Waridi wa BBC : Kutana na mwanadiplomasia ambaye ni fundi seremala

    • Author, Martha Saranga
    • Nafasi, BBC SWAHILI
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Umoja wa mataifa unakadiria asilimia 85 ya vijana duniani wanaishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati, ambapo sekta kama kilimo na ujasiriamali binafsi kujiajiri ni muhimu kwa maisha yao.

Witness Wilson Kimath ni miongoni mwa vijana waliogeukia fani ya ujasiriamali wa ufundi seremala.

Ni baada ya kuondokewa na baba yake mzazi tukio lililomuumiza na kumtikisa kwa kiasi kikubwa Witness Wilson Kimath 24 alilazimika kusimamisha kwa muda masomo yake ya diplomasia nchini Tanzania.

Uamuzi wa kusitisha masomo yake kwa muda ulifuatiwa na kuelekeza nguvu, akili, na hisia zake zote katika kukuza kipaji chake cha ufundi seremala, kazi ambayo kwa wengi haikuwa ya kawaida kwa msichana wa umri na elimu yake.

"Baba yangu alipofariki tu, nilipata hali kama ya kuchanganyikiwa hivi na nikashindwa kabisa kuendelea na masomo kwa wakati huo," anasimulia Witness, mkazi wa jiji la Dar es Salaam, akizingatia jinsi msiba huo ulivyokuwa kigezo cha kubadili uelekeo wa maisha yake.

Witness anakumbuka mara kadhaa Jirani yao ambaye alikuwa fundi seremali alipenda kumtuma kupeleka bidhaa kwa wateja au kumsaidia kufanya shughuli ndogo ndogo zinazohusu ufundi huo.

Huo ulikuwa mwanzo wa Witness kujifunza na kupenda kazi hiyo ya ufundi seremala.

Anasemam waka 2023 akiwa mwanafunzi wa Chuo cha diplomasia ndipo alipojaribisha ujuzi wake huo kwa kuchukua kazi za kuwatengenezea vitanda baadhi ya marafiki tu ambao yeye anasema "aliwamudu".

Ingetokea nimeharibu kazi ya rafiki yangu ningeweza kujitetea au kumrejeshea pesa yake kwa sababu ninawafahamu.Lakini nilifanya kazi nzuri na tangu hapo nikapata nguvu ya kuendelea na kazi hiyo.

'Kazi ni kazi ilimradi tu iwe halali'

"Kazi ni kazi ilimradi tu iwe halali," anasisitiza kwa kujiamini. "Sivunji sheria za nchi, sikosei wazazi wangu wala Mungu wangu. Ninafanya kazi hii kwa amani kabisa na moyo mweupe bila kuchagua wala kuona aibu."

Kuhusu kumalizia masomo yangu ya diplomasia nitarejea bila kuacha.

Ninatamani sana kuwa mwanadiplomasia fundi seremala.

Inathibitisha kuwa mtu anaweza kuwa msomi, lakini bado akang'ara na kupiga hatua kubwa katika fani nyingine ya mikono.

Japo haikuwa rahisi kwake kukubalika na jamii alipojitosa kwenye sekta hii inayotawaliwa zaidi na wanaume, jitihada zake za makusudi na kujiamini vimeendelea kumfanya aonekane, kuheshimika, na kuwa mfano wa kuigwa na wasichana wenzake.

Wasichana wengi mtandaoni hunitafuta na kuniambia niwafundishe au kuniuliza nilianzaje?

Nitapenda siku moja kuwa na kampuni kubwa itakayoajiri vijana zaidi katika fani hii y aufundi seremala.

Ninatumia mitandao ya kijamii kutafuta kazi kwenye mahoteli ya kitalii au hata ofisi na watu binafsi.

Hivi sasa, Witness ndiye mmiliki na mbunifu mkuu wa karakana ya Home of Best Pallets iliyopo jijini Dar es Salaam.

Kupitia karakana hiyo, anabuni na kutengeneza samani mbalimbali za kisasa, kazi inayozidi kuwavutia wateja na kuonyesha picha mpya ya ujasiriamali kwa vijana.

Aidha hivi leo Witness anajivunia kuweza kumudu gharama za maisha na kukidhi mahitaji yake binafsi bila kumtegemea mtu yeyote, yote haya yakitokana na jasho la mikono yake katika ufundi seremala.

Kwake yeye, mtazamo wa jamii kuhusu aina ya kazi haujawahi kuwa kikwazo cha kufikia malengo yake.