Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani na Iran zafanya mazungumzo ya kwanza tangu Juni baada ya Trump kutishia "kuiangamiza"

Hakuna mafanikio yaliyoripotiwa kufikiwa katika mazungumzo hayo yaliyosimamiwa na Qatar, na yaliyowahusisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pamoja na mjumbe maalumu wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi

  1. Kifaa cha kurushwa kutoka angani chagonga meli ya mizigo Hormuz

    Shirika la Uendeshaji Biashara ya Baharini la Uingereza (UKMTO) limesema meli ya mizigo imegongwa na kifaa kisilojulikana katika Mlango-Bahari wa Hormuz, na kusababisha moto mkubwa na uliokwamisha meli hiyo baharini.

    Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo, wafanyakazi wote waliokuwamo ndani ya meli wamehamishwa, huku watu wawili wakijeruhiwa katika tukio hilo.

    UKMTO, ambalo linafanya kazi chini ya Jeshi la Wanamaji la Uingereza, limesema mamlaka husika zimeanzisha uchunguzi kubaini chanzo na mazingira ya shambulio hilo lililotokea Jumatano.

    Shirika hilo pia limeeleza kuwa mpaka sasa hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu uharibifu wa mazingira uliosababishwa na tukio hilo. Mamlaka zinaendelea kufuatilia hali ya eneo hilo huku uchunguzi ukiendelea.

  2. Wahouthi waionya Marekani kutoingilia mgogoro wa Yemen

    Mshauri wa kijeshi wa waasi wa Kihouthi nchini Yemen ameonya kuwa kundi hilo litashambulia maslahi ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati ikiwa Washington itaingilia kati vita vya Yemen kwa kuisaidia Saudi Arabia au kujaribu kufungua tena Mlango wa Bahari wa Bab al-Mandab.

    "Ikiwa Marekani itathubutu kuingilia kijeshi kupitia meli zake za kivita au kujaribu kudhibiti Bab al-Mandab, watakuwa wamevuka mstari mwekundu na kwa upande mwingine wowote," Abdel Mohammed al-Thawr alisema katika mahojiano na shirika la habari la AFP.

    Waasi hao wanaoungwa mkono na Iran hivi karibuni walidhibiti njia hiyo nyembamba ya usafirishaji wa majini inayounganisha Bahari ya Shamu na maeneo mengine ya kimataifa, huku Saudi Arabia ikiripotiwa kuomba msaada kutoka kwa Marekani na jumuiya ya kimataifa ili kukabiliana na Wahouthi.

    Vizuizi vya majini vya Wahouthi katika eneo la Bab al-Mandab umeongeza shinikizo kwa Saudi Arabia, ambayo ndiyo muuzaji mkubwa zaidi wa mafuta duniani.

    Hali hiyo, pamoja na vikwazo vya usafiri wa majini katika Mlango wa Hormuz vinavyotokana na mvutano wa vita kati ya Marekani na Iran, imechangia kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

  3. Netanyahu akerwa na kauli ya Macron kuhusu Ukingo wa Magharibi

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amemkosoa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kufuatia kauli yake ya kulaani vitendo vya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa wakati wa hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

    Akihutubia mkutano huo, Macron alisema hatua za Israel katika Ukingo wa Magharibi zinaendelea licha ya kundi la Hamas kutokuwa na shughuli kubwa katika eneo hilo. Hata hivyo, Netanyahu alipinga kauli hiyo akisema Hamas imehusika katika mashambulizi kadhaa ndani ya Ukingo wa Magharibi, na kuyataja matamshi ya rais huyo wa Ufaransa kuwa "ya kipuuzi."

    Mvutano huo unaongeza tofauti za kidiplomasia ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara kati ya Ufaransa na Israeli katika miaka ya hivi karibuni.

    Ufaransa imeendelea kuunga mkono suluhisho la mataifa mawili katika mzozo wa Israeli na Wapalestina, huku pia ikikosoa baadhi ya operesheni za kijeshi za Israeli katika Ukanda wa Gaza, msimamo ambao mara kadhaa umekosolewa vikali na viongozi wa Israel.

    Maelezo zaidi:

  4. Ndege za Iran zaendelea kwenda China licha ya vikwazo vipya vya Marekani

    Ndege ya shirika la Mahan Air kutoka Tehran imetua kusini mwa China, kulingana na taarifa za FlightRadar24, licha ya kuanza kutumika kwa vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya sekta ya usafiri wa anga ya Iran.

    Safari hata hiyo haikuonekana katika orodha ya safari zilizochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Uwanja wa Ndege wa Guangzhou Baiyun, licha ya taarifa za FlightRadar24 kuonyesha kuwa ndege namba 093 ya Mahan Air ilitua mjini Guangzhou saa 10:39 jioni kwa saa za huko, Jumatano.

    Wakati huo huo, mashirika kadhaa ya ndege ya Iran yameendelea na shughuli za kawaida katika njia ya Yerevan-Tehran. Taarifa kutoka Uwanja wa Ndege wa Zvartnots nchini Armenia zinaonyesha kuwa ndege za mashirika ya Caspian Airlines, Fly Air na Kish Air ziliondoka Yerevan kuelekea Tehran, huku safari mbili kati ya sita zilizokuwa zimepangwa zikiahirishwa.

    Hatua hizo zinajiri wakati Marekani ikianza kutekeleza vikwazo dhidi ya mataifa yanayoruhusu ndege za Iran kutumia viwanja vyao vya ndege. Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, ameonya kuwa nchi yoyote itakayotoa huduma za kutua kwa ndege za Iran inaweza kuondolewa kwenye mfumo wa matumizi ya dola za Marekani.

    Bessent amesema pia kuwa kuanzia Septemba 23, mashirika yote ya ndege ya Iran yatakabiliwa na hatua kali za vikwazo. Hata hivyo, hakutoa maelezo kuhusu safari za moja kwa moja za ndege za Iran kuelekea China.

    Mashirika ya ndege ya Iran yanaendelea na safari za mara kwa mara kuelekea Armenia na miji mikubwa ya China, ikiwemo Beijing, Shanghai na Guangzhou.

    Soma pia:

  5. Marekani yamnyima visa mkuu wa jeshi la Sudan kuhudhuria UN

    Marekani imemnyima visa mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al Burhan, ambaye alitarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

    Kwa mujibu wa Reuters, uamuzi huo unaonekana kuhusishwa na pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano nchini Sudan kwa siku 90. Pendekezo hilo, lililotolewa na mshauri mkuu wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika na Arabuni, Massad Boulos, linataka kusitishwa kwa mapigano, kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu na kuanza kwa mazungumzo mapana ya kisiasa.

    Jeshi la Sudan linaloongozwa na Burhan limeonyesha kutoridhishwa na pendekezo hilo, likisema mapatano ya awali ya kusitisha mapigano yaliipa nafasi RSF kujipanga upya.

    Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric, amesema Katibu Mkuu António Guterres ana wasiwasi kuhusu suala hilo na amewasiliana na maafisa wa Marekani. Amesisitiza kuwa ushiriki kamili wa wajumbe wa nchi wanachama katika shughuli za Umoja wa Mataifa ni muhimu kwa utendaji wa shirika hilo.

    Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Al Harith Idriss, amesema Khartoum imeomba Guterres kuingilia kati. Sudan inasema imetimiza masharti ya ziara ya Burhan na kwamba Marekani ina wajibu chini ya makubaliano ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuruhusu wawakilishi wa nchi wanachama kuhudhuria mikutano ya UN.

    Marekani, hata hivyo, imesema jeshi la Sudan pamoja na RSF na viongozi wao hazina uhalali wa kikatiba wa kuiongoza Sudan, huku Washington ikisema itaongeza shinikizo kwa pande zote zinazopigana nchini humo.

    Uamuzi huo unakuja baada ya Marekani kumwekea Burhan vikwazo Januari 2025, ikimtuhumu kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kuzuia juhudi za amani.

    Maelezo zaidi:

  6. Watu 11 wauawa kwa kupigwa risasi ndani ya nyumba Afrika Kusini

    Takriban watu 11 wameuawa kwa kupigwa risasi katika nyumba moja ya makazi karibu na jiji la Durban, Afrika Kusini.

    Polisi wamesema watu wenye silaha waliingia katika nyumba hiyo iliyoko katika mtaa wa KwaMakhutha Jumanne usiku na kuwafyatulia risasi watu 14.

    Watu 10 waliuawa papo hapo, huku wengine wanne wakipelekwa hospitalini. Mmoja wao alifariki baadaye kutokana na majeraha, polisi wamesema.

    Polisi wamesema baadhi ya waathiriwa walikuwa chini ya uangalizi wao kuhusiana na shughuli haramu, lakini hawakuweza kutoa maelezo zaidi kwa sasa ili kulinda uchunguzi unaoendelea.

    Sababu ya shambulio hilo bado haijathibitishwa, ingawa polisi hawajapuuza uwezekano wa kuwa kulikuwa na mzozo kati ya makundi hasimu.

    Kwa mujibu wa polisi, watu 13, wanaume, pamoja na mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa mjamzito, walikuwa wakisherehekea ndani ya nyumba hiyo wakati wanaume watatu walipofika na kuanza kuwafyatulia risasi. Mwanamke huyo ni miongoni mwa waliouawa.

    Mwandishi wa kituo cha televisheni cha eNCA aliyekuwa eneo la tukio alisema washambuliaji pia waliichoma moto gari lililokuwa likimilikiwa na mmoja wa waathiriwa kabla ya kutoroka. Picha kutoka eneo hilo zilionyesha mabaki ya gari hilo yakiwa yameteketea.

    Polisi wameanzisha msako wa kuwatafuta washukiwa wa shambulio hilo.

    Afrika Kusini ina miongoni mwa viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani. Takwimu za polisi zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 60 huuawa kila siku kwa wastani nchini humo.

    Maelezo zaidi:

  7. Safari za ndege Tigray zafutwa huku mvutano ukiongezeka

    Safari zote za ndege kuelekea eneo la Tigray zimesimamishwa baada ya vikosi vya Tigray kutangaza kuwa vimechukua udhibiti wa viwanja vya ndege katika eneo hilo leo alasiri.

    Shirika la Ndege la Ethiopia lilitangaza kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook Jumatano kwamba safari za ndege kuelekea Tigray zimesimamishwa kwa muda.

    Mvutano umekuwa ukiongezeka katika eneo hilo katika miezi ya hivi karibuni, baada ya chama cha TPLF kuiondoa serikali ya mpito ya Tigray iliyoteuliwa na serikali kuu.

    Aidha, mashambulizi kwa kutumia ndege zisizo na rubani yamekuwa yakitekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Tigray kwa nyakati tofauti.

    Kusimamishwa kwa safari za ndege kumetokea baada ya wapiganaji wa Tigray kudai kuchukua udhibiti wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Alula Aba Nega mjini Mekelle.

    Katika siku za hivi karibuni, makundi yenye silaha yenye misimamo na maslahi tofauti yameunda muungano unaoitwa "Alliance for Existence", ukiwa na lengo la kuiondoa madarakani serikali ya shirikisho inayoongozwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed na kuunda serikali ya mpito "jumuishi".

    Muungano huo unajumuisha Fano Amhara National Movement, FAB, Tigray People's Liberation Front, TPLF, Oromo Liberation Army, OLA, Ogaden National Liberation Front, ONLF, Afar National Unity Revolutionary Front, Ugugumo, Benishangul Peoples' Liberation Movement na Gumuz Peoples' Democratic Movement.

    Kumekuwa na wasiwasi kwamba muungano huo unaweza kuongeza zaidi mvutano kati ya serikali ya shirikisho na vikosi vya Tigray.

    Soma zaidi:

  8. Marekani kujenga kambi mbili za kijeshi Greenland

    Marekani, Denmark na Greenland zimetia saini makubaliano ya ulinzi yatakayoruhusu Washington kujenga kambi mbili mpya za kijeshi katika eneo hilo la Aktiki, huku yakithibitisha tena mamlaka ya Denmark juu ya Greenland.

    Kabla ya hafla ya kusaini makubaliano hayo katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Washington itaanza mara moja mchakato wa kujenga uwepo mkubwa wa kijeshi katika maeneo yatakayofaa.

    Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, alisema makubaliano hayo ni manufaa kwa Marekani, Denmark na Greenland, pamoja na Ulaya na NATO.

    Waziri Mkuu wa Greenland, Jens Frederik Nielsen, aliyasifu makubaliano hayo kuwa manufaa kwa pande zote tatu.

    Viongozi hao watatu walitia saini makubaliano hayo, hatua inayoonekana kumaliza mvutano wa zaidi ya mwaka mmoja kuhusu mustakabali wa eneo hilo la Aktiki.

    Trump alikuwa ametishia kuichukua Greenland, akisema wasiwasi wa usalama wa taifa ndio uliomsukuma kutoa kauli hiyo. Alitaja pia umuhimu wa kimkakati wa eneo hilo katika masuala ya ulinzi pamoja na utajiri wake wa madini.

    Kauli hizo zilisababisha malalamiko kutoka kwa wakazi wa Greenland, Denmark na viongozi wa Ulaya, ambao walitoa taarifa ya pamoja wakisema matamshi ya Trump yalidhoofisha uhusiano kati ya Ulaya na Marekani na kuhatarisha kuzorota zaidi kwa uhusiano wa pande hizo.

    Soma pia:

  9. M23 yapinga tuhuma za kuwaua wachimbaji na kusafirisha madini Rwanda

    Kundi la AFC/M23 limekanusha tuhuma za Amnesty International kwamba limewaua na kuwanyanyasa wachimbaji wadogo, pamoja na kusafirisha kwa magendo dhahabu na koltani kwenda Rwanda.

    Katika taarifa iliyotolewa mjini Goma Jumanne, AFC/M23 ilisema Amnesty International haijatoa ushahidi wa kuaminika unaoweza kuthibitisha tuhuma hizo.

    Katika ripoti iliyochapishwa Jumatatu, Amnesty International ililituhumu kundi hilo kwa mauaji, mateso, kuweka watu kizuizini kiholela, kufanya kazi za kulazimishwa na kuwalazimisha watu kujiunga na makundi yenye silaha.

    Shirika hilo lilisema matukio hayo yalitokea katika mgodi wa koltani wa Rubaya, Kivu Kaskazini, na mgodi wa dhahabu wa Lomera, Kivu Kusini. Amnesty ilisema iliwahoji watu 26 na kuchambua picha pamoja na video zilizorekodiwa katika maeneo hayo.

    AFC/M23 ilisema uzito wa tuhuma hizo unahitaji ushahidi unaoonyesha ni lini na wapi uhalifu huo ulifanyika, nani waliohusika na uhusiano wao na watu waliokuwa au wanaoongoza kundi hilo.

    Kuhusu tuhuma za kusafirisha madini kwa magendo kwenda Rwanda, AFC/M23 ilisema kusikia watu wakizungumza Kinyarwanda au kuwaona raia wa Rwanda katika eneo hilo hakutoshi kuthibitisha kwamba serikali ya Rwanda inahusika.

    Kundi hilo lilisema Kinyarwanda huzungumzwa na jamii nyingi katika Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, na kuonya kwamba kuwahusisha wanaozungumza lugha hiyo na utaifa wa Rwanda kunaweza kuchochea mgawanyiko.

    Amnesty International ilikuwa imetoa wito kwa nchi na mashirika kuacha kununua dhahabu na koltani kutoka Rwanda hadi Kigali ithibitishe kuwa madini hayo hayakusafirishwa kwa magendo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Soma Pia:

  10. Ni meli ngapi hupita katika Mlango Bahari wa Hormuz?

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba idadi ya meli zinazopita katika Mlango Bahari wa Hormuz imeongezeka, akisema mafuta mengi zaidi yanapita katika njia hiyo kuliko wakati wowote tangu kuanza kwa vita vya Iran.

    Trump alisema takriban meli 22, 25, 30, 32 na hadi 37 zinaachiliwa kupita kila siku na kila usiku.

    Hata hivyo, takwimu kutoka kampuni ya kijasusi ya masuala ya usafirishaji baharini, Kpler, zinaonyesha picha tofauti.

    Kpler inakadiria kuwa jumla ya meli za aina zote zilizopita katika Mlango Bahari wa Hormuz wiki iliyopita ilikuwa kati ya meli 9 na 24 kwa siku.

    Idadi hiyo iko chini kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wastani wa takriban meli 140 kwa siku uliokuwepo kabla ya vita.

    Takwimu za Kpler pia zinaonyesha kuwa wastani wa mapipa milioni 8.1 ya mafuta ghafi kwa siku ulipita katika Hormuz wiki iliyopita, ikilinganishwa na wastani wa mapipa milioni 13.5 kwa siku kabla ya vita.

    Hivyo, wakati Trump akieleza ongezeko la meli zinazopita katika njia hiyo, takwimu za Kpler zinaonyesha kuwa trafiki ya meli na kiasi cha mafuta kinachopita Hormuz bado kiko chini ya viwango vya kabla ya vita.

    Zaidi soma hapa:

  11. Trump apendekeza AI iitwe 'Super Intelligence'

    Rais wa Marekani Donald Trump amependekeza jina jipya la teknolojia ya akili bandia, AI, akiiita Super Intelligence, au SI.

    Akizungumza katika hotuba yake, Trump alisema matumizi ya neno “artificial”, linalomaanisha bandia, yanaweza kufanya teknolojia hiyo ionekane kana kwamba si kitu halisi.

    Alisema, “Kutumia neno ‘bandia’ kunafanya ionekane kama kitu ambacho si halisi. Si hivyo, kwa kweli ni jambo la kushangaza. Lakini tunapaswa kuwa waangalifu.”

    Trump pia alisema, “Karibuni katika ulimwengu mpya wa akili iliyoboreshwa, AI.”

    Hapo awali, Trump amesema nchi itakayoshinda katika mashindano ya AI itakuwa mshindi, huku akipinga kwa kiasi kikubwa kuwekwa kwa kanuni kali za kudhibiti teknolojia hiyo.

    Msimamo huo unatofautiana na ule wa baadhi ya viongozi na wawakilishi wanaoshiriki mkutano huo.

    Huku maendeleo ya AI yakiendelea kwa kasi, mjadala sasa ni iwapo diplomasia na juhudi za kuweka kanuni za kimataifa zinaweza kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia hiyo.

    Soma Pia:

  12. Tetesi za Soka Ulaya: Man Utd na Liverpool zapigana vikumbo kwa Mitchell

    Manchester United na Liverpool zinaonyesha nia ya kumsajili beki wa Crystal Palace, Tyrick Mitchell, huku kiungo mshambuliaji wa Aston Villa, Alejandro Garnacho, akifuatiliwa na vilabu vya La Liga baada ya kushindwa kufanya vizuri tangu alipohamia Villa Park kwa mkopo akitokea Chelsea. Wakati huo huo, Bayern Munich inamtaka kiungo wa Nottingham Forest, Morgan Gibbs White.

    Beki wa kushoto wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Tyrick Mitchell, mwenye umri wa miaka 27, anaendelea kuvutia Manchester United na Liverpool. (Teamtalk)

    Kiungo mshambuliaji wa Aston Villa, Alejandro Garnacho, anafuatiliwa na vilabu vya La Liga baada ya kushindwa kung'aa zaidi Villa Park tangu alipohamia kwa mkopo kutoka Chelsea katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi. (Mail plus - subscription required)

    Julian Ward anatarajiwa kurejea katika nafasi ya mkurugenzi wa michezo wa Liverpool. Ward mwenye umri wa miaka 45 ataacha nafasi yake ya sasa ya mkurugenzi wa ufundi katika Fenway Sports Group na kuchukua nafasi ya Richard Hughes. Awali aliwahi kushikilia nafasi hiyo Liverpool katika msimu wa 2022 hadi 2023. (The Athletic)

    Bayern Munich inamvizia kiungo wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya England, Morgan Gibbs White, mwenye umri wa miaka 26. (Talksport)

    Arsenal itatumia mapumziko ya mechi za kimataifa ya Septemba kukamilisha maelezo ya mkataba mpya wa muda mrefu na kiungo wa England, Declan Rice, mwenye umri wa miaka 27. (Football Transfers)

    Arsenal ina kipengele kinachoiwezesha kuongeza mkataba wa sasa wa Rice kwa mwaka mmoja zaidi, lakini klabu hiyo inapendelea kumfunga kwa mkataba wa muda mrefu, kulingana na sera yake ya kuwaongezea mikataba wachezaji wanaoonekana kuwa muhimu katika mipango ya kocha Mikel Arteta. (Guardian)

    Liverpool bado imejikita katika kuhakikisha inapata kiwango bora kutoka kwa kiungo mshambuliaji wa Ujerumani, Florian Wirtz, mwenye miaka 23, licha ya wawakilishi wa mchezaji huyo kuwasiliana na Bayern Munich. (Teamtalk), external

    Chelsea inamfuatilia kwa karibu kiungo wa Gambia mwenye umri wa miaka 15, Adama Jeng, ambaye pia anavutia Bayern Munich, Benfica, Sporting na Paris FC. Jeng anakipiga katika klabu ya Samger FC. (Mail plus - subscription required)

    AC Milan na Roma zinaonyesha nia ya kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Real Madrid, Endrick, mwenye umri wa miaka 20, iwapo rais wa Real Madrid, Florentino Perez, ataruhusu Mbrazil huyo kuondoka. (Calciomercato - in Italian)

    Barcelona imemfuatilia beki wa Brazil mwenye umri wa miaka 19, Arthur Dias, anayekipiga katika klabu ya Athletico Paranaense. Mchezaji huyo aliwahi kuvutia kwa kiasi kikubwa Tottenham. (ESPN Brasil - in Portuguese)

    Arsenal ilikuwa karibu sana kumsajili mshambuliaji wa Brazil, Vinicius Jr, kutoka Real Madrid katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi kiasi kwamba baadhi ya wachezaji wenzake walidhani tayari ilikuwa imekubalika kuwa angejiunga na Gunners. (Cadena SER - in Spanish)

    Pia unaweza kusoma:

  13. Ufaransa yaandaa azimio kuhusu kufunguliwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz

    Taarifa kutoka katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa Ufaransa, kwa ushirikiano na Marekani, imeanza kuandaa azimio litakalowasilishwa kwa Baraza hilo.

    Maafisa wa kidiplomasia wamesema Jumanne kuwa azimio hilo linalenga kuanzisha operesheni ya kimataifa ya kurejesha usafirishaji wa meli katika Mlango Bahari wa Hormuz.

    Hatua hiyo inakuja baada ya juhudi za awali za Ufaransa za kuandaa azimio kama hilo kushindikana.

    Mpango huo mpya umefuatia mazungumzo kati ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Rais wa Marekani Donald Trump yaliyofanyika Jumatatu jioni, wakati viongozi hao walipokuwa mjini New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

    Baada ya mkutano huo, Macron alisema:

    “Chaguzi kadhaa zilijadiliwa. Katika saa zijazo, tutafanya kazi kutafuta suluhisho za kidiplomasia ambazo zinaweza kuruhusu meli nyingi zaidi za mizigo na mafuta kupita, hata kama makubaliano kamili hayatapatikana.”

    Baadhi ya maafisa wa ujumbe wa Ufaransa wamesema Macron anatarajia kuwasilisha rasimu ya azimio hilo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni.

    Soma Zaidi:

  14. Trump athibitisha mazungumzo ya Marekani na Iran ya kumaliza vita

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jumanne kwamba wawakilishi maalum wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, wamekutana na wapatanishi kujadili uwezekano wa makubaliano ya kumaliza vita kati ya Marekani na Iran.

    Wakati huo huo, Shirika la Utangazaji la Iran limeripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alikutana na Steve Witkoff pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York.

    Kwa mujibu wa shirika hilo, lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kuwasilisha masharti ya Iran ya kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz.

    Iran imetaja kuondolewa mara moja kwa kizuizi cha majini, kuachiliwa kwa mali zake zote zilizogandishwa na kusitishwa kwa mapigano katika maeneo yote yanayohusisha makundi yanayoiunga mkono, kuwa miongoni mwa masharti yake.

    Viongozi mbalimbali wa nchi wako mjini New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulioanza leo.

    Pakistan na Qatar ndizo nchi mbili zinazohusika katika juhudi za upatanishi kati ya Iran na Marekani.

    Maelezo zaidi:

  15. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 23/09/2026.