Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Miaka 75 baadaye, viziwi bado wanaitaka dunia iwasikie
- Author, Damaris Kamande
- Nafasi, BBC Nairobi
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Wakati Shirikisho la Viziwi Duniani (WFD) likitimiza miaka 75, wanaharakati wanasema ujumuishaji wa kweli unahitaji kuvuka hatua za kawaida za usaidizi na kutambua haki za Viziwi kama haki za msingi za kiraia.
Kila mwezi wa Septemba, jamii kote ulimwenguni huadhimisha Mwezi wa Kimataifa wa Uhamasishaji kuhusu Viziwi, kampeni inayofikia kilele wakati wa Wiki ya Kimataifa ya Viziwi, tarehe 21 hadi 27 Septemba, pamoja na Siku ya Kimataifa ya Lugha za Ishara.
Mwaka huu una umuhimu wa pekee kwa WFD, ambayo inatimiza miaka 75 tangu kuanzishwa kwake. Kaulimbiu ya kimataifa ya mwaka 2026 ni: "Kutangaza Haki za Kibinadamu za Viziwi."
Barani Afrika, inakadiriwa kuwa watu milioni 40 wanaishi na tatizo kubwa la kutokusikia, wakiwemo takriban milioni 2.75 nchini Kenya. Kwa wanaharakati, mwezi huu ni fursa ya kuangazia vikwazo vinavyowazuia Viziwi kushiriki kikamilifu katika maisha ya umma, elimu na uongozi.
Wanahoji kuwa huduma kama ukalimani wa lugha ya ishara na mawasiliano yanayofikika bado mara nyingi huchukuliwa kama msaada wa hiari badala ya haki inayopaswa kuhakikishwa.
Wito wa kutambuliwa kwa lugha za ishara
Kote duniani, zaidi ya Viziwi milioni 70 wanategemea lugha za ishara kama njia yao kuu ya mawasiliano na sehemu muhimu ya utambulisho wao.
Hata hivyo, chini ya nusu ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinatambua kisheria lugha zao za kitaifa za ishara. Hali hiyo inaweza kuwazuia baadhi ya Viziwi kupata taarifa za dharura, huduma za afya, taratibu za kisheria na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa na kijamii.
Changamoto hizi zinaonekana pia katika sekta ya elimu, ambako tofauti za lugha zinaweza kuathiri fursa za wanafunzi viziwi.
Ndani ya madarasa ya Kenya: Kizingiti cha fursa sawa
Katika darasa moja huko Isinya, kusini mwa Nairobi, Eddah Bitengo anajibu maswali kwa lugha ya ishara kwa kujiamini. Mwanafunzi huyo wa Kidato cha Tatu anapenda hisabati na ana ndoto ya kuwa daktari.
Lakini anapofikia Kiingereza cha kuandika, mambo huwa magumu zaidi.
"Kiingereza ni tofauti na Lugha ya Ishara," Eddah anaeleza kupitia mkalimani.
Uzoefu wake unaonyesha changamoto inayowakabili baadhi ya wanafunzi Viziwi katika mfumo wa elimu. Ingawa Lugha ya Ishara ya Kenya (KSL) ndiyo lugha ya kwanza kwa watoto wengi Viziwi nchini humo, sarufi yake hutofautiana na ile ya Kiingereza cha kuandika.
Kwa mfano, Kiingereza hutumia mara nyingi muundo wa Somo-Kitenzi-Kielezi (SVO). Sentensi ya Kiingereza "This boy is taking my pen" kwa Kiswahili ni "Mvulana huyu anachukua kalamu yangu."
Katika Lugha ya Ishara ya Kenya, mpangilio wa maneno unaweza kuwa tofauti. Sentensi hiyo inaweza kuwasilishwa kwa mtindo unaokaribiana na "Mvulana kalamu hii yangu chukua."
Kwa kuwa mitihani ya kitaifa, elimu ya juu na ajira rasmi hutegemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa kutumia Kiingereza cha kuandika, baadhi ya wanafunzi Viziwi hukumbana na changamoto wanapohitimu shule, jambo linaloweza kuathiri fursa zao za elimu na ajira.
"Ujumuishaji lazima uwepo kila mahali"
Kwa waelimishaji na wanaharakati, changamoto hizi zinahitaji mabadiliko ya kisera na kimfumo badala ya kutegemea kampeni za uhamasishaji pekee.
"Tunaendelea kuwatenga Viziwi kwa kutowaruhusu kushiriki kikamilifu katika jamii," anasema Vincent Owino, mwanaharakati wa elimu jumuishi na aliyekuwa mwalimu katika Shule ya Viziwi ya Murang'a.
"Tunahitaji kufanya lugha iwe jumuishi na inayofikika kwao kila mahali, kuanzia ofisi za serikali hadi madarasani."
Benson Muhuhu, mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Viziwi ya Isinya, anasisitiza umuhimu wa kuboresha uwezo wa wanafunzi katika kusoma na kuandika ili waweze kuwa na fursa zaidi katika soko la ajira.
"Tunapaswa kutilia mkazo zaidi ufundishaji wa Kiingereza cha kuandika sambamba na KSL kwa sababu nataka wanafunzi wangu wapate kazi nzuri na kufanikiwa kwa usawa," anasema.
Wito wa hatua
Kwa jamii za Viziwi na wanaharakati, maadhimisho ya mwaka huu yanatoa fursa ya kuangalia zaidi ya uhamasishaji na kushughulikia vikwazo vinavyowazuia watu Viziwi kutumia haki zao kikamilifu.
Kutambua lugha za ishara, kuwekeza katika elimu ya lugha mbili na kuhakikisha huduma za umma zinapatikana kwa njia zinazofikika ni miongoni mwa hatua zinazotajwa kuleta ushiriki sawa wa Viziwi katika jamii.
Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa WFD, mjadala sasa unaangazia namna ya kuhakikisha haki hizo zinatambuliwa na kutekelezwa, badala ya kutegemea msaada wa hiari.
Imehaririwa na Asha Juma