Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Uingereza yatangaza 'kuisaidia kijeshi' Saudi Arabia dhidi ya Wahouthi

Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, amesema Uingereza itatoa msaada wa kujihami wa kuongeza mafuta angani kwa Saudi Arabia, kufuatia mashambulizi ya Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen dhidi ya Saudi Arabia.

Muhtasari

Uingereza yatangaza msaada wa kijeshi dhidi ya Wahouthi kwa ombi la Saudi Arabia

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. EU yailaumu Urusi kwa kuwatia hofu wanachama wake

    Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, ameilaumu Urusi kwa kujaribu kupunguza uungwaji mkono wa nchi wanachama wa EU kwa Ukraine kwa kueneza hofu barani Ulaya.

    “Ulaya inashuhudia ongezeko kubwa la mashambulizi ya siri na vitendo vya hujuma, pamoja na ukiukaji wa anga yake,” alisema Kallas.

    Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Kallas alisema: “Kadiri Urusi inavyozidisha vitendo vyake vya uharibifu, “Ulaya nayo lazima iongeze shinikizo dhidi ya Urusi na kuhakikisha inalipa gharama kwa vitendo hivyo.”

    Kallas amesema hatua mbili zinazoweza kuongeza shinikizo kwa Urusi ni kuchukua hatua kali dhidi ya meli zinazotumiwa na nchi hiyo kusafirisha mafuta ili kukwepa vikwazo, pamoja na kuimarisha vikwazo dhidi ya sekta yake ya kijeshi na ulinzi.

  2. Trump aanzisha kituo kipya cha habari huku vyombo vya habari vikichukua hatua

    Ikulu ya Marekani imezindua kituo cha televisheni mtandaoni kinachoitwa Trump TV, hatua inayokuja saa chache baada ya mitandao mikubwa ya televisheni nchini humo kusitisha kwa pamoja matangazo yao kutoka Ikulu.

    Hatua hiyo ya vyombo vya habari imekuja baada ya Rais Donald Trump kuzuia CNN, MS NOW na Politico kuingia Ikulu, akivituhumu kwa kusambaza taarifa za uongo. Vyombo hivyo vimefungua kesi dhidi ya utawala wa Trump, vikidai hatua hiyo inakiuka haki zao za kikatiba za uhuru wa vyombo vya habari.

    Tovuti ya Ikulu imeeleza Trump TV kuwa “kituo muhimu cha kupata taarifa muhimu”.

    Katika taarifa yake, utawala wa Trump umesema kupata fursa ya kufanya kazi Ikulu ni “upendeleo, si haki” kwa kila mtu. Pia umesema rais halazimiki kuruhusu kile ilichokiita chombo cha habari chenye uhasama kufanya kazi ndani ya Ikulu.

    Wakati huo huo, mitandao mingine mikubwa ya televisheni, ikiwemo ABC, CBS, NBC na Fox News, imesitisha matangazo ya matukio ya rais kwa kutumia mfumo wa pamoja wa kuripoti Ikulu, kufuatia kuzuiwa kwa CNN.

    CNN, MS NOW na Politico zimesema zitapinga hatua hiyo mahakamani, zikidai kuwa inalenga kuzuia kazi yao ya uandishi wa habari na inakiuka uhuru wa vyombo vya habari.

  3. Uturuki, Iraq na Georgia zapiga marufuku ndege za Iran

    Baada ya Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessant, kutangaza kuwa mashirika ya ndege ya Iran yatapigwa marufuku kufanya safari za kimataifa katika siku zijazo, Iraq na Georgia zimejiunga na Uturuki kupiga marufuku ndege za Iran kuingia katika nchi zao.

    Shirika la ndege la Mahan Air lilisema awali kuwa Uturuki imelijulisha kusitisha safari zake kwenda nchini humo.

    Vyanzo viwili nchini Iraq viliiambia AFP Jumatatu kuwa Baghdad itasitisha safari za mashirika ya ndege ya Iran, kufuatia tangazo la Wizara ya Hazina ya Marekani.

    Taarifa zinazoendelea kupatikana zinaeleza kuwa Georgia pia imepiga marufuku mashirika ya ndege ya Iran kuingia katika anga yake.

  4. Tetesi za Soka Jumanne: Liverpool yaingia kwenye kinyang'anyiro cha kumnasa Read

    Liverpool wanaendelea kumfuatilia beki wa kulia wa Feyenoord, Givairo Read, mwenye umri wa miaka 20. Hata hivyo, Manchester City na Arsenal pia zinamtaka kinda huyo wa timu ya taifa ya Uholanzi chini ya miaka 21(Teamtalk)

    Mshambuliaji wa Brazil, Raphinha, mwenye umri wa miaka 29, anataka kuendelea kuichezea Barcelona, huku mazungumzo ya awali kuhusu mkataba mpya yakiwa yameanza. Mkataba wake wa sasa unaisha mwaka 2028.(AS - in Spanish)

    Tottenham haitafanya juhudi za kumsajili mshambuliaji wa Argentina, Mauro Icardi, mwenye umri wa miaka 33, ambaye yuko huru kusajiliwa baada ya kumalizika kwa mkataba wake. (Football Insider)

    Brighton & Hove Albion na Aston Villa zote zinamuwania kinda wa Paraguay, Mauro Coronel, mwenye umri wa miaka 18, anayekipiga Nacional. (Teamtalk)

    Newcastle inalenga kumsajili beki wa kati mwenye umri mdogo na mshambuliaji anayepiga upande wa kulia katika dirisha la usajili la Januari na kuendelea. (The I)

    Barcelona inatarajiwa kuweka kipengele cha kuvunja mkataba cha pauni milioni 428, sawa na euro milioni 500, katika mkataba mpya wa kiungo wa Uhispania, Marc Bernal, mwenye umri wa miaka 19.(Mundo Deportivo - in Spanish)

  5. Walinzi wa Mapinduzi Iran IRGC wadai kuimarisha uwezo wa kijeshi

    Naibu kamanda wa Walinzi wa Mapinduzi wa Iran, Mustafa Ezadi, amesema vikosi vya kijeshi vya Iran vinaendelea kuimarisha uwezo wao wa kijeshi.

    Kwa mujibu wa BBC Persian, vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa Ezadi alikaribisha kuendelea kwa wafuasi wa serikali kujitokeza mitaani nyakati za usiku, akisema:

    “Iwapo uwepo wa wananchi utaendelea, njama nyingi za adui zitazuiwa.”

    Naibu kamanda huyo amesema Iran kwa sasa inaendelea kuimarisha uwezo wake katika maeneo ya makombora, ndege zisizo na rubani, makombora ya kusafiri, mifumo ya mtandao, vita vya kielektroniki na ulinzi wa anga.

  6. Uingereza yatangaza msaada wa kijeshi dhidi ya Wahouthi kwa ombi la Saudi Arabia

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, amesema Uingereza itatoa msaada wa kujihami wa kuongeza mafuta angani kwa Saudi Arabia, kufuatia mashambulizi ya Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen dhidi ya Saudi Arabia.

    Uingereza imesema msaada huo utaanza kutolewa katika siku chache zijazo na utahusisha ndege ya Uingereza aina ya Voyager, itakayoendesha shughuli zake kutoka kituo cha jeshi la anga cha RAF Akrotiri nchini Cyprus.

    Waziri Mkuu amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Saudi Arabia kuomba “msaada wa kijeshi”, ombi alilolidhinisha kwa ushauri wa Waziri wa Ulinzi Wes Strating na Waziri wa Mambo ya Nje Ed Miliband.

    Maafisa wa Uingereza wamesema msaada huo utatolewa kwa “muda mfupi” na awali unaweza kudumu kwa “wiki kadhaa”.

    Wahouthi wanapigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa na inayoungwa mkono na Saudi Arabia.

    Katika siku za hivi karibuni, Wahouthi wamesema wamefanya mashambulizi kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu dhidi ya mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, pamoja na miundombinu ya nishati katika pwani ya Bahari ya Shamu.

    Kwa mujibu wa maafisa wa Uingereza, msaada huo wa “kujilinda” unaweza pia kuhusisha kusaidia ndege za jeshi la anga la Saudi Arabia kuzuia makombora na ndege zisizo na rubani zinazoelekezwa nchini humo.

    Saudi Arabia inakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na mashambulizi ya Wahouthi nchini Yemen, ambao wanaonekana kuwa na upatikanaji wa mara kwa mara wa ndege zisizo na rubani na makombora, huku wakilenga nchi hiyo jirani ya kaskazini.

    Yemen imekuwa katika vita vya vipindi tangu mwaka 2014. Kuongezeka kwa mapigano hivi karibuni kumezidisha hali hiyo, hasa kutokana na uungwaji mkono wa Wahouthi na Iran, wakati Iran yenyewe ikiwa katika mzozo wa vipindi na Marekani.

    Soma Zaidi:

  7. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 22/09/2026.