Je, Ebola imedhibitiwa nchini Kenya baada ya kuthibitishwa kwa wagonjwa tisa?

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Kenya inakabiliwa na mlipuko wake wa kwanza kabisa wa ugonjwa wa Ebola, ugonjwa ambao nchi jirani kama Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimewahi kukabiliana nao mara kwa mara.
Hadi sasa, visa tisa vimethibitishwa, vikiwemo vya mgonjwa wa kwanza ambaye alisafiri kutoka DRC na kufariki dunia wiki mbili zilizopita.
Watu wanne wa familia ya mwathirika huyo wa kwanza, wahudumu watatu wa afya pamoja na mfanyakazi mmoja wa usafi hospitalini wamethibitika kuambukizwa virusi hivyo, jambo linaloonyesha kuwa visa vyote hivyo vinahusiana moja kwa moja na mgonjwa huyo wa kwanza.
Hata hivyo, wasiwasi unaongezeka kwamba virusi hivyo vinaweza kuendelea kuenea zaidi, licha ya juhudi za serikali kuwahakikishia wananchi kwamba hali inadhibitiwa.
Marekani imewaonya raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Kenya kutokana na mlipuko huo, huku nchi jirani kama Uganda, Ethiopia na Somalia nazo zikiwa katika hali ya tahadhari ya juu kufuatilia uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa huo.
Wizara ya Afya inasema wagonjwa wote tisa ni sehemu ya kundi moja la maambukizi, huku asilimia 99.3 ya watu waliokuwa katika orodha ya walio karibu na wagonjwa wakifuatiliwa na kuwekwa karantini.
Mamlaka zinasema hadi sasa hakuna ushahidi wa maambukizi nje ya kundi hilo.
Mgonjwa wa kwanza alifariki, huku wagonjwa wengine wanane wakiendelea kupata huduma za matibabu na uangalizi wa karibu. Wizara imesema wagonjwa hao wameonyesha kuimarika kwa kiasi kikubwa na hali zao ni thabiti.
Aidha, Kenya imepokea dozi 500 za dawa kwa ajili ya kusaidia matibabu ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola.
Je, Wakenya wanapaswa kuwa na wasiwasi?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakenya wengi wamekuwa wakieleza wasiwasi wao kwamba ugonjwa huo unaweza kuendelea kusambaa kwa kiwango kikubwa zaidi nchini humo.
Zaidi ya watu 4,000 wamefariki dunia tangu ugonjwa wa Ebola uthibitishwe nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) mwezi Mei, na kuufanya mlipuko huo kuwa wa pili kwa kusababisha vifo vingi zaidi katika historia ya ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa International Rescue Committee (IRC), ikiwa na zaidi ya visa 9,500 vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya inaendelea kuwa katika hatari ya kupokea wagonjwa wapya kupitia mipaka yake. Shirika hilo limekuwa likifanya kazi kwa ushirikiano na serikali za nchi hizo mbili katika juhudi za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
Mlipuko wa sasa unasababishwa na aina ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo, ambayo ni nadra kutokea. Hadi sasa, hakuna chanjo wala tiba iliyoidhinishwa rasmi dhidi ya aina hiyo, ingawa majaribio ya chanjo na matibabu yanaendelea.
Tangu mwanzo wa mlipuko huo, Wakenya wamekuwa wakihoji jinsi mgonjwa wa kwanza alivyoweza kukaa katika eneo lililoathiriwa zaidi na Ebola nchini DR Congo kisha kusafiri kupitia nchi nyingine mbili kabla ya ugonjwa wake kutambuliwa. Mtu huyo alifariki dunia siku chache baada ya kuwasili nchini Kenya.
Kwa kuwa Kenya ni kitovu muhimu cha usafiri na biashara katika eneo la Afrika Mashariki, kuna hofu kwamba ugonjwa huo unaweza kusambaa kwa urahisi zaidi kupitia safari za ndani na za kimataifa.
Chama cha madaktari nchini Kenya, kimeeleza wasiwasi wake kuhusu kile ilichokiita "mapungufu" katika udhibiti wa afya kwenye baadhi ya vituo vya mipakani, ikiwemo mipaka ya Uganda na Tanzania, pamoja na uwanja mkuu wa ndege wa Kenya.
Mwakilishi wa chama hicho, Dennis Miskellah, aliiambia BBC kwamba vituo vya mipakani na bandari vinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi, hali inayoweza kudhoofisha juhudi za kugundua na kudhibiti visa vipya vya Ebola mapema.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya nchini Kenya, Patrick Amoth, alijaribu kuwahakikishia wananchi Jumanne jioni kwa kusema kwamba wagonjwa wanane waliobainika kuambukizwa Ebola wanaendelea kuimarika na wanaitikia vyema matibabu wanayopokea.
Hatua zinazochukuliwa kudhibiti kuenea kwa ugonjwa
Wakati kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kilipotangazwa, mamlaka ziliwahimiza wananchi kutokuwa na hofu, zikiwahakikishia kuwa hatua za ufuatiliaji zimeimarishwa katika viwanja vya ndege na maeneo ya kuvukia mipaka ili kubaini na kudhibiti visa vyovyote vinavyoweza kuingia nchini.
Mamlaka hizo zilisema kuwa uchunguzi wa afya kwa wasafiri, pamoja na uangalizi wa karibu katika vituo vya kuingia na kutoka nchini, umeongezwa kama sehemu ya juhudi za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Kenya tangu wakati huo imeanzisha hatua za kuimarisha uchunguzi wa wasafiri wanaowasili kutoka nchi 10 zinazochukuliwa kuwa na hatari kubwa ya Ebola: DRC, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Angola, Zambia, Ethiopia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wasafiri wanaowasili kutoka nchi hizo wanatakiwa kujaza fomu ya kidijitali ya ufuatiliaji wa afya kabla ya kupanda ndege, na kuwasilisha msimbo wa QR kwa maafisa wa afya bandarini wanapowasili.
Serikali ya Kenya pia imeagiza kuimarishwa kwa ukaguzi wa afya kwa ndege zote zinazowasili kutoka nchi hizo, katika jitihada za kuzuia kuingia kwa visa vingine vya Ebola kutoka nje ya nchi.
Ndani ya Kenya, serikali imekuwa ikitoa ujumbe wa elimu kwa umma kuhusu Ebola ili kuongeza uelewa wa wananchi. Ujumbe huo unawahamasisha watu kuripoti mara moja visa vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola na kutafuta huduma za afya hospitalini bila kuchelewa.
Aidha, serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa hatua za usafi na kinga, ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka mawasiliano ya karibu na watu wanaoonesha dalili za ugonjwa.
Serikali pia imetenga vituo maalumu vya matibabu na kutenga wagonjwa katika maeneo mbalimbali nchini, huku wahudumu wa afya wakipewa mafunzo ya kushughulikia ugonjwa huo kwa usalama na ufanisi.
Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini Kenya, Patrick Amoth, amesema pia kuwa maabara maalumu imeanzishwa katika Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza cha Kenyatta National Hospital kwa ajili ya kufanya vipimo vya Ebola.
Alieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuhakikisha maabara kuu ya hospitali hiyo hailazimiki kushughulikia sampuli za Ebola na hivyo kupunguza hatari ya uchafuzi au maambukizi ya maabara.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Nchini Kenya, watu 134 kati ya 135 waliotambuliwa kuwa waliwasiliana kwa karibu na mgonjwa wa kwanza wa Ebola bado wako karantini. Hii ina maana kwamba takribani asilimia 99 ya watu wote waliokuwa kwenye hatari ya maambukizi wamepatikana na kutengwa, hatua inayolenga kuzuia ugonjwa huo kusambaa kwa jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa International Rescue Committee (IRC), ukweli kwamba watu wote waliothibitishwa kuambukizwa hadi sasa walikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mgonjwa wa kwanza unaonyesha kuwa hatua za awali za Kenya za kukabiliana na mlipuko huo zinafanya kazi vizuri.
Serikali ya Kenya pia inaendelea kushirikiana na washirika wa kimataifa, wakiwemo Africa Centres for Disease Control and Prevention (Africa CDC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), kuimarisha hatua za udhibiti wa ugonjwa huo. Ushirikiano huo unahusisha ufuatiliaji wa visa, utoaji wa taarifa kwa umma, na ushirikishwaji wa jamii katika juhudi za kuzuia maambukizi.
Aidha, serikali imeweka nambari maalumu ya dharura isiyotozwa malipo, 719, ambayo wananchi wanaweza kutumia kuripoti dalili zinazoshukiwa kuwa za Ebola au kupata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa afya.
Hatua hizi zinaonyesha kwamba mamlaka za afya nchini Kenya zinaendelea kuchukua tahadhari kali ili kudhibiti mlipuko huo na kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.
Je, Kenya iko tayari ikiwa Ebola itaanza kusambaa zaidi?
Amoth amesema kwamba hakuna hata mmoja wa watu waliokutana na wagonjwa wa kwanza aliyeonesha dalili zozote kabla ya kuwekwa karantini, na hivyo hatari ya kueneza ugonjwa huo kwa watu wengine ilikuwa ndogo sana, karibu kutokuwepo kabisa.
Kipindi cha kujitokeza kwa dalili za ugonjwa wa Ebola ni kati ya siku mbili hadi 21.
Hii ina maana kwamba mtu aliyekumbana na virusi hivyo anaweza kuchukua wiki kadhaa kabla ya kuanza kuugua. Ebola huenea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa, kama vile damu, matapishi au majimaji mengine ya mwili.
Hata hivyo, Kenya imeendelea kujiandaa kukabiliana na tishio hilo. Wizara ya Afya ya nchi hiyo imesema kuwa karibu wahudumu wa afya 5,000 wamepewa mafunzo ya kushughulikia visa vya Ebola katika ngazi ya kitaifa na za kaunti. Aidha, vituo maalumu vya afya vimetengwa na kuandaliwa kwa ajili ya kupokea na kutibu wagonjwa wa Ebola iwapo kutatokea maambukizi nchini.
Wizara ya Afya imewasihi wananchi kubaki watulivu lakini waendelee kuwa makini dhidi ya dalili za Ebola. Pia imewataka Wakenya kuepuka kuwanyanyapaa watu waliotambuliwa kuwa waliwasiliana na wagonjwa wa Ebola, ikionya kwamba unyanyapaa unaweza kuathiri juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.
Kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO), wizara hiyo imeandaa mabango na vifaa vya elimu ya afya ili kuwasaidia wananchi kuelewa ugonjwa wa Ebola na namna ya kuzuia kuenea kwake. Moja ya jumbe hizo inasema:
"Komesha unyanyapaa, chagua kutoa msaada. Unyanyapaa unaweza kuwazuia watu kuripoti dalili zao au kushirikiana na timu za afya zinazoshughulikia mlipuko wa ugonjwa."
Mamlaka za afya zinaeleza kuwa ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kutambua visa vipya mapema, kufuatilia waliokutana na wagonjwa na kudhibiti maambukizi.
Aidha, serikali imeendelea kuimarisha maandalizi yake kwa kununua na kusambaza vifaa vya kujikinga (PPE), vikiwemo glavu, barakoa, mavazi maalumu ya kinga na vifaa vingine vinavyohitajika na wahudumu wa afya wanaohudumia wagonjwa wa Ebola.
Kuna jitihada za kutosha za kuwalinda wahudumu wa afya?
Hata hivyo, si kila mtu anaamini kuwa Kenya imejiandaa vya kutosha. Kenya Medical Practitioners, Pharmacists and Dentists Union (KMPDU) imeeleza wasiwasi wake kuhusu kiwango cha maandalizi ya nchi hiyo kukabiliana na Ebola.
Baada ya wahudumu watatu wa afya na mfanyakazi mmoja wa usafi hospitalini kuthibitishwa kuambukizwa Ebola, maswali yameibuliwa kuhusu iwapo serikali inaweza kufanya zaidi kuwalinda wafanyakazi wa sekta ya afya walio mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Wahudumu wa afya na walezi wako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa Ebola kwa sababu kazi yao huwahusisha moja kwa moja na wagonjwa. Wakati wa kutoa huduma, wanaweza kugusana na damu, matapishi au majimaji mengine ya mwili kutoka kwa mtu aliyeambukizwa, ambayo ndiyo njia kuu ya maambukizi ya virusi vya Ebola.
Dennis Miskellah, naibu katibu mkuu wa KMPDU, aliiambia BBC kwamba vifaa vya kujikinga vinapaswa kutolewa kwa hospitali ili kuhakikisha wahudumu wa afya wanalindwa kikamilifu, hasa pale ambapo wagonjwa wenye dalili hawataeleza kwamba wametoka katika maeneo yaliyoathiriwa na Ebola.
Amesema serikali inapaswa kuendesha elimu sahihi ya afya kwa umma ili kuondoa unyanyapaa unaohusishwa na virusi vya Ebola, jambo ambalo litawahamasisha watu kutoficha dalili zao.
Kwa upande mwingine, Shirika la Kimataifa la Uokoaji (International Rescue Committee - IRC) limeitaka serikali kuendelea kufadhili shughuli za ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa, uchunguzi katika mipaka, pamoja na mafunzo kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele nchini Kenya.
Je, kutakuwa na vizuizi kama marufuku ya kusafiri?
Kenya inaendelea kuwa wazi bila vikwazo vyovyote kuhusu usafiri, biashara au mikusanyiko ya umma.
Licha ya kuthibitisha visa vinane vya ugonjwa huo, mamlaka zimeeleza wazi kuwa hakutakuwa na amri ya kukaa ndani ya kitaifa wala marufuku ya jumla ya kusafiri kwa Wakenya.
Jumatatu, Marekani ilitoa tahadhari ikiwashauri raia wake kufikiria upya safari za kwenda nchini Kenya kutokana na wasiwasi kuhusu Ebola. Nchi nyingine pia zimetoa tahadhari za kiafya, ikiwemo Uingereza, ambayo imewaonya raia wake kuwa wanaweza kukabiliwa na ukaguzi mkali zaidi wa afya. Canada nayo imewashauri raia wake kufuatilia hali zao za afya kwa siku 21.
Hata hivyo, hakuna nchi yoyote iliyoweka marufuku ya moja kwa moja kwa raia wake kutembelea Kenya, wala Wakenya hawajazuiwa kuingia katika nchi nyingine kutokana na hofu ya Ebola.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Je, biashara na shughuli za utalii vimeathirika?
Wachambuzi wameeleza wasiwasi kuhusu athari zinazoweza kutokea kwa safari za kimataifa na sekta ya utalii kutokana na hofu za afya ya umma, lakini hadi sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa hali hiyo imeathiri safari au utalii.
Hata hivyo, hali inaweza kubadilika iwapo mlipuko huo utaenea zaidi miongoni mwa wananchi na kuingia katika jamii kwa kiwango kikubwa.
Kuna Wakenya wangapi nchini DRC?
Idadi halisi ya Wakenya wanaoishi DR Congo haijulikani wazi. Ripoti iliyotayarishwa mwaka uliopita na taasisi ya utafiti ya Centre for Strategic and International Studies (CSIS) ilikadiria kuwa kulikuwa na takribani Wakenya 2,500 wanaoishi mashariki mwa DR Congo, wakiwemo karibu wawekezaji 50. Ripoti hiyo pia ilibainisha kuwa idadi ya Wacongo wanaoishi katika jiji la Nairobi pekee ilikuwa karibu mara nne ya idadi hiyo.
Ubalozi wa Kenya nchini DR Congo, uliopo katika mji mkuu wa Kinshasa, ambao pia unawakilisha maslahi ya Kenya katika nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo-Brazzaville na Gabon, umewahi kuwahimiza Wakenya wanaoishi katika eneo hilo kujisajili rasmi ili uweze kuwahudumia na kuwasaidia kwa ufanisi zaidi.
Nchi jirani zimechukua hatua gani?
Nchi kadhaa katika ukanda huu zimetangaza kuimarisha hatua za ufuatiliaji na uchunguzi wa afya kwa wageni wanaoingia nchini.
Nchini Somalia, mtu mmoja aliyekutana na mwanaume aliyefariki nchini Kenya amewekwa karantini, huku sampuli zake zikitumwa Kenya kwa ajili ya uchunguzi wa maabara.
Serikali ya Somalia pia imesema imechukua hatua za tahadhari, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji katika vituo vya mipakani, kutokana na hali inayoendelea kubadilika katika ukanda huu na harakati za watu kati ya nchi mbalimbali.
Mtu huyo anayeshukiwa kuwa na maambukizi nchini Somalia alikuwa amesafiri kupitia Ethiopia, ambayo nayo imetangaza kuimarisha ufuatiliaji ili kuzuia uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa huo.
Nchini Tanzania, wageni wanatakiwa kufuatiliwa afya zao kila siku kwa muda wa siku 21 kupitia mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji. Hatua hiyo ilitangazwa baada ya Kenya kuthibitisha visa kadhaa vya maambukizi ya Ebola.
Kwa upande wake, Uganda ilisema baada ya Kenya kuthibitisha kisa chake cha kwanza cha Ebola kuwa itaendelea kudumisha hatua madhubuti za ufuatiliaji ili kulinda afya ya umma.
Mfanyabiashara huyo Mkenya alikuwa amepitia Uganda akiwa njiani kurejea nyumbani kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Uganda iliripoti vifo viwili vya Ebola muda mfupi baada ya mlipuko huo kuripotiwa DR Congo, lakini baadaye Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa nchi hiyo imefanikiwa kudhibiti mlipuko huo na haina maambukizi ya Ebola.



































