Sudan Kusini yapanga uchaguzi Desemba huku hofu ya vita kurejea ikiongezeka

Chanzo cha picha, BBC Monitoring
Baada ya miaka ya ucheleweshaji, Sudan Kusini inatarajiwa kufanya uchaguzi mwezi Desemba mwaka huu, licha ya nchi hiyo kuwa katika hatari ya kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wataalamu wanaonya uwezekano wa kurejea kwa vita kamili huku majeshi ya serikali chini ya Rais Salva Kiir yakipambana na makundi yanayohusishwa kwa kiwango fulani na Makamu wa Rais Riek Machar.
Ghasia hizo zimelazimisha makumi ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao, huku mashirika ya misaada yakishambuliwa mara kwa mara na kushindwa kutekeleza shughuli zake ipasavyo.
Waziri wa Habari Ateny Wek Ateny aliwaambia waandishi wa habari mjini Juba kuwa serikali inafanya jitihada za kukusanya fedha kutoka mapato ya mafuta na yasiyo ya mafuta ili kufadhili uchaguzi huo.
“Serikali ina fedha kwa sababu mafuta bado yanazalishwa, ingawa kuna changamoto,” akiongeza kuwa “mapato yasiyo ya mafuta yapo,” na kwamba uchaguzi utafadhiliwa na serikali, asema Ateny Wek Ateny.
Makubaliano ya amani ya mwaka 2018 yalimaliza vita vya mwisho kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wake Riek Machar.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, uchaguzi ulipaswa kufanyika mwaka 2022 lakini uliahirishwa mara kadhaa.
Hata hivyo, Waziri wa Habari amesisitiza kuwa uchaguzi lazima ufanyike mwaka huu.
Iwapo uchaguzi utafanyika, huo utakuwa uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka Sudan miaka 15 iliyopita.
Hata hivyo, baadhi ya masharti ya makubaliano ya amani bado hayajatekelezwa, ikiwemo kuunganishwa kwa majeshi hasimu, huku nchi hiyo pia ikikabiliwa na changamoto kubwa za rushwa na umaskini.
Soma zaidi:










