Trump aagiza Ziwa Ontario kuitwa Ziwa Amerika
Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo la kiutendaji linalolenga kubadili jina la Ziwa Ontario na kuliita Ziwa Amerika.
Hatua hiyo inakuja baada ya mazungumzo ya kibiashara kati ya Marekani na Canada kuvunjika wiki iliyopita, huku Marekani ikiweka ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa za Canada zenye thamani ya dola bilioni 20.
Trump amekuwa akitishia mara kadhaa kubadili jina la ziwa hilo, ambalo ni miongoni mwa maziwa makuu matano yanayopatikana katika eneo la Marekani na Canada.
Kwa mujibu wa agizo hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Marekani imepewa siku 30 kusasisha jina hilo katika hifadhidata rasmi ya majina ya maeneo ya kijiografia nchini humo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, amepinga hatua hiyo, akisema jina Ziwa Ontario lina historia ya zaidi ya miaka 400.
Carney amesema ziwa hilo linaitwa Ontario na litaendelea kuitwa hivyo.
Hii si mara ya kwanza kwa Trump kujaribu kubadili jina la eneo linaloshirikisha nchi nyingine. Mwaka 2025, alisaini agizo la kubadili jina la Ghuba ya Mexico kuwa Ghuba ya America, hatua ambayo Mexico imeikataa.
Pia unaweza kusoma: