Simulizi ya saa 24 za mwisho za mtaalamu aliyejidunga sumu ya nyoka

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati akifanya utafiti kuhusu nyoka mwenye sumu kutoka Afrika, mtaalamu wa viumbe Carl P. Schmidt aling'atwa na nyoka huyo.
Katika hali kama hiyo, mtu yeyote wa kawaida angeenda hospitalini kupata matibabu, lakini Schmidt alikataa matibabu ili aweze kuchunguza kinachotokea hasa wakati mtu anapokufa kutokana na kung'atwa na nyoka, na akaandika maelezo kamili ya hali iliyokuwa ikimkabili kabla ya kufariki dunia.
Mnamo Septemba 1957, mkurugenzi wa Bustani ya Wanyama ya Lincoln Park jijini Chicago alituma nyoka mdogo kwenye Makumbusho ya Historia ya Asili ya Field (Field Museum of Natural History) ya jiji hilo ili atambuliwe.
Nyoka huyo, mwenye urefu wa sentimita 76, alipaswa kuchunguzwa na Carl Patterson Schmidt, mtaalamu mashuhuri wa viumbe wanaotambaa na amfibia ambaye alikuwa amelifanyia kazi makumbusho hayo kwa miaka 33.
Alikuwa bingwa wa masuala ya nyoka wanaoishi chini ya ardhi. Alistaafu kazi yake kama msimamizi mkuu wa makumbusho hayo mwaka wa 1955. Katika kipindi chake cha kazi cha miaka 33, alikusanya aina mbalimbali za amfibia na idadi kubwa ya viumbe watambaao.
Hivyo, baada ya kustaafu, alipoombwa kuchunguza na kumtambua nyoka huyo mdogo, alikubali mara moja.
Kuumwa na Nyoka
Nyoka huyo alikuwa na mistari ya rangi angavu mwilini mwake, na kichwa chake kilifanana na kile cha nyoka wa kijani wa mitini wa Afrika Kusini, anayejulikana pia kama *boomslang*. Schmidt aligundua maelezo hayo.
Hata hivyo, walishangazwa kuona kwamba eneo karibu na tundu lake la haja kubwa halikuwa na mpasuko.

Chanzo cha picha, Chicago Daily Tribune
Mara tu alipomuinua nyoka huyo, ilimshambulia Schmidt na kumng'ata kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kushoto. Kidole gumba cha Schmidt kilionyesha alama mbili ndogo za damu na kuanza kuuma.
Mara moja, Schmidt alianza kukinyonya kidole chake. Lakini badala ya kutafuta msaada wa kimatibabu, alianza kurekodi athari za sumu hiyo mwilini mwake.
Alifariki dunia ndani ya saa 24 baada ya kushambuliwa na nyoka huyo.
Siku ya mwisho ya Schmidt
Wakati huo, wataalamu wote wa nyoka, akiwemo Schmidt, waliamini kuwa nyoka wa aina ya 'blue snake' hakuweza kuingiza sumu ya kutosha mwilini mwa binadamu kiasi cha kuhatarisha maisha.
Hivyo, baada ya kung'atwa na nyoka huyo, Schmidt alirejea nyumbani na kuandika kumbukumbu za athari za sumu hiyo mwilini mwake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Video yenye kichwa 'Diary of a Snakebite Death' (Shajara ya Kifo kwa Kung'atwa na Nyoka) ilirushwa hewani katika kipindi cha Science Friday cha kituo cha redio cha serikali ya Marekani, PRI.
Ilitoa taarifa kuhusu maelezo ambayo Schmidt mwenyewe aliandika katika shajara yake. Maelezo ya Schmidt yalikuwa kama ifuatavyo:
- Nilijihisi kichefuchefu kikali nilipokuwa nikisafiri kurudi nyumbani kwa treni kati ya saa 10:30 na 11:30 jioni. Hata hivyo, sikutapika.
- Saa 11:30 jioni – 12:30 jioni: Hali ya hewa ilibadilika na kuwa ya baridi kali, na mwili wangu ulianza kutetemeka. Kisha nikapata homa ya nyuzi joto 101.7º F [38.7º C].
- Saa 11:30 jioni, damu ilianza kutoka kwenye fizi.
- Nikula vipande viwili vya mkate uliokaushwa wenye maziwa (milk toast) saa 2:30 usiku.
- Nililala vizuri kuanzia saa 3:00 usiku hadi saa 6:20 usiku.
- Nilijisaidia haja ndogo saa 6:20 usiku. Kulikuwa na kiasi kidogo cha damu kwenye mkojo.
- Saa 10:30 alfajiri, nilikunywa glasi moja ya maji. Baada ya hapo, nilipatwa na kichefuchefu kikali na kutapika. Chakula chote nilichokula usiku kilitoka nje; hii ina maana kwamba hakikuyeyushwa tumboni. Hata hivyo, baadaye nilijihisi nafuu na kulala vizuri tena hadi saa 12:30 asubuhi.
Kukataa matibabu
Masaa machache kabla ya kifo chake, Schmidt aliombwa amuone daktari, lakini alikataa kutafuta matibabu, akisema kuwa kufanya hivyo kungeingilia athari za sumu ya nyoka mwilini mwa binadamu.
Badala yake, kutokana na udadisi wa kisayansi, alianza kuandika kila maelezo baada ya kifungua kinywa.

Chanzo cha picha, Chicago Daily Tribune
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Septemba 26, saa 12:30 asubuhi: Homa ya nyuzi joto 98.2 (36.7 ºC). Kiamsha kinywa kilikuwa nafaka, mkate uliochomwa (toast), mayai, mchuzi wa tufaha, na kahawa.
Hakukuwa na hata tone la damu kwenye mkojo uliotolewa kila baada ya saa tatu. Kulikuwa na damu inayotoka mfululizo puani na mdomoni, lakini si kwa wingi.
Kama ilivyoripotiwa katika kipindi cha Science Friday, neno la mwisho katika shajara ya Schmidt lilikuwa 'kupita kiasi' (*excessive*).
Alikula chakula cha mchana yapata saa 7:30 mchana na kuanza kutapika. Alimpigia simu mkewe. Wakati msaada wa kimatibabu ulipofika, alikuwa amepoteza fahamu na mwili wake wote ulikuwa umelowa jasho.
Madaktari waliitwa mara moja na juhudi zilifanyika kumfufua Schmidt kabla ya kupelekwa hospitalini.
Schmidt alitangazwa kufariki dunia saa 9:00 alasiri kutokana na 'kupooza kwa mfumo wa kupumua' (*Respiratory Paralysis*), hali iliyomfanya ashindwe kupumua.
Ripoti ya uchunguzi wa mwili wake ilionyesha kuwa alipata shida ya kupumua kutokana na kuvuja damu ndani ya mapafu yake.
Alifariki dunia kutokana na kuvuja damu machoni, mapafuni, kwenye figo, moyoni, na kwenye ubongo.
Sumu kali sana
Karibu miongo miwili baada ya kifo cha Schmidt, majaribio ya kisayansi yalifanywa kwa nyoka aina ya *boomslang*, na kugundulika kuwa ni mmoja wa nyoka hatari zaidi barani Afrika.
Kuumwa na nyoka huyu husababisha hali ya *disseminated intravascular coagulation* (DIC). Hali hii husababisha kuganda kwa damu katika sehemu nyingi ndogo ndani ya mishipa ya damu, na hivyo damu kupoteza uwezo wake wa kawaida wa kuganda. Hii husababisha kuvuja kwa damu katika viungo mbalimbali vya mwili wa mwathiriwa na hatimaye kusababisha kifo.
Nyoka hawa wanaoishi mitini hupatikana kwa wingi katika maeneo ya Afrika ya Kati na Kusini. Nyoka aina ya *boomslang* aliyekomaa huwa na urefu wa sentimita 100 hadi 160. Baadhi ya nyoka hao wanaweza kufikia urefu wa sentimita 183.
Nyoka huyu hula mijusi, vyura wa mitini, na vyura wa kawaida. Pia, mara kwa mara hula wanyama wadogo wenye uti wa mgongo (mamalia), ndege, na mayai yaliyomo kwenye viota.
Hata hivyo, huchukuliwa kuwa nyoka mwenye tabia ya kujificha na kutopenda fujo. Kwa kawaida huepuka kula mawindo makubwa sana.
Kulingana na mashuhuda, Schmidt alikuwa mzembe wakati akimshughulikia nyoka huyo, na huenda hiyo ndiyo sababu iliyomfanya nyoka huyo kushambulia.
Nyoka huyo wa aina ya *boomslang* alikuwa mdogo sana. Pia, Schmidt aliumwa na jino moja tu. Jeraha lilikuwa dogo, lenye ukubwa wa takriban milimita tatu, na Schmidt alikuwa na afya njema. Kwa hiyo, kwa ujumla inaaminika kuwa Schmidt na wenzake hawakulichukulia kwa uzito mkubwa suala la kuumwa na nyoka huyo.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanaamini kuwa Schmidt alijua kuwa dawa ya kukabiliana na sumu ya *boomslang* haikuwepo wakati huo, na kwamba hakukuwa na chochote angeweza kufanya isipokuwa kutumaini kupata nafuu.
Vyovyote vile vilivyokuwa vikiendelea akilini mwa Schmidt katika saa hizo muhimu za mwisho baada ya kuumwa na nyoka, jambo moja la hakika ni kwamba hakurudi nyuma kwa hofu, bali alikabiliana na hali hiyo kwa ujasiri.
End of Pia unaweza kusoma:
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi
































