Jinsi Urusi inavyojaribu kukuza ustawi na maendeleo ya Korea Kaskazini

Chanzo cha picha, R 24
Mtandao wa Redio na Televisheni unaomilikiwa na serikali ya Urusi ulirusha makala maalum kwa ushirikiano na Radio Korea (yenye makao yake nchini Urusi), ukionyesha Korea Kaskazini kama nchi yenye uchumi unaokua, huduma pana za kijamii, na sekta ya viwanda inayoendelea kustawi.
Makala hiyo, iliyorushwa siku tatu baada ya kumbukumbu ya miaka miwili ya operesheni ya Ukraine katika eneo la Kursk nchini Urusi, ilisifu msaada wa kijeshi wa Korea Kaskazini kwa Urusi katika kukabiliana na operesheni hiyo na kuionyesha Pyongyang kama mshirika pekee rasmi wa Moscow katika uwanja wa vita.
Katika makala hiyo, ushirikiano wa kijeshi kati ya Urusi na Korea Kaskazini unaonyeshwa kama ishara ya "ushirikiano wa kimkakati" kati ya nchi hizo mbili, huku ikisisitizwa nafasi ya Pyongyang katika kuunga mkono misimamo ya Moscow.
Licha ya umakini ulioelekezwa kwenye kipindi hiki na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi, makala hiyo haijapata mjadala mpana miongoni mwa wachambuzi na watoa maoni wengi mashuhuri.
Hata hivyo, chombo cha habari kinachopinga utawala wa Kremlin kilidhihaki ubora duni wa utayarishaji wa makala hiyo, kikielezea kuwa ni jaribio lililofeli la kuionyesha Korea Kaskazini kama mfano wa mafanikio ya kiuchumi na kijamii.
Kituo cha Urusi 24 kilirusha hewani makala ndefu ya video yenye kichwa "Muujiza wa Korea: Jinsi Korea Kaskazini Inavyopiga Hatua Licha ya Vikwazo vya Magharibi." Makala hiyo inaonyesha safari ya mwandishi wa habari wa Urusi, Mikhail Popov, kwenda Pyongyang.
Mikhail Popov anasema anataka kupinga dhana iliyoenea kwamba wananchi wa Korea Kaskazini wanahangaika na uhaba mkubwa wa chakula.
Katika safari hiyo, anaambatana na Andrei Shin, mhariri mkuu wa Radio Korea yenye makao yake nchini Urusi, ambaye anasema ilichukua takriban miezi 16 kupata kibali cha kurekodi filamu nchini humo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwanzoni mwa safari kuelekea Pyongyang, filamu hiyo ya makala inataja ukosefu wa huduma ya intaneti. Hata hivyo, badala ya kuonyesha hali hiyo kama kikwazo, inaielezea kama jambo la faraja.
"Unapowasili Pyongyang, hakuna intaneti kwenye simu yako ya mkononi, na hisia ya kwanza ninayopata ni ile ya kuwa huru kutoka kwenye intaneti," anasema Andrei Shin.
Ingawa upatikanaji wa intaneti unaelezwa kuwa mdogo katika filamu hiyo, hali ya upatikanaji wa umeme katika mji mkuu wa Korea Kaskazini inaonyeshwa kuwa nzuri.
"Picha hizi hazikutengenezwa kwa kompyuta wala kwa kutumia akili mnemba (AI)," anasema Mikhail Popov, akirejelea picha za angani za Pyongyang wakati wa usiku. "Pyongyang kwa kweli hung'aa hivi usiku, kinyume na madai ya vyombo vya habari vya Magharibi kwamba baada ya saa nne usiku, mji mkuu wa Korea Kaskazini hugeuka kuwa eneo lenye giza na lisilo na umeme."
Ingawa filamu hiyo inatangazwa kama simulizi kuhusu Pyongyang ya kisasa, sehemu kubwa yake inajikita kwa viongozi wa Korea Kaskazini.
Kipindi hicho kinasifu urithi wa Kim Il-sung na Kim Jong-il na kumpongeza kiongozi wa sasa, Kim Jong-un, kwa kuleta mabadiliko katika mji mkuu huo kupitia miradi ya kisasa ya maendeleo.
Filamu hiyo pia inasisitiza kile inachoelezea kuwa ni ubora wa juu wa huduma za serikali kwa wananchi. Kipindi hicho kinasema kuwa huduma za afya na programu za michezo, hasa taekwondo, ni bure, na kwamba uchumi wa nchi hiyo unakua licha ya vikwazo vya kimataifa.
"Wakati barabara mpya na makazi yakijengwa, uchumi wa Korea Kaskazini nao unakua," anasema Mikhail Popov. "Ukuaji unatarajiwa kufikia asilimia 4 mwaka 2025, kiwango cha juu zaidi tangu mwaka 2016."
Ili kuonyesha uwezo wa viwanda vya ndani, filamu hiyo inatembelea kiwanda kinachotengeneza mikoba ya shule.
Meneja wa kiwanda hicho anasema, "Kwa upande wa ubora, mikoba hii ni bora kuliko ile inayotoka nje ya nchi."
Kutambua mchango wa kijeshi wa Korea Kaskazini kwa Urusi

Chanzo cha picha, Vladimir SMIRNOV/POOL/AFP via Getty Images
Filamu hiyo ya makala ilionyeshwa siku tatu baada ya kumbukumbu ya miaka miwili ya operesheni ya kijeshi ya Ukraine katika eneo la Kursk nchini Urusi, ambapo vikosi vya Korea Kaskazini vilipigana bega kwa bega na vikosi vya Urusi.
Nafasi ya vikosi hivi ilionyeshwa kwa namna ya pekee kuanzia dakika za kwanza kabisa za makala hiyo.
"Korea Kaskazini ilituma wanajeshi elfu sita nchini Urusi. Walipigana kulinda nchi yao, nchi yetu, na kwa pamoja tulipata ushindi, tukiwafukuza Wanazi wa Ukraine kutoka ardhi ya Urusi," anasema Mikhail Popov, akirejelea "Mkataba wa Ushirikiano wa Kimkakati wa Kina" uliotiwa saini kati ya nchi hizo mbili wakati wa ziara ya Vladimir Putin jijini Pyongyang mwaka 2024.
Anaendelea kuielezea Korea Kaskazini kama "nchi pekee duniani iliyoiunga mkono Urusi rasmi katika uwanja wa vita."
Ingawa kipindi hicho kinatambulishwa kama sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala, hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu tarehe ya kuonyeshwa kwa sehemu ya pili au maelezo zaidi kuhusu mwendelezo wake.
Vyombo vya habari vinavyopinga Kremlin: Ni Filamu isiyo na ushawishi
Filamu hiyo haikupata mwitikio mkubwa mtandaoni wala miongoni mwa wachambuzi maarufu. Moja ya maoni machache yaliyotolewa yalitoka kwenye tovuti ya habari ya Tochka, inayoendeshwa na waandishi wa habari kutoka chombo cha habari cha *Mozhem Obyasnit* ambacho kinapinga Kremlin.
Katika uchambuzi wake wa filamu hiyo, Tochka ilihoji ubora wa utayarishaji wake pamoja na taswira inayotoa kuhusu maisha nchini Korea Kaskazini.
Chombo hicho cha habari kiliandika: "Ili kuthibitisha ustawi wa nchi hiyo, Mikhail Popov anaonyesha mgahawa wa hoteli ambapo timu ya televisheni ya serikali ya Urusi ilifikia.
Hata hivyo, mbali na Popov mwenyewe na wafanyakazi wa hoteli, hakuna mtu mwingine anayeonekana kwenye picha hizo. Ubora wa picha hizo pia ni duni; zinaonekana kana kwamba zilirekodiwa kwa kutumia simu ya mkononi ya mwaka 2010."
"Tochka" pia ilikosoa namna maisha ya kila siku nchini Korea Kaskazini yalivyoonyeshwa.
Chombo hicho kiliandika: "Televisheni ya serikali ya Urusi inaonyesha picha za raia wa Korea Kaskazini wakitembelea mahali alipozaliwa Kim Il-Sung.
Wamevalia nguo za zamani na zilizochakaa, jambo ambalo ni vigumu kulificha hata pamoja na sifa ambazo Popov anatoa kwa Korea Kaskazini.
Hakuna mazungumzo na watu mbele ya kamera, na kila kitu kinaendelea kulingana na mpango uliopangwa awali na maafisa wa Korea Kaskazini."














