Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nchimbi kujiuzulu: Nini kinafuata?
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt Emmanuel John Nchimbi, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo na kustaafu siasa pamoja na utumishi wa umma, katika uamuzi utakaobadilisha muundo wa uongozi wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Nchimbi ametangaza kwamba kujiuzulu kwake kutaanza rasmi Septemba 4, 2026. Katika taarifa iliyochapishwa leo kwenye akaunti yake rasmi ya Instagram, amesema amemwandikia Rais Samia kumjulisha uamuzi huo na ametumia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama msingi wa uamuzi wake.
Lakini tofauti na kujiuzulu kwa waziri au kiongozi mwingine wa Serikali, kuondoka kwa Makamu wa Rais kunafungua mchakato maalumu wa kikatiba wa kujaza nafasi hiyo.
Kwa hiyo, baada ya Nchimbi kuondoka, kinachofuata si uchaguzi mwingine wa kitaifa. Ni Rais kumteua Makamu wa Rais mpya na Bunge kuthibitisha uteuzi huo.
Sasa mchakato huo utafanyikaje, na utachukua muda gani?
Rais ana siku 14 kumteua Makamu wa Rais mpya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweka utaratibu maalumu pale nafasi ya Makamu wa Rais inapokuwa wazi.
Ibara ya 50(4) inaeleza kwamba endapo nafasi hiyo itakuwa wazi, Rais atamteua mtu mwingine kuwa Makamu wa Rais ndani ya siku 14 tangu nafasi hiyo kuwa wazi. Uteuzi huo lazima uthibitishwe na Bunge kwa kura ya wabunge walio wengi.
Hii ina maana kwamba baada ya Nchimbi kuacha rasmi nafasi hiyo Septemba 4, Rais Samia atakuwa na kipindi cha hadi siku 14 kumteua mtu atakayechukua nafasi yake.
Baada ya uteuzi huo, Bunge litapiga kura kuamua kama linathibitisha uteuzi huo.
Iwapo atathibitishwa, Makamu wa Rais mpya ataapa na kuanza rasmi majukumu yake. Katiba inaeleza kwamba Makamu wa Rais aliyeteuliwa kwa utaratibu huu ataingia madarakani baada ya uteuzi wake kuthibitishwa na Bunge.
Kwa hiyo, nafasi hiyo haiwezi kujazwa na uteuzi wa Rais pekee; Bunge lina jukumu la kuthibitisha mtu anayependekezwa.
Nchimbi alikuwa Makamu wa Rais kwa muda gani?
Nchimbi alichaguliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia katika uchaguzi wa mwaka 2025 na akaanza rasmi kuwa Makamu wa Rais baada ya kuapishwa Novemba 3, 2025.
Alimrithi Dkt Philip Isdor Mpango, aliyekuwa Makamu wa Rais tangu mwaka 2021.
Kwa hiyo, kujiuzulu kwa Nchimbi Septemba 2026 kunamaliza kipindi chake cha chini ya mwaka mmoja katika nafasi hiyo.
Pia safari yake ya kisiasa huenda ikagota hapa kamac atasimamia msimamo ulioonekana kwenye taarifa, kwani taarifa imesema hatastaafu tu nafasi ya Makamu wa Rais bali pia anasitisha siasa na utumishi wa umma.
Hatua inayofuata sasa ni kusubiri Rais Samia kutumia hadi siku 14 kumteua Makamu wa Rais mwingine.
Kisha jina hilo litapelekwa Bungeni kwa ajili ya uthibitisho.
Hii ina maana kwamba ndani ya kipindi kifupi Tanzania itakuwa na Makamu wa Rais mpya, ambaye atakuwa sehemu ya uongozi wa Serikali kwa kipindi kilichobaki cha muhula wa sasa.
Kwa sasa, hakuna jina lililotangazwa rasmi kuwa mrithi wa Nchimbi.
Na baada ya kujiuzulu kwa Nchimbi, macho sasa yanaelekezwa Ikulu: Rais Samia atamteua nani, na mabadiliko hayo yataashiria nini kwa Serikali yake katika kipindi kinachofuata?