Marekani inataka nini hasa kutoka kwa Iran?

Meli

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Marekani inaitaka Iran itangaze hadharani kwamba Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kubaki wazi na kuahidi kusitisha mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara.

Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti, vikinukuu maafisa ambao hawakutajwa majina, kwamba Iran ilikubaliana kwa siri na washauri wa Rais Donald Trump kwamba kushambulia meli hizo kulikuwa kosa.

Hata hivyo, taarifa zimeeleza kuwa Iran imehusisha shambulio hilo na moja ya makundi ya waasi ambayo haina udhibiti nayo.

Trump alisema kuwa pande hizo mbili zimekubaliana kuendelea na mazungumzo, ingawa Washington ilisema kuwa mapigano yaliyotokea katika Mlango wa Hormuz wiki hii yalikuwa ukiukaji wa makubaliano ya usitishaji mapigano.

'Iran lazima ikubali kosa lake, la sivyo itakabiliwa na madhara'

Mnamo Juni, Marekani na Iran zilifikia makubaliano ya usitishaji mapigano. Chini ya makubaliano hayo, Iran pia ilikubali kuhakikisha meli za kibiashara zinapita salama katika Mlango Bahari wa Hormuz.

Maafisa waandamizi wa Marekani wameiambia CBS News, mshirika wa BBC Marekani, kwamba Iran inasema "kundi lililopotoshwa" linajaribu kuhujumu mazungumzo kwa kushambulia meli za kibiashara.

"Kisha Wairani walirejea kwenye mazungumzo na kusema, 'Tulifanya kosa. Hebu tuendelee na mazungumzo,'" afisa mmoja aliiambia CBS News.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ijumaa, maafisa wa Marekani walisema walituma ujumbe kwa viongozi wa Iran kupitia wapatanishi wa kikanda, wakiitaka Iran itoe tamko linalothibitisha kwamba Mlango wa Bahari wa Hormuz unaendelea kuwa wazi na kwamba imekoma kushambulia meli za kibiashara.

Taarifa hizi zimetajwa na vyombo vingi vya habari.

"Iran lazima itoe tangazo hilo, la sivyo itakabiliwa na madhara makubwa," Reuters ilinukuu maafisa wa Marekani wakisema.

Kwa mujibu wa ripoti ya CBS News, Ikulu ya White House pia inaitaka Iran ikiri hadharani kwamba ilikosea kwa kushambulia meli za kibiashara.

Mali katika mlango bahari

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mazungumzo nchini Oman yataongozwa na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, pamoja na maafisa wawili muhimu wanaoshughulikia mazungumzo ya Mashariki ya Kati, akiwemo mjumbe maalum Steve Whitaker na mkwe wa Rais Trump, Jared Kushner.

Wakati huo huo, ujumbe kutoka Qatar uliwasili nchini Iran siku ya Ijumaa kwa ajili ya kujadili njia za kupunguza mvutano na kuwezesha meli kupita kwa usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeomba tuendelee na mazungumzo yetu," Trump alisema katika chapisho kwenye Truth Social siku ya Ijumaa.

"Tulikubaliana na ombi hilo, lakini Marekani iliwaweka wazi kwamba usitishaji wa mapigano sasa umevunjika," alisema.

Hakukuwa na mashambulizi mapya siku ya Ijumaa tangu mapigano yalipoanza katika eneo la Ghuba mapema wiki iliyopita.

Mapigano hayo ya mapema wiki iliyopita yalikuwa makabiliano makubwa zaidi ya kijeshi kati ya Marekani na Iran tangu kusainiwa kwa makubaliano ya muda kati ya nchi hizo mbili mwezi Juni.

Meli tatu zilizokuwa zikielekea Oman kupitia njia ya baharini iliyopendekezwa na Marekani zililengwa katika mashambulizi.

Iran imesisitiza mara kwa mara kwamba njia pekee iliyo salama kwa meli ni kupitia maji yake ya eneo.

Hatima ya Mlango wa Hormuz katika makubaliano

Baadhi ya maendeleo yalipatikana katika mazungumzo haya wakati Marekani na Iran ziliposaini Hati ya Makubaliano yenye vipengele 14 mwezi uliopita, yenye lengo la kudumisha usitishaji wa mapigano na kumaliza mgogoro kila mahali.

Chini ya makubaliano hayo, Iran na Oman zinatarajiwa kufanya mazungumzo na nchi nyingine za Ghuba ili kuamua mustakabali wa Mlango wa Hormuz na kuweka utaratibu wa huduma za usafiri wa baharini.

Wakati wa mzozo huo, Iran ilijaribu kusisitiza mamlaka yake juu ya Mlango wa Hormuz.

Katika hatua hiyo, ilitangaza kuwa itaanzisha Mamlaka ya Mlango wa Ghuba ya Uajemi na kutoa "vibali vya usafiri salama" kwa meli zinazopita katika eneo hilo.

Shirika la habari la Fars la Iran liliripoti kuwa, chini ya makubaliano mapya na Marekani, Mlango wa Hormuz hatimaye utasimamiwa kwa uratibu kati ya Iran na Oman.

Hatua hiyo pia inatarajiwa kujumuisha ada ya huduma itakayotozwa kwa meli zinazopita katika njia hiyo muhimu ya maji.