Moja kwa moja, Hichilema atangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais Zambia
Mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile anadai uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro nyingi ikiwemo tofauti kati ya matokeo ya vituo vya kupigia kura na yale yaliyotangazwa na ECZ.
Wazee wako kwenye hatari kubwa zaidi ya joto kali kuliko ilivyodhaniwa — Utafiti
Chanzo cha picha, Getty Images
Wanasayansi
wanaonya kwamba athari za ongezeko la joto duniani kwa afya ya wazee hazijapewa
uzingativu unaostahili.
Watafiti
katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani wanasema tafiti zilizopita
zililenga zaidi watu wenye umri mdogo ambao wana uwezo mkubwa wa kutoa jasho na
wana mioyo yenye nguvu zaidi.
Wanasema
nchi zilizo katika hatari kubwa zaidi ni pamoja na India, Pakistan, Bangladesh
na Niger, ambako umaskini na upatikanaji mdogo wa mifumo ya kupoza joto
huongeza hatari ya kuathirika.
Wanasayansi
hao wanaonya kuwa joto kali na kuongezeka kwa idadi ya wazee duniani kunaweza
kuleta changamoto mpya za kibinadamu, kuongeza shinikizo kwenye sekta ya
kilimo, na kuchochea uhamiaji wa kutoka nchi moja hadi nyingine.
Mzozo wa Ethiopia waporomosha mfumo wa afya
Mzozo wa wenyewe
kwa wenyewe ulioikabili Ethiopia kwa muda mrefu umesababisha kuporomoka kwa
mfumo wa afya kutokana na kulengwa kwake na mashambulizi.
Ripoti mpya
ya utafiti iliyotolewa na Makundi mawili ya Haki za binadamu Physicians for
Human Rights -PHR- na lile linalohusiana na masuala ya Haki na Uwajibikaji
katika eneo la pembe ya Afrika -OJAH imesema makundi yenye silaha mara kwa mara
yamekuwa yakilenga sekta hiyo ya afya katika maeneo yaliyokumbwa ya Tigray,
Amhara na Afar.
Ripoti hiyo
inaangazia jinsi makundi yenye silaha yalivyolenga mara kwa mara hospitali,
kliniki, na wahudumu wa afya, na hivyo kufanya mashambulizi dhidi ya sekta ya
afya kuwa mbinu ya kawaida ya kivita.
Hiyo ni kwa
mujibu wa tathmini iliyofanywa kati ya mwaka wa 2024 na 2026 katika maeneo ya
Tigray, Amhara, na Afar.
Utafiti pia
umeonesha kuwa Jeshi la Ethiopia, Jeshi la Ulinzi la Eritrea, Wapiganaji wa
Tigray, wanamgambo wa Amhara Fano na polisi wa maeneo hayo walihusishwa katika
mashambulizi hayo yaliyodhoofisha huduma za afya.
Lindsey
Green, Naibu Mkurugenzi wa kitengo cha Utafiti katika shirika linalohusika na
haki za binadamu la Physicians for Human Rights amesema vitendo vya uporaji au
kuuawa kwa mfanyakazi wa afya ni matukio ya mara kwa mara.
Hali hiyo
pia imesababisha eneo la Tigray kuwa na uhaba wa dawa, mafuta, vifaa, pamoja na
wafanyakazi wa afya wasiolipwa wakati Amhara migogoro inayoendelea imepunguza
upatikanaji wa huduma muhimu.
Mbali na
mashambulizi hayo ripoti hiyo pia imeelezea ukatili wa kingono.
Ripoti hiyo
ya mashirika ya haki za binadamu inaeleza pia kuwa wakati mapigano kwa kutumia
silaha yakianza tena katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, na kuendelea katika
maeneo ya Amhara na Afar, ni lazima vikosi vyote vyenye silaha visitishe
mashambulizi ya makusudi dhidi ya hospitali na wahudumu wa afya.
Mashirika
hayo yametoa wito kwa wanajeshi kusitisha mashambulizi ya makusudi dhidi ya
hospitali na wafanyakazi wa afya na kuitaka serikali ya Ethiopia na jumuiya ya
kimataifa kulinda vituo vya afya, kuwawajibisha wahusika na kutoa haki kwa
walionusurika.
Kushner asema Hamas kuachia silaha katika siku 30 zijazo
Chanzo cha picha, Getty Images
Mjumbe wa Rais wa Marekani ambaye pia ni Mkwe wa Rais Donald Trump Jared Kushner amesema hatua za kuwapokonya sialaha wanamgambo wa Hamas zinasonga mbele na huenda zikaanza kutekelezeka katika kipindi cha mwezi mmoja ujao kuambatana na makubaliano ya amani kuhusu Gaza.
Baada ya kufanya mazungumzo na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv hapo jana Jumatatu, Bwana Kushner amesema huenda wakaanza kuona matokeo ya yaliyofikiwa katika siku thelathini zijazo na kuwa hilo litaanza kwa kuondolewa kwa silaha Gaza.
'Ikiwa Hamas watasalimisha silaha na mahandaki yao kwa hiari yao katika muda wa siku 60 hadi 90 zijazo, bila shaka hilo litakuwa ni kuondolewa kwa tishio kubwa la kiusalama kwa Israel, mafanikio makubwa ambayo huenda hayakutarajiwa. Na iwapo hawatatimiza ahadi yao sasa, kila mtu ataona kwamba hawana nia ya dhati kuhusu amani, na kisha Israel itapata uungwaji mkono mkubwa zaidi kutoka Marekani na wengine kwenda na kumaliza kazi hiyo kwa njia inayofaa'.
Kauli hiyo inakuja baada ya Kushner na Netanyahu kukubaliana kuwa Jenerali wa Jeshi la Marekani ndiye atakahakiki kuwa wanamgambo wa Hamas wanaweka chini silaha zote huku Bwana Netanyahu akisisitiza kuwa majeshi ya Israel hayataondoka katika ukanda wa Gaza hadi pale Hamas itakaposalimisha silaha zake zote.
Waziri huyo Mkuu wa Israel amekuwa akisita kuridhia makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani kuhusu kupatikana amani Gaza, akikabiliwa na shinikizo la kisiasa nchini mwake kutolegeza kamba dhidi ya Hamas.
Siku ya Jumapili, Bwana Kushner ambaye pia ni rafiki wa muda mrefu wa Netanyahu, alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na kiongozi mpya wa Hamas Khalil al-Hayya nchini Misri. Hamas imeahidi kukabidhi silaha zake kwa uongozi mpya wa Palestina utakaosimamia Gaza.
Netanyahu, waziri mkuu wa Israeli aliyedumu kwa muda mrefu zaidi ambaye hatma yake kisiasa iko mashakani katika uchaguzi unaotarajiwa mwezi Oktoba mwaka huu, anaonekana kuzidi kupinga mitizamo ya mshirika wake wa karibu Rais Trump.
Waziri mkuu huyo pia ameweka wazi kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Trump wa kusitisha vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran vilivyoanzishwa mwishoni mwa Februari na badala yake kufuata njia ya kutafuta makubaliano na viongozi wa wa Iran.
Katika mahojiano yaliyoibua hisia kubwa miongoni mwa nchi za Kiarabu, Itamar Ben Gvir, waziri wa usalama wa taifa wa Israel mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia hivi karibuni alisema kuwa Israeli inapaswa kuua watu 30 hadi 40 kila usiku huko Gaza.
Kwa upande wake,Rais wa Israel Isaac Herzog, alipokutana na Kushner hapo jana, alisifu juhudi za Bodi ya Amani iliyoanzishwa na Rais Trump kwa kuhakikisha mustakabali mzuri na salama zaidi kwa Israel, Gaza na kanda ya Mashariki ya Kati kwa jumla.
Operesheni za kijeshi za Israel zimewaua takriban Wapalestina 1,265 tangu makubaliano ya kusitisha vita yalipofikiwa mwezi Oktoba mwaka jana.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemueleza Rais Trump kuwa Israel inawashambulia Wapalestina wa Gaza wakati ambapo awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha vita inapaswa kuwa inatakelezwa.
Uturuki iko tayari kuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran - Erdogan
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki
Recep Tayyip Erdogan amesema ipo haja ya kuendeleza mazungumzo ya kidiplomasia na Iran na Uturuki iko
tayari kushiriki katika juhudi hizo.
Haya yanajiri
baada ya Ofisi ya Rais wa Uturuki kutangaza kwamba kiongozi huyo amefanya
mazungumzao kwa njia ya simu na mwenzake wa Marekani Donald Trump na kukariri utayari wa Ankara wa kuunga mkono
juhudi za amani.
Awali, mjumbe wa
Rais Trump, Jared Kushner,alisema kuwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani
yalikuwa mazito na ya kina, lakini pande hizo mbili bado hazijafikia mwafaka.
Bw. Kushner, ambaye pia ni mkwe wa Donald Trump,
aliambia kituo cha habari cha Fox News kuwa mazungumzo kati ya Marekani na
taasisi mbalimbali za serikali ya Iran.
Hichilema atangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais Zambia
Chanzo cha picha, EPA
Rais Hakainde Hichilema ametangazwa kuwa mshindi wa
uchaguzi wa urais wa Zambia wa mwaka 2026 baada ya kupata zaidi ya asilimia 60
ya kura zilizopigwa.
Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) ilitangaza matokeo
ya mwisho yaliyojumuishwa kutoka majimbo yote 226, yakionyesha kuwa Hichilema,
wa chama cha United Party for National Development, alipata kura 2,965,326
(asilimia 60.49). Mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile wa chama cha National
Reconciliation Party for Unity and Prosperity, alipata kura 1,856,217 (asilimia
37.87). Tofauti ya kura kati ya Hichilema na mpinzani wake ni kura 1,109,109.
Jumla ya wapiga kura 8,786,300 walisajiliwa kushiriki uchaguzi huo. Wagombea
wengine walikuwa nyuma sana, wakiongozwa na Harry Kalaba (Citizens First)
aliyepata kura 19,070 na Kelvin Fube Bwalya (Zambia Must Prosper) aliyepata
kura 17,078.
Ushindi wa Hichilema unampa muhula wa pili wa miaka
mitano. Chini ya mfumo wa uchaguzi wa Zambia, mgombea anahitaji zaidi ya
asilimia 50 ya kura hili kushinda katika duru ya kwanza na kuepuka duru ya
pili.
Matokeo haya yanakuja baada ya mchakato
uliokabiliwa na changamoto na malalamiko. Mundubile alikuwa amedai ushindi
akiegemea kwenye hesabu huru za kura zilizofanywa na timu yake ya kampeni na
kudai kuwepo kwa kasoro nyingi, ikiwemo tofauti kati ya matokeo ya vituo vya
kupigia kura na yale yaliyotangazwa na ECZ, pamoja na madai ya kuhusika kwa
jeshi katika vituo vya kujumlisha kura.
Pia aliishutumu Tanzania kwa kutuma watu kuingilia
kati uchaguzi huo, madai ambayo serikali ya Tanzania iliyakanusha na kuyataja
kuwa ya uongo.
Bado haijabainika ikiwa upinzani utapinga matokeo
hayo ya uchaguzi.
Siku moja baada ya upigaji kura, ECZ ilisitisha kwa
muda zoezi la kuhesabu na kutangaza matokeo, ikitaja ripoti za vurugu dhidi ya
wafanyakazi wa uchaguzi na wizi wa karatasi za kura zilizopigwa katika baadhi
ya maeneo. Kusitishwa huko kuliondolewa siku hiyo hiyo.
Waangalizi wa uchaguzi wa kikanda na kimataifa walielezea
Siku ya Uchaguzi kuwa ya amani kwa kiasi kikubwa katika vituo walivyofuatilia
na kuzitaka pande zote kuwa watulivu na kuheshimu mchakato rasmi. Hichilema
sasa anatarajiwa kuanza muhula wake wa pili kama rais wa Zambia.