Majaribio ya dawa ya kuzuia Ebola yaanza DR Congo na Uganda

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza kuanza kwa majaribio ya kwanza ya kitabibu ya dawa ya kuzuia Ebola kwa watu waliokaribiana na walioambukizwa virusi hivyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda.
Majaribio hayo, yanayojulikana kama EBO PEP, yanalenga kutathmini uwezo wa dawa ya obeldesivir kuzuia maambukizi ya aina ya Bundibugyo Ebola kwa watu waliowahi kukutana na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo.
Dawa hiyo ya majaribio, inayotengenezwa na kampuni ya Marekani ya Gilead Sciences na kutumiwa kwa njia ya kumeza, imeonyesha matokeo ya kutia matumaini katika tafiti za awali.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuanza kwa majaribio hayo ni hatua muhimu katika juhudi za kukabiliana na Ebola.
"Kila mafanikio huanza na matumaini. Ikiwa dawa hii itathibitika kuwa na ufanisi kwa watu walio katika hatari kubwa baada ya kuathiriwa, inaweza kuwa hatua kubwa mbele katika kuzuia maambukizi ya Ebola," alisema Tedros.
WHO imesema iwapo dawa hiyo itafanikiwa, inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuwalinda wahudumu wa afya, wanafamilia na jamii wakati wa milipuko ya Ebola.






