Polisi wa China wamkamata mtu mmoja baada ya video za mateso kwa mbwa kuzua hasira mtandaoni
Mamlaka nchini China zimemkamata mwanaume aliyesababisha hasira kubwa miongoni mwa umma kwa madai ya kuwatesa mbwa na kurekodi ukatili huo ili kuuza video hizo mtandaoni.
Mwanaume huyo anadaiwa kujifanya kuwa mtu mwenye shauku ya kuasili wanyama, lakini baadaye aliwafanyia ukatili paka na mbwa kadhaa aliowachukua.
Vitendo vyake vilifichuliwa baada ya rafiki wa mwanamke aliyekuwa ameweka watoto wa mbwa kwa ajili ya kuasili kusimulia matendo hayo mtandaoni.
Zaidi ya watu 100 walikusanyika nje ya nyumba ya mwanaume huyo mapema wiki hii katika mji wa Chongqing kusini-magharibi mwa China wakipinga matendo yake.
Polisi hawajafichua ni kosa gani hasa mwanaume huyo anachunguzwa nalo. Ukatili dhidi ya wanyama kwa sasa si kosa linaloadhibiwa kisheria nchini China. Hata hivyo, uelewa kuhusu ustawi na haki za wanyama umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
Mwanaume huyo, anayejulikana kwa jina la ukoo la Li, aliweka tangazo kwenye Douyin mapema mwezi huu akisema kuwa anataka kuasili mbwa bila malipo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya eneo hilo, alidai kwamba watoto wake wawili "waliwapenda sana watoto wa mbwa."
Siku ya Jumapili, wanaharakati wa kundi la kutetea haki za wanyama waligundua mmoja wa watoto wa mbwa waliokuwa wameasiliwa akiwa ametupwa kwenye ngazi za jengo analoishi Li. Mbwa huyo alikuwa na mguu uliovunjika, mkia uliokatwa na kichwa kilichovimba.
Video zilizosambazwa mtandaoni zinaonesha zaidi ya watu 100 wakikusanyika nje ya nyumba yake, huku baadhi yao wakibeba mabango ya kupinga vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya wanyama.