‘Maandamano Saba saba’: Ulinzi mkali waendelea Dar Es Salaam

Hali ya ulinzi imeonekana kuimarishwa zaidi katika jiji kuu la kibiashara la Tanzania Dar es Salaam, huku mamia ya maafisa polisi na jeshi wakionekana kutanda katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Hatua hii inafuatia wito wa maandamano kutoka kwa baadhi ya wanaharakati wa mitandaoni, wakidai mabadiliko na uwajibikaji kwa serikali.
BBC imeshuhudia doria za vyombo vya usalama katika maeneo mbali mbali ya jiji hilo.
Hata hivyo, maafisa hao hawajaweka vizuizi vya barabarani na wananchi wapo huru kuendelea na shughuli zai za kawaida. Hata hivyo kuna idadi ndogo ya magari na watu barabarani, leo ikiwa ni sikukuu nchini humo.
BBC imeshuhudia uwepo wa maafisa usalama waliojihami kwa silaha makutano ya barabara za Ali Hassan Mwinyi na Sam Nujoma eneo la Mwenge na Makutano ya Ali Hassan Mwinyi n Barabara ya Kawawa/Mwai Kibaki eneo la Kinondoni Morocco.
BBC pia imeshuhudia uwepo wa Askari wenye silaha katika vituo vingi vya mabasi ya mwendokasi jijini humo. Maafisa hao pia wameonekana katikati ya jiji eneo la Posta ambapo walikuwa wamejihami na gari ambayo humwaga maji ya kuwasha.
Kumeshuhudiwa ulinzi mkali pia katikati njia za kuingia katika bandari kuu ya Dar Es Salaam pamoja na eneo la bandari lenye maghala ya kuhifadhia mafuta upande wa Kigamboni.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata hivyo duru zinzonesha kuwa hofu ya ghasia na kumbukumbu za mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa Oktoba mwaka jana pamoja na kushindikana kwa maandamano yaliyoitishea Desemba 9 mwaka jana huenda kukapungunga matarajio ya kufanyika kwa maandamano hayo siku ya leo.
Makundi kadhaa ya haki za binadamu na upinzani yanasema maelfu ya watu waliuawa katika machafuko yaliyotokana na uchaguzi wa Oktoba 2025, huku takwimu rasmi za serikali zikisema ni takribani watu 500 ndio waliofariki.























