Waziri Mkuu wa Israel
Benjamin Netanyahu amelaani mashambulizi yaliyofanywa na walowezi wa Israel
dhidi ya vijiji vya Wapalestina vya Qusra na Jalud katika Ukingo wa Magharibi
unaokaliwa kwa mabavu.katika
tukio la hivi punde la mivutano ambayo imedumu kwa karibu wiki tatu.
Katika hatua
isiyo ya kawaida, Netanyahu alilaani kile alichokiita "vitendo vya uhalifu
na vurugu" vilivyofanyika katika vijiji viwili vya Wapalestina siku ya
Jumamosi. Aliwataja walowezi hao kama "kundi dogo la wahuni wasioheshimu
sheria."
Katika taarifa,
alisema, "Ninelaani vikali vitendo vya uhalifu na vurugu vilivyofanywa
katika vijiji vya Qusra na Jalud na wahuni wachache wasioheshimu sheria; watu
ambao wanaitendea dhuluma kubwa jamii ya Wayahudi wanaoheshimu sheria, wanazuia
kazi ya jeshi la Israel katika kutekeleza majukumu yake, na kuharibu taswira ya
Israel katika nyanja ya kimataifa."
Rais wa Israel
Isaac Herzog alilaani vurugu hizo, akizielezea kama "uvukaji wa mstari
mwekundu uliofanywa na watu wanaokiuka sheria, ambao wanatenda kinyume kabisa
na sheria na maadili ya Taifa la Israel," na kusema kuwa kilichotokea ni
"doa kwa sifa ya Israel."
Wakazi wa Qusra na
jeshi la Israel walisema kuwa makumi ya walowezi walivamia kijiji hicho,
wakawarushia mawe wakazi na kuwalazimisha baadhi yao kujifungia majumbani mwao.
Ripoti zaidi zinasema
walowezi wa Israel waliovaa barakoa waliwashambulia na kuwajeruhi wafanyakazi
wa NBC News pamoja na mwanamke Mpalestina katika kijiji cha Jalud, karibu na
Qusra, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Wakati huo huo, raia
mmoja Mpalestina mwenye uraia wa Marekani alikuwa akielekea Qusra akisema
anataka kufika kwa familia yake iliyokuwa imezingirwa na walowezi.
Jeshi la Israel
limesema lilituma wanajeshi na polisi wa mpakani eneo hilo baada ya kupokea
taarifa za makabiliano kati ya waandamanaji wa Israel na Wapalestina,
yaliyojumuisha kurushiana mawe.