo cha matibabu cha Ebola nchini Kenya hadi kusikilizwa na kuamuliwa kwa ombi la kupinga mradi huo.

    Kesi hiyo iliwasilishwa huku kukiwa na wasiwasi mkubwa wa umma kufuatia ripoti kwamba Marekani ilikuwa inafikiria kuwatuma raia wa Marekani walioathiriwa na virusi vya Ebola nchini Kenya kwa ufuatiliaji na matibabu kama sehemu ya juhudi kubwa za kudhibiti mlipuko katika eneo hilo.

    Soma zaidi:

  6. Mkuu wa WHO kuzuru katikati mwa mlipuko wa sasa wa Ebola

    Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni anasafiri kuelekea katikati mwa mlipuko wa sasa wa Ebola - mkoa wa Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Tedros Adhanom Ghebreyesus anazuru nchi hiyo ili kuimarisha juhudi za kudhibiti kuenea kwa virusi hatari.

    Ameonya kuwa kuna changamoto nyingi - kwa sababu ni virusi adimu na hadi kufikia sasa bado hakuna chanjo na eneo lenyewe linakabiliwa na migogoro na watu wengi kuhama makazi yao, na kuchangia kueneza ugonjwa huo.

    WHO inasema uwezo wa kufanya vipimo umeimarika.

    Awali, Shirika hilo lilisema kuna visa 906 vinavyoshukiwa vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ikiwa ni pamoja na vifo 223 vinavyoshukiwa ambavyo vinachunguzwa.

    Mlipuko wa aina adimu ya virusi vya Bundibugyo mashariki mwa nchi hiyo unatishia kulemea mamlaka za afya, huku visa vikiripotiwa pia nchini Uganda.

    Kumekuwa na visa 125 vilivyothibitishwa vya Ebola nchini DRC, ikiwa ni pamoja na vifo 17 vilivyothibitishwa huko Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, tangu mlipuko huo ulipoanza takriban miezi miwili iliyopita.

    Pia kumekuwa na visa tisa vilivyothibitishwa vya Ebola nchini Uganda, karibia vitatu kati ya hivyo chanzo chake ni DRC, na kifo kimoja. Hata hivyo, hakuna maambukizi ya jamii yaliyoripotiwa, WHO ilisema.

    Soma zaidi:

  7. Bunge Ghana lapitisha muswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja

    Bunge nchini Ghana limeidhinisha muswada mpya unaoharamisha mapenzi ya jinsia moja na uendelezaji wa shughuli za LGBTQ+.

    Kujitambulisha kama mpenzi wa jinsia moja, mtu aliyebadili jinsia au mpenzi wa jinsia zote mbili kunaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka mitatu jela.

    Muswada huo pia unaanzisha "wajibu wa kuripoti" vitendo vilivyopigwa marufuku kwa polisi.

    Viongozi wa kidini wamemshinikiza Rais John Dramani Mahama, ambaye bado anahitaji kuidhinisha sheria hiyo, kuimarisha sheria zinazopinga mapenzi ya jinsia moja tangu alipoingia madarakani mwaka jana.

    Marufuku hiyo imekosolewa vikali na mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Human Rights Watch, ambayo ilisema inaweka maisha ya watu wa LGBTQ+ hatarini huku pia "ikiwahimiza raia kufuatiliana na kusemana".

    Mahusiano ya jinsia moja yamepigwa marufuku nchini Ghana chini ya sheria zilizoanzia enzi ya ukoloni wa Uingereza.

    Katika hotuba yake kwa Bunge, aliyeleta muswada huo Mchungaji John Ntim Fordjour alisema unalinda familia na maadili ya kitamaduni ya Ghana.

    Aliongeza kuwa marufuku hiyo mpya itafanya sheria zilizopo kuwa "imara zaidi, zenye kujumuisha mengi zaidi, na masharti magumu zaidi katika kukabiliana na desturi za LGBTQ+".

    Mtu yeyote anayejitambulisha kama "mshirika", wa neno la jumla linalomaanisha mfuasi wa watu wa LGBTQ+, anaweza pia kukabiliwa na kifungo jela.

    Soma zaidi:

  8. 'Muuzaji wa sumu' mtandaoni aliyekiri kusaidia wengi kujiua

    Mwanamume mmoja amekiri mashtaka 14 ya kusaidia wengine kujiua nchini Canada baada ya kuuza sumu mtandaoni.

    Kenneth Law, mwenye umri wa miaka 60, alikiri kosa hilo katika mahakama ya Ontario siku ya Ijumaa, kama sehemu ya makubaliano na waendesha mashtaka, ambao waliondoa mashtaka makubwa zaidi ya mauaji.

    Mamlaka zilisema mpishi huyo wa zamani aliuza takriban vifurushi 1,200 vya sumu kwa wateja - ambao alikutana nao katika mijadala ya kujiua mtandaoni - katika nchi 40, takriban robo ya vifurushi hivyo vikitumwa Uingereza.

    Mashtaka yote yanahusiana na waathiriwa wa Canada - lakini familia za waathiriwa wa Uingereza zimesema zimekasirika kwamba waendesha mashtaka wa Uingereza hawangemshtaki Law kuhusiana na vifo vya Waingereza 79, ambavyo mamlaka inasema vinahusiana na bidhaa alizouza eneo hilo.

    Barua kutoka Huduma ya Mashtaka ya Kifalme, iliyoonekana na BBC, ilisema Law hatakabiliwa na mashtaka nchini Uingereza kwa sababu anaweza kupinga kupelekwa kwake baada ya kupatikana na hatia ya makosa kama hayo nchini Canada.

    Law alikamatwa mnamo mwezi Mei 2023, kufuatia uchunguzi tata uliofanywa na takriban mashirika 11 ya kutekeleza sheria na kuwahusisha wachunguzi kutoka takriban nchi kumi na mbili, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Italia na Marekani.

    Kukamatwa kwake kulikuja wiki moja baada ya uchunguzi wa Times kudai alikuwa akiwauzia vijana sumu, baada ya mwandishi wa habari kujifanya mteja na kuzungumza na Law moja kwa moja.

    Inasemekana Law alimshauri mwandishi wa habari jinsi ya kutumia bidhaa zake ili "kuhakikisha anakufa".

    Makachero wa Canada waliiambia BBC mnamo 2023 kwamba Law aliendesha tovuti nyingi zinazotoa vifaa na sumu ili kuwasaidia watu kujiua.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Marekani haijasema lolote baada ya mkutano wa kuamua 'hatma' ya Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa na mkutano na wasaidizi wake wakuu ili kufanya "maamuzi ya mwisho" kuhusu mfumo wa kuongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran, lakini ulihitimishwa bila ufafanuzi kuhusu hatua zinazofuata.

    Trump alisema Iran lazima ikubali kwamba haitawahi kuwa na silaha ya nyuklia au bomu, ili Mlango-Bahari wa Hormuz ufunguliwe tena kwa ajili ya "usafiri wa meli bila vikwazo kwa pande zote mbili", na mabomu yoyote katika njia ya maji "yaharibiwe".

    Mkutano wa Ijumaa ulifanyika katika Ikulu ya White House, katika sehemu inayotumika kushughulikia migogoro mikubwa. Iran awali ilisema haikuwa ikijadili kuhusu mpango wake wa nyuklia.

    Siku ya Alhamisi, nchi hizo mbili zilikubaliana kuhusu mfumo wa makubaliano - unaojulikana kama mkataba wa makubaliano - ukisubiri idhini ya Trump na uongozi wa Iran, kulingana na maafisa wa Marekani.

    Inaripotiwa kwamba makubaliano hayo yangeongeza muda wa kusitisha mapigano kwa siku 60 na kuanzisha mazungumzo kuhusu mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran.

    "Rais Trump atafanya tu makubaliano ambayo ni mazuri kwa Marekani na yanayoangazia masuala yenye kuleta utata. Iran haiwezi kamwe kumiliki silaha ya nyuklia," afisa mmoja wa Ikulu ya White House aliambia CBS News, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani.

    Tangu kuanzishwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano tarehe 8 Aprili, Trump amependekeza mara kwa mara kwamba Marekani na Iran ziko karibu kufikia makubaliano na mazungumzo yanaendelea, lakini hadi sasa hakuna matokeo yoyote ya msingi yaliyopatikana.

    Katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii mapema Ijumaa, Trump alisema alikuwa tayari kuondoa kizuizi cha Marekani kwenye utumiaji wa Mlango-Bahari wa Hormuz, na kuruhusu meli zilizokamatwa kwenye njia ya maji "kuanza mchakato wa 'kuelekea nyumbani!'"

    Soma zaidi:

  10. Hujambo na karibu katika taarifa zetu mubashara kukujuza yanayoendelea duniani. Leo ni tarehe 30/05/2026.