Jeshi la wanamaji la Marekani latumia silaha mpya kwa mara ya kwanza dhidi ya Iran

Chanzo cha picha, saronic.com/vessels
Jeshi la Marekani limesema limetumia kwa mara ya kwanza boti zisizo na nahodha ambazo hutumika kama silaha za mashambulizi ya mara moja au kama mabomu ya kujitoa mhanga.
Silaha hizi zinazojiendesha, zimetumiwa na jeshi la Marekani katika mashambulizi dhidi ya malengo tofauti nchini Iran. Zimeundwa ili kulipua au kuharibu lengo zinapolifikia.
Kituo kinachoendesha opareseni za kijeshi nchini Marekani CENTCOM, imesema kuwa boti hizo zisizo na nahodha zilitumika katika operesheni zilizolenga maeneo ya kijeshi ya Iran karibu na Mlango bahari wa Hormuz.
Mashambulizi mapya ya Marekani dhidi ya Iran, yaliyoanza tarehe 12 mwezi Julai yalilenga maeneo mbalimbali nchini Iran, yakiwemo mifumo ya ulinzi wa anga, vituo vya rada , pamoja na uwezo wao wa makombora na droni.
Kwa mujibu wa CENTCOM, operesheni hizo zilifanywa kwa kutumia ndege za kivita, meli za kijeshi, droni za mashambulizi ya mara moja, na kwa mara ya kwanza, boti zisizo na nahodha za mashambulizi ya kujilipua, ili kupunguza uwezo wa Iran wa kuvuruga usafirishaji wa kimataifa wa majini kupitia Mlango wa Hormuz.
Mapema mwezi Juni, jeshi la Marekani lilisema kuwa ndege isiyo na rubani au droni ilitumika kuwaokoa wanajeshi wawili waliokuwa kwenye helikopta ya kijeshi ya Marekani iliyopata ajali karibu na pwani ya Oman. Hii ilikuwa miongoni mwa matukio ya kwanza kuripotiwa hadharani ambapo droni ilifanya operesheni ya uokoaji.
Meli zisizo na nahodha ni nini, zinafanyaje kazi, na kwa nini nafasi yake katika vita vya kisasa vya majini inaongezeka?

Boti zisizo na nahodha za Marekani
Ingawa CENTCOM haijafichua jina au aina ya chombo cha majini kisicho na nahodha kilichotumika katika mashambulizi nchini Iran, Corsair inachukuliwa kuwa mojawapo ya mifano ya mifumo inayotumiwa na Jeshi la Wanamaji la Marekani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Boti hizi zisizo na nahodha zinazojulikana kama Unmanned Surface Vessels – USV, ni vyombo vya majini vinavyoweza kujiendesha vyenyewe au kudhibitiwa kwa mbali bila kuwa na wahudumu ndani yake.
Zinaweza kutumika kwa kazi mbalimbali, ikiwemo upelelezi, ulinzi wa maeneo ya bahari, kufuatilia meli za adui, vita vya kielektroniki, na katika baadhi ya mazingira kubeba au kutumia silaha za mashambulizi.
Mfumo kama Corsair umeundwa kusaidia operesheni za majini kwa kupunguza hatari kwa wanajeshi, kuongeza uwezo wa kufuatilia maeneo makubwa ya bahari, na kuruhusu jeshi kufanya mashambulizi au upelelezi kwa kutumia vyombo vidogo na vya gharama nafuu zaidi kuliko meli kubwa za kivita.
Hili lilikuwa miongoni mwa mifano ya kwanza ya operesheni ya uokoaji iliyofanywa na boti isiyo na nahodha ambayo maelezo yake yaliwekwa wazi kwa umma.
Kwa mujibu wa Rais wa Marekani Donald Trump, Iran iliidungua helikopta ya kijeshi ya Marekani aina ya Apache ilipokuwa ikikaribia Mlango bahari wa Hormuz.
Baada ya tukio hilo,CENTCOM ilisema kuwa operesheni ya uokoaji ilifanywa kwa kutumia boti isiyo na nahodha aina ya Corsair, na wahudumu wa ndege hiyo waliokolewa ndani ya takribani saa mbili.
Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni ya Texas inayotengeneza boti hizi zisizo na nahodha, Corsair ina urefu wa futi 24 takribani mita 7.3, inaweza kusafiri kwa kasi ya hadi takribani kilomita 64 kwa saa, na inaweza kubeba mzigo wa takribani kilo 454.
Brian Clark, mtaalamu wa boti hizi zinazojiendesha na zinazoendeshwa kwa mbali kutoka taasisi ya Hudson Institute, alisema:
"Corsair ina ukubwa unaokaribiana na boti ya uvuvi, ina sehemu ya juu tambarare ya kubebea mizigo, na imeundwa kwa ajili ya kusafirisha vifaa. Pia huenda inaweza kubeba watu watatu hadi wanne."
Brian Clark aliongeza kuwa Corsair ina kamera zinazoonyesha picha za mazingira yanayoizunguka. Pia ina rada kwa ajili ya urambazaji wa masafa marefu na vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki vinavyotumika kukusanya taarifa za kijasusi.
Wakati huohuo, Dkt. Stacie Pettyjohn, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa Marekani katika Kituo cha Usalama cha CNAS, anasema,"Corsair imekuwa ikitumika kwa miaka mingi.
"Jeshi la Wanamaji la Marekani lina takribani boti 50 za aina hii."
Aliongezea kuwa "Mara nyingi hutumiwa kwa kugundua na kufuatilia mabomu ya majini, lakini Jeshi la Wanamaji la Marekani bado linaendelea kufanya majaribio ya boti za Corsair katika Mlango wa Hormuz ili kutathmini uwezo wake na majukumu ambayo inaweza kutekeleza."
Jeshi la Wanamaji la Marekani linaendesha Kikosi Kazi cha Droni za Baharini 59 (Maritime Drone Task Force 59), ambacho ni kitengo cha kwanza cha Jeshi la Wanamaji la Marekani kilichojikita pekee katika matumizi ya mifumo isiyo na rubani au nahodha.
Kitengo hicho kilianzishwa mwaka 2021, na Marekani ilianza kukipeleka Mashariki ya Kati mwezi Machi.














