Zijue njia tano rahisi za kupunguza mafuta ya tumbo

Mafuta ya ziada ya mwili, ambayo yanaweza kudhoofisha usawa wa mwili, husababisha ugonjwa wa kisukari na ugonjwa wa moyo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mafuta ya ziada ya mwili, ambayo yanaweza kudhoofisha usawa wa mwili, husababisha ugonjwa wa kisukari na ugonjwa wa moyo.
    • Author, Sumeeran Preet Kaur
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Watu wengi hufanya mazoezi ili kupunguza mafuta ya tumbo, lakini baadhi yao hawazingatii kwa umakini suala hili.

Mafuta ya tumboni, yanayojulikana pia kama "tumbo la bia," ni tatizo la kawaida miongoni mwa vijana wanaojali muonekano na afya zao.

Kutokana na mkusanyiko wa mafuta haya kwenye tumbo, watu hushindwa kuvaa nguo zinazowatosha na kuwapa faraja. Hata hivyo, tatizo hili si la mavazi tu, imethibitishwa kuwa mafuta ya tumboni ni hatari kwa afya.

Mafuta haya yanaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya kama shinikizo la damu, kiwango cha juu cha sukari mwilini, na matatizo ya lehemu (cholesterol). Magonjwa haya hutokana na mafuta yanayokusanyika kwenye eneo la tumbo.

Pia huongeza hatari ya ugonjwa wa kisukari aina ya pili na magonjwa ya moyo.

rdf

Chanzo cha picha, Getty Images

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Harvard unaonyesha kuwa aina ya protini iitwayo cytokine huzalishwa kwa wingi zaidi pale mafuta yanapokusanyika tumboni, na husababisha uvimbe mwilini.

Mafuta ya tumboni pia huzalisha protini nyingine iitwayo angiotensin, ambayo inaweza kusababisha mishipa ya damu kubana na kuongeza shinikizo la damu.

Hali hii huongeza hatari ya kupata magonjwa kama kupoteza kumbukumbu (dementia), pumu, na baadhi ya saratani.

Kulingana na Dkt. Shiv Kumar Choudhry, daktari bingwa wa moyo katika Hospitali ya Fortis Escorts mjini Delhi, mafuta ya tumboni ni hatari zaidi kuliko yale yaliyoko sehemu nyingine za mwili.

"Seli za mafuta ya tumbo zinapopasuka, vitu vingi vya sumu hutolewa. Dutu hizi husababisha kuvimba kwa mishipa ya damu kwenye moyo, na kuongeza hatari ya ugonjwa wa moyo. Pia husababisha upinzani wa insulini, na kuongeza hatari ya ugonjwa wa kisukari," anafafanua.

Mafuta ya tumbo ni chanzo cha matatizo kama vile shinikizo la damu, sukari ya juu ya damu, na cholesterol kubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mafuta ya tumbo ni chanzo cha matatizo kama vile shinikizo la damu, sukari ya juu ya damu, na cholesterol kubwa.

Wataalamu wanasema sababu za kuongezeka kwa mafuta ya tumbo ni pamoja na urithi wa kinasaba, mabadiliko ya homoni, umri, uzito uliopitiliza, na kipindi cha ukomo wa hedhi (menopause).

Mtindo usiofaa wa maisha na lishe duni pia huchangia tatizo hili.

Hata hivyo, inawezekana kupunguza mafuta ya tumbo kwa kufuata lishe bora, kufanya mazoezi kila siku, na kuwa na mtindo mzuri wa maisha.

Mazoezi ni muhimu ili kudhibiti mkusanyiko wa mafuta katika eneo la tumbo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mazoezi ni muhimu ili kudhibiti mkusanyiko wa mafuta katika eneo la tumbo.

Zifuatazo ni njia tano muhimu:

1. Tofauti kati ya muda wa chakula cha jioni na kulala

Inashauriwa kuepuka kula ndani ya saa mbili hadi tatu kabla ya kulala.

Chakula kinacholiwa mchana hubadilishwa kuwa nishati, lakini cha jioni huweza kuhifadhiwa mwilini na kuongeza uzito.

2. Kula lishe bora na yenye uwiano

Vyakula vyenye nyuzinyuzi (fiber) hukufanya usishibe haraka. Pia husaidia kushiba kwa muda mrefu.

Ongeza protini kama mayai, dengu, maziwa, jibini, mtindi, samaki, kuku na soya - hupunguza njaa na kuongeza uchomaji wa kalori.

Ikiwa unatumia vyakula vyenye fiber, huwezi kuwa na njaa kwa muda mrefu na utakula kidogo, ambayo hupunguza hatari ya unene kupita kiasi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ikiwa unatumia vyakula vyenye nyuzinyuzi, huwezi kuwa na njaa kwa muda mrefu na utakula kidogo, ambapo hupunguza hatari ya unene kupita kiasi.

3. Epuka vyakula vilivyosindikwa sana

Vyakula vilivyokobolewa na vyenye sukari nyingi huongeza sukari kwenye damu haraka, na kusababisha njaa na kuongezeka uzito.

Chagua vyakula asilia kama matunda, karanga, na nafaka zisizokobolewa.

Punguza pombe na acha kuvuta sigara.

Wataalamu wanashauri kuepuka vitafunio vilivyochakatwa zaidi kama vile keki, vidakuzi na keki. Aina hizi za vyakula huchangia mkusanyiko wa haraka wa mafuta ya tumbo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wataalamu wanashauri kuepuka vitafunio vilivyochakatwa zaidi kama vile keki, vidakuzi na keki. Aina hizi za vyakula huchangia mkusanyiko wa haraka wa mafuta ya tumbo.

4. Pata usingizi wa kutosha

Ukosefu wa usingizi huongeza homoni ya njaa (ghrelin), na hivyo kuongeza hamu ya kula.

Msongo wa mawazo pia huongeza homoni ya cortisol, inayochochea kula kupita kiasi.

5. Fanya mazoezi mara kwa mara

Mazoezi husaidia kuchoma kalori na kupunguza mafuta ya tumbo.

Shughuli kama kutembea kwa kasi, kukimbia, kuendesha baiskeli, kuogelea au yoga husaidia pia kuboresha afya ya moyo na kuongeza kasi ya mwili kutumia nishati.

Kupunguza mafuta ya tumboni husaidia kupunguza hatari ya kisukari, shinikizo la damu, na magonjwa ya moyo.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi