Siku ya Bajeti Afrika Mashariki: Bajeti ‘kubwa zaidi’ Kenya na Rwanda
Kwa upande wake, Kenya inapanga kusoma bajeti ya $37.2 bilioni (Kes 4.84 trilioni) ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kuwasilishwa nchini humo. Katika mwaka wa kifedha uliopita, bajeti ya taifa hilo ilikuwa ya dola $33 bilioni.
Sekta ambazo zinaratajiwa kunufaika na ongezeko katika bajeti hii ni huduma za usalama wa ndani na ulinzi wa taifa, idara ya ujasusi, pamoja na sekta za nishati, elimu, afya na maji.
Hata hivyo katika vikao vya umma na pia mitandaoni, kumekuwa na maswali kuhusu iwapo taifa hilo kweli linahitaji bajeti kubwa kiasi hicho.
Rwanda nayo inatarajiwa kutangaza bajeti ya $5.4 bilioni (Rwf 7.8 bilioni), ambayo ni ongezeko la asilimia 12% kutoka kwa bajeti ya mwaka uliopita ya $4.8 bilioni.
Bajeti hiyo inatarajiwa kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Rwanda, na asilimia 68% inatarajiwa kufadhiliwa na mapato ya ndani.
Gharama ya maisha
Bajeti hizi zinawasilishwa wakati wananchi wakiendelea kukabiliwa na changamoto za kupanda kwa gharama za maisha, hususan bei ya mafuta kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati, pamoja na uhaba wa ajira.
Hizi ni baadhi ya kauli za wananchi tuliozungumza nao jijini Dodoma:
"Suala la mafuta ndio linalotuumiza sana. Serikali inatupa ahadi ya kila siku kuwa bei itapunguzwa, lakini hakuna mabadiliko," anasema mkazi mmoja.
Mwingine alisema: "Bajeti inasomwa lakini matumizi sio mazuri. Hii inapunguza mzunguko wa fedha mtaani."
Ongezeko la bei ya mafuta limeshuhudiwa katika mataifa yote ya Afrika Mashariki, hali ambayo imesababisha kupanda kwa nauli, chakula na gharama za kufanya biashara kwa jumla.
Kodi mpya
Wananchi watakuwa makini kuona ni mapendekezo gani ya kikodi ambayo yatatolewa na serikali za kila nchi ili kufadhili bajeti hizo, na yatakuwa na athari gani kwao.
Tanzania na Rwanda tayari zimesema zitalenga mapato ya ndani zaidi kufadhili bajeti zao – na wengi wanasubiri kuona ni maeneo gani ambayo yataguswa zaidi.
Nchini Kenya, bajeti huambatana na mswada wa fedha unaoelezea jinsi bajeti hiyo itakavyofadhiliwa kupitia kodi, mikopo na njia nyinginezo. Wananchi wamekuwa wakitoa maoni kuhusu mapendekezo ya mwaka huu, ambapo baadhi yamezua mjadala kama vile ushuru wa simu za mkononi, miamala ya fedha na mamlaka ya shirika la ukusanyaji ushuru KRA.