Iran yasema haina makubaliano rasmi ya kusitisha mapigano na Marekani

Vahid Ahmadi, mjumbe wa Kamati ya Usalama wa Taifa ya Bunge, amesema kuwa 'Wamarekani hawakufanikiwa kufikia malengo waliyojiwekea katika vita hivyo, sasa wanatushinikiza kiuchumi'.

Muhtasari

Skip Video and continue reading
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Usiku mwema

  2. Pentagon yaripoti wasiwasi kuhusu madai ya Israel kuwapeleleza maafisa wa Marekani

    G

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa Pentagon imepandisha kiwango cha tahadhari dhidi ya vitisho vya ujasusi vinavyohusishwa na Israel hadi kiwango cha juu zaidi kutokana na wasiwasi kuhusu shughuli za upelelezi.

    Shirika la NBC News, likinukuu maafisa wa Marekani, liliripoti kuwa Wakala wa Ujasusi wa Ulinzi wa Pentagon umeonya kwamba uwezo wa Israel wa "kuendesha ujasusi wa kibinadamu na kukusanya taarifa za kijasusi kwa kutumia teknolojia" umefikia kiwango cha "hatari sana".

    Kwa mujibu wa NBC News, hatua hiyo ya kuongeza kiwango cha tahadhari imekuja wakati kukiwa na wasiwasi kuhusu juhudi za Israel za kuwapeleleza maafisa wa Marekani ili kupata taarifa kuhusu "uchunguzi wa ndani na maamuzi ya utawala wa Trump kuhusu migogoro ya Mashariki ya Kati".

    Wakati huo huo, gazeti la New York Times limesema kuwa mashirika ya ujasusi ya Marekani yameeleza wasiwasi katika ripoti zao za hivi karibuni kuhusu madai ya Israel kusikiliza mawasiliano ya maafisa wa Marekani, akiwemo Steve Whitaker, mwakilishi mkuu wa Rais Donald Trump katika mazungumzo na Iran.

    Gazeti hilo lilisema ripoti yake imetegemea maafisa kadhaa wa sasa na wa zamani wa Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina yao kutokana na unyeti wa suala hilo.

    Soma zaidi:

  3. Umati mkubwa wajaa mitaa ya Madrid kuhudhuria misa ya wazi ya Papa

    h

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Zaidi ya watu milioni moja walijitokeza kwenye mitaa ya Madrid, Hispania, siku ya Jumapili kumshuhudia Papa Leo XIV akiongoza misa ya wazi, kwa mujibu wa waandaaji wa tukio hilo.

    Papa aliwasalimia waumini akiwa kwenye gari lake maalumu (popemobile) katika siku ya pili ya ziara yake rasmi nchini humo.

    Miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo walikuwa Mfalme Felipe VI na Malkia Letizia.

    Waumini walipeperusha bendera za Hispania na Vatican huku wakipaza sauti za "Papa aishi milele", wakati wengine wakirusha maua alipowasili katika uwanja wa Plaza de Cibeles.

    Katika mahubiri yake, Papa aliwahimiza waumini kuonesha imani yao kwa kuwasaidia wahitaji, akisema Mungu hujitambulisha kwa maskini, waliodhulumiwa na waliotelekezwa.

    Aliongeza kuwa dini haipaswi kuonekana kama kumbukumbu ya zamani bali shule ya imani inayotoa mwongozo hata kwa maisha ya leo.

    Mamlaka ziliweka ulinzi mkali kwa ajili ya misa hiyo na maandamano yaliyofuata katikati ya jiji, huku mitaa ikipambwa kwa mabango yenye picha ya Papa na maelfu ya maua meupe na ya njano yanayoakisi rangi za bendera ya Vatican.

    Soma zaidi:

  4. Msako wa washukiwa wa shambulio lililoua watu 12 Ohio waendelea

    g

    Chanzo cha picha, WTOL

    Polisi nchini Marekani wanasema wanaendelea kuwatafuta washukiwa baada ya watu wasiopungua 12 kupigwa risasi karibu na tamasha la Old West End Festival mjini Toledo, katika jimbo la Ohio huko Marekani.

    Idara ya Polisi ya Toledo imesema watu 10 wako katika hali nzuri, huku wawili wakiwa katika hali mahututi.

    Polisi walipokea taarifa ya tukio hilo majira ya saa kumi na moja jioni kwa saa za eneo hilo siku ya Jumamosi.

    Naibu Mkuu wa Polisi wa Toledo, Joe Heffernan, amesema inaonekana watu wawili walifyatua risasi na huenda walikuwa wakishambuliana.

    Video zilizosambazwa mtandaoni, ambazo bado hazijathibitishwa kwa uhuru, zinaonyesha watu wakikimbia na kupiga mayowe huku milio ya risasi ikisikika.

    Waliojeruhiwa wana umri kati ya miaka 16 mpaka 61.

    Meya wa Toledo, Wade Kapszukiewicz, amesema wote wanatarajiwa kupona. Shahidi mmoja, Tito Aguilar, amesema alikuwa akiagiza chakula aliposhuhudia kundi la vijana likimshambulia kijana mwingine kabla ya risasi kuanza kusikika.

  5. Marekani yazikosoa sera za uhamiaji za Ulaya, yasema fukwe zake zinakabiliwa na ‘uvamizi’

    g

    Chanzo cha picha, AFP

    Marekani imezikosoa nchi za Ulaya kuhusu sera za uhamiaji, akisema zimeruhusu kile alichokiita "uvamizi" katika eneo lao.

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth,alitoa kauli hiyo wakati wa hotuba ya kuadhimisha kumbukumbu ya D-Day nchini Ufaransa.

    Waziri huyo wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alikuwa akizungumza mjini Normandy na kurejelea kuwa miaka 82 baada ya vikosi vya washirika kutua kwenye fukwe za Ufaransa mwaka 1944 ili kuikomboa Ulaya kutoka chini ya utawala wa Wanazi.

    "Kwa bahati mbaya, leo fukwe tofauti za Ulaya zinakabiliwa na uvamizi wa itikadi tofauti na hatari," alisema Hegseth.

    "Fukwe za Hispania, Italia, Ugiriki na Bulgaria zinapokea boti na watu wanaowasili bila vibali. Ni lini miji mikuu ya Ulaya itachukua hatua dhidi ya uvamizi huo?"

    Suala la uhamiaji limekuwa mjadala mkubwa wa kisiasa barani Ulaya, huku vyama vinavyounga mkono sera kali za kudhibiti uhamiaji vikiongeza umaarufu katika kura za maoni.

    Utawala wa Rais Donald Trump unaona kukabiliana na uhamiaji haramu kuwa moja ya vipaumbele vyake vya sera za ndani, na umeomba mabilioni zaidi ya dola kufadhili taasisi za utekelezaji wa sheria za uhamiaji.

    Kauli za Hegseth zinaashiria mwendelezo wa ukosoaji wa sera za uhamiaji za Ulaya kutoka kwa viongozi waandamizi wa utawala wa Trump.

    Aidha, Siku ya D-Day ilikuwa operesheni kubwa zaidi ya kijeshi ya uvamizi kwa njia ya bahari kuwahi kufanyika, ikihusisha kutua kwa maelfu ya wanajeshi kutoka Uingereza, Marekani na Kanada kwa wakati mmoja kwenye fukwe tano tofauti za Normandy, kaskazini mwa Ufaransa.

    Soma zaidi:

  6. Iran yasema haina makubaliano rasmi ya kusitisha mapigano na Marekani

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vahid Ahmadi, mjumbe wa Kamati ya Usalama wa Taifa ya Bunge, amesema kuwa "kuna uwezekano wa kuzuka kwa vita vipya."

    Akizungumza na tovuti ya habari ya Fararoo, Ahmadi alisema: "Ukweli ni kwamba hatuna makubaliano rasmi ya kusitisha mapigano na Marekani. Kimsingi, tuko katika hali ya kusitisha mapigano kwa muda. Wamarekani hawakufanikiwa kufikia malengo waliyojiwekea katika vita hivyo, na sasa wamegeukia mzingiro wa baharini kwa matumaini ya kutushinikiza kiuchumi, jambo ambalo pia hawajafanikiwa kulitekeleza."

    Ahmadi aliongeza kuwa: "Kuna uwezekano wa kuzuka kwa vita vipya, na Iran ina uwezo mpya ambao inaweza kuutumia."

    Pia aliikosoa kwa miaka mingi nchi za Ghuba, akisema kuwa "zimekabidhi kila kitu kwa Marekani na zimekuwa zikiomba usalama kutoka kwake. Hata hivyo, vita vya karibuni vimeonyesha kuwa usalama hauwezi kupatikana kwa njia hiyo."

    Soma zaidi:

  7. Mwanafunzi wa kwanza kati ya 16 waliofariki katika moto wa shule ya Utumishi Academy azikwa leo

    h

    Chanzo cha picha, SOCIALS

    Mazishi ya Zuhura Rama, mwanafunzi wa kwanza miongoni mwa waathiriwa 16 wa moto wa shule ya Utumishi Academy nchini Kenya yamefanyika adhuhuri katika kijiji cha Mkwakwani, Wadi ya Ukunda, Kaunti ya Kwale.

    Hii ni baada ya mwili wake kutambuliwa na kukabidhiwa babake, Rama Higa, katika hifadhi ya maiti ya Naivasha baada ya mchakato wa utambuzi wa vinasaba vya DNA kukamilika.

    Baadaye mwili huo ulisafirishwa kwa ndege hadi kaunti ya Mombasa kwa ajili ya mazishi.

    Mamlaka ziliruhusu mwili huo kukabidhiwa mapema kwa kuzingatia taratibu za Kiislamu zinazotaka mazishi kufanyika haraka.

    “Tumemchukua binti yetu. Kwa utamaduni wetu, mazishi hufanyika haraka,” alisema Adam Ali, imam wa Naivasha.

    Kwa sauti ya uchungu, mama wa Zuhura alisema: “Ninaumia! Ninaumia! Nilitaka kuuona mwili huo hata kama usingetambulika vizuri, ili nijue kwamba nimemzika mwanangu.”

    Familia 15 zilizobaki zitaendelea kusubiri huku serikali ikikamilisha mipango ya ibada ya pamoja ya kuwaenzi waathiriwa kabla ya miili yao kuachiliwa kwa mazishi.

    Huzuni ulitanda katika hifadhi ya maiti ya Naivasha familia zilipokuwa zikipokea matokeo ya utambuzi wa DNA.

    Baadhi ya wazazi walishindwa kuyakubali matokeo hayo kutokana na hali mbaya ya miili iliyoteketea kwenye moto huo.

    “Kulikuwa na miili iliyoungua vibaya sana, lakini tuliweza kulinganisha sampuli zote na kuzitambua,” alisema Joseph Kimani, mtaalamu wa uchunguzi wa vinasaba katika Idara ya sayansi nchini humo.

    Wakati huo huo, kamati ya maandalizi ya mazishi inatarajiwa kutangaza tarehe mpya ya ibada ya pamoja ya kuwaaga marehemu baada ya familia zilizofiwa kukataa tarehe iliyopendekezwa awali.

    Serikali imetangaza msaada wa kifedha wa shilingi 200,000 (dola 1,546) kwa kila familia iliyopoteza mpendwa wake, pamoja na kugharamia ada za hifadhi ya maiti na gharama za mazishi za waathiriwa wote.

    Familia ya Faith Koskei, aliyefariki katika ajali ya barabarani alipokuwa akikimbilia shuleni baada ya kupata taarifa za moto huo, pia itanufaika na msaada huo.

    Mwili ukitayarishwa kabla ya kusafirishwa hadi Mombasa, Kenya

    Chanzo cha picha, Socials

    Maelezo ya picha, Mwili ukitayarishwa kabla ya kusafirishwa hadi Mombasa, Kenya

    Unaweza kusoma;

  8. Korea Kaskazini yasema mpango wake wa nyuklia hauko kwenye mazungumzo

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kim Yo-jong, dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, amesema katika taarifa kwamba mpango wa nyuklia wa nchi hiyo “hauwezi kujadiliwa kabisa”.

    “Taasisi yetu kuhusu nguvu za nyuklia haiwezi kujadiliwa kwa namna yoyote,” alisema katika taarifa hiyo iliyochapishwa na gazeti rasmi la chama tawala, Rodong Sinmun.

    Aliongeza pia kuwa Korea Kaskazini “haitavumilia vitisho vyovyote”.

    Kim Yo-jong, ambaye ni mmoja wa viongozi muhimu katika masuala ya mawasiliano na sera za nje za Korea Kaskazini, ameoa kauli hizo kabla ya ziara ya Rais wa China Xi Jinping nchini Korea Kaskazini, inayotarajiwa kuanza Jumatatu na kuendelea hadi Jumanne, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

    Ziara hiyo ya Xi Jinping mjini Pyongyang itakuwa ya kwanza katika kipindi cha miaka saba.

    Hii inakuja baada ya rais huyo wa China kufanya mfululizo wa mikutano na Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin mwezi uliopita.

    China inachukuliwa kuwa mmoja wa washirika muhimu zaidi wa kisiasa na kiuchumi wa Korea Kaskazini.

    Soma zaidi:

  9. Rais Tshisekedi amtunuku Fally Ipupa tuzo ya kitaifa kwa kuitangaza Congo kimataifa

    m

    Chanzo cha picha, PRESIDENCE RDC/X

    Rais Félix Tshisekedi amemtunuku mwanamuziki wa Congo Fally Ipupa nishani ya kitaifa kufuatia mafanikio yake ya kihistoria ya kufanya maonesho mawili mwezi Mei katika Stade de France jijini Paris.

    Fally Ipupa amekuwa msanii wa kwanza wa Afrika anayezungumza Kifaransa na kuishi barani Afrika kuwa msanii mkuu wa tamasha katika uwanja huo maarufu.

    Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Tshisekedi alisema heshima hiyo haitambui msanii pekee bali pia “safari yake, nidhamu, uthabiti, bidii, sauti yake, umahiri wa jukwaani na uwezo wa kipekee wa kubeba roho ya Wakongo kuvuka mipaka ya kijiografia.”

    “Kupitia muziki wako, sehemu ya Congo inasafiri, inavutia, inaunganisha watu na kuzungumza na ulimwengu,” alisema Rais Tshisekedi.

    Rais huyo pia amewapa heshima magwiji waliochangia kujenga hadhi ya muziki wa Congo kimataifa, akiwemo Papa Wemba, Jossart N’Yoka Longo, Koffi Olomide, Werrason, JB Mpiana na Ferré Gola, akisema kila mmoja ameendelea kuitangaza nchi kwa mtindo wake na hadhira yake.

    Alisisitiza kuwa tuzo hiyo “haiweki daraja kati ya vipaji tofauti wala haimfungii yeyote mlango. Kinyume chake, inafungua njia ya Jamhuri inayojua kuwaheshimu mabinti na wanawe wanapoitumikia taifa kwa ubora, umaarufu na uwezo wa kuhamasisha wengine.”

    Jumatano, amri ya rais ilisomwa kupitia televisheni ya taifa ikitangaza kupandishwa hadhi kwa Fally Ipupa katika Daraja la Taifa la Heshima, hatua iliyotekeleza ahadi iliyotolewa na mkuu huyo wa nchi wakati wa mkutano na waandishi wa habari tarehe 6 Mei 2026.

  10. Marekani yataka mali za Iran zitumike kufidia washirika wake wa Ghuba

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa Waziri wa Hazina wa nchi hiyo, Scott Bessent, anazingatia uwezekano wa kutumia mali za Iran zilizozuiwa kufidia uharibifu unaodaiwa kusababishwa na mashambulizi ya Iran dhidi ya mataifa ya Kiarabu katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

    Kwa mujibu wa ripoti hizo, ambazo bado hazijathibitishwa rasmi, Bessent pia ameagiza timu ya wataalamu kufanya tathmini ya gharama za ukarabati wa miundombinu na mali zilizoharibiwa katika mashambulizi hayo.

    Kwa upande wake, Iran inaitaka Marekani kuachilia zaidi ya dola bilioni 20 za mali zake zilizowekwa zuio.

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, ambaye pia ni mjumbe wa timu ya mazungumzo kati ya Tehran na Washington, amesema kuwa:

    "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa asilimia 50 ya mali zake zilizowekewa zuio zitolewe mara moja baada ya kutiwa saini kwa hati ya makubaliano."

    Pendekezo la kutumia mali za Iran zilizowekewa zuio kufidia uharibifu wa vita katika mataifa washirika wa Marekani linaonekana kufanana na mapendekezo yaliyowahi kutolewa ya kutumia mali za Urusi zilizozuiwa kugharamia ujenzi upya wa Ukraine kufuatia vita vya nchi hiyo na Urusi.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Tetesi za soka Ulaya: PSG yajiunga na Arsenal kumwinda Gibbs-White

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Arsenal F.C. huenda ikakumbana na ushindani mkali kutoka kwa Paris Saint-Germain katika harakati za kumsajili kiungo mshambuliaji wa Nottingham Forest F.C., Morgan Gibbs-White.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 yuko kwenye orodha ya Arsenal kama mbadala anayetarajiwa wa nyota wa Aston Villa F.C., Morgan Rogers, mwenye umri wa miaka 23.

    Hata hivyo, PSG pia inafuatilia kwa karibu hali yake.

    Wakati huo huo, inaelezwa kuwa winga wa Georgia wa PSG, Khvicha Kvaratskhelia, ndiye mchezaji ambaye rais wa Real Madrid C.F., Florentino Pérez, anapanga kumsajili iwapo atashinda uchaguzi wa urais wa klabu hiyo. (Teamtalk).

    Kocha mpya wa Real Madrid, José Mourinho, naye anaripotiwa kutaka huduma za kiungo wa Ureno Bernardo Silva baada ya nyota huyo kuondoka Manchester City F.C. mwishoni mwa msimu. (AS - in Spanish)

    Kwa upande mwingine, wakala wa Jürgen Klopp amesema Mjerumani huyo hana mpango wa kurejea kufundisha klabu yoyote kwa sasa, baada ya mgombea wa urais wa Real Madrid, Enrique Riquelme, kudai angejaribu kumshawishi kujiunga na klabu hiyo endapo angechaguliwa. (Sky sports-Germany)

    Tottenham Hotspur F.C. bado ina nia ya kumsajili winga wa Brazil Savinho. Inadaiwa mchezaji huyo mwenye miaka 22 yuko tayari kushinikiza uhamisho huo baada ya Manchester City kukataa ofa ya Spurs msimu uliopita. (Mirror).

    Mshambuliaji wa Italia Federico Chiesa amesema anahitaji kupata muda zaidi wa kucheza akiwa Liverpool na atazungumza na kocha mpya wa Reds, Andoni Iraola, kabla ya kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wake. (Gazzetta dello Sport - in Italian)

    Liverpool pia haina mpango wa kumuuza winga chipukizi wa England Rio Ngumoha mwenye miaka 17, licha ya taarifa kwamba FC Bayern Munich inamfuatilia kwa ajili ya usajili wa majira ya joto.(Sky Sports)

    Kwingineko, winga wa Newcastle United F.C., Harvey Barnes, ameibuka kulengwa kusajiliwa na Aston Villa. (Football Insider)

    Nazo Leeds United F.C. na Ipswich Town F.C. zinashindania saini ya kipa wa England Nick Pope kutoka Newcastle. (Sun)

    Aidha, kocha Russell Martin yuko katika mazungumzo ya hatua za mwisho na Leicester City F.C. huku akitafakari kurejea kwenye ukocha. (Telegraph - subscription required)

    Pia unaweza kusoma:

  12. Iran yadai maafisa wake wamezuiwa kuingia Marekani licha ya wachezaji kupewa visa vya Kombe la Dunia

    f

    Chanzo cha picha, TABNAK

    Iran imeishutumu Marekani kwa kuwanyima viza baadhi ya maafisa muhimu wa benchi la ufundi na uongozi wa timu yake ya taifa ya soka, saa chache baada ya Washington kuthibitisha kuwa wachezaji wa Iran wamepewa ruhusa ya kusafiri kushiriki Kombe la Dunia lijalo.

    Maafisa wa Marekani walisema Ijumaa kuwa viza zimetolewa kwa wachezaji wote pamoja na “wahudumu muhimu wa timu”, siku kumi kabla ya Iran kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya wapinzani wake mjini Los Angeles tarehe 15 Juni.

    Hata hivyo, maafisa hao waliongeza kuwa Iran haitaruhusiwa “kutumia vibaya mfumo huo kuwaingiza magaidi nchini Marekani kwa kisingizio cha ushiriki wa michezo”.

    Ubalozi wa Iran nchini Uturuki uliishutumu Marekani kwa kile ulichokiita “uingiliaji wa kisiasa wenye upendeleo katika michezo” baada ya kuwanyima viza sehemu kubwa ya viongozi wa timu, maafisa wa utawala na washauri wa kiufundi.

    Vyombo vya habari vinavyohusishwa na serikali ya Iran viliripoti kuwa maafisa 15 wa utawala, akiwemo rais wa shirikisho la soka la Iran, naibu wake na mkurugenzi wa habari, ni miongoni mwa waliozuiwa kuingia Marekani.

    Timu hiyo iliondoka katika kambi yake ya mazoezi nchini Uturuki siku ya Jumamosi kuelekea Mexico, ambako itakuwa imeweka makazi yake wakati wa mashindano hayo. Inatarajiwa kuwasili mapema Jumapili baada ya safari ya saa 20.

    Kwa mujibu wa masharti ya viza walivyopewa, wachezaji na maafisa watakaoruhusiwa kusafiri watalazimika kuingia na kuondoka Marekani siku hiyo hiyo ya mechi zao, kwa mujibu wa balozi wa Iran nchini Mexico.

    Katika taarifa yake, Iran ilielezea tangazo la Marekani kuwa ni “jaribio la kuficha ukweli”, ikisema: “Sasa mmefikisha kiwango cha juu kabisa cha matendo ya makusudi na ya kibaguzi dhidi ya timu ya taifa ya Iran.” Maafisa wa ubalozi wa Iran pia wameitaka FIFA kuingilia kati suala hilo.

    Kombe la Dunia la mwaka 2026, ambalo linaandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico, linatarajiwa kuanza tarehe 11 Juni.

    Iran ilifuzu mashindano hayo baada ya kumaliza kinara wa kundi lake la kufuzu mwezi Machi 2025, karibu mwaka mmoja kabla ya kuzuka kwa vita.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Kenya yaagiza waajiri kuwalipa wafanyakazi wa nyumbani angalau dola 140 kwa mwezi

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kanuni mpya za mishahara ya chini kwa wafanyakazi wa majumbani nchini Kenya zimeongeza kiwango cha chini cha mshahara wao wa kila mwezi hadi shilingi 18,047 za Kenya, sawa na takriban dola 140 za Marekani.

    Waajiri watakaokiuka masharti hayo wanakabiliwa na kifungo cha hadi miezi mitatu jela au faini ya shilingi 50,000 pesa za Kenya.

    Awali, wafanyakazi wa nyumbani walitakiwa kulipwa dola $123.69, mshahara ambayo baadhi yao wamelalamikia kuwa haujatekelezwa kikamilifu na waajiri wao.

    Marekebisho hayo yanafuatia uamuzi wa hivi karibuni wa serikali wa kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kwa asilimia 12, hatua inayolenga kuwasaidia wafanyakazi kukabiliana na ongezeko la gharama za maisha.

    Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, viwango hivyo vipya vinawahusu maelfu ya wafanyakazi wa majumbani, wakiwemo wasaidizi wa nyumbani, walezi wa watoto, watunza bustani na wafanyakazi wengine wa huduma za nyumbani kote nchini.

    Chini ya muundo huo mpya wa mishahara, wafanyakazi wa majumbani katika miji mikuu ikiwemo Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na Eldoret sasa wanastahili kulipwa angalau shilingi 18,047 kwa mwezi.

    Ongezeko hilo ni sehemu ya mageuzi mapana ya sekta ya ajira yanayolenga kuboresha ustawi wa wafanyakazi na kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi nchini Kenya.

    Hata hivyo, wakenya wameingia mitandaoni na kueleza kutoridhishwa kwao na agizo hilo mpya.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Papa Leo aipongeza Uhispania kwa kupinga vita vinavyoendelea mashariki ya kati

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Papa Leo XIV, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, ameipongeza Uhispania kwa kile alichokitaja kuwa ni “kujitoa kwake kwa amani na umoja miongoni mwa mataifa” wakati wa ziara rasmi nchini humo siku ya Jumamosi.

    Serikali ya Uhispania imekuwa ikipinga vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza, Iran na Ukraine katika miaka ya karibuni.

    “Ninatoa shukrani zangu za dhati kwa taifa lenu, ambalo daima limezingatia sheria za kimataifa na mfumo wa ushirikiano wa kimataifa wa pande nyingi. Msimamo huu unaonesha wazi kujitolea kwake kwa amani na mshikamano kati ya mataifa,” Papa alisema wakati wa hafla ya mapokezi iliyofanyika katika Kasri la Kifalme mjini Madrid.

    Kauli hiyo imekuja huku Uhispania ikiendelea kusisitiza suluhu za kidiplomasia na kuheshimu sheria za kimataifa katika kushughulikia migogoro mbalimbali ya kimataifa.

    Soma zaidi:

  15. Jeshi la Marekani lasema limedungua ndege mbili zisizo na rubani za Iran katika Mlango wa Hormuz

    g

    Chanzo cha picha, AFP VIA Getty

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika Mashariki ya Kati (CENTCOM) imedai kuwa imedungua ndege mbili zisizo na rubani ambazo ilisema zilirushwa na Iran.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, CENTCOM ilisema:

    "Vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati vilidungua ndege mbili za mashambulizi zisizo na rubani za Iran ambazo zilikuwa zikitishia usafirishaji wa kimataifa katika Mlango wa Hormuz."

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa vikosi vya Marekani vinaendelea kubaki katika maeneo yao ya operesheni na viko tayari kuendelea kujilinda dhidi ya kile ilichokitaja kuwa uchokozi wa Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya tarehe 07 mwezi Juni 2026.