Mwanamke atuhumiwa kumuua mumewe kwa dawa ya kusafishia choo

Chanzo cha picha, GETT
Mwanamke mmoja nchini India amekamatwa kwa tuhuma za kumuua mumewe kwa kushirikiana na wanaume wengine wawili, katika tukio ambalo polisi wanasema lilihusisha kumpa dawa za kumlewesha, kumtupa kutoka kwenye roshani na kumdunga dawa ya kusafishia choo.
Onyo: Habari hii ina maelezo ambayo yanaweza kuwasumbua baadhi ya wasomaji.
Inspekta Suresh Kumar wa wilaya ya Nazimabad katika jimbo la Telangana alisema watuhumiwa walidaiwa kutekeleza mpango huo baada ya kuamini kuwa mume huyo, aliyekuwa amerejea hivi karibuni kutoka Saudi Arabia, angezuia uhusiano wa mwanamke huyo na mpenzi wake.
"Tulimkamata mwanamke mmoja pamoja na wanaume wawili kwa tuhuma za kumpa dawa za kulevya mume wa mwanamke huyo, kumtupa kutoka kwenye roshani na kumdunga dawa ya kusafishia choo ili kumuua," alisema Inspekta Suresh Kumar.
Polisi wanasema watuhumiwa walijaribu kumuua mwanaume huyo mara mbili ndani ya kipindi cha saa 24 kabla ya kufariki dunia tarehe 30 Juni.
Kwa mujibu wa polisi na familia ya marehemu, Dayani Prashant mwenye umri wa miaka 36 alifunga ndoa ya kupangwa na Scindia miaka 12 iliyopita. Wawili hao walikuwa na watoto wawili, wa miaka tisa na saba.
Kabla ya ndoa, Scindia alikuwa amepata mafunzo ya uuguzi na alikuwa akifanya kazi kama muuguzi katika hospitali binafsi mjini Nazimabad.
Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku watuhumiwa wakikabiliwa na tuhuma za mauaji.























