Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, unapaswa kuosha kuku mbichi?
- Author, Esther Kahombi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Je, huwa unaosha kuku kabla ya kumpika?
Hili ni swali ambalo limekuwa likizua mjadala mkali kwa miaka mingi miongoni mwa familia, kwenye mitandao ya kijamii, na miongoni mwa marafiki.
Miongozo rasmi ya usalama wa chakula katika nchi za Magharibi iko wazi kuhusu jambo hili: usioshe kuku mbichi kwani kufanya hivyo kunaweza kusambaza bakteria hatari.
Hata hivyo, wapishi wengi duniani hufanya hivyo, na ni desturi ya muda mrefu inayohusishwa na dhana ya usafi na umakini.
Baadhi ya wapishi, kama vile April Jackson, mpishi wa televisheni na mwandishi—hufurahia kujadili mada hii mtandaoni.
"Hasa huwa naweka video fupi nikiosha kuku kwa sababu najua ni mada inayozua mjadala mkali. Watu husema sipaswi kuosha kuku kwenye sinki au bakuli, na wengine husema ni jambo la kuchukiza na linalosababisha uchafuzi," anasema.
Lakini kundi jingine linaamini kuwa kula kuku ambaye hajaiva vizuri ni jambo lisilo la usafi.
Fadwi Halili, mtayarishaji wa maudhui na mpiga video wa TikTok anayeshiriki mbinu ya hatua 10 ya mama yake wa Kioroko ya kuosha kuku, anasema anafurahia kusoma maoni ya watu kwenye mitandao ya kijamii kuhusu suala hilo.
"Kila mtu anasema, 'Kumbe ndiyo maana huli nyumbani kwa watu wengine au kwenye meza ya chakula kazini,'" anasema.
Kutokuwa na uhakika iwapo kuku huoshwa ni jambo la kawaida katika kaya nyingi barani Asia, Karibiani, Amerika Kusini, Afrika, na baadhi ya tamaduni za eneo la Mediterania.
Sayansi inasemaje? BBC ilitembelea maabara ya chakula ili kufahamu.
Kwa nini ni hatari kuosha kuku mbichi?
Kuku mbichi huwa na bakteria aina ya Campylobacter na Salmonella, ambao husababisha sumu mwilini kutokana na chakula.
"Unapoosha kuku mbichi jikoni, matone yenye vijidudu hatari husambaa huku na huko," anasema Dkt. Kimon Andreas Karatzas, profesa wa mikrobiolojia ya chakula katika Chuo Kikuu cha Reading nchini Uingereza.
Matone haya yanaweza kusambaza bakteria wasioonekana kwa wingi hadi kwenye sinki, jikoni, au hata kwenye vyakula vingine vilivyo karibu.
Ili kudhihirisha hili, Dkt. Karatzas alifanya jaribio kwa kupaka kemikali kwenye kuku mbichi iliyowezesha bakteria kuonekana chini ya mwanga wa 'ultraviolet'. Kisha aliweka kuku huyo chini ya maji yanayotiririka kwa muda usiozidi sekunde kumi, na kuruhusu maji kuruka juu ya kuku na kuzunguka sinki.
Kwa macho ya kawaida, yalionekana kuwa matone ya maji tu ambayo yanaweza kufutika, lakini mwanga wa 'ultraviolet' ulifichua kuwepo kwa uchafuzi (kuhamia kwa vijidudu kutoka kitu kimoja kwenda kingine).
Matone yenye bakteria yalikuwa yametapakaa kwenye kabati, kwenye koti la maabara la profesa, kwenye kamera, na pia kwenye majani ya saladi na karoti ambazo huliwa zikiwa mbichi.
Hii ina maana kwamba hata ukimpika kuku huyo, bado unaweza kuugua kutokana na vyakula vingine kugusana na maeneo yaliochafuliwa.
"Hii ndiyo sababu kuu ya sisi kuugua kutokana na bakteria wa Salmonella na Campylobacter; chakula unachokula kibichi huchafuliwa kupitia maambukizi kutoka kwa vijidudu vilivyopo kwenye chakula unachopika," anasema Dkt. Karatzas.
Kwa nini Campylobacter ni hatari sana?
Shirika la Afya Duniani linasema: "Campylobacter ni mojawapo ya visababishi vinne vikuu vya magonjwa ya kuhara duniani kote na ndiyo bakteria wanaoongoza kusababisha ugonjwa wa kuvimba kwa utumbo na tumbo (gastroenteritis), hali inayosababisha kuhara na kutapika, hasa kwa watoto wadogo."
Bakteria hawa ni hatari zaidi kuliko Salmonella kwa sababu kiwango cha Salmonella katika kuku kimepungua kutokana na programu za chanjo, lakini hakuna chanjo dhidi ya Campylobacter.
Aina zote mbili za bakteria huishi kiasili ndani ya utumbo wa kuku. Wakati wa mchakato wa kuchinja na kuandaa nyama, yaliyomo tumboni mwa kuku yanaweza kuchafua nyama hiyo.
"Unapaswa kuchukulia kuku kana kwamba wana bakteria wa Salmonella au Campylobacter wakati wote," anasema Dkt. Karatzas.
"Kuku wengi duniani hufugwa nje. Hawafugwi katika mazingira yenye udhibiti mkali, na matokeo yake, hubeba bakteria wa Salmonella na Campylobacter."
Kiasi cha Campylobacter kinachohitajika kusababisha ugonjwa ni kidogo sana; tone moja tu linaweza kuwa na trilioni 10 za Campylobacter, idadi ambayo ni kubwa mara elfu moja kuliko idadi ya wanadamu duniani.
"Kama tone dogo tu la Campylobacter au mchuzi wa kuku litagusa kitu chochote, linatosha kukufanya uwe mgonjwa sana," anasema Dkt. Karatzas.
راحتی بیمار کند».
Je, ni zipi dalili za maambukizi na ugonjwa?
Shirika la Viwango vya Chakula la serikali linasema kuwa nchini Uingereza pekee, zaidi ya watu 250,000 huugua kutokana na bakteria hawa kila mwaka.
Dalili za ugonjwa huu kwa kawaida hujitokeza siku mbili hadi tano baada ya maambukizi, na dalili kuu ni kuharisha mara nyingi kukifuatana na damu, pamoja na maumivu ya tumbo, homa, maumivu ya kichwa, usumbufu wa tumbo, na kichefuchefu.
Watu wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na watoto wako katika hatari kubwa zaidi ya kuugua vibaya, na baadhi ya watu hupata dalili kali na za muda mrefu zinazohitaji matumizi ya dawa za antibiotiki.
Wakati mwingine, ugonjwa huu husababisha matatizo mengine ya kiafya, kama vile ugonjwa wa utumbo wenye msukosuko (irritable bowel syndrome), baridi yabisi (arthritis), na katika hali nadra aina ya kupooza kwa muda inayojulikana kama ugonjwa wa Guillain-Barré.
Hata hivyo, watu wengi hawaunganishi magonjwa ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula na utayarishaji wa nyama ya kuku. Wataalamu wanasema maambukizi mengi hayagunduliki, na takwimu hujumuisha tu visa ambapo mtu ameugua kiasi cha kwenda kwa daktari na kupimwa sampuli.
"Tunachokiona ni sehemu ndogo tu ya tatizo, na idadi halisi ya visa ni kubwa mara kumi zaidi," anasema Dkt. Karatzas.
.
Kwa nini watu bado wanaosha nyama ya kuku?
Mwaka 2024, utafiti uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Food Control ulibaini kuwa asilimia 96 ya washiriki katika nchi nane za Kusini-Mashariki mwa Asia huosha nyama ya kuku. Katika muongo uliopita, tafiti nchini Marekani, Ulaya, na Australia zilionyesha kuwa kati ya asilimia 70 na 39 ya watumiaji walisema hufanya hivyo.
Katika nchi nyingi za Magharibi, nyama ya kuku huzalishwa chini ya kanuni na udhibiti mkali na huuzwa ikiwa tayari imesafishwa kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, katika maeneo mengi, kuku bado huchinjwa ndani ya jamii husika, wakati mwingine katika masoko ya wazi, karibu na maji yanayotiririka, na kwenye maeneo yenye viwango tofauti vya usafi.
Katika mazingira kama hayo, kuosha nyama ya kuku huonekana kuwa jambo la lazima.
Hata hivyo, baadhi ya watu hawafanyi hivyo kwa ajili ya usafi, bali kama sehemu ya utambulisho na mtindo wa maisha waliokulia nao, pamoja na njia ya kudumisha uhusiano na maeneo yao ya asili.
Mpishi Jackson alipokwenda Uingereza na kuona kwenye kifungashio ushauri wa kutokuosha kuku mbichi, alishangaa sana kiasi cha kupiga picha na kuituma kwa familia yake huko Jamaica.
Anasema anaelewa sababu za kisayansi, lakini anaeleza: "Tunapoosha kuku, tunaona maji yakibadilika rangi na kuwa na mawingu, na hatutaki kunywa maji machafu na yenye mawingu ya namna hiyo."
Wengi wanahoji kuwa jambo la msingi ni namna kuku anavyooshwa. Wapishi wote wawili waliambia BBC kuwa wao huosha kuku kwenye bakuli, mara nyingi wakitumia siki au maji ya limau, na kisha husafisha na kuua vijidudu katika eneo hilo.
"Mama yangu husafisha vizuri sinki kwa sabuni na maji na kisha kulinyunyizia dawa ya kuua bakteria," anasema Bi. Halili.
Wale wanaosisitiza sana kuoshwa kwa kuku wanasema kuwa ushauri wa jumla wa kutokuosha kuku ni ishara ya kutokwenda sambamba kwa mambo katika miongozo ya usalama wa chakula.
"Kwa mfano, ukiosha ubao wa jikoni na kukatia kuku juu yake, bado kunaweza kuwa na hatari sawa ya maambukizi," anasema Jackson.
Anaendelea kusema: "Katika mapishi ya Kifaransa, kuku huwekwa kwenye maji yenye chumvi kabla ya kupikwa, na hakuna anayesema kuwa hilo ni jambo lisilo la usafi, lakini njia hiyo haina tofauti na kuosha kuku."
Dkt. Karatzas anakubali kuwa kuosha kuku kwenye bakuli ni salama zaidi, lakini anasema kuwa njia hii pia ina hatari zake na kwamba kuosha kwa kutumia maji ya limau na siki hakupunguzi viwango vya bakteria kwa uhakika.
"Njia pekee ya kuua bakteria ni kupika kuku, na mara nyingi kuku anayeandaliwa huwa tayari ameshashwa, hivyo hakuna sababu ya kufanya hivyo tena," anasema.