Vita vya Iran na usitishaji mapigano - tulifikaje hapa?
Huu ni muhtasari wa jinsi usitishaji mapigano mawili katika nyanja tofauti za mgogoro wa Mashariki ya Kati ulivyofikiwa
Marekani na Iran
Tarehe 8 Aprili: Pakistan kama mpatanishi ilitangaza usitishaji mapigano wa muda wa wiki mbili kati ya Marekani na Iran, uliopangwa kumalizika tarehe 22 Aprili.
Trump alisema makubaliano hayo yalifikiwa kwa sharti la kufunguliwa tena kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz. Pakistan ilisema Lebanon pia ilihusishwa, jambo ambalo Iran ilikubali lakini Marekani na Israel walipinga.
Tarehe 11 Aprili: Maafisa wakuu wa Marekani na Iran, akiwemo Makamu wa Rais JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, wanakutana Pakistan. Baada ya mazungumzo ya saa 21, Washington na Tehran bado walikuwa mbali kuhusu masuala muhimu.
Tarehe 12 Aprili: Trump anatangaza mzingiro wa usafirishaji wa meli za Iran huku Iran ikiendeleza mzingiro wake wa Hormuz baada ya mazungumzo ya Islamabad kushindwa.
Tarehe 21 Aprili: Trump anakubali kuongeza muda wa usitishaji mapigano bila muda maalum ili mazungumzo yaendelee.
Israel na Lebanon
Tarehe 14 Aprili: Lebanon na Israel wanafanya mazungumzo ya kidiplomasia kwa mara ya kwanza tangu 1993, yakilenga kumaliza mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, linalofanya kazi kusini mwa Lebanon.
Tarehe 16 Aprili: Marekani inatangaza usitishaji mapigano wa siku 10 kati ya Israel na Lebanon, uliopangwa kumalizika tarehe 26 Aprili.
Trump alitoa wito kwa Hezbollah kuzingatia makubaliano hayo, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisema wanajeshi wataendelea kuwepo kilomita 10 ndani ya kusini mwa Lebanon licha ya usitishaji mapigano.
Soma zaidi: