Zaidi ya watu 1,000 wakamatwa katika operesheni ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu
Zaidi ya watu 1,000 wamekamatwa katika operesheni ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu iliyofanyika katika nchi 59.
Operesheni hiyo, iliyoratibiwa na Interpol na kujulikana kama Operation Global Chain, iliwalenga wahusika wa biashara haramu ya binadamu kwa madhumuni ya unyonyaji wa kingono, ajira za kulazimishwa, uhalifu wa kulazimishwa na kuwalazimisha watu kuombaomba.
Kwa mujibu wa mamlaka, mtandao uliokuwa ukiwasafirisha waathiriwa kwenda Cambodia kwa ajili ya ulaghai wa mtandaoni ulivunjwa, pamoja na mtandao mwingine uliokuwa ukiwalazimisha wasichana wenye umri mdogo waliopatikana kupitia mitandao ya kijamii kujiingiza katika biashara ya ngono barani Ulaya.
Kwa jumla, waathiriwa 2,070 au watu wanaoshukiwa kuwa waathiriwa walitambuliwa, wengi wao wakiwa wanawake. Kati ya waliokamatwa, watu 334 wanakabiliwa na tuhuma za biashara haramu ya binadamu, huku 690 wakikabiliwa na makosa mengine yanayohusiana na uhalifu huo.
Interpol, ambayo iliratibu operesheni hiyo kwa kushirikiana na Europol na Shirika la Ulaya la Kulinda Mipaka (Frontex), ilisema matokeo ya operesheni hiyo yamebaini njia na mbinu mpya zinazotumiwa na mitandao ya biashara haramu ya binadamu.
Operesheni hiyo iligundua mwenendo mpya ambapo waathiriwa kutoka Amerika ya Kusini wanasafirishwa kwenda Ulaya kwa ajili ya kazi za kulazimishwa. Takribani asilimia 10 ya waathiriwa waliotambuliwa walikuwa watoto kutoka bara la Amerika waliolazimishwa kufanyiwa unyonyaji wa kingono.
Katika hatua nyingine, mamlaka nchini Colombia zilianzisha kampeni ya uhamasishaji katika viwanja vya ndege ili kuwaonya wasafiri kuhusu hatari ya matangazo ya ajira za ulaghai nje ya nchi.
Interpol pia ilisema Polisi wa Brazil walitambua waathiriwa 406, raia 83 wa Brazil na raia 323 wa kigeni, waliokuwa sehemu ya mtandao wa kimataifa uliokuwa ukiwasafirisha watu kwenda Cambodia, ambako walilazimishwa kushiriki katika ulaghai wa mtandaoni.
Unaweza kusoma;