Netanyahu alaani vurugu za walowezi Ukingo wa Magharibi

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelaani mashambulizi yaliyofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya vijiji vya Wapalestina vya Qusra na Jalud katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.katika tukio la hivi punde la mivutano ambayo imedumu kwa karibu wiki tatu.
Katika hatua isiyo ya kawaida, Netanyahu alilaani kile alichokiita "vitendo vya uhalifu na vurugu" vilivyofanyika katika vijiji viwili vya Wapalestina siku ya Jumamosi. Aliwataja walowezi hao kama "kundi dogo la wahuni wasioheshimu sheria."
Katika taarifa, alisema, "Ninelaani vikali vitendo vya uhalifu na vurugu vilivyofanywa katika vijiji vya Qusra na Jalud na wahuni wachache wasioheshimu sheria; watu ambao wanaitendea dhuluma kubwa jamii ya Wayahudi wanaoheshimu sheria, wanazuia kazi ya jeshi la Israel katika kutekeleza majukumu yake, na kuharibu taswira ya Israel katika nyanja ya kimataifa."
Rais wa Israel Isaac Herzog alilaani vurugu hizo, akizielezea kama "uvukaji wa mstari mwekundu uliofanywa na watu wanaokiuka sheria, ambao wanatenda kinyume kabisa na sheria na maadili ya Taifa la Israel," na kusema kuwa kilichotokea ni "doa kwa sifa ya Israel."
Wakazi wa Qusra na jeshi la Israel walisema kuwa makumi ya walowezi walivamia kijiji hicho, wakawarushia mawe wakazi na kuwalazimisha baadhi yao kujifungia majumbani mwao.
Ripoti zaidi zinasema walowezi wa Israel waliovaa barakoa waliwashambulia na kuwajeruhi wafanyakazi wa NBC News pamoja na mwanamke Mpalestina katika kijiji cha Jalud, karibu na Qusra, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Wakati huo huo, raia mmoja Mpalestina mwenye uraia wa Marekani alikuwa akielekea Qusra akisema anataka kufika kwa familia yake iliyokuwa imezingirwa na walowezi.
Jeshi la Israel limesema lilituma wanajeshi na polisi wa mpakani eneo hilo baada ya kupokea taarifa za makabiliano kati ya waandamanaji wa Israel na Wapalestina, yaliyojumuisha kurushiana mawe.
Soma pia:






















