Trump: Iran imechelewa kufikia makubaliano, sasa italipa gharama
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran imechelewa mno kufikia makubaliano na Marekani na sasa italazimika “kulipa gharama” ya kuchelewa huko.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social Jumatano, Trump amesema Iran imepata pigo kubwa na kwamba imebaki kutoa matamshi pekee bila kuchukua hatua za maana.
"Mnyanyasaji wa Mashariki ya Kati sasa ameshindwa," alisema Trump.
Aliongeza kuwa Iran ilichelewesha kwa muda mrefu kufikia makubaliano ambayo, kwa mujibu wake, yangekuwa na manufaa makubwa kwa taifa hilo.
"Walichelewa mno kufikia makubaliano ambayo yangekuwa bora kwao. Sasa watalazimika kulipa gharama yake," alisema.
Kauli hiyo imekuja huku mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea kuongezeka tangu Jumatano asubuhi, ambapo pande zote mbili zimedai kufanya mashambulizi dhidi ya malengo ya upande mwingine.
Mapema leo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani Mashariki ya Kati (CENTCOM) ilisema vikosi vyake vilichukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran kujibu kuangushwa kwa helikopta ya kijeshi ya Marekani.
"Operesheni hii ni jibu kwa uchokozi wa Iran ambao haukuchochewa," ilisema CENTCOM katika taarifa yake.
Kwa upande wake, Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran walidai kuwa Marekani ilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo kadhaa ya Jask, Sark na Qeshm, yaliyosababisha kuharibiwa kwa mnara wa mawasiliano na matangi mawili ya maji ya matumizi ya raia.
Katika taarifa yao, Walinzi hao walidai kuwa walijibu kwa kushambulia malengo manne muhimu ya kijeshi ya Marekani kwa kutumia makombora ya masafa marefu.
Shirika la habari la Iran, IRNA, lilinukuu Walinzi wa Mapinduzi wakisema kuwa malengo hayo yalijumuisha maghala ya ndege za kivita aina ya F 35 na kituo cha amri na udhibiti wa jeshi la Marekani katika eneo la Al Azraq nchini Jordan.
Picha za video zilizosambazwa na IRNA zilionyesha makombora ya masafa marefu ya Qadr, Emad na Khyber Shakan yakifyatuliwa kuelekea malengo ya Marekani katika eneo hilo. Hata hivyo, BBC haijaweza kuthibitisha kwa njia huru uhalisi wa picha hizo.
Awali, Trump alikuwa ameishutumu Iran kwa kuangusha helikopta ya kijeshi ya Marekani aina ya Apache.
Kwa mujibu wa CENTCOM, wanajeshi wawili waliokuwa ndani ya helikopta hiyo waliokolewa na ndege isiyo na rubani ya jeshi la majini la Marekani.
Unaweza kusoma;