Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran hupata wapi vifaa vya kutengeneza ndege zake zisizo na rubani?
Mnamo Septemba 2023, Wizara ya Fedha ya Marekani ilisema kuwa ndege zisizo na rubani za Iran aina ya Shahed-136 zilikutwa zikiwa na vifaa vilivyonunuliwa kupitia mtandao wa kimataifa wa wasambazaji.
Miongoni mwa vifaa vilivyopatikana kwenye ndege ya Urusi iliyotumika katika vita nchini Ukraine kulikuwa na mota ndogo ya servo, inayotumika kudhibiti mwendo wa sehemu mbalimbali za ndege.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha ya Marekani, kampuni moja ya Iran ilitumia mawakala wa biashara walioko Hong Kong, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu kusafirisha maelfu ya mota hizo kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC).
Iran inakabiliwa na vikwazo vingi vya kimataifa na inategemea kwa kiasi fulani vifaa vinavyoagizwa kutoka nje kwa ajili ya kutengeneza ndege zake zisizo na rubani.
Nyaraka za vikwazo vya Marekani zinaeleza jinsi kampuni na mawakala wa biashara wanavyohusika katika kusambaza vifaa vinavyohitajika na Iran. Ripoti hii, inayotegemea nyaraka hizo, taarifa zilizochapishwa na maelezo ya wataalamu, inachunguza namna mitandao hiyo inavyofanya kazi na jinsi vikwazo vinavyoathiri upatikanaji wa vifaa vya ndege zisizo na rubani nchini Iran.
Damien Splitters, mtafiti wa silaha na mwanzilishi wa kampuni ya Heimdall, aliiambia BBC Persian kuwa ufanisi wa vikwazo mara nyingi hupimwa kwa vigezo visivyo sahihi.
Amesema ili kuelewa mnyororo wa usambazaji wa vifaa hivyo, ni muhimu kuchunguza tofauti kati ya mahali vinapotengenezwa, wanaoviuza na njia vinazopitia hadi kumfikia mtumiaji wa mwisho.
Maafisa wa Iran wamekuwa wakieleza mara kwa mara kuwa mpango wa kutengeneza ndege zisizo na rubani ni ushahidi wa uwezo wa nchi hiyo kujitegemea katika masuala ya ulinzi. Ushahidi kutoka kwenye medani za vita na tafiti mbalimbali unaonyesha kuwa Iran imepanua uwezo wake wa kubuni, kutengeneza, kuunganisha na kunakili ndege hizo katika miongo kadhaa iliyopita.
Hata hivyo, uchunguzi wa mabaki ya ndege zisizo na rubani za Iran zilizotumiwa na Urusi katika vita nchini Ukraine umeonyesha kuwa ndege hizo zilikuwa na vifaa vilivyoagizwa kutoka nchi za nje.
Kinyume na dhana iliyozoeleka, vifaa vingi vinavyotumika kutengeneza ndege hizo si vya teknolojia ya hali ya juu sana wala si ghali.
Keith Koren, naibu mkurugenzi wa mpango wa uchumi katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati (CSIS), alisema katika video iliyotolewa hivi karibuni na taasisi hiyo kuwa ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran hutegemea kwa kiasi kikubwa vifaa vinavyoagizwa kutoka nje.
Kwa mujibu wa Koren, Iran haina uwezo wa kutengeneza saketi jumuishi za kielektroniki zinazohitajika katika ndege hizo na makombora yake, hivyo hulazimika kuziagiza kutoka nje.
"Nimewahi kuona sehemu za ndani za ndege hizi zisizo na rubani," alisema Koren. "Bado zinatumia vifaa vidogo na vyepesi vya kielektroniki vinavyofanana na vya kompyuta, vinavyotengenezwa na kampuni ya Marekani na vilivyoingia sokoni kwa mara ya kwanza mwaka 2008."
Iran hupataje vifaa hivyo?
Splitters, mwanzilishi wa Heimdall, amekuwa akifuatilia kwa miaka mingi biashara ya silaha na mitandao haramu inayosafirisha teknolojia hiyo.
Amesema visa vilivyorekodiwa vinaonyesha kuwa taasisi zinazohusika na ununuzi wa vifaa vya kijeshi nchini Iran hutumia mawakala wa biashara katika nchi nyingine, zikiwemo China, Hong Kong na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao ulisitisha biashara na Tehran mwezi Agosti 2026, ulikuwa mojawapo ya njia muhimu zilizotumiwa kuingiza bidhaa za kigeni nchini Iran. Hii ilitokana na nafasi kubwa ya nchi hiyo katika biashara ya kikanda.
Athari za vikwazo
Splitters amesema kuwa upatikanaji wa bidhaa unapozuiwa kupitia watengenezaji na wasambazaji rasmi, wanunuzi hulazimika kutegemea mawakala ambao huenda ikawa vigumu kuthibitisha uhalisi na ubora wa vifaa wanavyoingiza nchini.
Kwa sababu hiyo, nchi zinazokabiliwa na vikwazo na vita zinaweza kuwa katika hatari kubwa ya kuingiziwa vifaa bandia katika minyororo yao ya usambazaji.
Jim Lemson, mchambuzi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), alitathmini katika makala iliyochapishwa mtandaoni mwezi Oktoba 2026 kuwa mashambulizi ya Marekani yalikuwa yameharibu sehemu kubwa ya miundombinu ya Iran ya kutengeneza makombora na ndege zisizo na rubani.
Kwa mujibu wake, Iran inaweza kuendelea kutengeneza au kuunganisha baadhi ya silaha zake katika kipindi cha karibu kwa kutumia vifaa ilivyohifadhi kabla ya vita.
Hata hivyo, kujenga upya sekta ya kijeshi kwa njia endelevu kutahitaji upatikanaji wa mashine na vifaa vipya.
Swali linalobaki ni kwa kiwango gani sekta ya kijeshi ya Iran itaweza kupata vifaa inavyohitaji ndani ya nchi au kutoka nje, kufuatia hasara ilizopata hivi karibuni.